Ni matumaini yangu umzima wa afya kabisa ndugu msomaji wa makala hizi za wanyamapori. Ni muda sasa umepita tangu nilipo kuletea makala iliyopita na naimani ulijifunza mengi sana kupitia makala ile huku ukibaki na furaha sana kujua nini kinaendelea kuhusu mnyama yule. Kama ilivyo kawaida leo tena tunaingia darasani kumuangalia mnyama mwingine huku nikiendelea tena kukusihi kufuatilia makala zijazo uweze kujifunza mengi zaidi na kufurahia maliasili zetu hapa nchini.
Leo tutamjia vizuri mnyama ajulikanae kwa jina la “KURO” (Waterbuck) Wanyama hawa hususani hapa Afrika mashariki wapo wa jamii mbili ambazo ni
- Kuro defassa na
2.Kuro wa kawaida.
Tofauti kati ya jamii hizi mbili ni alama za rangi nyeupe kwenye maeneo ya kiuno.
Kuro defassa ana alama nene nyeupe kwenye pande zote mbili za kiuno huku kuro wa kawaida akiwa na alama nyeupe zilizo tengeneza alama kama ya mikunjo kiunoni. Sifa nyingine zilizobaki wanyama hawa wana fanana kwa asilimia kubwa sana.
UTANGULIZI
Kuro ni baadhi ya wanyama wapatikanao maeneo mengi hapa Barani Afrika hasa katika hifadhi za wanyamapori. Lakini mbali na kupatikana maeneo mengi hapa Barani Afrika, mnyama huyu huwezi kumuona sehemu nyingine yoyote nje ya Bara la Afrika. Yani kwaufupi Kuro ni wanyama ambao wanapatikana Bara la Afrika tu.
Sasa twende kwa undani zaidi ili kumjua mnyama kuro yupoje pamoja na sifa hali kadhalika tabia za mnyama Kuro kwa ujumla. Bila kusahau mazingira na changamoto zinazo wakumba wanyama hawa pamoja na uelekeo wa wanyama hawa kwa sasa.
SIFA NA TABIA ZA KURO
1.Wana miili yenye manyoa marefu yenye rangi ya kijivu-kahawia ambayo kwa haraka haraka inataka kufanana na wekundu na miguu yenye rangi ya kufifia.
2.Wana alama nyeupe usoni ambayo imezunguka pua na mdomo na sehemu ya juu ya jicho. Alama hii pia huonekana maeneo ya kwenye koo.
3.Wana masikio mafupi yenye umbo la duara yenye rangi nyeupe kwa ndani na rangi nyeusi kwenye ncha za masikio kwa upande wa pembeni na juu.
4.Dume huwa na pembe ndefu na zenye nguvu ambazo huwa zinaota kuelekea upande wa nyuma na kadri zinavo refuka huanza kupinda na kuelekea mbele. Pembe hizi huweza kufikia urefu wa hadi sentimita 99, Jike huwa hana pembe kabisa.
5.Ni wanyama ambao huishi kwenye kundi hasa kina mama ambapo kundi linaweza kuwa na idadi ya wanyama hadi 25. Japo madume ambao bado ni wadogo nao pia hutengeneza makundi yao na kutembea pamoja.
6.Tofauti na jamii za wanyama wengine walao majani ambao baadhi huweka alama kwenye himaya zao kwa kutumia mkojo au kinyesi, Kuro dume huweka alama kwa hutoa vitu kama mafuta mwilini mwake ambavo huwavutia majike na pia kuwafanya madume wengine wasisogee eneo hilo.
7.Mafuta yatokayo mwilini mwa dume na kubaki kwenye manyoa yake humfanya Kuro kuwa na harufu mbaya hasa kwa wanyama walao nyama. Na hii humsaidia mnyama huyu kutopendelewa sana na wanyama kama Simba au Fisi katika mawindo.
8.Ni miongoni mwa wanyama wenye mikia mifupi ambayo huwa na sentimita 33sm – 40sm
KIMO, UREFU NA UZITO WA KURO
Kimo= Kuro mkubwa hufikia kimo cha futi 3.9 – 4.5
Urefu=Hufikia urefu wa sentimita 177sm – 235sm.
Uzito= Dume huwa mzito kidogo kuliko jike huku akiwa na uzito wa kilogramu kati ya 200kg – 300kg, wakati jike huwa na uzito wa kilogramu kato ya 160kg – 200kg.
