Moja ya vitu vinavyofanya ujangili uendelee katika nchi zetu za Afrika ni uwezekano wa usafirishaji wa bidhaa hizo haramu kwenda sehemu husika. Kila kukicha mapambano yanaendelea vita vinaendelea, hatuwezi kuweka silaha chini wakati tunaona wanyamapori wetu muhimu kama vile tembo na faru wanazidi kuteketea na kupotea kwenye makazi yao.
Majangili na wote wanaohusika katika maandalizi ya kufanya biashara hizi haramu za wanyamapori na bidhaa zao wana mtandao mkubwa ambao ni makini muda wote, wanatumia njia za kila aina kufanikisha adhma yao haramu, wanatumia kila aina ya udhaifu kwenye ulinzi na usalama kwenye bandari na viwanja vya ndege ili kusafirisha bidhaa zao haramu kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine, mara zote inakuwa kutoka Afrika kwenda katika nchi za Asia.
Moja ya ripoti maarufu iliyotoka Septemba 2017, inayojulikana kwa jina na Pandants, Powder and Pathways inaelezea kwa kina namna ambavyo majangili wanaojuhusisha na usafirishaji wa pembe za faru, na bidhaa nyingine ambazo husafirishwa kwa njia haramu wanavyotumia mianya ya udhaifu, iliyopo katika sehemu za usimamizi na ukaguzi, sehemu za usalama na sehemu za bandari na viwanja vya ndege ili kusafirisha bidhaa na nyara za faru na wanyamapori wengine kama vile tembo, kakakuona, simba na tiger nk.
Ripoti hii inayoonyesha jinsi ambavyo nchi ya Afrika Kusini ilivyo kitovu cha kusafirisha bidhaa hizo za wanyamapori walio hatarini kutoweka inaeleza mbinu nyingi ambazo wanatumia majangili kusafirisha nyara hizo ili wasijulikane kirahisi.
Wakati nasoma ripti hii iliyosheheni tarifa na mbinu nyingi za ujangili na njia nyingi za panya katika usafirishaji wa wanyamapori na nyara zao, inahusisha mtandao mkubwa sana wa watu na ni mtandao ambao upo makini kweli, na wana mbinu na njia nyingi za kutumia ili wasigundulike kuwa wanafanya biashara hizi haramu. Kwa mujibu wa ripoti hii inaonyesha jinsi walivyo wepesi kubadili mfumo wao na njia zao endapo wanaona kiashiria cha kugundulika au kukamatwa na askari au wakaguzi kwenye vituo vya usafirishaji.
Naamini kuna jambo ambalo tunatakiwa kujifunza mapema na kulifanyia kazi hasa kwenye udhibiti na usafirishaji, sehemu zote ambazo hutumika kusafirisha bidhaa kimataifa, zinatakiwa kufanyiwa uchunguzi na upelelezi mara kwa mara ili kubaini mbinu na njia zao wanazotumia kusafirisha nyara hizi kwa njia haramu.
Wakati mwingine nyara hizi husafirishwa kwa kushirikiana na mawakala na wasimamizi wa waserikali zetu. Na hapa ndipo kuna mlango mkubwa sana wa rushwa, ufisadi na ubadhirifu. Kweli serikali zetu hazijui kuwa bandari na sehemu zetu za usafirishaji zinajihusisha na biashara haramu? Kwa namna yoyote ile bidhaa haramu inaporuhusiwa kupita kwenye bandari zetu na viwanja vya ndege bila kuwepo kwa uwepo wa wazi wa rushwa kwenye maeneo hayo.
Rushwa inachochea sana vitendo vya ujangili kwenye hifadhi za wanyamapori, kuziba midomo ya wasimamizi maeneo ya ukakaguzi na kuzima kabisa juhudi za uhifadhi wa rasilimali zetu muhimu.
Kwa jinsi ambavyo tunachewa kuchua hatua kupambana na mitandao ya ujangili wa wanyamapori ndivyo tunavyoiruhusu mitandao hiyo kushamiri na kuota mizizi. Na matokeo yake tunakuwa na kazi kubwa ambayo itatugharimu kuifanya ili kuzuia majangili kwenye maeneo ya wanyamapori na kudhibiti njia zote za usafirishaji. Ni wakati wa kuchukua hatua sasa kuokoa wanyamapori wetu na mazingira yao ya asili.
Asante sana kwa kusoma makala hii.
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 862 481/+255 742 092 569
www.mtaalamu.net/wildlifetanzania