Ni matumaini yangu umzima wa afya ndugu msomaji wa makala hizi za wanyamapori na mazingira yao kwa ujumla. Pole na pongezi kubwa sana kwa utekelezaji wa majukumu ya kila siku na ujenzi wa taifa huku tukiendelea kulinda amani ya taifa letu kwani ndo misingi imara na inayohitajika kwenye kila taifa. Basi kama ilivo kawaida leo tena tutaingia darasani kujifunza mambo machache na yenye thamani kubwa sana kwenye maliasili zetu hususani wanyamapori tuliyo jaaliwa kuwanao hapa nchini katika hifadhi zetu za taifa na baadhi ya maeneo mengine ya hifadhi za wanyamapori.
Katika mfululizo wa Makala za hivi karibuni nimekuwa nikizungumzia sana wanyama jamii ya swala kwani kundi hili lina wanyama wengi sana. Makala hii pia itajikita katika kumzungumzia swala mwingine na mfululizo huu utaendelea mpaka pale tutakapo maliza wanyama jamii ya swala. Ni wazi kwamba tulio wengi hatuwafahamu wanyama hawa kitu ambacho mtu akikutana na mnyama jamii ya swala na ukamwambia kuwa huyu ni swala basi atakataa kabisa kwasababu yeye anamjua swala ni swala paa pekeyake.
Basi nikusihi kuwa nami mwanzo hadi mwisho wa makala hii kumjua mnyama ajulikanae kama “KORONGO” ambae kwa lugha ya kingereza anaitwa “Roan antelope”. Jina hili la korongo linatumika pande mbili kwa ndege na mamalia. Kama ni msomaji wa makala hizi nadhani utakuwa sio mgeni wa jina hili kwa upande wa ndege kwani tayari nimesha muelezea ndege aitwae korongo katika mfululizo wa makala hizi. Bonyeza hapa; Jifunze Kuhusu Korongo-Taji Kijivu Kwenye Makala Hii
UTANGULIZI
Korongo ni miongoni mwa wayama jamii ya swala ambao wanapatikana bara la Afrika tu na si kwingine kokote duniani. Hapa nchini Tanzania wanyama hawa wanapatikana kwa wingi kwenye hifadhi zetu za taifa hususani Hifadhi ya Taifa ya Katavi na maeneo ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na maeneo ya Rungwe. Ni wanyama ambao huishi kwa makundi na maranyingi huwa hawana makazi maalumu hivyo huishi kwa kuhama hama kutokana na mahitaji ya chakula na mahitaji mengine ya kiikolojia.
Katika mazingira wanayoishi wanyama hawa wanakumbana na chagamoto na matishio mbalimbali kitu ambacho kina hatarisha uwepo wa wanyama hawa katika maeneo ya hifadhi za wanyamapori. Kupitia makala hii utajifunza mambo mengi sana kuhusu mnyama huyu kama sifa na tabia zake, kuzaliana, uzito, kimo na urefu bila kusahau kuzaliana na uhifadhi wa wanyama hawa.
SIFA NA TABIA ZA KORONGO
Ukiwachunguza vizuri wanyama hawa wana fanana sana na farasi na hata pia baadhi ya sifa za kupigana na nyinginezo wanyama hawa wana shabihiana na farasi kwa kiasi kikubwa sana.
Wana manyoa mengi ambayo yamesimama na yameanzia sehemu ya katikati ya masikio mpaka karibu na sehemu ya juu ya mabega.
Wote madume na majike wana pembe nene, nzito na zenye miduara na zimepinda kuelekea upande wa nyuma ya kichwa ambapo pembe hizi huweza kurefuka na kufikia urefu wa hadi mita moja.
Usoni wana mpangilio wa rangi nyeusi na nyeupe hasa ukiwaangalia sehemu za juu ya macho utaona kuna kama alama ya mstari mweupi uliokaa sambamba na jicho na kushuka hadi maeneo ya puani.
Ni warefu wenye nguvu na mashingo manene mfano wa farasi.
Wana masikio marefu, membamba na yaliyo chongoka huku yakiwa na manyoa mengi.
Rangi ya miili ya wanyama hawa huwa ipo tofauti tofauti kutokana na mazingira wanayoishi. Japo mara nyingi huwa na rangi ya kijivu au wekundu na manyoa ya dume huwa yamekolea rangi zaidi hasa sehemu za nchani mwa manyoa. Sehemu ya chini wanyama hawa wana rangi nyeupe.
