Habari msomaji wa makala za wildlife Tanzania, karibu tuendelee na uchambuzi wa sheria ya wanyamapori Tanzania naamini unaendelea kupata maarifa mazuri na muhimu kwenye makala hizi za uchambuzi wa wanyamapori. Kwa makala iliyopita tulichambua hadi kufikia sehemu ya saba na kufikia kifungu (38) kifungu kidogo cha (11), naamini tulijifunza mambo mazuri na muhimu kwa sehemu zote za uchambuzi wa sheria hii. Leo tunaendelea na kifungu kidogo cha 12 ambapo tutachambua mwendelezo wa sheria ya uhifadhi wa wanyamapori. Karibu twende pamoja tujifunze. Lakini kwa mtiririko mzuri nitaanzia kifungu kidogo cha (11).

(11)  Waziri mwenye damana atahakikisha kwa kila namna au mfumo mzima unaotumika katika ugawaji wa vitalu vya uwindaji unakuwa  na uwazi na unaendana na misingi ya kanuni nzuri za utawala. Hapa anasisitiza kuwa mfumo wote wa upatikanaji wa vitalu vya uwindaji unatakiwa uendeshwe kwa uwazi na kwa kufuata misingi ya sheria hii. Hili ni jambo ambalo linatakiwa kueleweka kwa watu wengi na wanaohusika kwenye kitengo hiki.

(12) Licha ya mapendekezo yaliyotolewa katika kifungu hiki, waziri anaweza, kwa muda wowote kabla ya muda wa kuisha kwa kipindi au muhula wa uwindaji, kuzuia ugawaji wa vitalu vya uwindaji, pale ambapo kuna ushahidi wa kutosha kuwa muhusika amegawiwa kitalu cha uwindaji na pia-

(a) endapo ameshindwa kutimiza matakwa yoyote yaliyotakiwa na Waziri na kuyatilia manani;

(b)endapo ametoa taarifa za uongo katika kufanya maombi ya kitalu cha uwindaji;

(c ) ambaye amepatikana na makosa au hatia kwa mujibu wa sheria hii;

(d) ambaye ameshindwa kulipa ada muhimu au ana deni linalo muhusu kuhusiana na vitalu vya uwindaji;

(e) amepangisha au ametoa sehemu kitalu chake cha uwindaji kwa mtu mwingine.

(13) Hakuna maamuzi yoyote ya kusitisha ugawaji wa vitalu yatachukuliwa mpaka muhusika apewe nafasi ya kusikilizwa. Kwa hiyo katika kusitisha ugawaji wa vitalu vya uwindaji, maamuzi ya pande zote yanatakiwa kuchukuliwa kwa makini na kusikilizwa na pande zote, hapo ndipo kutakuwa na nafasi ya kufanya maamuzi sahihi.

(14) Mtu yeyote ambaye hataridhika na maamuzi ya Waziri anaweza kufanya moambi tena kwa utawala kuyapitia kwa waziri.

(15) Baada ya kupokea maombi ya utawala na kuyapitia, waziri atayawasilisha maombi hayo kwa Kamati ya Ushauri ya Ugawaji wa Vitalu kwa maoni  na maependekezo.

(16) Palea ambapo Waziri amekwisha kushauriwa na kwamba atafanya uamuzi ambao utakuwa ni wa mwisho lakini ikiwa muhusika hajakubaliana na maamuzi hayo ya Waziri anaweza kwenda kukata rufaa Mahakama Kuu.

(17) Ofisi ya wajumbe wamiliki, mikutano na njia nyingine za mambo ya Kamati ya Ushauri ya Ugawaji wa Vitalu vya Uwindaji inatakiwa kuwa sawa kama ilivyotokea kwenye Jedwali la Kwanza la Sheria hii.

(18) Licha ya mapendekezo yaliyotolewa na kifungu cha sehemu hii, mtu hatafikiriwa kugawiwa kitalu cha uwindaji, isipokuwa-

(a) ana ubia na kampuni ambayo imeandikishwa na uandikishwaji wa makampuni; na

(b) kampuni hiyo inanuia kujihusisha na uwindaji wa wanyama.

Waziri anaweza kusitisha utoaji wa leseni na vibali

Katika kipengele hiki kwenye sheria hii tutaangalia majukumu ya waziri mwenye dhamana kusitisha vibali na leseni ya uwindaji kama tutakavyoona kuanzia kifungu cha cha 39.

39.-(1) Waziri anaweza, baada ya kutoa taarifa kwenye Gazeti la Serikali, kumtangaza mtu yeyote au aina yoyote ya mtu ambaye mwanzo alihusika,  kuwa na hatia kwa mujibu wa sheria au sheria nyingine zinazohusiana kwenye mamlaka husika ya kisheria  hatapewa lesseni yoyote ya uwindaji kuhusiana na mnyama yoyote ambaye ametajwa kwenye kanuni.

(2) Pale ambapo maelekezo yatakapokuwa yametolewa kwenye kifungu kidogo cha (1) kuhusiana na mtu yeyote, mtu ambaye hatakuwepo kwenye aina hiyo hataruhusiwa kuomba au kupata lesseni ya uwindaji kulingana na mnyama yoyote ambaye anaelezwa kwa mujibu wa sehemu hii ya sheria na lesseni yoyote itakayotolewa kwa mtu huyo itakuwa batili.

