Dunia tuliyo nayo sasa imepitia vipindi mbali mbali ambavyo vimeacha alama kwenye maisha ya viumbe hai walopo ndani yake. Tangu historia ianze kundikwa kuhusu mwenendo wa dunia na mabadiliko yake kuna mengi yamegunduliwa na kuwekwa wazi ili kusaidia kuelewa baadhi ya taarifa muhimu ili tuweze kuchukua hatua muhimu.
Kuna ajenda nyingi sana ambazo hujadiliwa wanapokutana wakuu wa nchi hapa duiani, kuna vitu vingi vikubwa ambavyo vinaweza kutuunganisha na kutufanya kukaa meza moja na watu kutoka mataifa mbali mbali. Ni jambo kubwa sana kuona wakuu wa nchi, viongozi wa ngazi za juu sana hapa duniani na watalaamu wa masuala mbali mbali wakikutana kwa ajili ya kujadili ajenda ambazo zinaweza kuleta madhara makubwa endapo juhudi za makusudi za kila mmoja hazitatumika.
Kati ya ajenda kubwa zinazojadiliwa na wakuu wa nchi na Umoja wa Mataifa wanapokutana kwenye mikutano na vikao vyao, ni amani, ugaidi, umasikini, uchumi, biashara haramu, na mabadiliko ya tabia nchi. Kuna ajenda nyingine nyingi sana ambazo tunazisikia sana kwenye vyombo vya habari lakini kwakweli hayo niliyoyataja lazima moja wapo walijadili na kulitaja kama jambo muhimu kwa mustakabadhi wa kuifanya dunia kuwa sehemu salama ya kuishi.
Kati ya ajenda zote hizo na nyingine nyingi ambazo sijazitaja hapo zinajadiliwa sana na umoja wa mataifa, wakuu wa nchi na watalaamu kutoka kila pembe ya dunia ni MABADILIKO YA TABIA NCHI, kwa lugha ya kingereza wanasema “Climate Change”. Mabadiliko ya tabia nchi yamekuwa yakiundiwa vikao na mikutano mingi inayohusisha wakuu na watalamu kutoka kila pembe ya dunia ili kutafuta njia bora ya kuweka mambo sawa ili kuiokoa dunia.
Kwanini unafikiri mabadiliko ya tabia nchi yanapewa kipaumbele katika ajenda za kimataifa? Hii ni kwa sababu ni jambo ambalo linagusa kila nchi, kila mkoa, kila wilaya, kila Kijiji, kila mtu. Hivyo ni muhimu yakajadiliwa kwa kupata mawazo na mitazamo ya kila mmoja. Kwa sababu hakuna aliye salama katika hili, hakuna anayeweza kukwepa matokeo yake, kila mtu ataguswa, uwe unajua au hujui lazima utaguswa na jambo hili.
Kwa sehemu kubwa kabisa mabadiliko mabaya ya tabia nchi yanasababishwa na mtindo wetu wa maisha ya kila siku, mifumo na mipango ya serikali za nchi zetu katika uzaishaji na ukuaji wa uchumi vina mchango mkubwa sana katika kusababisha athari mbaya za mabadiliko ya tabia nchi.
Kwa mfano, ukuaji wa teknolojia ya viwanda vikubwa kwa vidogo, upanuzi wa mashamba kwa kukata miti na misitu ya asili, matumizi ya mbolea na kemikali ardhini vyote hivi na vingine vingi wanasayansi na watalaamu wa mazingira wanasema vinasababisha uzalishaji mkubwa wa hewa ya ukaa au kabonidayoksaidi ambayo ni hatari sana katika mfumo wa hewa huko angani; hivyo husababisha kuharibu kabisa blangeti ambalo huzuia mionzi mikali ambayo inatoka kwenye jua kuja moja kwa moja duniani.
Kwa ufahamu kidogo, katika sayansi ya mambo ya anga na jografia ni kwamba huko angani kuna kitu ambacho kipo kama blangeti au zulia kwa kingereza wanaita “Ozone layer” ambayo husaidia sana kuzuia mionzi mikali ya jua kupenya na kuja moja kwa moja duniani. Mionzi hii endapo haitazuiwa na uwepo wa ozone layer hii husababisha madhara mabaya kwa viumbe hai na vitu vingine vilivyopo hapa duniani. Mionzi hii endapo itakuja moja kwa moja duniani si kwamba itaharibu tu uoto wa dunia na viumbe hai wengine la hasha! Pia italeta magojwa mabaya kama vile kansa ya ngozi na kuongezeka kwa joto duniani nk.
Hata hivyo sayansi hii inasema, hewa ya ukaa inayozalishwa kwa wingi na viwanda tulivyo navyo, moshi wa magari, na mifumo mingine ambayo huzalisha hewa hii husababisha ongezeko kupita kiasi la hewa hii ya ukaa katika anga. Na kwa sababu ya uharibifu wa mazingira kwa kukata miti hovyo na kuchoma misitu kunasababisha hewa hii ya ukaa kutopungua kwasababu miti na mimea mingine hufyonza hewa ya ukaa kwa ajili ya matumizi ya utengenezaji wa chakula na virutumisho vingine muhimu kwa mimea. Hivyo kupungua kwa uoto wa misitu na miti asilia kutokana na mipango ya kilimo na maendeleo ya miundombinu kunasababisha kuharibiwa kwa kiasi kikubwa sana cha hekari za miti na misitu ambayo ingesaidia sana kupungua kwa hewa hii katika anga.
Aidha, katika kufikiri haya yote na matokeo yake, nini ambacho nitaweza kufanya mimi kama raia wa kawaida, uelewa sahihi wa mambo haya utasaidia sana kuchukua hatua sahihi za kupunguza majanga yanayoweza kuendelea kutokea. Kuna kitu kimoja tunatakiwa kujipa kitu hiki hakiitaji kuanza na makundi ya watu, ni kitu ambacho wewe rafiki yangu unayesoma makala hii unaweza kuanza kukifanya hapo ulipo, na kitu hicho ni utunzaji wa mazingira yanayokuzunguka.
Hapa kwenye utunzaji wa mazingira yanayokuzunguka nataka ujipe jukumu na wajibu huu kwenye maisha yako yaliyobakia hapa duniani, kuwa hutakata mito hovyo bila mpangilio, lakini pia utajipa jukumu jingine la kupanda miti kwenye eneo lako. Sambamba na jukumu hili jipe jukumu jingine la kutochoma misitu maana kwa kufanya hivyo utaharibu sio tu misitu hiyo bali na viumbe hai wengine kama vile wanyama na wadudu ambao ni muhimu katika mfumo wa ikolojia.
Kila mtu hapa Tanzania na duniani akaamua kujipa jukumu hili, hakika tungepunguza kwa kiasi kikubwa madhara yanayosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi. Na pia tungeokoa fedha nyingi sana ambazo hutumika katika harakati za kupambana na hali hii. Tukumbuke kuwa gharama za madhara ya mabadiliko mabaya ya tabia nchi ni kubwa kuliko tahadhari na hatua chache tutakazochukua kukabiliana na hali hii. Hivyo basi kazi ni kwetu kuweka mambo haya sawa na kuifanya dunia kuwa sehemu salama ya kuishi.
Ahsante sana kwa kusoma makala hii hadi mwisho!
Hillary Mrosso
+255 683 862 481/255 742 092 569
www.mtalaamu.net/wildlifetanzania