Wanyama hawa huishi kwa makundi, kundi moja huwa na wanyama 5 hadi 35 lenye kujumuisha kina mama, watoto na dume mmoja ambae ni mtawala wa kundi ili kuzuia madume wengine wasiingie ndani ya himaya yake.
Wanyama hawa huwa hawana makazi ya sehemu moja, hali hii humfanya dume mtawala wa kundi la majike na watoto kuwafukuza madume wengine umbali zaidi ya mita 500 kutoka katika himaya yake kwani majike na watoto huwa wanatembea eneo kubwa kwa ajili ya chakula na mahitaji mengine ya kiikolojia.
Korongo ni wanyama ambao wanafanya shughuli zao na kuwa mahiri kipindi cha asubuhi, mchana na mida ya jioni wakati jua linazama.
Korongo ni wanyama ambao hawana wasiwasi wala uoga sana hasa katika maeneo wanayoishi. Wanapohisi kuna hatari hukimbia umbali mdogo kisha wanasimama na kuhakikisha au kutaka kujua kuna hatari gani inayo wakabili.
Mbali na kutokuwa na wasiwasi na kumbia umbali mfupi wanapohisi kuna hatari, wanyama hawa ni miongoni mwa wanyama wenye uwezo mkubwa sana wa kukimbia. Wana uwezo wa kukimbia hadi kilometa 54 kwa saa hasa pale wanakuwa wanafukuzwa na maadui zao. Anapozidiwa huamua kujitetea.
Wanapozidiwa huamua kujitetea kwa kupigana. Hutumia pembe kujihami na inasemekana pembe zake zikimpata adui vizuri basi huweza kusababisha kifo kwa adui huyo.
Hupendelea kuishi mazingira ambayo sio mbali sana na vyanzo vya maji. Inakadiriwa kwamba wakienda mbali zaidi basi huwa haizidi kilometa 4 kutoka sehemu ya vyanzo vya maji.
Ni marachache sana kukuta makundi mawili tofauti ndani ya himaya moja na hii ni kutokana na tabia ya madume kufukuza wenzao zaidi ya mita 500 kutoka kwenye himaya zao.
KIMO, UREFU NA UZITO WA KORONGO
Kimo= wanyama hawa huwa na kimo kati ya futi 4.6 hadi 5.3
Urefu=kuanzia kichwani hadi mwisho wa kiwiliwili korongo huwa na urefu wa futi 7.3 hadi 8.8 huku mkia ukiwa na urefu wa futi 2 hadi 2.3.
Uzito=huwa kuna tofauti kidogo kati ya uzito wa dume na jike, dume huwa mzito kidogo kuliko jike ambapo huwa na uzito kati ya kilogramu 242-300 huku jike akiwa na wastani wa uzito wa kilogramu 232-280.
MAZINGIRA NA CHAKULA
Wanyama hawa wanapendelea sana mazingira ambayo yapo wazi na yenye majani majani marefu na ya kimo cha kati hasa maeneo yaliyo karibu na maji. Mara nyingi korongo huepuka sehemu zenye majani mafupi na zennye mlundikano wa wanyama wengine walao majani pamoja na sehemu zenye maadui wengi.
Hawa ni miongoni mwa wanyama walao majani na hupendelea sana kula mimea midogo midogo hasa ile ya jamii ya michongoma. Hunywa maji mara kwa mara nah ii ndio sababu ya wanyama hawa kupendelea kuishi karibu na vyanzo vya maji.
KUZALIANA
Wanyama hawa huwa hawana kipindi maalumu cha kuzaliana kama ilivyo kwa baadhi ya jamii za swala nyingine. Mara tu baada ya kupandana jike hubeba mimba kwa muda wa siku 268-280. Muda wa kuzaa unapo karibia jike hujitenga na kundi kisha hutafuta sehemu salama kwa ajili ya kwenda kuzaa na huzaa mtoto mmoja tu. Mama hurudi kundini baada ya wiki moja wakati huo humuacha mtoto akiwa katika eneo la maficho kwani bado huwa hawezi kuongozana na wenzie ndani ya kundi na hujitahidi kurudi kwa ajili ya kumnyonyesha mtoto hasa majira ya asubuhi na mchana.
Baada ya takribani wiki tano mama hurudi kwenye kundi rasmi na mtoto kisha kwa wakati huu kwasababu mtoto anakuwa amesha changamka basi hujiunga na kundi la watoto wenzie kwa michezo mbalimbali japo bado huwa yupo chini ya uangalizi wa mama.
Watoto wa kike huweza kuanza kuzaa mara tu wafikishapo miaka miwili huku wakiume ni hadi kuanzia miaka mitatu. Wanapo fikisha umri wa miaka miwili na nusu, watoto wa kiume hufukuzwa ndani ya kundi na dume mtawala kisha hujikusanya na kwenda kuanzisha kundi lao wenyewe huku watoto wa kike wakibaki ndani ya kundi la kina mama.
Japo mtoto huwa chini ya uangalizi wa mama kwa zaidi ya miezi miwili na kuendelea, korongo jike huweza kubeba mimba mara baada ya wiki tatu tu baada ya kujifungua. Hali hii huwafanya korongo hasa majike kuwa na uwezo wa kuzaa kila baada ya miezi kumi au miezi kumi na nusu. Kwa haraka haraka hili pia linapelekea wanyama hawa kuweza kuzaliana haraka haraka za kuwa na idadi kubwa endapo changamoto kama ujangili hazita wakumba sana.
Korongo ni wanyama ambao wanakadiriwa kuwa na uwezo wa kuishi hadi myaka 17 katika umri wote wa maisha yao hasa wawapo katika mazingira asili.
UHIFADHI
Ndugu msomaji hii huwa ni sehemu muhimu sana hasa tunapozungumzia umuhimu wa Makala hizi basi sehemu ya uhifadhi ndo imebeba dhana kubwa ya makala hizi za wanyamapori. Kwani kupitia kipengele hiki ndipo mtu utajifunza na kutambua ni kwanini tunatakiwa kuwatunza wanyama hawa. Hivyo basi nakusihi kukisoma kipengele hiki kwa umakini zaidi japo ni kifupi ila kina maana kubwa sana.
Kutokana na takwimu zilizo tolewa na shirika la umoja wa mataifa linaloshughulika na uhifadhi wa maumbile asili (International Union for Conservation of Nature-IUCN) za mwaka 2017, zinaonesha kuwa idadi ya wanyama hawa inapungua siku hadi siku. Kuna baadhi ya nchi kama Gambia wanyama hawa tayari wamesha toweka kabisa huku nchini Swaziland wanyama hawa pia walikuwa wametoweka kabisa na sasa wamefaywa kurudishwa kutoka nchi nyingine ili waweze kuzaliana tena. Nchi kama Burundi na Eritrea wanyama hawa wamesha toweka kwenye baadhi ya maeneo.
Takwimu hizo za IUCN zinaonesha kuwa idadi ya wanyama hawa kwa bara zima la Afrika inakadiriwa kuwa ka Korongo 76,000 huku nchi ambazo zinaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wanyama hawa zikiwa ni Burkina faso(>7,370), Kameruni(>6,070), Zambia(>5,080) na Tanzania(>4,310).
Kwa tafiti zilizo fanyika hapa Tanzania mwaka 2014 kwa Wanyama hawa, baadhi ya maeneo ambayo wanyama hawa wanapatikana kwa kuridhisha ni mazingira ya Ruaha-Rungwe yenye idadi ya korongo wapatao 1,000-1,500, Pori la akiba la Ugalla na Moyowosi na maeneo ya ziwa Sagara zenye idadi ya korongo 1,200 huku Hifadhi ya Taifa ya Katavi ikiwa na idadi ya korongo wapatao 450.
Katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti wanyama hawa wamekuwa wakionekana kwa kubahatisha sana tofauti na ilivokuwa hapo zamani. Hii imetokana na changamoto mbalimbali ambazo tutaziona katika kipengele kinacho fuata.
Japo bado Wanyama hawa hawajawekwa katika kundi la wanyama walio hatarini kutoweka duniani, ila kama pasipokuwa na usimamizi mzuri wa uhifadhi wa wanyama hawa basi itafika kipindi wataingizwa katika kundi hilo. Kwani ni wazi kabisa tumeona nchi kama Gambia wanyama hawa hawapo tena na Swaziland walitoweka kwa sasa wamefanywa kurudishwa tena kutoka nchi nyingine ili waweze kuzaliana tena.
CHANGAMOTO NA TISHIO KWA KORONGO
Katika mazingira asilia ya wanyama hawa kuna maadui ambao kwa hakika ni lazima wawepo ili kuweka usawa wa kimazingira kutokana na idadi ya wanyama hawa. Kwa lugha ya kiingereza wanasema “ECOSYSTEM BALANCE”. Maadui hawa asilia wa korongo ni simba, chui, fisi na mbwa mwitu.
Kutokana na takwimu na tafiti mbalimbali, tishio na changamoto kubwa kwa wanyama hawa ni ujangili na uharibifu wa mazingira.
Ujangili ni tatizo kubwa sana kwenye rasilimali hizi za wanyamapori. Wanyama hawa wamekuwa wakiwindwa kwa kiwango kikubwa sana tena bila vibali kitu ambacho kinasababisha idadi yao kupungua sana katika hifadhi zetu za taifa. Hebu chukulia mfano wa Hifadhi ya Taifa ya Katavi pamoja na kuwa na eneo kubwa lakini wanyama hawa wanakadiriwa kuwa 450 kutokana na sensa ya mwaka 2014. Hali ni mbaya zaidi katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambayo ni hifadhi maarufu zaidi duniani na urithi wa dunia lakini kwasasa wanyama hawa wamekuwa wakionekana kwa nadra sana katika hifadhi hii. Ujangili unatishia sana uwepo wa wanyama hawa hapa nchini na kwingineko barani Afrika kitu ambacho tusipokuwa makini katika kupambana na kutokomeza ujangili kitatufikisha sehemu ya kukumbuka kama historia kwamba tulikuwa na wanyamahawa lakini kwa sasa hawapo tena.
Uharibifu wa mazingira pia ni miongoni mwa changamoto zinazo wakumba wanyama hawa kwa kiasi kikubwa sana. Hapo juu nimeeleza kidogo kwenye kipengele cha sifa na tabia za wanyama hawa kuwa miongoni mwa sifa za wanyama hawa hawapendi maeneo yenye maadui wengi na wanyama wengine walao majani hasa kutokana na upungufu wa chakula utakao jitokeza. Hivyo shughuli za kibinaadamu hasa ukataji miti na uchomaji nyasi kwa ajili ya makazi au kupanua mashamba hali kadhalika uanzishwaji wa makazi bila mpangilio ni tatizo kubwa sana kwa wanyama hawa kwani wanakosa mahitaji muhimu sana ya kiikolojia kitu ambacho kina sababisha wanyama hawa kuhama baadhi ya maeneo. Kama hali hii itazidi basi wanyama hawa watakosa kabisa sehemu ya kukimbilia na hatimae watazidi kupungua na mwisho kutoweka kabisa hapa nchini.
Kuna tatizo lingine ambalo tunaweza kuliangalia kwa jicho la tatu kama uingizwaji wa mifugo katika maeneo ya hifadhi za wanyamapori. Hali hii imekuwa ni changamoto kubwa sana kwa miaka ya hivi karibuni kwasababu wanyamapori wamekuwa wakikosa chakula cha kutosha kutokana na kugombania chakula na mifugo. Idadi ya mifugo imekuwa ikiongezeka sana katika maeneo ya hifadhi za wanyamapori na hasa kutokana na ukweli kwamba jamii za wafugaji hukimbilia maeneo haya kwa ajili ya malisho ya mifugo yao huku wakiacha maeneo mengi sana yenye nyasi na chakula cha kutosha kwa ajili ya mifugo yao.
SULUHISHO KWA CHANGAMOTO HIZI DHIDI YA KORONGO
Nikianza na suala la ujangili, serikali kupitia wizara husika ambayo ni wizara ya maliasili na utalii ijitahidi kuongeza idadi ya askari waaminifu ili kuongeza ufanisi wa doria za kila mara katika maeneo ya hifadhi za wanyamapori. Kwa kufanya hivyo itasaidia kwa kiasi kikubwa sana kupunguza vitendo vya ujangili kwa wanyama hawa ambao ni muhimu hasa kwa kuliingizia taifa fedha za kigeni kutokana na shughuli za kitalii.
Sambamba na kuongeza idadi ya askari wa wanyamapori, ni lazima kupambana zaidi na biashara haramu ya rasilimali ya wanyamapori kwani biashara hii ndio chanzo kikubwa cha kuwepo kwa ujangili katika maeneo ya hifadhi zetu za wanyamapori. Ufuatiliaji mzuri wa wauzaji na wanunuzi wa malighafi za wanyamapori utasaidia kwa kiasi kikubwa sana kutokomeza suala la ujangili hapa nchini.
Ushirikishwaji wa jamii katika uhifadhi wa wanyamapori ni jambo muhimu sana kwani jamii hizi zinaweza kutupatia mabalozi wazuri sana hasa watakao tusaidia kufichua majangili wa wanyamapori ni kina nani na wanaishi sehemu gani. Ni dhahiri kwamba majangili tunaishi nao kwnye jamii zetu hivyo watu wanashindwa kuwataja kutokana na kukosa hamasa au motisha kutoka kwenye mamlaka husika.
Nikirudi upande wa tatizo la uharibifu wa mazingira hapa ni lazima kuwepo na usimamizi wa sheria na sera za makazi kwasababu watu wamekuwa wakivamia maeneo bila vibali na kuanzisha makazi bila kujali mamlaka ya eneo husika. Wizara ya makazi kwa kusaidiana na wizara ya maliasili na utalii kupitia mamlaka mbalimbali za usimamizi wa wanyamapori kwapamoja wasaidiane kupunguza wimbi hilila uhamiaji na uharibifu wa mazingira ili kunusuru wanyama hawa ambao idadi yao inapungua siku hadi siku.
Yapo maeneo mengi sana ambayo ni mazuri kwa kilimo, makazi na hata ufugaji hivyo watu waelekezwe katika maeneo haya ili kupunguza tatizo pia la migogoro baina ya watu na wanyamapori kwani mtu anapolima karibu na eneoe au ndani ya eneo la wanyamapori na mazao yake yakaharibiwa basi ni lazima ataweka chuki na mamlaka husika lakini pia na wanyama wenyewe. Hali ambayo itasababisha kuuwawa kwa wanyama hawa lakini pia hata kuongezeka kwa tatizo la ujangili kwa wanyamapori.
HITIMISHO
Japo inonekana wanyama hawa wana uwezo wa kuzaliana kwa kasi kubwa lakini tatizo la ujangili limekuwa lisababisha wanyama hawa kupungua sana. Kwa pamoja kama wazalendo tunahitaji kupambana na kuzisaidia mamlaka husika katika kazi kubwa sana hii ya uhifadhi wa wanyama hawa. Tusingoje watu kutoka nje ndio waje kutusaidia kuwatunza wanyama hawa kwani mwisho wa siku wao watafaidika na sisi tutabaki kuwa ni watumwa tu kwenye rasilimali zetu.
Nawapongeza sana TANAPA, TAWA, na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro kwa kazi kubwa sana wanayoifanya ya usimamizi na uhifadhi wa wanyamapori kwani ni jukumu kubwa sana na hatimae mpaka leo bado tunawaona wanyama hawa katika baadhi ya hifadhi zetu za taifa. Pongezi pia kwa waziri wa maliasili na utalii Dkt. Kingwangalla kwa mwanzo mzuri na weledi mkubwa sana anao uonyesha katika suala zima la kusimamia maliasili hususani wanyamapori hasa kwa kuendeleza hamasa ya kuongeza idadi ya askari na kuanzisha mafunzo kwa baadhi ya maeneo ambayo yalikuwa hayana utaratibu wa mafunzo kwa askari hawa wa wanyamapori.
Tuwalinde wanyama hawa kwaajili ya vizazi vijavyo kwani kama wazee wetu wasinge watunza wanyama hawa basi hata sisi tusinge wakuta. Ni dhambi kubwa sana kuharibu mali tulizo jaaliwa kwa matamanio yetu na kusahau vizazi vyetu kwani wao inabidi wafaidike kutokana na sisi.
Mwisho…..
Kwa mengi zaidi kuhusu wanyamapori lakini pia ushauri kuhusu makala hizi na maswali basi usisite kuwa siliana na mimi kupitia
Sadick Omary
Simu=0714 116963 / 0765 057969 / 0785 813286
Email= swideeq.so@gmail.com
Au tembelea= www.mtaalamu.net/wildlifetanzania
……..I’M THE METALLIC LEGEND…..