Habari msomaji wa makala za wildlife Tanzania, naamini siku yako imekuwa bora, karibu kwenye makala yetu ya leo ambayo nitakueleza sababu  na umuhimu wa kuapata maarifa haya ya wanyamapori Tanzania.  Tanzania ina eneo kubwa sana limetengwa kwa ajili ya matumizi ya maliasili na pia hifadhi za wanyamapori na mimea. Hivyo ufahamu wa maeneo na jinsi mambo yanavyoenda kwenye maeneo haya ya uhifadhi wa wanyamapori ni muhimu sana kwa ajili ya kulinda, kusimamia na kufaidika na uwepo wa maliasili hizi muhimu kwa nchi yetu. Kuna sababu nyingi sana za kuwa msomaji na mfuatiliaji wa blogu hii ya Wildlife Tanzania, hapa nimekushirikisha chache ili tuweze kwenda pamoja na, hapa nimekuandalia sababu kumi za umuhimu wa kupata maarifa haya.

1.Elimu na Maarifa

Elimu ni jambo muhimu sana kwa maisha ya binadamu yeyote, nilianzisha blogu hii kwa lengo kubwa kutoa elimu kwa watanzania wote kwa kutumia lugha rahisi kabisa ili kila mtu anayejua Kiswahili asome na afahamu mambo ya msingi yaliyopo kwenye hifadhi, na maliasili nyingine  za nchi yetu. Hivyo elimu na maarifa utakayopata hapa yatakusaidia kuamua vizuri namna ya kuboresha maisha yako na kuinua uchumi kwa nchi. Pia itakuwa sehemu za kuwasaidia wataalamu na watu wanaofanya kazi kwenye sekta hii kuwa na uwanja mkubwa wa kufanya maamuzi kupitia maarifa na taarifa hizi.

  1. 2. Njia nzuri za kutangaza Utalii wetu

Tanzania ina maeneo mengi sana yenye mvuto na yanayowafanya watu kupenda kuyatembelea, karibu kila mkoa kwenye nchi hii kuna vivutio na mandhari nzuri ambazo zikitumiwa vizuri zinaweza kuinua hali ya uchumi wa mkoa na Taifa. Hakuna njia nzuri ya kuutangaza utalii na utajiri wa maliasili tulizo nazo bila kuwashirikisha watanzania kufanya hivyo, hii ndo maana lengo na nia yangu ni kuamsha utamaduni wa kutembelea hifadhi na maeneo yenye vivutio kwa watanzania wote. Itakuwa kazi rahisi sana kwa watanzania kutangaza kwa watu wengine kitu ambacho wanakifahamu na kukiona, watanzania tuna wajibu wa kutangaza nchi yetu kwa maliasili tulizo nazo kwa kuwa na utaratibu wa kutembelea maeneo hayo.

  1. 3. Kuvumbua na kutumia vivutio vilivyo sahaulika

Naamini kila mkoa kwenye nchi hii kuna kitu cha tofauti ambacho kinaweza kuwa kivutio kwa watu wengine. Hivyo kwa kuwa msomaji wa makala hizi kwa pamoja tutashirikiana kuyajua na kuyatumia maeneo hayo kama sehemu nzuri ya kuukuza mkoa na wilaya au Kijiji, kuna mikoa ambayo haijulikana kwa lakini kupitia blog hii tutahakikisha kila kilicho cha kipekee tutakiweka wazi ili watanzania waanze kwenda kutembelea na kujionea sehemu hizi kwenye mikoa hiyo.

  1. Umuhimu wa kutunza Mazingira

Hakuna kitakacholeta mvuto kama Hakuna mazingira mazuri yaliyotunzwa, kwa utafiti wangu nimegundua watu wengi sana wanapenda sana vitu vya asili, wanapenda kutembelea mazingira ya asili na wanapenda vitu viendelee kubaki hivyo kwa miaka mingi ili kuendelea kuvutia zaidi. Ndio maana mazingira yaliyohifadhiwa na kusimamiwa vizuri yanakuwa na mvuto sana kuliko maeneo mengine. Hivyo kupitia blogu hii tutashirikishana mambo yote ya msingi ili tupate uelewa mzuri na pia tushiriki kwenye shuguli zote za utunzaji, na usimamizi wa mazingira yetu.

  1. Sharia mbali mbali za uhifadhi wa wanyamapori na Maliasili

Migogoro mingi inayoendelea kwenye jamii yetu ni kutokana na kutojua mambo ya msingi, kwa migogoro mingi ya ardhi ni kutoelewa matakwa ya sharia kwenye eneo husika, migogoro ya wafugaji na wakulima ni kutojua maeneo yao kisheria na haki zao kisheria, migogoro kati ya wafugaji na hifadhi za wanyamapori ni kutojua na ktoelewa sharia zinasemaje kwa pande zote mbili. Uonevu na ukandamizaji kwenye maeneo haya ni kutojua haki za muhusika kisheria. Hivyo kupitia blogu hii tutajifunza hayo yote kwa pamoja.

  1. Mchango wa sekta ya maliasili na utalii kwenye ukuaji wa Uchumi

Hapa tutajuzana umuhimu wa sekta hii nyeti na tutaona jinsi inavyochangia kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi. Hivyo watanzania tuanatakiwa kuelewa pesa hizi zinapatikanaje na ni aina gani ya utalii wenye manufaa kwa muda mrefu. Tutajifunza hayo yote hapa.

  1. 7. Kushiriki vita dhidi ya Ujangili wa Wananyamapori

Kama nilivyoeleza kwenye makala mbali mbali, ujangili ni mtandao wa muda mrefu na wenye mikono mingi ambayo kamwe hauwezi kusha bila juhudi za kila mmoja wetu kushiriki kwa namna ambayo itasaidia kuzuia na kupinga na kutoa taarifa sehemu husika ili ujangili ukomeshwe kwenye maliasili zetu. Hivyo kwa kuapa maarifa haya kupitia wildlife Tanzania kila mtanzania atajua namna anavyoweza kushiriki kwenye vita dhidi ya ujangili wa wanyamapori.

  1. Fursa za uwekezaji kwenye sekta ya Wanyamapori

Tanzania ina maeneo makubwa na mengi  sana kwa uwekezaji maeneo haya ni kwenye sekta ya maliasili na utalii, kuna mapori mengi sana, kuna hifadhi nyingi sana kuna maeneo makubwa yanayofaa kwa uwekezaji wowote wa kitalii, kuna maeneo yanafaa kwa uwindaji wa kitalii. Hivo kwa kuendelea kuwa pamoja tushirikishane mambo haya na fursa ambazo watanzania wengi hawajui. Hivi ndivyo utakavyonufaika kwa kupata maarifa haya hapa.

  1. Ufahamu wa wanyamapori mbali mbali, sifa ,tabia nk

Pia hapa tutakua tunachamua mnyamapori moja baada ya mwingine, ndege na reptilia mbali mbali, hivyo kwa wale watakao kuwa wanapenda sana kujua na kujifunza tabia za wanyama na sifa zao basi hapa patakuwa maahali sahihi, na pia utapata nafasi ya kuuliza maswali na utajibiwa kwa ufasaha kabisa. Hivyo huu ni mtandao wa watanzania wote wanaotaka kujua vitu mbali mbali vinavyoendelea kwenye maliasili zetu.

  1. Sehemu ya kupata taarifa mbali mbali muhimu

Nimekuwa nikiposti na kuandika taarifa mbali mbali kwenye blog hii ya wildlife Tanzania mara kwa mara, mfano kwenye sherehe za Nane nane, kulikuwa na ofa ambayo ilitolewa na TANAPA kutembelea hifadhi za Taifa za Tarangire na Ruaha. Kwa wakazi wa Dodoma, hivyo mimi nami nilishiriki kuwapa taarifa wafuatiliaji wa blogu hii ili wapate nafasi ya kutembelea hifadhi za taifa. Hivyo tutaendelea kuwa pamoja kwenye jambo hili watanzania waelewe kinachoendelea kwenye maeneo ya hifadhi za wanyamapori.

Hivyo basi kwa sababu zote hizo, na nyingine nyingi bado tutaendelea kushirikishana kila kitakachokuwa na msaada kwetu. Natamani tujenge kwa pamoja Tanzania mpya yenye uzalendo na maliasili zao, kwa kuwa wakwanza kutembelea na kutalii maeneo yenye vivutio. Naamini kwa kufanya jambo hili kwa pamoja tutakuza sana utalii wa ndani katika nchi yetu. Lazima tuwajibike na tulifanyie kazi jambo hili ili tuwe na kizazi cha kizalendo.

Ahsante sana kwa kusoma makala hii, nakuomba Rafiki yangu usiache kumshirikisha mtu yeyote maarifa haya muhimu, fanya hivyo uwe sehemu ya kujenga na kuitangaza Tanzania ya utalii wa wanyamapori na mambo ya asili. Kwa pamoja tunaweza kuifanya Tanzania kuwa taifa la watu mashuhuri na wzaalendo.

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 248 681/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania