Alternatively effective: a conference on substitutes to bear bile in traditional Chinese medicine in Malaysia

Matumizi ya sehemu za miili na viungo vya wanyamapori kwa ajili ya dawa za asili limekuwa ni jambo la muda mrefu kwenye nchi za Asia hasa China, wanyamapori mbali mbali wanahusishwa na matumizi ya dawa za asili kwa ajili ya kutibu magojwa mbali mbali kwenye mwili wa binadamu. Tulizoea kusikia meno ya tembo na pembe za faru kutumika kama dawa za asili kutibu magonjwa mbali mbali, na sasa mnyama mwingine ameingia kwenye orodha ya wanyamapori muhimu ambao wanauliwa kila kukicha kwa ajili ya matumizi ya dawa za asili.

Sun Bear, Helarctus malayanus, ni mnyama anayewindwa kikatili katika nchi ya Malasia kwa sababu ya umuhimu wake kutibu baadhi ya magonjwa yanayowasumbua watu. Katika makala iliyoandikwa na Latita Gomez, katika jarida la Traffic bulletin lililotoka mapema Oktoba mwaka 2017 inaelezea kwa kina jinsi ambavyo wanyamapori hawa wanakabiliwa na hali mbaya ya baadaye kutokana na ujangili uliokithiri dhidi ya wanyamapori hawa, sababu kuu ya wanyama hawa kuuwawa ni Imani waliyonayo kwamba “nyongo” (bile) yake ni moja ya dawa muhimu za asili kutibu maradhi. Viungo na sehemu za miili ya wanyama hawa inaripotiwa na jarida hili kuonekana zikitumika sehemu mbali mbali za Asia.

Katika uchunguzi uliofanywa na jarida la Traffic mwaka 2012 nchini Malasia unaonyesha kabisa 48% ya biashara ya nyongo ya sun bear inayoendelea kufanyika katika maduka ya kuuza dawa za asili nchini China, wanafanya biashara hiyo kwa uwazi na bila wasiwasi wowote kwa sababu ni kama vile imehalalishwa kuuzwa. Wachambuzi wa maswala haya wanaendelea kusema kuwa kiasi cha 60% ya viungo vya wanyama hawa hupatikana kutoka sehemu za chini kabisa ambazo ndio kwenye maeneo au makazi ya wanyama hawa, jambo ambalo linahatarisha idadi yao kwenye hifadhi zao. Pia inaonyesha kwa taarifa za mwaka 2010 hadi 2011, katika nchi 17 ambazo zilifanyiwa utafiti na Traffic, nchi ya Malasia ndio inaonekana kinara wa ujangili wa wanyamapori hawa.

Licha ya ukali wa sheria ya uhifadhi wa wanyamapori hawa, na pia katika nchi ya Malasia bado kuna idadi kubwa ya wanyama hawa wanauwawa, inakadiriwa kuwa kwa takwimu za mwaka 2015 hadi machi 2017 taarifa za jarida hili zinaonyesha sun bear 10 walikuwa wanauwawa. Kutokana na tamaa ya fedha na Imani dhidi ya matumizi ya dawa za asili imepelekea uwindaji kuzidi kushika kasi katika nchi ya Malasia, matumizi mbali mbali ya silaha kama vile mitego ya waya, bunduki na mikuki inatumika kuwawinda wanyamapori hawa kwa sababu hutumika kama dawa za asili.

Kutokana na hali hiyo inayowakabili wanyamapori hawa, nchi ya Malasia iliamua kuchukua hatua za dharura na kuitisha mkutano na wadau wote wanaohusika na masuala ya dawa za kifamasia na dawa za asili kutoka sehemu mbali mbali duniani ambako wanyamapori hawa huwindwa kwa matumizi ya dawa za asili, ili kwa pamoja waje na mkakati mzuri ambao utapunguza mauaji ya sun bear kwa ajili ya dawa za kienyeji au dawa za aili. Jambo ambalo walilifanya mapema na kuandaa kongamano waliloliita “Alternative Effective”, namna nyingine bora zaidi ya kubadili matumizi ya nyongo na viungo vya sun bear kutibu maradhi ambayo ndio sababu ya ujangili wa sun bear.

Hakika, naamini kwa machache kati ya mengi yaliyopo kwenye makala hii umepata mwanga wa namna hali ya mambo inavyokwenda kwenye masuala ya uhifadhi wa wanyamapori katika nchi za wenzetu. Hii ni ishara tosha kwetu kufahamu kama hatua za makusudi hazitachuuliwa basi tutapoteza wanyamapori wetu walio wa thamani kwa ajili ya tamaa za watu wachache.

Wanyamapori sasa wana matumizi mengi kwenye nchi za wenzetu, matumizi ambayo ni kinyume na asili kabisa, hivyo basi mambo yanayoendelea katika nchi za wenzetu yatufanye tufikiri na kujua jambo kama hilo linaweza kutokea kwa wanyamapori na maliasili zetu, inaweza isiwe tena tembo na faru, lakini inaweza ikaenda kwenye wanyamapori wengine ambao uwepo wao porini ni muhimu kwenye ikolojia na mfumo mzima wa maisha ya viumbe hai hapa duniani.

Nakushukuru sana Rafiki kwa kusoma makala hii hadi mwisho, naamini umepata mwanga kwenye masuala haya ya uhifadhi wa maliasili zetu. Karibu tuendelee kujifunza zaidi kwenye makala ijayo hapa hapa kwenye mtandao wako wa Wildlife Tanzania. Pia usiache kuwashirikisha wengingi haya uliyojifunza hapa.

Hillary Mrosso

+255 683 862 481

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtalaam.net/wildlifetanzania