Habari msomaji wa  makala za wildlife Tanzania, karibu kwenye uchambuzi wa makala ya sheria ya wanyamapori ya mwaka 2009. Tunachambua ili kila mmoja wetu ajue uzito na jinsi ambavyo sheria ilivyoweka mkazo na inavyotambua kila kiumbe na kila maliasili iliyopo kwenye ardhi ya Tanzania. Leo tunaendelea na sehemu ya nne ambayo tunachambua maeneo na sehemu ambazo zimetengwa na kutangazwa kuwa ni hifadhi ya wanyamapori, maeneo haya yanayotambuliwa na sheria hii mara nyingi ni njia na mapitio ya wanyamapori kwa hiyo sheria inayatambua na kuyalinda. Maeneo haya nimeyataja kwenye kichwa cha makala hii ambayo ni Wildlife Corridor (Ushoroba), Dispersal Areas (Maeneo ya Mtawanyiko wa Wanyamapori), Buffer Zones (Maeneo yanayotumika kupunguza athari, maeneo ya amani), Migratory Routes ( Njia za Mapitio ya wanyamapori).

Kuna maneno mengine ya kingereza yaliyotumika kwenye sheria hii hayana misamiati mizuri ya Kiswahili, hivyo nimejaribu kuyaelezea dhima yake na pia mengine nimeyaandika kama yalivyo ili yasipungue maana yake kwenye kila kilichokusudiwa. Hivyo Rafiki karibu twende pamoja tujifunze sehemu hii muhimu. Leo tunaendelea na kifungu cha 22 ya sheria ya wanyamapori.

21.- (1) Waziri anaweza, baada ya kushauriana na mamlaka husika za eneo hilo na pia kwa kutoa taarifa kwenye Gazeti la serikali kuteua eneo kuwa wildlife corridors (Ushoroba), maeneo ya mtawanyiko wa wanyamapori (dispersal areas), maeneo yanayotumika kupunguza athari za migogoro (buffer zones), na njia za mapitio ya wanyamapori (migratory routes). Sehemu zote hizo zipo kwenye uwezo wa waziri kutangaza na kuteua eneo au sehemu fulani kuwa hifadhi ya wanayamapori na viumbe wengine. Hivyo njia zote za wanyamapori zinatambulika kisheria na zinalindwa kisheria.

(2) Waziri anaweza, baada ya kushauriana na mamlaka husika, kuagiza kwa mapendekezo ya kanuni kwenye Gazeti la serikali kuwepo na usimamizi wa maeneo hayo aliyoyateua kama ushoroba, maeneo ya mtawanyiko wa wanyamapori, njia za mapitio ya wanyamapori na maeneo yanayotumika kupunguza athari za migongano na jamii. Hivyo waziri ana wajibu na pia anatakiwa kuweka usimamizi na uongozi mzuri kwenye kuhakikisha maeneo haya yanayotumiwa na wanyamapori kama njia na mapitio yanalindwa na kutunzwa kwa mujibu wa sheria hii.

(3) Kanuni zilizotungwa na Waziri kwenye kifungu kidogo cha (2) cha sehemu hii ya sheria kinatakiwa kutamka kuwa ni haki ya jamii au wanajamii wanaohusika moja kwa moja na sehemu hii ya  uhifadhi wanyamapori.

(c) SPECIES MANAGEMENT AREAS (MAENEO YA USIMAMIZI WA SPISHI)

Hiki ni kipengele kingine ndani ya sehemu hii ya sheria ambacho kinatambua maeneo yenye spishi za viumbe hai na kuyasimamia kisheria. Sheria imeweka wazi kabisa na kutambua maeneo ya namna hii, kwa sababu maeneo hayo yanaweza kuwa sehemu mbali mbali na watu bila kujua maeneo hayo yapo kwa kusudi gani wakayaharibu, lakini sheria inayatambua na kuyalinda, hivyo msomaji wangu tunapaswa kuyafahamu maeneo haya na kushirikiana kuyahifadhi kwa mujibu wa sheria.

  1. – (1) Waziri anaweza, baada ya kushauriana na mamlaka husika na kwa kutoa taarifa kwenye Gazeti la serikali kutangaza eneo lolote kuwa eneo la usimamizi wa spishi (Spicies management areas). Hivyo eneo lolote la ardhi ya Tanzania linaloonekana lina biyoanuai nyingi au linalotoa makazi kwa viumbe hai muhimu linatakiwa kutangazwa kisheria kuwa katika usimamizi wa serikali na shughuli nyingine za kibinadamu kwenye eneo hili lazima zizuiwe.

(2) Maeneo ya usimamizi wa spishi yanatakiwa kuanzishwa kuwa kusudi la kulinda kila mnyama au daraja (class) ya mnyama au mazingira au makazi yake. Kwa hiyo uanzishwaji wa maeneo haya ya usimamizi wa spishi inatakiwa iwe kwa kusudi hilo, kuhakikisha wanyama wote au wadudu kwenye eneo hilo wanalindwa na kusimamiwa vizuri kabisa.

  1. –(1) Mtu yeyote ambaye bila ruhusa kutoka kwa Mkurugenzi atachoma uoto, atawinda, atakamata, akajeruhi, akusumbua au akaua spishi au mnyama yoyote kwenye maeneo ya usimamizi wa spishi, anafanya kosa na atakuwa na hatia itakayomgharimu yafuatayo;

(a) atakapokiri kufanya kosa au ameoneka na kuwa na hatia ya kuwinda, kukamata, ao kuua wanyama waliohifadhiwa na kulindwa, atakwenda jela kwa kifungo kisichopungua miaka mitatu na kisichozidi miaka saba au kulipa faini isiyopungua mara mbili ya thamani ya mnyama aliyemuwinda, kumuua au aliyemkamata au vyote kwa pamoja. Hivyo ndivyo sheria hii ilivyo kali kwa watu wasiotaka kufuata utaratibu na sheria kwenye maeneo ya hifadhi za wanyamapori.

(b) kwa jambo lingine lolote atalipa faini isiyopungua shilingi laki moja (100,000) lakini isiyozidi shilingi laki tano (500,000) au kwenda jela kwa kifungo kisichopungua miezi mitatu na kisichozidi miaka miwili.

(2) Mtu yeyote hataruhusiwa kujeruhi, kuumiza,au kusumbua spishi yoyote iliyohifadhiwa na kulindwa. Kwenye maeneo ya hifadhi na usimamizi wa spishi za wanyama mtu hataruhusiwa kujeruhi, kusumbua na kuumiza wanyama walipo kwenye maeneo hayo, kwani kufanya hivyo ni kosa na adhabu yake ni kubwa sana kwa mijibu wa sheria.

Naamini mpaka hapa umepata mambo ya kukusaidia, hivyo endelea kufuatilia na kujifunza zaidi kuhusu kila kitu kwenye mtandao huu. Na pia washirikishe marafiki zako na watu wengine maarifa haya kwa kushare link hii au kwa kuwaambia wafungue na kusoma makala za blog hii. Tuendelee kuwa pamoja kwa kujifunza na kuchukua hatua ili kuhifadhi wanyamapori wetu.

Ahsante sana!

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 248 681/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania