Tafadhali soma hii ni muhimu sana hasa eneo la uhifadhi.

Habarini kwa mara nyingine tena ndugu zangu katika uhifdhi.

Leo narudi tena kidogo kwa upande wa mamalia katika kujuzana machache kuhusu wanymapori.

Leo nitaongelea mnyama ambae yupo kwenye kundi jamii ya swala.

Jina “SWALA” nipana sana na limebeba wanyama wengi na jamii nyingi sana ndani yake. Walio wengi wanaposikia jina swala basi fikra na mawazo yao huwatuma kuwa swala ni jina la mnyama mmoja tu. Kumbe mnyama huyo wanae mfahamu kwa jina la swala tu jina lake haliishii hapo nakumbe anaitwa “swalapala”

Kama ni wewe ni mfatiliaji mzuri wa masuala ya wanyama pori ambayo nimekuwa nikituma mara kwa mara humu, nimewahi kutaja baadhi ya wanyama ambao wote kwa ujumla wao wanaitwa swala lakini kinacho watofautisha swala hawa ni jamii zao au aina ya swala husika. Labda leo nirudie japo kwa uchache uweze kuwajua swala wengine ambao nadhani ulikuwa huwafahamu kama nao ni jamii ya swala. Mfano Nyumbu,Pofu,Kongoni,Swalapala,Pongo,Digidigi,Minde nawengine wengi hawa wote kwa jina moja wanaitwa swala.

Sasas leo napenda tumfahamu  aina ya swala ambae “ANAPATIKANA NCHINI TANZANIA TU” na huwezi kumpata sehemu yoyote ile duniani. Aina hii ya swala anajulikana kwa jina la “MINDE”

 MINDE ni mnyama jamii ya swala ambae anapatikana nchini Tanzania tu na si kwingine kokote duniani. Mnyama huyu hupendelea sana maeneo ya misitu  na yakujificha zaidi. Kadri tutakavozidi kuendelea na somo tutaona hapa nchini Tanzania wanapatikana maeneo gani na si kila eneo utawwza kumuona minde. Minde kwa mara yakwanza kabisa alipigwa picha mwaka 2003 na ilikuwa ni kutokana na kamera ambazo zilifungwa msituni katika suala zima la kufatilia maisha ya wanyamapori. Utaweza kuona ni hivi karibuni tu tangu mnyama huyu kugundulika vizuri na kwa ufasaha zaidi. Na hii imepelekea baadhi ya sifa zake kutofahamika zaidi hasa kwa upande wa kuzaliana japo kuna tafiti zilifanyika nakuona kwamba majira yao yakuzaliana hayana tofauti sana na wanyama jamii yao. Tutakapofika kwenye kuzaliana tutaona angalau kwa uchache kuhusu minde.

SIFA ZA MINDE

1.Ana mwili mfupi na uliojengeka imara zaidi.

2.Ana miguu mifupi na minene pia shingo yake ni fupi.

3.Rangi yake ni kahawia ilio pauka kidogo lakini inakuwa kama yenye kiza hasa upnde wa chini maeneo ya kifuani na tumboni.

4.Uso wake una rangi ya majivu iliyo pauka na manyoya marefu yenye rangi kahawia katikati ya pembe.

5.Ana pembe fupi na zilizo chongoka zaidi zenye urefu wa sentimita 8-12

6.Mkia mfupi enye manyoa yenye rangi nyeusi pembezoni.

UKUBWA

Minde jike na dume hawana tofauti kubwa sana na hivyo ukubwa wa miili yao nima ifuatavyo

Urefu sentimita 97-140sm

Mkia sentimita 8-13sm

Uzito kilogramu 50-60kg

TABIA ZA MINDE

Kutokana na usiri na asili yao ni tabia chache sana za minde ambazo zinafahamika nazo ni kama ifuatavyo

1.NI wanyama ambao wanapenda sana kutembea mida ya usiku ukilinganisha na mchana.

2.Ni mnyama msiri na asiependa kuonekana mara kwa mara kama walivyo baadhi ya swala

MAZINGIRA

Minde hupendele maeneo yenye misitu minene na yenye miinuko kutoka usawa wa bahari kuanzia mita 1,300-2,700. Lakini wakati mwingine huonekana mpaka maeneo yenye muinuko wa mita 4,000 kutoka usawa wa bahari. Minde wakubwa pia huweza kuonekana katika maeneo yenye misitu ilioharibiwa kutokana na shughuli za kibinadamu na pia misitu ya upili ambayo labda ni yakupanda au iliyoota baada ya misitu ya zamani kuharibiwa. Ni mara chache sana kumuona minde katika maeneo ambayo sehemu kubwa ya ardhi imetawaliwa na majani.

SEHEMU ANAZO PATIKANA MINDE

Minde wanapatikana maeneo makuu matatu hapa nchini. Maeneo haya ni milima ya tawa la mashariki. Mlima Kilimanjaro na maeneo ya Nyanda na juu Kusini. Ninapoongelea milima ya tawa la mashariki hapa na zungumzia hasa safu za milima ya Usambara na safu za milima ya Uluguru. Kwa upande wa Nyanda za juu Kusini tunazungumzia maeneo ka Mikoa ya Iringa, Njombe na Ruvuma.

CHAKULA CHA MINDE

Chakula kikuu cha minde ni majani na wakati mwingine hula baadhi ya matunda yaliopo misituni.

Lakini pia minde hujulikana kama mnyama ambae anakula viumbe walio hai hasa kutokana na picha ilioonekanana akiwa anakula chura.Hii nadhani anaweza kuwa muwindaji pia.

KUZALIANA

Kama nilivo tangulia kusema hapo juu kuwa ni machache sana yanayofahamika kuhusu kuzaliana kwa minde. Lakini utafiti unaonesha kuwa kuna baadhi ya wanyama ambao ni jamii ya swala na wana ukaribu sana na minde ambao wanaweza kufananishwa nao. Japo pia watoto wa minde huwa wanaonekana sana kuanzia miezi ya tisa na kumi. Hii ilifanya watafiti kuhisi kwamba minde huenda wana zaa mara moja tu kwa mwaka.

IDADI YA MINDE

Sensa iliyo fanyika mwaka 2008 ili kuchukua takwimu na kutambua idadi ya minde kwa ujumla ilitoa majibu kuwa idadi ya minde nchini ilikuwa ni chini ya 1,500. Kwasasa tunasubiria takwimu nyingine tuone je wameongezeka au wamepungua wanyama hawa.

CHANGAMOTO NA TISHIO

Upungufu wa minde unatokana na sababu nyingi sana na hizi hapa ni sababu kuu zaidi.

1.Ujangili ulio kithiri tena hasa kutokana na mitego. Minde wamekuwa wakiwindwa sana misituni kwa mitego ya waya na vitanzi hatimae wakinasa tu basi ndio unakuwa mwisho wa maisha yao.

2.Uharibifu wa mazingira unaosababishwa na ukataji wa misitu hasa kwa ajili ya nishati ya kuni ma malighafi za ujenzi. Wakazi wa vijiji vingi vinavyo pakana na misitu hukata sana miti nakuharibu mazingira hivyo kupelekea kupotea kwa minde. Na hii hasa imeonekana maeneo karibu na Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa.

3.Uvamizi wa misitu kwa ajili ya makazi ya watu hili pia ni tatizo kubwa sana linaloonekana kuhatarisha maisha ya minde katika misitu.

4.Kuongezeka kwa maeneo ya kilimo hasa karibu na hifadhi za taifa hususani Udzungwa kumepelekea sana kupungua kwa idadi ya minde maeneo hayo.

Japo pia watoto wa minde wanapokuwa wadogo hushambuliwa na wanyama kama chui na fisi lakini hii hatuwezi kusema ni sababu ya wanyama hawa kutoweka kwasababu ukisoma maumbile asili utagundua hii ni lazima iwepo ili kuweka usawa wa idadi ya wanyama katika mazingira husika.

Suala linguine pia ni magonjwa ya wanyama ambapo pia sio tatzo linloweza kuingizwa kuwa tishio la kutoweka kwa minde katika misitu yetu.

UHIFADHI

HII NDO SEHEMU MUHIMU SANA. ISOME KWA UMAKINI ZAIDI TAFADHALI.

