Matumizi makubwa ya nyamapori yamesababisha kutoweka kwa idadi kubwa ya spishi za wanyama na mimea. Maeneo mengi yaliyo na rasilimali za wanyamapori yanakabiliwa na changamoto ya uvunaji haramu, biashara haramu na matumizi haramu ya wanyamapori. Kwa kiasi kikubwa jamii nyingi zinazoishi kando kando ya maeneo ya hifadhi za wanyamapori ndio huwa wanufaika wakubwa wa nyamapori kutokana na urahisi wa kupatikana.
Picha hii imepigwa na Basani Bafana, ikionyesha idadi kubwa ya wanyamapori iliyovunwa kwa njia haramu kwa ajili ya nyamapori.
Hata hivyo, tafiti nyingi kama zilifanywa hivi karibuni na Daniel Ingaram (2021), zinaonyesha kuwa matumizi ya nyamapori sio tu yameshamiri kwenye maeneo ya vijiji vilivyopakana na hifadhi za wanyamapori bali hata katika miji mikubwa. Kumekuwa na biashara haramu ya kusafirisha nyamapori kutoka vijijini sehemu ambazo wanyama hao huvunwa hadi mjini ambapo kuna watumiaji wakubwa wa nyamapori.
Mfano, utafiti uliofanyika hivi karibuni na Hillary Mrosso (2022), katika eneo la Ruaha nchini Tanzania uanaonyesha kuwa matumizi ya nyamapori kama kitoweo ndio yamechangia kwa kiasi kikubwa uwindaji haramu wa wanyamapori. Imebainika kuwa, matumizi makubwa ya nyamapori sehemu mbali mbali duniani imewavutia wengi kuingia katika biashara hii haramu ambayo ina madhara makubwa kwa wanyamapori na mazingira yao.
Licha ya nyamapori kuwa ni sehemu muhimu ya mlo wa jamii nyingi, tafiti zinaonyesha watumiaji wengi wa nyamapori hawajui madhara ya kiafya yanayoweza kusababishwa na matumizi holela ya nyamapori. Moja kati ya tafiti za hivi karibuni uliofanywa na Yohani Foya (2023) zinaonyesha zaidi ya 57% ya watumiaji wa nyamapori hawajui madhara ya kiafya yanayoweza kusababishwa na matumizi ya nyamapori iliyovunwa kwa njia haramu.
Pamoja na hayo, nyamapori imekuwa na mahitji makubwa licha ya kuwa inapatikana kwa njia haramu; ujangili kwa ajili ya kupata nyamapori ni kosa kwa mujibu wa sheria za ndani ya nchi na hata sheria za kimataifa. Licha ya wengi kujua kuwa kufanya ujangili ni kosa kisheria, bado wengi wamekuwa wakijihusisha na shughuli za uwindaji bila kibali.
Machapisho mengi yameonyesha kuwa kinachowafanya wengi kuingia kwenye ujangili ni ugumu wa maisha na umasikini. Jamii nyingi zinazoishi karibu na maeneo ya hifadhi za wanyamapori ni masikini sana na zinakabiliwa na mahitaji muhimu ya kila siku kama vile chakula, nguo, matibabu na fedha kwa ajili ya kulipia gharama za shule, na michango mingine ya vijijini.
Hata hivyo, mwandishi Ingramu pamoja na wenzake wameripoti kuwa watu wanaotegemea nyamapori kama sehemu muhimu ya mlo wao wa siku ni ngumu sana kushauriwa kuacha kufanya ujangili au kula nyamapori. Hii ni kwasababu karibia nusu au robo tatu ya mahitji yake ya maisha ya kila siku anayapata kwa kuwinda na kuuza nyamapori.
Itakuwa ni jambo gumu sana kuacha kufanya ujangili endapo mtu huyo anategemea ujangili kuendesha maisha yake. Endapo zitatumika nguvu nyingi kuzuia watu wa aina hii wasifanye ujangili italeta migogoro mingi isiyoisha kati ya hifadhi za wanyamapori na jamii.
Edapo tunataka watu wanaotegemea nyamapori kama kitoweo au sehemu muhimu ya kuendesha maisha yao waachane na nyamapori lazima tujue tunawapa aina gani ya shughuli za kipato na kuboresha maisha yako.
Hii ni moja ya changamoto kubwa sana kwa usimamizi wa wanyamapori sio Tanzania tu, hata duniani kwa ujumla. Hivyo basi, tunatakiwa kuunganisha nguvu na kuangalia namna bora ya kutatua changamoto hii kubwa inayopelekea wanyamapori wengi kutoweka.
Serikali na mamlaka zake za usimamizi wa wanyamapori zinafanya kazi kubwa kuweka ulinzi na usimamizi maeneo mengi yenye rasilimali hizi, lakini changoto bado ni kubwa licha ya juhudi zote hizi. Hivyo, tunatakiwa kushiriki katika kupiga vita ujangili wa wanyamapori wetu, na kama jamii inatakiwa kutafuta namna nyingine ya kukidhi mahitaji yao ya lazima bila kufanya ujangili wa wanyamapori.
Asante kwa kusoma makala hii, washirikishe wengine wajifunze pia.
Imeandaliwa Na Hillary Mrosso, +255 683 862 481