Hifadhi ya taifa ya Ruaha ni kati ya maeneo machache yaliyobaki hapa duniani kwa kuwa na hali yake ya uhalisia, nikimaanisha kwamba pamoja na ukubwa wa eneo hili la hifadhi ya Ruaha bado kuna asilimia kubwa sana ya mimea na uoto wa asili kwa maeneo mengi ya hifadhi hii. Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ina Wanyama wa kipekee sana jamii ya Tandala wakubwa na wadogo ambao  hupatikana kwa kiasi kikubwa katika hifadhi hii. Hifadhi hii ipo katika mkoa wa Iringa, hivyo kutoka Iringa mjini haadi getini, geti la hifadhi ni kilomita 100.

Kilichonisukuma niandike makala hii kuhusu hifadhi ya Ruaha ni sababu nyingi sana ambazo zinzvutia na ni za kipekee sana kuliko hifadhi nyingine zozote zilizopo Tanzania.

  1. Ukubwa wa Hifadhi yenyewe;

Hifadhi ya ruaha inahistoria yake ya kuvutia hadi kufikia kuwa hifadhi kubwa kuliko zote Tanzania na Afrika Mashariki, ikiwa na ukubwa wa eneo la kilomita za mraba takribani 20,226. Hifadhi hii ina eneo kubwa sana kuliko hifadhi zote Tanzania, na hivyo kuwa hifadhi ya kipekee yenye idadi kubwa ya makundi ya tembo, Nyati, pundamilia, twiga, simba, swala, nk.

  1. Historia Ya kuvutia ya Hifadhi hii

Hifadhi hii ya Taifa ya Ruaha ilianzishwa mwaka 1964 kwa kupandishwa hadhi eneo la hifadhi ya lililokuwa Pori la Saba ambalo lilianzishwa mwaka 1910. Kipindi ambacho kilikuwa chini ya utawala wa Wingereza. Jina la Hifadhi limetokana na neon la Kihehe “Luvala” likimaanisha mto Mkuu ambao ni Ruaha. Pia ukubwa wa eneo la Hifadhi hii ya Ruaha ilisababishwa na kuongezwa kwa eneo la Usangu kwenye Hifadhi ya Ruaha mnamo mwaka 2008, na kufanya kuwa hifadhi kubwa kuliko hifadhi nyingine Tanzania.

  1. Mto Ruaha Mkuu

Najua wengi wetu tunasikia sana habari za mto  Ruaha mkuu, kwa kusoma au kwa kusikia katika vyanzo mbali mbali vya habari. Hifadhi ya Ruaha inategemea sana maji kutoka katika mto mkubwa wa Ruaha, Mto huu ndio moyo wa hifadhi hii yenye viumbe adimu.  Hivyo basi kwa kuja kwako utaona maajabu ya mto huu unaosifika duniani kote kwa kuwanywesha maelfu ya Wanyama na ndege waliopo katika hifadhi ya Ruaha na maeneo mengine ya karibu. Inawezekana umewahi kutembelea hifadhi hii miaka ya nyuma  kipindi ambacho mto huu ulukuwa mwembamba, lakini kwa siku za hivi karibuni kutokana na mvua kuongezeka, mto huu umepanuka sana.  Njoo uone moyo wa hifadhi ya Ruaha.

  1. Darajani

Unapotembele Hifadhi ya Ruaha kupitia langu kuu yaani getini lazima utasima pale darajani, watu wengi na watalii wengi wanaotembelea hifadhi ya Ruaha wakifika darajani lazima wasimame kwanza, unajua kwanini wanasimama pale darajani? Nitakueleza kwa nini, kwasababu ya kwanza ni uwepo wa Mto Ruaha Mkuu, ambapo ndio daraja kubwa na refu sana. Chini ya daraja hili ndio utakuta mto huu mkuu umekatiza hapo, lakini maajabu ya hapa darajani ni kwamba kuna maji au bwawa ambalo lipo ndani yam to huu ambalo huifadhi idadi kubwa ya mamba na viboko. Hivy watalii wengi hupenda kusimama hapa na kuangalia mandhari nzuri na ya kuvutia sana chini yam to huu, utawaona viboko wamelala na mamba wametoka nje ya maji wakota jua zuri la asubuhi. Pia kuna miamba myeusi ndani yam to huu inayovutia wengi kupiga picha na kufurahia mandhari ya eneo hili. Kama ulitaka kuja Ruaha kuangalia Wanyama kama kiboko na mamba basi safari yako inaweza kuishia hapa darajani.

  1. Uwanja wa ndege,

Ndani ya Hifadhi ya Ruaha kuna uwanja wa ndege ambao unaruhusu baadhi ya ndege ndogo kutua katika eneo hili. Uwanja huu ambao kwa kiasi kikubwa umezungukwa na Wanyama wa aina mbali mbali kama vile swala, pundamilia na tembo, endapu utafika hifdhi ya Ruaha kwa ndege basi utafikiri hawa Wanyama walikuwa wanakusubiri kwa hamau ili wakupokee.

  1. Daraja la Kmaba

Ukifika hifadhi ya Taifa ya Ruaha usikubali kurudi bila kufika au kutembelea daraja la Kamba, hili ni daraja la ajabu sana, limetengenezwa kwa mbao chini na kushikizwa na kamba ngumu sana kiasi kwamba huwezi kukata hata kama ni mzito, daraja hili si tuu hutumika kama kivutio kwa watu, bali hutumika pia kama njia ya Wanyama kuvuka mto kipindi cha mvua, ambapo mto huo hutiririsha maji. Daraja hili linanesanesa na kukufanya ujisikie vizuri sana baada ya kufanya safari ndefu ukiwa umekaa ndani ya gari, ni sehemu pekee unaweza kushuka kwenye gari lako na kutembea kidogo, kupata hewa safi na kufurahia mneso wa Kamba hizo.

  1. Kipindi kizuri cha kutembelea Hifadhi ya Ruaha

Mara nyingi kwa watalii na watu wengine wanashauriwa kutembelea hifadhi ya Ruaha kipindi cha kuanzia May hadi kuendelea mwezi December. Kwenye kipindi hiki ndio utawaona Wanyama vizuri sana na pia ni kipindi kizuri sana kwa kusafiri kwa kutumia barabara za magari. Vipindi vingingine vya mwaka vinakuwa na hali ya mvua sana na barabara zinakuwa na shida kwenye usafiri. Vile vile hata uonekenaji wa Wanyama unakuwa wa shida.

Kuna mambo mengi sana ya kuandika kuhusu hifadhi ya Taifa ya Ruaha, lakini kwa hayo machache unaweza kuhamasika na kufanya safari ya kutembelea hifadhi ya Ruaha. Unaweza kutumia usafiri wako binafsi au ukatumia magari ya kitalii ili kutembelea hifadhi hii kubwa Tanzania.

Nakukaribisha sana Hifadhini;

Hillary Mrosso

0742092569

hillarymrosso@rocketmail.com

 

Shares:
Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *