Kwa miongo kadhaa iliyopita masula ya kutembelea hifadhi za wanyama na vivutio vingine kwa watanzania hayakuwa kipaumbele kwa maisha ya watanzania wengi. Hii ilisababishwa na mambo mengi sana ambayo yalipelekea watu kuchelewa kuzitumia fursa za kutembelea hifadhi za wanyama na vivutio vilivyo ndani ya nchi hii. Lakini kwa kadri siku zinavyokwenda mambo yanabadilika na watu wanachukua hatua kwa sababu ya uwepo wa teknologia na njia nyingine za kufanya watu wafahamu zaidi kuhusu vivutio vya nchi yao.
Tafiti zinaonyesha idadi ya watanzania wanaotembelea vivutio vya utalii imeongezeka, na inaendelea kuongezeka kwa kadri siku zinavyokwenda. Na hili ni jambo zuri sana kwenye maendeleo ya nchi yetu na ukuaji wa utalii wa ndani. Kwa miaka ya nyuma watanzania wengi hawakuweza kutembelea hifadhi za wanyamapori au maeneo mengine yenye vivutio vya utalii kutokana na kutoelewa na kufahamu vizuri mambo hayo, na pia mtazamo wa watanzania wengi kwenye sekta hii ulikuwa kwa kiasi kikubwa ni kufikiri sehemu hizi za vivutio ni kwa ajili ya wazungu tu na wegeni wengine kutoka nje ya nchi.
Kuna nafasi ya Tanzania kuendelea kufanya vizuri zaidi kwenye utalii wa ndani kwa sababu ya juhudi kubwa zinazofanywa kwenye sekta hii na serikali na wadau wengine wa maliasili na utalii. Ingawa kuna changamoto kwenye baadhi ya sehemu muhimu za vivutio vya kitalii lakini naamini zitashughulikiwa mara moja na itakuwa ni jambo rahisi sana kwa watanzania kujipanga kutembelea hifadhi na vivutio mbali mbali vya utalii.
Kuna sababu nyingi ambazo zinasababisha Tanzania iendelee kufanya vizuri kwenye sekta ya utalii na hapa nasisitiza watanzania kuchukua hatua na kukuza utalii wa ndani. Utalii wa ndani maana yake watanzania waliopo hapa hapa Tanzania ndio wanakuwa watalii kwenye vivutio na rasilimali za nchi yao, na hii ndio njia bora kabisa ya kufanya utalii wa nje kuongezeka na kukua kwa kasi. Lakini utalii wa ndani ukisua sua na utalii wa nje utasua sua pia, hivyo tukiweka mipango mizuri na mikakati mizuri ya kuinua utalii wa ndani, itakuwa ni kazi rahisi kufikia na kupata wageni wengi kwenye utalii wa nje. Sababu kubwa ya kufanya utalii na sekta ya utalii kufanya vizuri zama hizi ni baadhi ya mambo ya msingi sana kama ifuatavyo.
Njia rahisi ya kupokea na kupata taarifa kutoka sehemu yoyote uliyopo, kwa sasa katika zama hizi ni rahisi kutuma taarifa kwenda sehemu yoyote ile duniani. Ukuaji wa teknolojia ya mawasiliano, simu, na hata vyombo vya kisasa vya habari kama radio, television na mitandao ya kijamii imerahisisha sana upatikanaji wa taarifa. Hii ni fursa nzuri sana tunaweza kuitumia kama taifa kukuza na kuinua utalii wetu wa ndani, kwa kutangaza na kuonyesha maonyesho ya aina mbali mbali yenye kulenga kukuza na kuhamasisha watanzania kutembelea vivutio vya utalii kwenye nchi yao. Njia hii moja pekee inawea kuleta mabadiliko makubwa kwenye sekta hii ya utalii.
Hivi sasa karibu kila mtanzania anamiliki simu, na simu ndio imekuwa kichocheo kizuri sana cha kusambaa kwa taarifa, kumekuwa na simu janja (smartphone) hizi ni simu zenye uwezo mkubwa wa kupata na kutuma taarifa yoyote ya maandishi, ya sauti au hata ya video. Simu hizi ni chachu nzuri sana kwa ukuaji wa utalii wa ndani. Hii ni fursa nzuri kwenye ukuaji wa utalii wetu wa ndani. Kwani mtu mwenye simu hii anaweza kusoma au kuona tangazo lolote lililowekwe kwenye mitandao ya jijamii. Hapo bado sijataja maonyesho, vitabu, magezeti, mabango makubwa na njia nyingine nyingi husaidia sana kwenye ukuaji wa utalii.
Kwa maoni, maswali na ushauri wasiliana nami kwa mawasiliano yaliyopo hapa chini mwisho wa makala hii.
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 862 481/+255 742 092 569
www.mtaalamu.net/wildlifetanzania