Habari msomaji wa mtandao wako wa wildlife Tanzania, karibu kwenye makala ya leo tujifunze jambo moja zuri ambalo tunaweza kuwafanyia watoto wetu kama zawadi. Hakuna kitu kizuri unachoweza kuwaahidi watoto wako kama utawaahidi kufanya kitu fulani, endapo watafanya vizuri au watatimiza kitu fulani unachotka wafanye. Kuna wale wazazi wanao waahidi watoto wao wasome kwa bidi wakifanya vizuri darasani watanunuliwa vitu vizuri na wanavyo vipenda watoto. Nakumbuka nilipokuwa mtoto baba aliwahi kuniambia nikifanya vizuri kwenye mitihani yangu ataninunulia baiskeli, nilijitahidi kusoma kwa bidiii sana na kwa nguvu zangu zote ili nipate zawadi ile ya baiskeli.

Kama wazazi na walezi wa watoto tunaweza kuwapa watoto ahadi nyingine nzuri zaidi sio lazima iwe kununua baiskeli, au nguo, na vitu vingine waahidi watoto wako endapo watafaulu na kufanya vizuri shuleni utawapeleka sehemu nzuri sana zenye vivutio na mvuto kwao, kama vile mbuga za wanyama, fukwe za bahari, sehemu za kihistoria na sehemu ambazo mtoto atajifunza na kufurahia maisha kwa upande mwingine. Mpe mtoto nafasi ya kutembelea na kuona sehemu nyingi ili awe na upeo mkubwa na ufahamu wake ujue mambo mapya na mazuri. Hii ndio zawadi pekee ambayo itamwacha mtoto wako na kumbukumbu isiyoisha kwenye akili yake, na pia ni kumbukumbu ambayo unamjengea na ataendelea kujifunza na kuifuatilia hata kama mzazi utaondoka hapa duniani bado utakuwa umepanda kitu kikubwa kwa watoto wako.

Ukimnunulia nguo atazisahau, ukimnunulia baiskeli ataisahau, ukimnunulia chakula au vitu vya kula atavisahau, lakini ukimpeleka sehemu tofauti, kwenye mazingira yanayovutia kama hifadhini au kwenye mbuga za wanyama hatosahau kamwe kwenye maisha yake, kwanza utakuwa umechora na kuandika kwenye ufahamu wake mambo mazuri na kumbukumbu nzuri ambayo hataisahau. Kwa njia hii utakuwa umemfungulia mtoto wako milango mingi ya ufahamu na kujifunza kutoka kwa viumbe hai wengine, unaweza usijue ndoto ya mtoto wako mpaka pale atakapoona vitu fulani kwenye maisha yake, au atakapoona mtu anafanya vitu fulani anavutika na kuwa na hamasa isiyoisha ya kufanya kama alivyoona.

Wazazi wahaidi watoto wako utawapeleka kutembelea hifadhi, wambie utawapeleka sehemu nyingine wakaone vitu vizuri. Badala ya kuamua kuwanunulia vitu kila mara, unaweza kuwaambia kuwa utawapeleka sehemu kwa ajili ya kufurahia na kujifunza, sehemu zenye utulivu na sehemu ambayo uaweza kuongea vizuri na watoto wako na familia yako kwa ujumla. Anza jambo hili kama ulikuwa huna utaratibu wa kufanya hivyo, jnpange na uone namna unavyoweza kuipa familia yako na watoto wako mambo mazuri yasiyofutika kwenye kumbu kumbu zao.

Hivi ndivyo tunavyoweza kubadili kizazi chetu na kukifanya kuwa na misingi mizuri ya kizalendo na kujali maliasili za nchi yetu, sisi ndio wahusika wakuu, tuijenge nchi yetu kwa kuhimiza  utalii wa ndani, na utalii wa ndani unaanza ndani ya familia zetu.

Ahsante sana

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 862 481/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania