Zama tunazoishi ni zama ambazo kila kitu kinatakiwa kufanyika kwa haraka na kwa ufanisi, tunajua wote kwa asilimia kubwa tuna adhiriwa na ukuaji wa teknologia mbali mbali, ambazo zimebadili kabisa mifumo mingi ya maisha ambayo ilikuwa imezoeleka kwa muda mrefu. Kwa sasa kasi katika ufanyaji wa mambo umekuwa mkubwa sana. Hivyo tabia nyingi za watu zimebadilika sana kutokana na ukuaji wa teknologia hizi, kwa mfano unaweza kujua kinachoendelea China au Marekani ukiwa hapo hapo kijijini kwenu au sehemu yoyote ile.Uendeshwaji wa mambo kwa kasi ndicho watu wanachotegemea na kuhitaji kwa kipindi hiki, hakuna mtu anayetamani kupoteza muda wake, kila mtu anataka afanye mambo mengi kwa muda kidogo alio nao. Kwa nchi zilizoendelea ndio wanaopenda kanuni hii ya kutumia muda kidogo kwa kufanya mambo mengi. Katika masuala ya utalii watu wengi wanaokuja kutembelea hifadhi zetu wanaangalia vitu vingi sana ambavyo tunatakiwa kuviangalia kwa makini endapo tunataka kuwa na maendeleo kwenye utalii wetu.
Ukiachilia mbali rsilimali tulizo nazo katika hifadhi zetu, unaweza kukuta hifadhi ni nzuri sana na inawanyama wa kipekee, kuliko hifadhi nyingine, unakuta hifadhi ina mandhari nzuri na ya ubora mzuri lakini kikwazo kikubwa ni miundombinu ya usafiri wa barabara na viwanja vya ndege. Kuna siku nilikuwa na watalii fulani kutoka nchi mbali mbali waliotembelea hifadhi ya Taifa ya Ruaha, nikawauliza ni kitu gani kimewavutia kuja Ruaha, na sio maeneo mengine, walinijibu mambo mengi ambayo ni mazuri sana na walisema katika hifadhi zote walizotembelea hifadhi yahii ni ya kipekee sana na vitu vingi ni vya kuvutia. Nikamuuliza tena huwa unatembeleaga nchi nyingine tofauti na Tanzania, akajibu ndio; mwisho nikamuuliza unaonaje na kwa uzoefu wako wa kutembelea hifadhi nyingi duniani, unafikiri ni changamoto gani Tanzania tunayo hasa kwenye sekta ya utalii. Jibu lake lilikuwa ndio msingi na ndio kiini cha makala hii.
Tanzania inavivutio vingi sana ukiachilia mbali hifadhi za wanyamapori tulio nao, lakini jinsi ya kufika hapo kwenye hicho kivutio ndio changamoto yenyewe. Aliniambia watalii wengi wanaokuja Kutembelea hifadhi na vivutio vingine ni watu wenye pesa na wengine ni matajiri sana. Na wengi wao wanaheshimu sana muda kuliko hata pesa. Wanapenda waende sehemu hata kwa gharama kubwa lakini wafike hapo kwa wakati na waondoke hapo kwa wakati. Fikiria mtu anataka kukaa Tanzania kwa siku tano, na hizo siku tano amepanga kutembelea Serengeti, Ruaha, na Zanzibar. Mtu kama huyu mara nyingi huwa na hela nyingi za kutumia, lakini anapokuja na kuona usafiri kwa baadhi ya maeneo hakuna anasikitika sana na anaweza asirudi tena kutembelea hifadhi zetu. Lakini anapokuja na kukuta barabara ni nzuri, viwanja vya ndege vya kisasa, kuna magari mazuri ya kisasa, na vinapitika wakati wote inamsaidia sana kuokoa muda wake na pesa zake, na atamaliza vizuri ziara zake na kuondoka kwa furaha.
Ukiangalia barabara kuu zinazotoka mjini hadi hifdhini sio nzuri, kwa mfano barabara kuu ya kutoka Iringa mjini hadi hifadhi ya Ruaha ni ya vumbi na inaharibika mara kwa mara hasa kipindi cha mvua. Hivyo wawekezaji kwenye sekta ya utalii hawawezi kuwekeza sehemu amabayo miundombinu sio rafiki kwake, ndio maana utakuta magari ya kitalii sio mengi kwa sababu anajua barabara sio nzuri na barabara itaharibu magari yake na kumsababishia hasara ambayo hakupanga. Fikiria barabara hii ingekuwa na lami nzuri kutoka mjini hadi lango kuu la hifadhi naamini mapato ya utalii yangepanda zaidi ya ilivyo sasa, na watu wangekuwa na hamasa ya kuwekeza kwenye maeneo yote ya vivutio vya utalii. Na miundominu hii ya barabara isingesaidia tuu hifadhi kupata mapato mengi bali ingekuwa ni kichocheo kwa wanajamii au watu wengine wanaoishi maeneo yaliyo karibu na hifadhi.
Kwa kuwepo kwa miundombinu ya barabara za kisasa na viwanja vya ndege, tungeweza kusaidia hata asasi nyingine za kijamii kama vile Maeneo ya Usimamizi wa wanyamapori (Wildlife Manegement Areas) WMA, kama vile MBOMIPA kwa eneo la Ruaha na asasi nyingine za kijamii katika eneo maeneo ya hifadhi, hii ndio sababu kubwa kwa mapori tengefu, maeneo ya usimamizi wa wanyamapori, kwa upande wa kaskazini zina kusanya mapato mengi yanayosaidia kujiendesha yenyewe bila kutegemea mifuko na bajeti nyingine za serikali. Hivyo njia nzuri ya serkali kuzisaidia kifedha maeneo haya ya usimamizi wa wanyamapori, sio kuwapa pesa za kujiendesha bali kujenga miundombinu rafiki na imara kwa uwekezaji wenye tija kwa maliasili zetu. Ni ukweli usio pingika kabisa kwamba maeneo ya usimamizi wa wanyamapori kama MBOMIPA yana idadi kubwa sana ya vivutio vyote muhimu kwa watalii na watafiti wa wanyamapori.
Tunaweza kujenga misngi imara sasa ambayo itakuwa na mapato endelevu vizazi na vizazi. Serikali izingatie kuimarisha mapato ya nchi kupitia utalii wa ndani na utalii wa nje, kwa kuweka barabara nzuri. Tena kukiwa na barabara nzuri na zenye kupitika kwa urahisi utalii wa ndani unaweza kuongezeka zaidi ya hapa ulipo sasa. Kwani watanzania wengi hawana usafiri binafsi na hata wale weneye usafiri binafsi hawawezi kuja na magari yao mpaka hifadhini kwasababu ya ubovu wa barabara. Na kama kutakuwa na barabara nzuri gharama za kutembelea hifdhi zitapungua na kusababisha watu wengi kuingia hifadhini mara kwa mara.
Tunatakiwa kujenga mazingira mazuri yatakayosababisha rasilimali zote tulizonazo zinazalisha na kuinua uchumi wa nchi yetu na kuboresha maisha ya watanzania. Tunatakiwa kuweka kila kitu kinachotakiwa kuwa sawa ili kila mtu apate faida kubwa ya hifadhi za wanyamapori na maliasili nyingine. Kuwa na rasilimali nyingi ambazo hazina msaada kwa jamii, au kuwanufaisha watu wachache, jamii haitatoa ushirikiano kwenye utunzaji wa rasilimali hizo. Jamii ikipata faida za moja kwa moja kutokana na uwepo wa rasilimali hizo, hakutakuwa na nguvu kubwa ya kuwaomba au kuwashawishi watu wawajibike kwenye utunzaji na uhifadhi wa rasilimali zao. Kukosekana kwa ushirikiano kwenye mambo ya msingi, ni ishara ya kukosekana kwa haki kwenye mambo ya msingi. Tujipange sawasawa tunaweza kwenda mbali zaidi ya hapa tulipo na tulikotoka.
Nakushukuru kwa kusoma makala hii iliyoandaliwa na kuandikwa na;
Hillary Mrosso
0742092569