Siku moja jioni niliingia katika mtandao wa X (Twitter) na kuona hii picha kwenye ukurasa wa mtu mmoja, simkumbuki tena jina, yule aliyeposti hii picha alijharibu kuweka maoni yake. Lakini kila nikiangalia hii picha ilinipa huzuni na mawazo mengi.
Picha hii ya kiota cha ndege, sijui ni ndege gani, lakini kilichoteka umakini wangu kwenye hii picha ya kutisha ni namna hayo makinda ya ndege walivyokufa kifo kibaya. Ndio, niliwaza kuwa hawa watakua ni makinda ya ndege waliokuwa wakisubiria chakula kutoka kwa mama yao.
Picha hii inaweza kuwa picha halisi ilipigwa mahali, au inaweza kuwa picha ya kutengenezwa, lakini ni picha yenye ujumbe muhimu kwa kila moja wetu. Kwanamna picha ilivyo, inaonyesha kifo cha kutisha kilichowaua hao ndege taratibu kwa muda mrefu.
Hii ndio sababu ya kuiita picha la kutisha kutokana na aina ya kifo, nimehusisha kifo hicho na njaa ya muda mrefu. Watoto wa ndege walimsubiria mama yao aliyeenda kuwatafutia chakula lakini hakufanikiwa kuwarudia tena.
Tafsiri na ujumbe ambao niliupata kwenye hii picha ya kutisha ilinifanya kukaa chini na kuandaa makala hii, ili nikushirikishe baadhi ya vitu nilivyoviona kwenye hii picha. Naamini kuna ujumbe muhimu sana kwa jamii kuhusu uhifadhi wa ndege na wanyamapori kwa ujumla.
Unaweza kuangalia hiyo picha ukuona mafuvu ya vitoto vitano vya ndege, huenda vilikufa kwa njaa baada ya kukosa chakula kwa muda mrefu. Niliwaza sana nini kilitokea mama yao hakurudi kuwaletea chakula? nini kilimkuta mama yao asiweze kurudia watoto wake?
Huenda mazingira hayo hayakuwa na chakuala kwa ajili ya watoto hao, hivyo ikamlazimu mama yao kwenda umbali mrefu kutafuta chakula cha watoto wake. Jinsi chakula na mahitaji ya muhimu yanapokuwa mbali na nyumbani, hatari ni nyingi za kusafiri umbali mrefu, huenda aliuliwa na ndege wengine, au wanyama wengine hivyo akafia huko hakurudia tena watoto wake.
Pia niliwaza uharibifu wa makazi na mazingira muhimu husababisha ndege hao kukosa chakula, jambo hili limfanya ndege kusafiri umbali mrefu ambao una hatari nyingi kwa ajili chakula na mahitaji mengine muhimu kwa ajili ya familia yake.
Pia niliwaza wakati anasafiri kwenda kutafuta chakula kwa ajili ya watoto wake, aligongwa na magari. Kama ilivyoripotiwa na Lyamuya na wenzake katika utafiti wao wa mwaka 2021 kuwa, asilimia 60 ya ndege wanauwawa kwa kugongwa na magari. Babaraba zetu hasa zinazopita hifadhini zinaleta maafa makubwa kwa wanyama na ndege. Jisomee hapa zaidi, Kilio Kisichoisha Ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi
Picha hii ilinifanya nifikiri, huenda mama ya watoto hao wa ndege aliuwawa na wawindaji haramu. Ndio, inawezekena maana ndege ni viumbe ambao wanawindwa sana kwa ajili ya kitoweo na pia kwa ajili ya biashara au kufuga, hivyo akashindwa kurudi kuwaona watoto wake.
Wakati huo huo pia niliwaza huenda ndege huyo aliwekewa sumu na wawindaji haramu. Ndio, kwasababu, tafiti zinaonyesha ndege wengi wanawindwa na kuuwawa kwa kuwekewa sumu hasa kwenye vyakula wanavyokula. Huenda walimtegea chakula chenye sumu akala akafa hivyo akashindwa kuwarudia watoto wake.
Niliwaza tena nikaona inawezekana huyu ndege aliuwawa kwasbabu ya mambo ya kishirikina. Ndio, inawezekana maana jamii zetu kuna watu wanaamini baadhi ya ndege sio wazuri, hivyo hawataki kuwaona baadhi ya ndege kwenye maeneo yao, mfano ndege aina ya bundi. nk.
Baadhi ya mitazamo tuliyonayo kuhusu wanyamapori ni hasi, mfano kuna watu wanawahusisha wanyamapori kama fisi, popo na mambo ya uchawi na ushirikina. Jambo hili husababisha watu kuwa na mitazamo hasi kwa wanyama, ndege na wadudu. Soma zaidi kufahamu imani za jamii yetu zilivyo kwa baadhi ya wanyamapori Mitazamo Na Imani Za Watu Wengi Kwenye Jamii Zetu Sio Rafiki Kwa Wanyamapori Na Viumbe Hai Wanaoishi Karibu Na Makazi Yetu.
Sababu nyingine inaweza kuwa ndege huyu aliuwawa kwa kuchomwa na moto. Ndio, unajua maeneo mengi ya hifadhi za wanyamapori wanachoma moto kwa ajili ya sababu za kiuhifadhi, huenda mama aliuwawa kwa kuungua na moto, au watoto waliungua na moto kwa kukosa msaada wa mama yao.
Licha ya faida za moto katika ikolojia, ni vizuri pia wahifadhi wakawa wanafikiria viumbe wasioweza kukimbia moto kama watoto wa ndege, kobe, kakakuona, na viumbe wengine wasiweza kukimbia moto unapowaka hifadhini.
Lakini pia nikawaza inaweza kuwa ni mioto inayowashwa na watu wanapoandaa mashamba, au wanaporina asali porini. Mioto hii inaweza kuleta madhara kwa viumbe wadogo kama ndege na pia mioto hiyo inakuwa haijachomwa kwa utaratibu hiyo huleta madhara kwa wanyama na ndege.
Picha hii imenifanya nifikiri mifumo ya ikolojia na kutegemeana kwenye mazingira. Mfano, hapo kama mama ndege ameuwawa na ameacha watoto ambao ni tegemezi, ni wazi kuwa watoto hao hawawezi kupona. Kizazi kizima kimeuwawa.
Hii inanikumbusha sharia za uwindaji, endapo mnyama mwenye mimba au mwenye watoto wanaomtegemea wanatakiwa wasiwindwe hata kama kuna kibali cha kufanya hivyo. Ndio hapa tunapohitaji elimu za tabia za wanyama na ndege ili kufahamu tabia za wanyama ili tufanye maamuzi mazuri tunapotaka kuwinda wanyamapori au ndege, tuzingatie mambo muhimu kama ilivyoandikwa kwenye sheria uhifadhi.
Kuna ujumbe mwingine kwenye hii picha, kuna baadhi ya ndege wanapenda kuishi karibu na makazi ya watu. Nadhani wengi wetu tunaweza kuwa mashahidi wazuri kwenye hili. Kuna ndege wanajisikia wapo salama endapo wataishi kwenye nyumba zetu, kwenye bustani zetu au kwenye miti iliyopo kwenye makazi au mashamba yetu. Unaweza kusoma zaidi hapa, Fahamu Umuhimu Wa Ndege Kama Kiashiria Cha Hali Ya Mifumo Ya Ikologia Katika Maeneo Mbali Mbali
Hivyo, ukiona ndege wamekuja karibu na nyumba yako, usianze kukakazana kuwaua, kuwafukuza au kuwawekea sumu ili uwaue. Wakaribishe na wala usiondoe mazingira ambayo wameyapenda. Inawezekana hapo nje ya nyumba yako kuna mti wameupenda, unachoweza kufanya ni kuuacha huo mti, ili wajisikie vizuri kukaa karibu yako.
