Habari ndugu msomaji wa makala hizi za wanyamapori. Tunaendelea na mfululizo wa uchambuzi wa nyoka jamii ya swila na leo nakuletea aina nyingine ya swila ambao wanapatikana pia hapa nchini Tanzania na Afrika mashariki kwa ujumla. Makala ya leo nakusogezea swila ajulikanae kama SWILA MWEKUNDU (RED SPITTING COBRA) ambae kwa jina la kisayansi hujulikana kama NAJA PALLIDA.

Nakusihi ndugu msomaji wa makala hii tuwe Pamoja mwanzo mpaka mwisho ili uweze kujifunza mambo mengi kuhusu swila huyu adimu hapa nchini hasa kutokana na maeneo ambayo wanapatikana. Kuna sababu mbali mbali ambazo zinapelekea swila hawa kuwa adimu ambazo kwa asilimia kubwa hutokana na sisi binaadamu. Moja wapo ni uharibifu wa mazingira ambayo ni mazalia ya swila hawa na sehemu yao ya kiikolojia.

JINSI YA KUWATAMBUA SWILA MWEKUNDU

  • Rangi ya swila hawa hutofautiana hasa kutokana na mazingira wapatikanayo. Kwa hapa Tanzania, mashariki na kusini mwa Kenya swila hawa huwa na rangi ya machungwa au nyekundu huku shingoni wakiwa na mraba mpana wenye rangi nyeusi. Kadri wanavyozidi kuwa wakubwa rangi hubadilika na kuwa nyekundu au kahawia huku alama nyeusi shingoni nayo huanza kupotea.
  • Wana alama ya mshono yenye rangi nyeusi kwenye magamba chini ya macho ambayo huwafanya waonekane kuwa na alama kama tone la machozi.
  • Hawa ni miongoni mwa swila ambao sio wanene sana wala sio wembamba sana ambao wana vichwa vidogo na macho makubwa yenye mboni za duara.
  • Miili yao ina umbo la bomba, mikia yao ni mirefu ya wastani ambayo huchukua asilimia 15 mpaka 19 ya urefu mzima wa miili yao.
  • Wana magamba malaini sana ambayo yamejipanga kwa safu kati ya 21 mpaka 27 sehemu ya kiwiliwili, safu 197 mpaka 228 sehemu ya chini na safu 61 mpaka 72 sehemu ya nyuma.
  • Kama nilivo tangulia kukujuza hapo mwanzo swila hawa ni miongoni mwa swila wenye mili midogo, huwa na urefu wa kati ya sentimita 70 mpaka mita 1.2.

Swila mwekundu (Picha na ferrebeekeeper)

TABIA ZA SWILA MWEKUNDU

  • Hupendelea kuishi maeneo ya nchi kavu hasa ardhini jappo wana uwezo pia wa kupanda juu hasa kwenye vichaka na miti mifupi mifupi.
  • Wana uwezo wa kutambua hatari kwa haraka zaidi na uwezo wa kujongea kwa haraka sana hasa pale wanapopata upenyo wa kumkimbia adui au kuondoka sehemu ya hatari.
  • Kama zilivyo jamii nyingi za swila, swila hawa wana tabia pia ya kutanua mashingo yao pale wanapohisi hatari au utofauti wowote kwenye mazingira yao.
  • Swila mwekundu huweza kuinua shingo yake juu zaidi na kurusha sumu kama njia ya kujihami pale wanapohisi hatari. Hivyo kuwafanya swila hawa kuwa miongoni mwa jamii za swila ambao wanarusha sumu.
  • Swila hawa mara nyingi hufanya mawindo yao majira ya usiku na hupenda kupumzika kwenye mashimo ya mchwa, vichakani na kwenye magogo ya miti. Watoto mara nyingi huwa wanaonekana majira ya mchana.

Swila mwekundu (Picha na ferrebeekeeper)

MAENEO WAPATIKANAYO SWILA WEKUNDU

Swila hawa wanapatikana maeneo ya savana na maeneo ya nusu jangwa ambayo huwa na muinuko usiozidi mita 1200 kutoka usawa wa bahari. Wanapatikana nchi mbali mbali za Afrika mashariki isipokua Uganda tu.

Hapa nchini swila hawa wanapatikana eneo dogo sana ambazo ni kaskazini na sehemu chache kaskazini mashariki. Maneneo ya kaskazini ni Olduvai Gorge na Longido huku kaskazini mashariki wanapatikana eneo la pori la akiba Mkomazi.

CHAKULA

Chakula pendwa sana cha swila hawa vi viumbe jamii ya amfibia (vyura). Pamoja na vyura swila hawa huwa wanakula mamalia wado wadogo kama panya na jamii nyingine za wanyama kama mijusi na ndege.

KUZALIANA

  • Jike hutaga mayai kati ya 6-15 yenye ukubwa wa sentimita 5 x 2.5 ambayo huchukuwa takribani siku 80-120 mpaka watoto kutoka kwenye mayai.
  • Kama zilivyo jamii nyingine za swila, swila hawa hawana utaratibu ya kulinda mayai mara baada ya kutaga hivyo huyaacha bila usimamizi japo hutaga sehemu ambayo imejificha kiasi kwamba ni ngumu kwa maadui kuyaona.
  • Watoto wanapotoka kwenye mayai huwa pia hawana usimamizi au ulinzi toka kwa mama hivyo hulazimika kuanza maisha kwa kujitegemea wao kama wao.
  • Wachache sana hufikia umri wa kuzaliana kwani wengine hupoteza maisha kutokana na njaa au kuliwa na viumbe wengine.

SUMU

Athari ya sumu ya swila hawa haijulikani sana kwani matukio ya nyoka hawa kumuuma binaadamu ni machache sana. Sumu yake inaaminika pia kushambulia misuli kama ilivyo sumu ya swila wa Msumbiji na pia huweza kuzalisha kiwango kikubwa sana cha sumu . Kuna baadhi ya maeneo huwa waanaamini mtu anapoumwa na swila hawa basi anaweza kula kitu chochote ambacho kitamfanya atapike ili kupunguza sumu ya nyoka hawa mwilini. Swila wa Msumbiji: Nyoka Mwenye Sumu Kali Ambaye Watu Wengi Hawamjui

Kama ilivyo kwa swila wengine ambao hurusha sumu, moja kati ya dalili za kuumwa na swila mwekundu ni kumuangalia mtu machoni kama ana ishara ya sumu au kuangalia dalili za sumu ambazo hufanana na zile za swila ambao nilikwisha waelezea katika makala zilizo pita.

MWISHO

Nakusihi mpenzi msomaji wa makala hizi kuendelea kufuatilia mfululizo wa makala hizi ili uzidi kujifunza mambo mengi sana kuhusu nyoka jamii ya swila. Katika makala ijayo nitakuwekea mezani spishi nyingine ya swila mpaka pale tutakapo wamaliza swila mwapatikanao Afrika mashariki hususani hapa nchuni Tanzania. Makala hii imehaririwa na Hillary Mrosso.

Kwa maswali, ushauri au maoni kuhusu makala hii usisite kuwasiliana nami,

 

Sadick Omary Hamisi

Simu; 0714116963

Email; swideeq.so@gmail.com

Instagram; wildlife_articles_tanzania

Facebook; Sadicq Omary Kashushu/Envirocare and wildlife conservation

Tovuti; www.wildlifetanzania.co.tz

 I’M THE METALLIC LEGEND…