Habari rafiki yangu, karibu kwenye makala yetu ya leo ambayo tunaangalia mambo mbali mbali kwenye eneo hilli la uhifadhi wa wanyamapori. Leo tunaangali jinsi ambavyo jamii na watu wengi tunavyo waua wanyama mbali mbali kutokana na Imani na mitazamo ambayo sio mizuri. Hivyo tutaenda kuangalia namna ambavyo tunawauwa wadudu, ndege, na hata nyoka ambao hawajafanya madhara yoyote kwetu, hali hii sio nzuri endapo tutaendelea nayo, inabidi mitazamo yetu ibadilike kwa elimu hii tunayokwenda kujifunza hapa leo.
Mitazamo na Imani tulizo nazo wakati mwingine sio rafiki kwa viumbe hai walio karibu na makzi yetu. Ninapozungumzia viumbe hai au wanyamapori ni wanyama ambao hawafugwi na binadamu, wenyewe wanajitegemea kwa kila kitu katika maisha yao. Tuelewe kuwa uhifadhi sio tu ndani ya hifadhi za Taifa na mapori ya akiba, na sehemu zilizotengwa tu, hapana, hata maeneo yetu ya nyumbani, kama vile shambani, au kwenye bustani zetu kunakuwa na viumbe hai wengi sana wanaopenda kuishi karibu na watu, hivyo ni vema tukaweka mitazamo yetu vizuri ili tusiwadhuri au kuwaua.
Naamini wanyamapori au wadudu wanaopenda kuishi karibu na makazi ya watu sio hatari, ni kweli kabisa wengi wa viumbe hai hawa sio hatari kwa maisha yetu. Ni viumbe amabao wanapenda kuishi karibu zaidi na shughuli za kibinadamu, na pia wanapenda kusikia watu wakiongea na kupiga stori mbali mbali. Hivyo hupenda kuja karibu kabisa na makazi ya watu. Na kutokana na mawazo yetu au mitazamo yetu ilivyo kwamba hawa wanyama ni hatari au wabaya, haraka haraka tunawaua, na kuwaondoa kabisa kwenye maeneo yetu.
Kuna wanayama na viumbe hai wengi wanapenda kuishi karibu na makazi ya watu, au sehemu zilizo na misitu ya karibu na mazingira ya watu, wanyama hawa ni nyoka, ng’edere, nyani, ndege, kaluguyeye, vinyonga na wengine wengi sana. Wanyamapori hawa wanauwawa sana na watu kwa kuwa wanasemekana ni hatari kwa maisha ya binadamu, jambo ambalo sio mara zote ni kweli.
Pia tujue kuwaua viumbe hai ni kinyume na sharia za wanyamapori, hivyo angalia kabisa ujue ni wanyama gani au wadudu gani ambao ni hatari ili uwatoe kwenye eneo lako. Siku zijazo nitakuletea makala ya aina mbali mbali za nyoka na wadudu wengine ambao wanapenda kuishi karibu na maeneo ya watu, na watu bila kujua huwauwa. Hali ya namna hii ya kuua wanyama, na viumbe hai wengine wanaotokea kwenye maeneo yetu ikiendekezwa kuna mengi tutapoteza, kwa mfano unweza kusababisha kutoweka kabisa kwa aina hiyo ya viumbe hai.
Viumbe hai hawa wanamanufaa sana wanapoishi kwenye jamii zetu, manufaa haya mengi ni kwa ajili ya kuzaana na kuendeleza maliasili, kuna viumbe hai wengine huchagua sehemu maalumu ya kuzaliana na hivyo wanaweza kuja karibu na makazi ya watu na kuazliana kwa sababu labda ndio wamaona ni sehemu salama au ni sehemu yenye chakula na mazingira mazuri ya kulea watoto wao. Sababu ambayo huwapelekea kuja hata maeneo ya watu, na endapo tutawaacha bila kuwauwa au kuwafukuza au kuwabugudhi, wanyama hawa watajiona wapo salama kabisa na watazaana sana kwa ajili ya kujaza hifadhi na nchi yetu vivutio vingi. Pia sambamba na hilo wanyama hawa ni kwaajili ya tafiti mbali mbali, nakumbuka tulivyokuwa chuo watu walikuwa wanatafuta viumbe hai mbali mbali kwa ajili ya tafiti zao za kumaliza elimu ya juu.
Hivyo rafiki na msomaji wangu, tunawajibu mkubwa wa kuielimisha jamii yetu kwenye mambo ya namna nyingi kuhusu wanyampori. Mitazamo na Imani zetu zisiwe ndio kikwazo kwa uwepo wa viumbe hai hapa duniani, kumbuka jinsi nilivyokwambia hapo juu kwamba asilimia kubwa ya viumbe hai wanaokuja vijijini kwetu au wanaopenda kuishi karibu na makazi ya watu hawana madhara kabisa, hata kama ni nyoka, nyoka wengi huwa hawana sumu, hivyo usiwaue kwa kuwa unawaogopa. Tubadilishe kabisa mitazamo yetu kwenye hili, kuna wengine watu wengine wana wauwa hadi vipepeo, hii yote nikukosa uelewa na mitazamo isio sahihi kwa viumbe hai hawa wanaoona fahari kuishi karibu na makazi ya watu. Tuishi nao vizuri, na kama wanakusumbua unaweza kuwasiliana na mamlaka husika, au viongozi wa kijiji au mataa wako, au unaweza kuwasiliana moja kwa moja na watu wa maliasili.
Nakushukuru sana kwa kusoma makala hii, naamini tutawatunza na kuwaacha wanyamapori au viumbe hai kwenye maeneo yetu salama, usikimbilie kuchukua hatua mkononi kwa kila unachokiona mbele yako, jifunze na angali kama kinaweza kuleta madhara kwako.
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
0742092569/0683248681