Tunaishi kwenye mfumo wa maisha ambao kila mara unabadilika kutokana na ukuaji wa teknologia, idadi ya watu, na ongezeko la makazi ya watu na sehemu za uzalishaji. Bila ubishi ongezeko la watu limepelekea ongezeko la mahitaji ya msingi ya kibinadamu kama vile chakula na maji. Mahitaji ya msingi ya binadamu yanayomfanya aendele kuishi na kupambana na hali yoyote ile kuhakikisha kuwa anapata kitu cha kula. Kwa sababu ya hali hii ni ngumu kwa watu kujizuia hata pale anapofikiri anafanya kitu ambacho sio sahihi, kutokanana na changamoto za maisha jamii yetu hasa jamii zinazoishi kando kando ya hifadhi za misitu na hifadhiza wanyamapori au kwenye vyanzo muhimu vya maji ni ngumu kuacha kuharibu sehemu hizi muhimu endapo zinasaidia kutatua changamoto zao za msingi.
Mfumo wa maisha na mfumo wa uchumi na upatikanaji wa mali kwenye jamii yetu umetengeneza matabaka makubwa sana ambayo ni matabaka ya walionacho na matabaka ya wasio nacho, hali ambayo inapelekea ugumu wa kuisha kwa ua masikini kwenye jamii yetu. Kuna wenye uwezo wa kupata chakula na mahitaji yote muhimu, lakini kuna ambao hawajui hata siku yao itaishaje kwa kukosa hata mlo wa siku moja, na watu walio kwenye tabaka la chini ni watu ambao wanaishi kando kando ya rasilimali muhimu sana kama vile wanyamapori, misitu, bahari, na madini. Jamii hizi zinalipa gharama kubwa sana kuishi kwenye maeneo haya yaliyo karibu na maliasili na rasilimali hizi muhimu.
Jamii hizi zinazoishi kwenye sehemu hizi zinakabiliwa na changamoto kubwa sana ya kuishi maisha yao na kupata mahitaji ya msingi. Licha ya sheria za uhifadhi na uharibifu wa mazingira kuwa kali na jamii kufahamu baadhi ya sheria hizo, bado kuna changamoto kwenye hifadhi zetu, bado kuna watu wanaua wanyamapori kwa ajili ya kupata chakula na fedha, bado kuna watu wanakata miti hovyo na kuchoma mkaa, bado kuna watu wanakata miti na kuharibu vyanzo muhimu vya maji kwa ajili ya kupata maeneo kwa ajili ya kilimo, pia maeneo haya yamekuwa yakikabiliwa na uharibifu unaosababishwa na mifugo na kuharibu maeneo haya muhimu kwenye jamii yetu.
Kutokana na hali hiyo, na maisha kuwa na changamoto kubwa jamii hizi zimejikuta zikiwa na utegemezi mkubwa kwenye maliasili hizi muhimu. Licha ya makatazo yanayotelewa na viongozi kuhusu matumizi ya rasilimali hizi na uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji, bado watu wamekuwa hawana njia nyingine mbadala ya kuyaishi maisha yao bila kutegemea moja kwa moja kutoka kwenye rasilimali hizi.
Licha ya kuwepo na mashirika na miradi mbali mbali kwenye maeneo haya, yenye lengo la kutoa elimu ya uhifadhi na njia mbadala za kujipatia kipato bado haijitoshelezi kugusa kila mwanajamii, lakini miradi hii na mashirika haya yamekuwa ni muhimu sana kwani kwa kiasi fulani imepunguza na kubadilisha mitazamo ya watu, na kuwafanya wafikiri namna nyingine ya kujipatia kipato bila kutegemea moja kwa moja kutoka kwenye rasilimali au maliasili zinazowazunguka.
Hvyo basi, serikali, wahifadhi na wadau wa mazingira tuna wajibu mkubwa wa kufikiri kwa kina zaidi, namna jamii hizi zinavyoishi na kukabiliana na changamoto za maisha bila kuharibu hifadhi za wanyamapori na misitu pia kuhakikisha vyanzo vya maji na mazingira yanaendelea kuwa salama kabisa kwa manufaa ya sasa na baadaye.
Asante sana kwa kusoma makala hii, karibu kwa makala nyingine nzuri zaidi.
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 862 481/+255 742 092 569
www.mtaalamu.net/wildlifetanzania