Ndege ni kiashiria kizuri sana cha afya ya mazingira, lakini pia husaidia kula baadhi ya wadudu hatari, pia ndege husaidia kwenye uchavushaji mimea, kusambaza mbegu za mimea kwenye maeneo mbali mbali. Kama wewe unapenda kutunza mazingira unaotesha miti, unalima bustani, lazima kuna aina ya ndege utawavutia kuja kukutembelea.
Ndege wanaathiriwa sana na uharibifu wa mazingira, mfano kuharibika kwa maeneo ya asili, kukauka kwa vyanzo vya maji, au uchafu wa vyanzo vya maji ni hatari kwa baadhi ya ndege wanaopenda kuishi kwenye maeneo yenye maji.
Ndege wamegawanyika kulingana na maeneo wanakopatikana. Mfano, kuna ndege wanaopatikana misituni tu, kuna ambao wanapatikana maeneo yenye maji, kuna ambao wanapatikana kwenye savanna, kwenye mashamba yaliyoachwa, wengine kwenye maeneo makavu, wengine kwenye makazi ya watu nk.
Kutonana mgawanyiko huo, tunatakiwa kufahamu tabia za ndege ambao wapo kwenye maeneo yetu, tuwatunze kasababu hawawezi kuishi sehemu nyingine tofauti na maeneo ya aina hiyo. Tusidhani ndege wanaishi maeneo yoyote tu, bali wanaishi hapo kwasababu hawana sehemu nyingine salama ya kuishi kama hapo walipo.
Niiombe jamii kuwa rafiki wa ndege, tuwasaidie ndege ambao wanakuja kwenye makazi yetu au kwenye maeneo yetu na kuishi. Tusiwaue wala kuwadhuru, tuwape nafasi ya kuishi karibu nasi. Najua, kuna baadhi ya ndege ni waharibufu wanakula mazao na kuleta hasara kwa kwa wakulima. Endapo kuna changamoto hiyo kuna njia ambazo zinapendekezwa za watu wa maliasili kuwafukuza ili wasilete hasara. Zaidi tunaweza kusoma makala hii, Wanyamapori Katika Mtego wa Imani: Uharibifu Usioonekana na Jinsi ya Kupambana Nao
Nchi yetu imebarikiwa kuwa na aina nyingi sana za ndege, wanyama, wadudu, vyura, nyoka, samaki nk. Ambao ni sehemu muhimu sana ya mazingira yetu na uchumi wetu. Tusipokuwa na mitazamo chanya kwenye viumbe hawa, tutawapoteza mapema.
Nitoe rai yangu kwa jamii kuwa, hatari zimekuwa nyingi sana kwa viumbe hai, kama vile shughuli za kibidadamu, mabadiliko ya tabiachi, ongezeko la watu na mahitaji ya watu. Yote haya yanachangia kuongeza hatari kwa wanyamapori na viumbe wengine kama ndege.
Kikubwa tunachotakiwa kufanya ni kutunza mazingira yetu, na mazingira ya viumbe hawa. Lakini pia kuachana na vitendo vya kuua, kuwinda au choma mioto hovyo ili kupunguza vifo kwa wanyama, ndege na wadudu ambao kwa kiasi kikubwa ndio wahanga.
Hayo ni baadhi ya mambo machache niliyoyaona kwenye hiyo picha, nakukaribisha unishirikishe pia mambo mengine ambayo wewe umeyaona kwenye hiyo picha.
Asante kwa kusoma makala hii, kwa mengi mazuri kuhusu uhifadhi, usiache kutufuatilia na kuwashirikisha wengine ujumbe wa makala hii.
Imeandikwa na Hillary Mrosso, +255 683 862 481, hmconserve@gmail.com