Habarini ndugu za siku kidogo ndugu zangu katika darasa letu huru la wanyamapori. Nilikuwa kimya kidogo kwasababu hali yangu kiafya haikuwa vizuri. Angalau kwa sasa namshukuru Mungu naendelea vizuri. Niliwakubuka sana hususani katika kujuzana machache kuhusu wanyamapori na kama ilivyo ada leo tena tunaingia darasani kujua machache kuhusu wanyama hawa. Makala mbili zilizopita tuliwasoma ndege ambao ni Korongo-Taji Kijivu na Mbuni.
Sasa leo tunarudi tena kwa mamalia, nikimaanisha wanyama ambao wana sifa ya kunyonyesha. Na moja kwa moja ungana nami katikja darasa hili kumjua mnyama aitwae “SWALA TOMI”
UTANGULIZI
Swala tomi ni jami ya swala ambao kwa hakika watu wengi wana wafahamu. Kwani wameenea sana Barani Afrika na hasa katika maeneo tengefu ya uhifadhi wa wanyamapori. Ni miongoni mwa swala ambao wanavutia sana kuwaangalia hasa kutokana na rangi zao na michezo yao ya kuruka wawapo katika maeneo ya hifadhi asilia.
Tukumbushane tu tunaposema neno swala basi linajumuisha wanyama wa aina mbalimbali walao majani, ambao kwa pamoja jina lao kuu huitwa swala. Mfano wa wanyama wengine ambao pia ni swani ni kama Nyumbu,Pofu,Swala pala na Minde.
SIFA NA TABIA ZA SWALA TOMI
- Wana miili mirefu kidogo huku wakiwa na rangi ya kahawaia iliyo pauka sehemu ya juu na pembeni na weusi kwenye ubavu. Sehemu ya chini yaani eneo la chini ya tumbo wana rangi nyeupe.
- Dume na jike wote wana pembe japo pembe zao huwa tofauti. Pembe za dume ni ndefu na zimejikunja kuelekea upande wa nyuma na zina maduara takribani ishirini (20) wakati pembe za jike ni fupi kidogo na zilizo nyooka.
- Swala tomi huishi kwa makundi na kila kundi hujumuisha kina mama na watoto. Katika kila kundi lina kuwa na watawala ambao wana maamuzi ya kuamrisha kundi kupumzika au kuendelea na safari na kuelekea ambapo watawala wa kundi wanaelekea.
- Watoto wa kiume mara tu wanapokua hufukuzwa kwenye kundi na hivyo kutengeneza kundi lao wenyewe ambalo huwa na madume watupu.
- Swala tomi wana uwezo mkubwa sana wa kusikia, kuona na hata kunusa au kuhisi harufu.
- Wanapo hisi kuna hatari basi huanza kuruka huku wakipiga miguu chini na hii ni kuwapa ishara wenzao ambao hawajamuona adui wajiandae kwa kukimbia.
- Wana uwezo wa kukimbia kwa mwendo kasi zaidi na utafiti unaonesha wana uwezo wa kukimbia kilometa themanini kwa saa (80km/saaa)
- Wana macho na masikio makubwa huku vichwa vyao vikiwa na umbo dogo.
- Wana mistari myeusi inayo anzia kwenye macho kushuka semu yachini puani.
- Wana mikia mifupi yenye rangi nyeusi ambayo muda wote huwa haitulii na kuichezesha kushoto na kulia au juu na chini.
JE UNAJUA?
- Swala tomi anapo kuwa anaruka ndio njia ambayo hutumia kuwapa wenzake taarifa ya hatari?
- Swala tomi anapokuwa anaruka humuonesha adui yake kwamba yupo vizuri kiafya na hata nguvu na uwezo wa kukimbia hivyo adui asijaribu kabisa kumkimbiza?
Swala tomi dume huweka alama ya mipaka kwenye eneo analo tawala majike kwa kutumia maji maji yanayo toka kwenye matezi yaliyopo kwenye macho?
KIMO NA UZITO
Kimo-Swala tomi huweza kufikia hadi kimo cha sentimita 60-90.
Uzito- Huweza kufikia uzito wa kilogramu 80kg
MAZINGIRA
Wanapatikana sana maeneo yenye aridhi iliyo shamiri majani na hasa tambarare. Wanapendelea pia maeneo ambayo wanyama wengine wakubwa walao majani wameyatumia sana kwa muda mrefu.
Swala tomi wana uwezo wa kuishi eneo moja kwa muda mrefu sana ambapo wanyama walao majani hasa pundamilia na nyumbu walipoondoka.Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo swala tomi wanapatikana sana pamoja na Kenya.
CHAKULA
Swala tomi ni wanyama ambao wanapendelea sana kula majani ya juu kama walivyo mbuzi. Na hii ni kutokana na maumbile ya midomo yao.
Kundi hutawanyika kwa kufuata muongozo mchana wakati wa kula. Kadiri jua linavyo zidi kuzama basi huanza kukusanyika sehemu moja kwa ajili ya kutafuta sehemu nzuri ya kulala.
Wanapendelea kula majani machanga, mbegu na majani ya kwenye miti. Wana hitaji maji ya kunywa kila siku na ndio maana swala tomi hupendelea kuishi maeneo ambayo upatikanaji wa maji unakuwa ni rahisi sana.
KUZALIANA
Kabla ya kuwa mtawala wa kundi la majike, madume huwa wanapigana sana na anaye shinda pambano basi huchukua kundi lote la majike na kuwa chiniyake. Huweka mipaka kwenye majani kwa kutumia maji maji yanayo toka kwenye matezi ya macho ili dume mwingine anapo kuja ajue tayari eneo hilo lina mtawala tayari na ukubwa wa eneo mara nyinyi huwa ni mita 20M.
Swala tomi hupandana mara mbili kwa mwaka na huzaa mara tu baada ya msimu wa mvua. Jike hukaa na mimba kwa taribani miezi 5-6. Unapo fika wakati wa kuzaa jike huondoka na kwenda mbali na kundi kwa ajili ya kuzaa na hasa eneo lenye usalama. Baada ya kuzaa jike hulazimika kumuacha mtoto mafichoni hasa kwenye nyasi ndefu na kwenda kutafuta sehemu yenye majani mazuri ili kuweza kula na hurudi mafichoni mara kwa mara hasa wakati wa mchana ili kumnyonyesha mtoto.
Huwa ni vigumu kwa maadui kumuona mtoto kutokana na mazingira ambapo mama anamuacha na pia rangi ya mtoto mara nyingi hushabihiana na mazingira aliyopo. Endapo kwa bahati mbaya mtoto akafa au kiliwa na maadui kama simba au duma basi mama hulazimika kupandwa tena na dume ili aweze kuzaa tena ndani ya mwaka huo huo. Swala tomi ni baadhi ya wanyama wachache sana wenye uwezo wa kuzaa mara mbili ndani ya mwaka mmoja.
Umri wa swala tomi ni taribani miaka kumi hadi kumi na tano (10-15)
UHIFADHI
Japo idadi ya swala tomi imekuwa ikipungua baadhi ya maeneo ya Afrika kutokana na kuwindwa na pia uharibifu wa mazingira, swala tomi bado hawajawekwa kwenye kundila wanyama waliyo kwenye tishio la kutoweka.
Hii ni kutokana na utafiti ulio fanywa na shirika la umoja wa mataifa linalo shughulika na uhifadhi wa maumbile asili duniani lijulikanalo kama (International Union for Conservation of Nature-IUCN).
MAADUI NA TISHIO KWA SWALA TOMI
- Maadui wa swala tomi ni Duma, Simba, Chui, Fisi a Mbwa mwitu.
- Ujangili ulio kithiri katika maeneo ya hifadhi za wanyamapori kutokana na kuongezeka kwa soko la uhitaji wa malighafi za wanyamapori dunuiani kumepelekea sana wanyama hawa kuwindwa kwa kiasi kikubwa sana.
- Uharibifu wa mazingira utokanao na shughuli za kibinadamu mfano uchimbaji wa madini na ukataji miti kwa ajili ya maeneo ya makazi na kutanua mashamba una sababisha swala tomi kuhama baadhi ya maeneo.
- Makampuni ya uwindaji yamekuwa yakikiuka sana sheria na mikataba ya uwindaji kwa kuzidisha idadi ya wanyama wanao takiwa kuwindwa au wakati mwingine kuwinda majike tena wenye mimba au kuwinda swala tomi wadogo.
- Siasa zisizo na tija kwenye uhifadhi na hasa hili limeonekana katika maeneo mengi sana ya uhifadhi kwani viongozi wamekuwa mstari wa mbele kurudisha nyuma shughuili za uhifadhi kwa maslahi ya kutaka kura kwa wananchi.
NINI KIFANYIKE KUWANUSURU SWALA TOMI HASA HAPA KETU TANZANIA
- Kupambana na ujangili hasa kuongeza idadi ya askari wa wanyamapori na kushirikisha jamii ili kufichua makazi ya majangili wahusika wakuu kwani wengi wamekuwa wakiishi karibu na jamii nyingi zinazo zunguka hifdhi.
- Wizara ya Mali asili na Utalii kwa kushirikiana na wizara ya mazingira ziongeze jitihada kupambana na uharibifu wa mazingira. Pongezi sana kwa Mh. January Makamba kwa kazi kubwa sana anayo ifanya ili kupunguza uharibifu wa mazingira na kwa kweli kazi yake inaonekana kwenye macho ya watu.
- Ufuatiliaji mzuri na wa uhakika wa makampuni ya uwindaji ili wafuate kanuni na taratibu zilizoandikwa kwenye mikataba na vibali vyao vya uwindaji ili kuepuka adha ya uwindaji wa idadi kubwa ya wanyama au kuwinda wanyama wasio stahili kuwindwa.
- Tuepuke sana kuingiza siasa ambazo hazina ulazima kwenye sekta ya uhifadhi kwani siasa imekuwa kama mwiba wenye sumu kali kwa maendeleo ya uhifadhi hapa nchini.
HITIMISHO
Kuna mambo mengi sana yanayo hitaji ufafanuzi hasa kuhusu uhifadhi wa wanyamapori na maendeleo ya jamii kwa ujumla. Hakuna mgeni yeyote atakae tuletea maendeleo yahifadhi zetu na maliasili tulizo nazo kama sisi wenyewe hatuna dhamira ya kuvitunza vile tulivyo jaalliwa na Mwenyezi Mungu.
Nalipongeza sana shirika la hifadhi za taifa Tanzania TANAPA bila kuisahau na mamlaka ya hifadhi ya eneo la Ngorongopro pamoja na mamlaka nyingine zote kwa kazi kuwa wanazo zifanya ili kulinda maeneo tengefu ya uhifadhi wa wanyamapori pamoja na mazingira yao.
Wito wangu kwetu sisi wananchi pia hatuna budi kuwaunga mkono wale wote wanao jitoa kwa dhati ili kunusuru rasilimali hizi tulizo nazo na tuwe tayari kutoa msaada kwa namna yoyote ile pale tutakapo hitajika kutoa msada huo.
Nakushukuru kwa kuwa pamoja nami kuanzia mwanzo mpaka mwisho wa makala hii katika darasa letu huru la wanyamapori. Nikusihi pia kutega jicho kwenye ukurasa wangu wa facebook na blog yetu ya wanyamapori ili kujua makala ijayo tutamzungumzia mnyama gani na kuyajua machache kuhusu mnyama huyo ajae hapo mbeleni.
Kwa mengi zaidi kuihusu wanyamapori lakini piana ushauri kutoka kwako msomaji wa makala hizi za wanyamapori wasiliana na mwandishi wa makala hii;
Sadick Omary
SIMU- 0714116963 / 0765057969 / 0785813286
Email – swideeq.so@gmail.com