Ujangili ni uwindaji haramu unaohusisha tendo la kuwinda wanyama, kukamata au kuua wanyama unaofanywa bila kibali au kinyume cha sheria za nchi husika. Ujangili hufanywa kwa sababu kadha wa kadha, pamoja na uhitaji wa ardhi kwa matumizi ya binadamu, uhitaji wa bidhaa adimu za wanyama kama vile meno ya tembo, manyoya, viungo, ngozi, mifupa, au meno huhesabika katika tishio la wanyama wengi kutoweka.
Ujangili ulianza katika miaka ya 1900 baada ya kuwepo kwa mifumo mingi ya utawala. Watawala wengi walimiliki maeneo makubwa yaliyosheheni aina mbalimbali za wanyamapori. Hata baada ya wanyamapori wengi kupungua watawala wengi waliamua kuendelea kusimamia haki zao za kuwinda wanyamapori wao wenyewe na familia zao za kitawala.
Mfumo huo wa kuwinda wanyamapori kwa familia za kitawala pekee uliletwa pia barani Afrika wakati wa ukoloni. Hata baada ya nchi nyingi barani Afrika kupata uhuru ziliweka sheria zilizolinda haki za wanyamapori pamoja na sheria na taratibu za uwindaji hivyo kupelekea kubana haki za wananchi kuwinda.
Hali hii ilipelekea ujangili hasa kwa wananchi waliokuwa na vipato vya chini kwa sababu walishindwa kumudu gharama za vibali vya uwindaji hivyo kukimbilia kufanya ujangili kwa lengo la kujipatia chakula na kuongeza kipato kupitia ujangili.
Ujangili umekuwa ni tishio kwa aina mbalimbali za wanyama hasa spishi ambazo baadhi ya viungo katika miili yao huwa na thamani kubwa sana.kwa mfano, tembo,faru na wanyama wengine pia kupelekea kutoweka kwa wanyama ambao hupatikana eneo moja na adimu kupatikana sehemu yoyote duniani.
Zipo sababu mbalimbali zinazopelekea ujangili nazo ni;

KULEGEZWA NA KUVUNJWA KWA SHERIA
Ujangili umekuwa ukiongezeka kwa kasi kwasababu ya kuvunjwa kwa sheria mbalimbali zinazolinda wanyamapori. Baadhi ya watumishi wa serikali wamekuwa si waaminifu na wamekuwa nyuma kusimamia sheria hizi zinazowalinda wanyama pori kwa sababu ni wanufaika wa moja kwa moja wa ujangili. Kwa mfano watu wanaosimamia sheria wamekuwa wakituhumiwa mara nyingi kwa masuala ya rushwa hivyo kupelekea usimamizi na utekelezaji mbovu wa sheria hivyo kupelekea watu wengi kutokuwa na hofu nakuendelea kujihusisha na masuala ya ujangili
BEI GHALI YA WANYAMA WAFUGWAO (PETS) NA SEHEMU YA VIUNGO VYA WANYAMA.
Soko haramu la wanyamapori ni soko ghali sana duniani. Watu huuza na kununua bidhaa ambazo ni wanyama, ndege,amphibia na reptilia na baadhi ya viungo vya wanyama vilivyo na thamani kubwa kama pembe za ndovu na pembe za faru kwa bei ghali sana. Hali hii hupelekea watu kujihusisha na ujangili kwa kufikiria faida kubwa watakayoipata endapo wakifanikiwa kuuza bidhaa zao.
IMANI POTOFU NA MATUMIZI KAMA DAWA.
Wanyama wengine huuliwa kutokana na imani potofu na wengine hutumiwa katika shughuli za kijamii kama sherehe. Vitu kama vile kwato, mikia, ngozi,manyoya,meno,vichwa,pembe na vinginevyo hutumika katika shughuli mbalimbali za kiimani.
Pia wanyama wengine kama vile faru huwindwa kwa imani kuwa pembe zao ni dawa ya kuongeza nguvu za kiume kwa kuwa faru hutumia muda mwingi kujamiana. Hili katika tafiti za kisayansi hakijathibitishwa kuwa na ukweli wowote ule.
MATUMIZI YA CHAKULA
Baadhi za wanyamapori kama pundamilia,simba,viboko,tembo,swala,nyoka,twiga,nyani na wengine wengi huliwa na jamii mbalimbali za watu barani Afrika. Huko bara la Asia vyakula vingi vitokanavyo na wanyamapori ni nyoka,kasa,popo,nyangumi na wengine.Vyakula hivi huuzwa ghali sana katika migahawa mikubwa iliyopo maeneo ya huko. Hivyo matumizi haya ya wanyamapori kama chakula huchochea na kusababisha ujangili kwa kiasi kikubwa
UKOSEFU WA MAKAZI NA KUTANUKA KWA MAENEO YA MAKAZI YA WATU.
Jumla ya idadi ya watu duniani inazidi kuongezeka na kukua kila siku na hivyo kupelekea watukuvamia maeneo ya hifadhi za wanyamapori ili kuanzisha makazi, kukuza miji na maeneo kwa ajili ya kilimo. Hii hupelekea wanyama kukosa sehemu ya makazi na hivyo kukosa chakula na hivyo kula mazao na mifugo na hivyo watu kuamua kuwaua kinyume cha sheria.
Shughuli hizi za ujangili huwa na madhara mbalimbali kwa wanyama wenyewe na wanaohusika katika kuwalinda kupitia hifadhi au maeneo tengwa ya wanyama.
KUTOWEKA KWA WANYAMA
Ujangili ni sababu kuu inayopelekea kutoweka kwa wanyamapori na wanyamapori wengine kubaki wachache sana, kwa mfano kati ya mwaka 2014-2017 zaidi ya tembo 100,000 waliuwawa kutokana na shughuli za ujangili kwa ajili ya kupata pembe zao na meno ya tembo. Pia faru wengi huuwawa kwa ajili ya kupata pembe zao na hii hupelekea kupungua kwa idadi ya wanyama hawa kwa kasi na hata kwa wanyama wengine hupotea kabisa.

KUPUNGUA KWA VUVUTIO VYA UTALII.
Watalii wengi hupendelea kutembelea katika maeneo yaliyo na vivutio vingi watakavyo vifurahia. Hivyo shughuli za ujangili hupunguza idadi ya watalii kwa sababu idadi ya wanyamapori pendwa kama faru na tembo kuadimika na kupotea kabisa katika baadhi ya hifadhi na hivyo kupelekea kutokuwa na vivutio vingi vya watalii na hivyo utalii kupungua katika hifadhi hizo na hivyo kupunguza pato la taifa liyolanalo na utalii.
KUSAMBAZWA KWA MAGONJWA.
Ulaji na matumizi ya wanyamapori huweza kupelekea kusambaa kwa magonjwa mbalimbali yatokanayo au kuambukizwa kutoka kwa wanyamapori na kuenda kwa wanadamu (zoonotic diseases) kama vile Ebola,Covid -19, mafua ya ndege na homa ya bonde la ufa. Magonjwa haya husambazwa na kuambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu baada ya matumizi ya wanyamapori hawa hasa kwa chakula. Na hii ni kutokana na wanyama hawa kuhifadhi vimelea vya magonjwa haya mwilini mwao(reserviors).
KUTOKUWA NA UWIANO KATIKA MFUMO WA KIIKOLOJIA.
Kila myama huwa na faida yake katika mfumo wa kiikolojia. Ili mfumo wa kiikolojia uwe sawa na imara inapaswa kuwepo ana uwiano wa wanyama wa aina zote.Wanyama wale walao wanyama (predators) na wale wanaoliwa(preys). Ujangili unapokithiri na kuathiri zaidi aina moja ya wanyama hupelekea kutokua na uwiano wa mfumo wa kiikolojia na hivyo kuweza kusababisha vifo zaidi kwa wanyama wengine.
VIFO VYA BINADAMU.
Majangili wengi huwauwa askari wa wanyamapori ili wao waweze kuingia na kufanya shughuli za ujangili kwa urahisi zaidi.Kutokana na ripoti ya “NATIONAL GEOGRAPHIC” inaonyesha zaidi ya askari wa wanyamapori 600 wameuliwa kutokana na shughuli za ujangili kwa mwaka 2009-2016. Pia katika nchi ya Jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo katika hifadhi ya taifa ya Virunga zaidi ya askari wa wanyamapori 170 waliuwawa kwa kwa wakati mmoja.
Kwa ujumla, baadhi ya wanyamapori wako katika hatari ya kutoweka duniani na hii ni kutokana na Ujangili. Nchini Tanzania wadau katika sekta ya wanyamapori wanaimarisha mikakati kadhaa kukomesha kadhia hiyo. Njia mbalimbali ambazo zinatumia kupambana na ujangili ni pamoja na kuihusisha jamii katika kupambana na ujangili kwa kuipa elimu juu ya umuhimu wa uhifadhi wa wanyamapori na madhara mengi yatokanayo na ujangili hivyo kuwa rahisi kwa raia kutoa taarifa kwa vyombo husika waonapo tukio la ujangili.
Pili, kuwapa mafunzo zaidi askari wa wanyamapori na wahifadhi kwa ujumla ili kuweza kukabiliana vizuri na tatizo la ujangili.
Tatu,kutunga sheria Kali zinazowalinda haki za wanyamapori na kusimamia utekelezaji wake kikamilifu.
Nne,kuweka mipaka kati ya maeneo ya hifadhi na maeneo ya watu wengine ili kuepuka migogoro ya wananchi kuvamia maeneo ya hifadhi.
Tano,kuwawekea vifaa vinavyoweza kuwafatilia wanyama( sensors and trackers) kwa wanyama hasa walio katika hatari ya kuwindwa na kupotea.
Na mwisho kabisa kuzivunja sheria na kutoruhusu biashara katika masoko ya kimataifa ambayo huwa ni kichochezi kikuu cha ujangili.TUUNGANE SOTE KUPINGA UJANGILI KWA MAENDELEO YA TAIFA NA KULINDA TUNU HIZI KWA VIZAZI VIJAVYO.
Cecilia Mwashihava
+255 747 268 217
Mhifadhi wanyama pori











Kaka uko vizuri sana, asante kwa ku share.
Asante sana Lowasa kwa feedback nzuri. Karibu tujifunze pamoja hapa