MAZINGIRA
Wanyama hawa hupendelea mazingira ya Savanna na miti mingi. Hupendelea maeneo yenye maji baridi na pia yenye majanio ya kutosha. Maeneo haya yenye majani marefu na miti mingi sio kwamba yanawasaidia kwa kupata chakula tu hapana, bali pia huwasaidia kujificha kutokana na maadui zao.
CHAKULA
Hawa ni miongoni mwa wanyama walao majani kama walivyo kina Nyati, Nyumbu, Twiga, Pofu na wengineo. Na maeneo wapendayo kuisho Kuro huwa na chakula takribani mwaka mzima.
Huwa wanakula kipindi cha asubuhi na usiku na kutumia muda wa mchana kucheuwa na kuyatafuna majani upya huku wakiwa wamepumzika sehemu yenye kivuli kizuri. Hupendelea kunywa maji mara kwa mara na hii ndo sababu wanyama hawa hupenda kuishi maeneo ambayo yana upatikanaji wa maji kwa urahisi zaidi.
KUZALIANA
Inapofika kipindi cha kuzaliana madume huwa wanapigana sana ili kutawala kundi la kina majike. Hupigana kwa kutumia pembe na anaeshinda basi humiliki kundi zima la majika nakuwa chini ya utawala wake. Kisha huanza kuzalisha kemikali mwilini mwake na kutumia kama ishara ya mipaka ya himaya yake ili kuzuiya madume wengine wasiingie maeneo hayo.
Mara baada ya kuwapanda majike, majike hukaa na mimba kwa takribani miezi minane na baada ya hapo huzaa mtoto mmoja tu. Mama humficha mwanae sehemu yenye majani mengi dhidi ya maadui na huwa anarudi mara tatu hadi nne kwa siku kumnyonyesha mtoto. Hali hii huchukua takribani wiki mbili hadi tatu mpaka kuanza kutembea na mwanae. Humnyonyesha mtoto kwa muda wa dakika tano hadi kumi na wakati huo huwa ana msafisha mtoto ili kuondoa harufu ambayo inaweza wafanya maadui kutambua mahali alipo mtoto huyo. Japo watoto wengi huwa wanauwawa wakiwa bado wadogo na ni wachache ndio hufanikiwa kuwa wakubwa.
Watoto huwa chini ya uangalizi wa kina mama kwa muda wa miezi 6 – 8 na hapo madume hufukuzwa kwenye kundi huku watoto wa kike wakijiunga na kundi la kina mama. Kuro hufikia umri wa kuzaa afikishapo miaka mitatu na nusu. Mara tu baada ya mama kumuacha mtoto huchukua wiki 2 – 5 kisha hubeba mimba tena hivyo kufanya idadi ya wanyama hawa kuwa inaongezeka kwa kiwango kizuri kutokana na maeneo japo kwa uhalisia idadi ya wanyama hawa inapungua.
UHIFADHI
Ni jambo la kushukuru kuwa bado idadi ya wanyama hawa inaridhisha na hawajawekwa kwenye kundi la wanyama waliyomo hatarini kutoweka duniani. Shirika linalo simamia Uhifadhi wa Maumbile Asili Duniani (International Union for Conservation of Nature – IUCN) lina saidia sana kutujuza uelekeo wa wanyama mbalimbali katika maeneo ya hifadhi za wanyamapori na kutufanya kuwa makini zaidi kupambana na upungufu wa wanyamahusika.
MAADUI NA TISHIO KWA KURO
Maadui wakuu wa wanyama hawa ni Fisi, Simba na Chui. Japo kuna maadui wengine pia huonekana wakiwashambulia Kuro ambao ni Mamba, Mbwa mwitu na Duma.
Tishio kubwa kwa wanyama hawa ni shughuli za kibinaadamu hasa ufugaji lakini pia na ujangili.
Tukianza na ufugaji, watu wamekuwa wakiingiza mifugo yako kwenye maeneo ambayo wanyama hawa wanaishi na kujipatia chakula cha kutosha. Sasa kuingia kwa mifugo eneo hilo kunafanya upungufu wa chakula kwa Kuro na kusababisha wanyama hawa kuhama eneo hilo kasha kulazimika kutafuta maeneo mengine mbali zaidi. Hii huwafanya kukumbana na adha ya maadui na kuliwa kwa kiasi kikubwa sana wakati wana tafuta mazingira ya kuishi mapya.
Ujangili pia umekuwa ni tatizo kwa wanyama hawa kwani watu huwawinda kwa matumizi ya nyama lakini pia biashara haramu ya malighafi za wanyamapori mfano kwato, pembe na ngozi vinasababisha wanyama hawa kuwindwa sana.
Uharibifu wa mazingiza hasa ukataji miti, uchomajiwa misitu kwa ajili ya kuanzisha makazi na uharibifu wa vyanzo vua maji umepelekea wanyama hawa kuhama baadhi ya maeneo kwani wanyama hawa hupenda sehemu yenye maji ya kutosha, sasa kama maji yanakuwa ni changamoto katika eneo hilo wanyama hawa hulazimika kuhama.
NINI KIFANYIKE ILI KUWALINDA KURO HUSUSANI HAPA NCHINI TANZANIA
Takwimu zinaonyesha kuwa Kuro hapa nchini wanapatikana sana katika Hifadhi ya Taifa ya Tarangine, Mikumi na Pori la Akiba la Selous. Sasa tutumie njia hizi kuwanusuru wanyama hawa wasije toweka katika maeneo hayo hapa nchini.
Jamii za wafugaji ambazo zinaishi karibu na hifadhi za Taifa zitafutiwe maeneo maalaumu ya kufugia ili kuepusha uingizwaji wa mifugo kwenye hifadhi za wanyamapori. Kwani tumeona hii imekuwa ikisababisha upungufu wa chakula kwa wanyama hawa kutokana na majani mengi kuliwa na mifugo na kuwafanya wanyama hawa kukosa chakula cha kutosha hivyo kulazimika kuhama baadhi ya maeneo.
Kupambana na uvamizi wa maeneo Tegefu kwa uhifadhi wa wanyamapori hasa kutokana na uanzishwaji wa makazi kwasababu watu wamekuwa wakiharibu mazingira sana kwa ajili ya kutafuta makazi. Hii inasababisha usumbufu mkubwa sana kwa wanyama na kuwafanya kuishi kwa wasiwasi na hatimae kulazimika kuhama maeneo hayo.
Kuongeza kwa idadi ya Askari Wanyamapori kuishirikisha jamii katika masuala ya uhifadhi wa wanyamapori ili wawe mabalozi wazuri sana katika kufichua majangili walipo. Ukweli ni kwamba majangili wengi wamekuwa wakiishi katika makazi yetu na sisi kuwafichia siri. Kitu ambacho kinasababisha kuendelea kupungua kwa wanyamapori kwa asilimia kubwa sana.
Uanzishwaji wa mitaala ya elimu kuhusu wanyamapori na umuhimu wa wanyama hawa kwa Shule za Msingi kwani kwa kuwafundisha watoto masuala ya wanyamapori wakiwa bado wadogo itasaidia kupunguza tatizo la ujangili katika hifadhi za wanyamapori.
HITIMISHO
Ndugu msomaji wa makala hizi ukweli ni kwamba, wanyamapori wana mchango mkubwa sana hasa katika pato la Taifa letu chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Tuna kazi kubwa sana ya kuhakikisha tunawatunza wanyama hawa kwa ajili ya vizazi vijavyo ili kuendelea kuingiza fedha nyingi za kigeni kupitia wanyama hawa.
Kumekuwa na changamoto nyingi sana katika uhifadhi ambazo husababisha mpaka migogoro baina ya mashirika ya uhifadhi na jamii zinazo zunguka maeneo hayo. Nawapa pongezi sana TANAPA pamoja na TAWA hali kadhalika Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro kwa kazi kubwa sana wanayoifanya kunusuru rasilimali hizi adimu duniani.
AHSANTENI
Nakukumbusha kuwa mwisho wa makala hii ndio mwanzo wa makala nyingine, hivyo endelea kutega jicho na kujua katika makala ijayo tutamzungumzia mnyama gani.
Kwamengi na ushauri juu ya makala hizi wasiliana na mwandishi;
Sadick Omary
Simu= 0714 116963/0765057969/0785813286
Email= swideeq.so@gmail.com
Au tembelea= www.mtaalamu.net/wildlifetanzania
“I’M THE METALLIC LEGEND”