(3) Waziri anaweza kutengeneza kanuni zinazoelezea ubia/hisa unatakiwa kumilikiwa na mzawa katika kampuni yoyote ya uwindaji, idadi ya vitalu vya uwindaji vinavyotakiwa kumilikiwa na kampuni, aina, kiasi/ukubwa na thamani ya vitalu vya uwindaji iwapo-

(a) hisa zinazomilikiwa na wazawa hazitakuwa chini ya asilimia ishirini na tano ya hisa zilizochangwa;

(b) asilimia ya umiliki wa kampuni za wageni ugawaji wa vitalu vya uwindaji unatakiwa usizidi asilimia kumi na tano ya jumla ya kampuni ya uwindaji katika muda wowote.

(4) Waziri atatengeneza kanuni kuamuru ada na jinsi ya kuhamisha kwa mtu mwingine umiliki wa kitalu cha uwindaji.

(5) Kila kampuni ya uwindaji ili waweze kulipia gharama za uendeshaji, watatakiwa kufungua akaunti benki ndani ya Jamhuri ya Muungano ambayo watakuwa wanaweka kila siku kiasi cha chini Dola za Kimarekani 800 kwa kila siku watakayopanga kwenda kuwinda.

(6) Waziri anaweza, kila baada ya muda au mara kwa mara, kuamuru kiasi cha ada kinachotakiwa kulipwa na kampuni za uwindaji sawa na kifungu kidogo cha (5). Kwa hiyo hapa waziri atawajibika kuwakumbusha kwa mujibu wa sheria hii wadau wote wanaojihusisha na uwindaji kuhusu ulipaji wa ada kama ilivyotokea kwenye sheria hii.

  1. Isipokuwa vinginevyo kama ilivyoelezwa kwenye sheria hii, mtu hatawinda mnyama yeyote ambaye ametajwa au kuwekwa kwenye jedwali isipokuwa kulingana na masharti ya lesseni ya uwindaji yaliyotolewa kwa muhusika huyo.
  2. Waziri anaweza, baada ya kutoa taarifa kwenye Gazeti la serikali, kubadili, kuongeza, kutofautisha au kuweka Jedwali jingine kwenye sheria hii.
  3. Mtu yeyote atakayemjeruhi mnyama atawajibika atatumia kila liwezekanalo kumua mnyama huyo katika hatua za mwanzoni kabisa.

Masharti ya Jumla kuhusiana na Lesseni ya Uwindaji

Katika kifungu hiki sheria inaelezea masharti mbali mbali ambayo yatakuwa yanatoa maelekezo namna ya kufanya uwindaji na kuendesha shughuli za uwindaji kwenye maeneo husika kama inavyoelezwa kwa mujibu wa sheria hii.

  1. (1) Leseni ya uwindaji inaweza kutolewa na ofisa wa utoaji wa lesseni kwa maombi yaliyofanywa kimaandishi ambayo imeelezwa kwenye fomu na malipo ya mwombaji pamoja na ada iliyotakiwa.

(2) Lesseni ya uwindaji haitatolewa kwa mwombaji ambaye ameshindwa kumridhisha ofisa wa lesseni-

(a) kwamba amefikisha umri wa miaka kumi na nane;

(b)kwamba anamiliki lesseni ya bunduki halali ambayo ni kwa ajili ya kutumiwa kwenye uwindaji;

(c ) kwa kesi ya kuwinda wanyama waliotajwa,kwamba yeye ni raia wa Tanzanaia au amekuwa makazi wa kawaida wa Tanzania kwa kipindi kisichopungua miezi kumi na mbili mara moja ikifuatiwa na tarehe ya kufanya maombi.

(d) kwamba ana ufahamu wa kutosha wa kutumia bunduki kwa kusudi la kuwinda wanyama kama alivyoshauri na Mkurugenzi.

(e ) kwamba hatakiwi kuwa alishakwisha kuwa na makosa na hatia au sawa na sheria zilizotungwa kwa uhifadhi na usimamizi wa wanyamapori Tanzania au mamlaka yoyote ile na;

(f) kwamba ana ufahamu wa kutosha kuhusu sheria na kanuni sawa na uwindaji,  kama itakavyoamuriwa na Mkurugenzi.

(3) Mamlaka ya lesseni inamtaka mwombaji wa lesseni ya uwindaji kutokea mbele na kujibu maswali au kutoa taarifa inayohusiana na mambo yoyote sawa na kifungu kidogo cha sheria (2) na bunduki inayopendekezwa kutumiwa.

Kwa kufikia hapa naamini umepata mwanga wa kukusaidia katika kuijua sheria hii ya wanyamapori hasa kipengele hiki cha uwindaji na utoaji wa vitalu. Kuna mambo mengi sana tunatakiwa kuyafahamu katka sheria hii ya wanyamapori. Hivyo ni jukumu letu kuchukua muda na kujifunza mambo haya muhimu.

Mwisho, nakukaribisha kwenye mwendelezo wa makala nyingine hapa hapa kwenye mtandao wako wa wildlife Tanzania. Karibu tuendelee kujifunza na kupata maarifa mbali mbali kwa ajili ya uhifadhi wa wanyamapori na viumbe hai wengine.

Ahsante sana!

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 248 681/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania