Habari msomaji wangu, karibu tena kwenye somo letu la kujifunza na kupata ufahamu kuhusu hifadhi za Taifa ambazo zinapatikana Tanzania, na leo tunaenda kuangalia moja kati ya hifadhi inazojulikana zaidi duniani, naamini kwa kiasi fulani utakuwa umewahi kusikia Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro, au umewahi kusikia kuhusu mlima Kilimanjaro. Hivyo basi tufuatane pamoja ili nikujuze mambo kadhaa muhimu ambayo yatakufanya uijue zaidi na pia upange kwenda kuitembelea hifadhi hii.

Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro ilianzishwa mwaka 1973, mwanzo ilijumuisha eneo lote la mlima na maeneo yote ya misitu ya mlima huu ambayo ni misitu ya akiba. Kutokana na shughuli nyingi za kibinadamu katika eneo hili kutishia uharibifu wa maingira ya hifadhi hii, hasa misitu ya milima hii ambayo imekuwa kama ndio inayozuia hifadhi hii kutoharibiwa. Kamati ya Dunia ya mambo ya Urithi iliridhia na kutaka eneo lote la Mlima Kilimanjaro pamoja na misitu yake kuwa hifadhi.

Mlima Kilimanjaro ni moja ya kati ya milima mikubwa duniani yenye volkano na vilele vyake kuwa na barafu, Mlima Kilimanjaro una vilele 3 vya volkano ambavyo ni Kibo, Mawenzi, na Shira vilele hivi vikiwa vimefunikwa na barafu nyeupe. Mlima kilimanjrao una hali nzuri sana ya hewa ambayo hupelekea kuwa na uoto wa aina nyingi sana, kama vile misitu mirefu na mikubwa na aina ya uoto wa kijangwa chini ya mlima huu mkubwa duniani. Ikumbukwe pia mlima Kilimanjaro ni mlima mrefu kuliko yote Afrika ambao umeinuka na kufikia mita 5895. ni mlima wenye kuvutia watu wengi sana kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Kutokana na uoto wa aina tofauti tofauti, hifadhi hii ya Kilimanjaro imekuwa ni kivutio kikuu hasa kwenye vilele vyake vyenye volkano kama vile Kibo, Mawenzi, na Shira, uoto unaobadilika kwa kadri unavyopandisha mlima pia umekuwa kivutio kwa wengi. Iko hivi rafiki kuanzia chini ya mlima jinsi unavyopandisha mlima huu na hali ya hewa inabadilika na pia uoto wake unabadilika, kutoka misitu minene hadi uoto wa nyasi nyasi za savanna, mpaka uoto wa nusu jangwa halafu hali ya ubarafu. Hii ni moja ya maajabu sana kwa mazingira ya mlima huu kuwa na hali yake ya hewa inayojitegemea ukilinganisha na hali ya hewa ya mkoa mzima wa Kilimanjaro.

Hifadhi hii ina vivutio vingi sana ukiachana na kivutio kikuu cha mlima Kilimanjaro, kuna mengi sana ya kuangalia unapotembelea hifadhi hii kuu ya Kilimanjaro, hivyo fuatana nami nikujuze hatua kwa hatua.

  1. Wanyamapori

Hifadhi hii ya ina wanayamapori wengi sana kutokana na hali ya hewa na pia sehemu ilipo hifadhi hii ina mwingiliano na hifadhi ya nchi jirani ya Kenya, hifadhi ya Amboseli, pia ina mwingiliano na hifadhi za Arusha na Tsavo iliyopo Kenya. Hali hii ndio husababisha mwingiliano mkubwa wa wanyama kutoka hifadhi moja kwenda nyingine na kufanya hifadhi hii ya Kilimanjaro kuwa na idadi kubwa sana ya wanyama mbalimbali.

  1. Ndege

Kama ilivyo kwa wanyamapori wengine kwenye hifadhi hii ya Kilimanjaro, ina idadi kubwa sana ya ndege wa kipekee ambao ni ndege walio lowea kwenye maeneo ya milima, mazingira mazuri ya kuvutia na hali nzuri ya hewa ndio kivutio kizuri zaidi kwa ndege wa aina mbali mbali wanaopenda kuishi sehemu zenye milima na sehemu zenye baridi. Hadi sasa spishi zaidi ya 179 za ndege zipo maeneo haya ya hifadhi ya Mlima Kilimanjaro.

  1. Vilele vitatu vya mlima vilivyofunikwa na barafu

Kitu kingine kinachofanya mwonekano mzuri wa hifadhi hii ni vilele vya Kibo, Mawenzi na Shira, ambavyo huonesha uzuri wa mlima huu mrefu kuliko yote barani Afrika, pia kilele cha kibo kina vilele vingine viwili ambavyo ni Stala na Girman, ambavyo navyo vimefunikwa na barafu. Hii ndio sababu wageni wengi hupenda kutembelea hifadhi hii na kupanda mlima Kilimanjaro. Hivyo nakujuza mambo mazuri ambayo yapo Tanzania pekee, karibu sana Kilimanjaro.

  1. Maundi kreta

Ndio ni kreta, licha ya kuwa na Ngorongoro kreta katika nchi yetu ya Tanzania, tuna kreta nyingine katika hifadhi hii ya Kilimanjaro, kreta hii ipo mlimani urefu wa mita 2700 kutoka usawa wa bahari. Hii ni sehemu nzuri sana kwa kupiga picha kutokana na muonekano na mandhari nzuri ya eneo hili la kreta ya Maundi. Hivyo ukitembelea hifadhi hii utafaidika na kufurahia vivutio vingi sana ambavyo huwezi kuviona sehemu nyingine.

  1. Ziwa Chala

Ziwa hili lipo upande wa Magharibi mwa hifadhi hii nzuri, ni ziwa ambalo limesababishwa na mgandamizo wa volkano, yani ni kaldera, ambapo limejaa maji mengi sana, katika ziwa hili linalosifika kwa kuwa na mamba wengi, hivyo huwezi kuogelea ndani ya ziwa hili. Kwa wale wanaopenda kuona viumbe hai wanaoishi majini, hapa ndio sehemu nzuri sana ya kuwaona mamba na viumbe wengine wanaoishi majini.

  1. Uoto wa kipekee

Hifadhi hii kwa kiasi kikubwa uoto wake ni wa kipekee kutokana na hali ya hewa ya kipekee inayotengenezwa na uwepo wa Mlima Kilimanjaro pamoja na milima mingine ya jirani, ndio imesababisha eneo lote la hifadhi hii kuwa na uoto wa kipekee sana, miti na nyasi zake zitakushangaza sana. Watafiti wengi wa mambo ya miti na mimea huja eneo hili kwa ajili ya kijifunza kuhusu uoto huu wa kipekee kwenye hifadhi hii. Njoo ujionee mwenyewe.

  1. Hali ya hewa (Climate)

Hali ya hewa kwenye hifadhi hii mara nyingi na wakati wote ni baridi sana, watafiti wa mambo ya hali ya hewa wanasema unapopanda Mlima Kilimanjaro unakutana na hali za hewa za aina tano tofauti, yani kwa kadri unavyopanda mlima hali ya hewa inabadilika na kuwa nyingine tofauti na hali ya kwanza. Hivyo wageni wanaotaka kupanda mlima wanatakiwa kujiandaa kwa mavazi vifaa na ushauri namna ya kuupanda Mlima Kilimanjaro.

Haya ndio mambo machache kati ya maengi ambayo unaweza kuyapata na kuyaona unapotembelea hifadhi za Taifa hasa hifadhi ya Kilimanjaro. Ni moja ya hifadhi zenye idadi kubwa sana za wageni kutoka nchi mbali mbali, na pia ni moja kati ya hifadhi zinazopendwa na kujulikana zaidi duniani. Hivyo panga namna unavyoweza kutembelea hifadhii hii ujionee mwenyewe mambo ambayo ulikuwa unajifunza na kusoma tu shuleni. Karibu sana katika hifadhi hii ya Kilimanjaro.

Ahsante sana kwa kusoma makala hii, nakutakia kila la kheri kwenye maandalizi yako ya kutembelea hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro.

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

0742092569/0683248681

Hillarymrosso@rocketmail.com