Kutokana na kupungua kwa idadi ya minde hapa nchini, wanyama hawa waliingizwa rasmi na IUCN katika kundi la wanyama ambao wapo hatarini kutoweka duniani. IUCN ni shirika la umoja wa mataifa linalo jihusisha na uhifadhi maumbile asili duniani na husaidia sana katika kuhakikisha maumbile asili yanabaki kama yalivyokuwa (IUCN kirefu chake ni INTERNATIONAL UNION FOR CONSERVATION OF NATURE). Kama tulivyoona hapo juu wanyama hawa wamekuwa wakiwindwa sana nakupelekea kupungua kwa kiasi kikubwa sana. Tuliona kuwa wanyama hawa walikuwa wakionekana maeneo ya mlima Kilimanjaro, milima ya tawa la mashariki na nyanda za juu kusini lakini kwa sasa inasemekana kuwa katika maeneo ya milima Uluguru wanyama hawa wamepotea na kwa miaka hii michache hawaonekani hali inayopelekea wasiwasi kusema kwamba katika milima Uluguru minde wametoweka.

Na changamoto kubwa hasa inayopelekea kupungua kwa minde hapa nchini ni kama tulivoona hapo juu kiasi kwamba tutawakosa kabisa wanyama hawa adimu.  Lakini kwa jibu sahihi ni kwamba namba ya minde inazidi kupungua siku baada ya siku na mwisho watabaki kuwa jina tu duniani kwamba walikuwepo Tanzania.

 NINI KIFANYIKE KUNUSURU WANYAMA HAWA WALIO HATARINI KUTOWEKA

1.Mamlaka husika zihakikishe zinaweka mipango thabiti katika kupambana na uvamizi wa misitu ili kupunguza janga la upotevu wa minde.

  1. Kuwe na ukaguzi mara kwa mara wa maeneo yote ya hifadhi za misitu kukagua mitego iliotegwa kwa ajili yakuwakamata minde.

3.Jamii ishirikishwe kwa ukaribu zaidi hususan zinazoishi pembezoni mwa misitu na hata walio mijini kuhusu masuala ya umuhimu wa uhifadhi wanyamapori na faida zake hasa kwenye pato la taifa.

4.Kuanzishwa kwa miradi mbalimbali yakimaendeleo katika vijiji ili kupunguza tatizo la ujangili na kuwafanya wananchi kuwa wachakarikaji kuokana na miradi iliyo anzishwa. Hii itafanya wana kijiji kuwa mabalozi wazuri hasa kuwafichua majangili katika vijiji vyao.

  1. Utekelezaji wa sheria kali zilizowekwa kwa yeyote atakae kamatwa kwa kosa la ujangili wa wanyamapori.

6.Tuepushe siasa kwenye suala la uhifadhi wanyamapori hii ni sumu kubwa sana katika sekta hii.

SHUKRANI sana kwa mamlaka za upande wa nyanda za juu kusini kwa kuleta mpango wakuajiri wawindaji na kutoa elimu juu ya mazingira na kuwatunza wanyamapori. Lakini pia kumfanya minde kuwa kama nembo muhimu sana hasa kwa maeneo ya nyanda za juu kusisini. Hongereni sana ndugu zangu na muendelee na wito huo mpaka mwisho.

HITIMISHO.

Inaskitisha sana kuona bado watanzania tulio wengi tupo nyuma katika kuona umuhimu wa uhifadhi wanyamapori hasa ukiangalia unafaida kubwa sana. Lakini pia inabidi tuguswe sana hasa na ufahari wa mnyama huyu minde ambae huwezi kumpata sehemu nyingine yoyote ile hapa duniani zaidi ya nchini kwetu Tanzania.

Tuzisaidie mamlaka husika katika kupambana na ujangili na hata pia uvamizi wa maeneo tengefu kwa ajili ya uhifadhi wa mistu na wanyamapori kwa ujumla.

Kama ilivyo ada huwa siachi kusema kuwa siku zote tusiingize siasa kwenye suala zima la uhifadhi wanyamapori na misitu maana lina changamoto kubwa sana.

AHSANTENI SANA

Kwa mengi kuhusu wanyamapori na uhifadhi lakini pia mawazo na ushauri tuwasiliane kupitia

Simu=0714116963/0765057969/0785813286

Email-swideeq.so@gmail.com

”I’M THE METALLIC LEGEND”