Uhifadhi wa wanyamapori una faida nyingi kuliko hasara wanazosababisha wanyamapori. Uwepo wa wanyamapori katika maeneo yao unaleta faida nyingi za kimazingira, kiuchumi, kitamaduni na kijamii. Endapo wanyamapori wataendelea kuwepo kwenye maeneo yao ya asili itasaidia sana kuimarisha mifumo ya kiikolojia ambayo ni muhimu sana kwa kukuza uchumi wa nchi husika kwa njia ya utalii.

Nchi nyingi, hasa zilizopo kusini mwa Jangwa la Sahara zina rasilimali nyingi za wanyamapori ambazo zinahitaji juhudi kubwa za pamoja katika uhifadhi wake. Hata hivyo, serikali za nchi hizi zenye wanyamapori zimejitahidi kuweka sheria na miongozo mbali mbali ya uhifadhi wa wanyamapori na mazingira yake asilia. Lakini kutokana na hali za kiuchumi za nchi hizi kuwa duni, imepelekea maeneo mengi ya uhifadhi wa wanyamapori kukabiliwa na changamoto nyingi za kiuhifadhi.

Changamoto nyingi zilizopo katika nchi za Afrika zina madhara makubwa sana katika kuwepo kwa uhifadhi endelevu, mfano, tafiti nyingi zinaonyesha nchi hizi zinakabiliwa na umasikini, kipato duni, magonjwa, rushwa, vita, siasa duni, mabadiliko ya matumizi ya ardhi, na athari za mabadiliko ya tabia nchi. Changamoto hizi na nyingine zimetajwa sana na watafiti kuwa zinachangia kuzorota kwa uhifadhi endelevu wa wanyamapori na kupelekea kushamiri kwa vitendo vya ujangili na biashara haramu za wanyamapori.

Kuwepo na kushamiri kwa ujangili na biashara haramu ya wanyamapori na nyara zake imekuwa ni tishio jingine kubwa katika uhifadhi, hii ni kwasababu ujangili na biashara haramu za wanyamapori una gharama kubwa sana kiuchumi, kimazingira na kijamii. Watafiti wa masula ya uhifadhi na mwenendo wa biashara haramu wanasema, kusamiri kwa ujangili kwenye ukanda huu wa Afrika kunaleta tena kukosekana kwa usalama, usawa na uimara katika tasnia ya uhifadhi wa wanyamapori.

Licha ya umuhimu wa wanyamapori na uhifadhi kwa ujumla, bado kumekuwa na kutofautiana kimawazo, kimatendo na kihisia linapokuja suala la uhifadhi wa wanyamapori. Watu kujihusisha na ujangilii na biashara haramu za wanyamapori kunaweza kutupa kujua mitazamo ya watu kuhusu uhifadhi na wanyamapori. Hivyo, tafiti za kina zinahitajika ili kubaini kwa kina sababu gani hasa zinasababisha watu kuingia kwenye ujangili na biashara haramu za wanyamapori.

Hata hivyo, nimebahatika kukutana na utafiti wa hivi karibuni wa Roz Price alioufanya mwaka 2017. Roz kwenye utafiti wake ameeleza kwa kina sababu za watu kuingia kwenye ujangili na biashara haramu. Moja ya mambo muhimu aliyoyataja katika utafiti wake nimekushirikisha kupitia makala hii. Hivyo, makala hii imejaa taarifa za kina zilizofanyiwa tafiti za kina. Karibu tujifunze pamoja kupitia makala hii muhimu.

Picha hii ikionyesha nyamapori zikiwa zimevunwa kwa njia haramu; Picha hii imetolewa kwenye mtandao wa https://www.africa.com

Baadhi ya sababu zinazopelekea watu kuingia kwenye ujangili na biashara haramu za wanyamapori

1.Umasikini;  kuna uhusiano mkubwa sana kati ya ujangili wa wanyamapori na umasikini; jamii nyingi zinazoishi kando ya hifadhi za wanyamapori zina kipato duni, hakuana ajira za kudumu na pia wanapata wakati mgumu kutimiza mahitaji yao muhimu kama vila chakula, afya, mavazi na mahitaji mengine ya familia. Hivyo kwasbabu ya ukosefu wa njia za kuingiza kipato na kukidhi mahitaji muhimu ya kimaisha watu wengi wanaoishi kando ya hifadhi za wanyamapori wameingia kwenye ujangili na biashara haramu za wanyamapori, lengo ikiwa ni kumudu gharama muhimu za maisha.

2.Kuongezeka kwa matumizi na mahitaji ya wanyamapori; kwa miaka ya hivi karibuni, wanyamapori wamekuwa na matumizi mengi sana hasa katika nchi za Asia kama vile China. Uhitaji wa nyara umekuwa mkubwa sana hivyo wengi wameingia kwenye ujagili na biashara haramu kwa ajili ya kutimiza mahitaji hayo. Hata hivyo,  kumekuwa na taarifa nyingi kwenye miji inayoendelea kuwa na uhitaji mkubwa wa nyamapori na mazao mengine ya wanyamapori kwa mahitaji mbali mbali kama vila chakula, urembo nk. Tafiti pia zinaonyesha kuongezeka kwa kipato kwa jamii nyingi za watu wa Asia, kuimarika kwa miundombinu ya usafirishaji kumechangia sana kushamiri kwa biashara haramu za wanyamapori. Mfano, karibia asilimia 67 ya nyara za meno ya tembo zilizokamatwa huko Asia, asilimia 33 zilinatoka Afrika, huku asilimia 80 ya nyara hizo zikiwa zinatoka katika nchi za Afrika Mashariki. Ilikadiriwa kuwa kutokana kupanda kwa vipato kwenye kaya za watumiaji wa wanyamapori katika nchi za Asia, ingehitajika zaidi ya tembo 163,000 kuuwawa ili kukidhi mahitaji ya jamii hizo kwa mwaka 2022.

3. Kupanda kwa bei ya mazao ya wanyamapori au nyara; nyara za wanyamapori zimepanda sana bei, kiasi cha kuvutia watu kuingia katika biashara hii haramu, mfano bei ya pembe ya faru ilikuwa dola za kimarekani 4,700 (sawa na zaidi ya shilingi milion kumi na moja za kitanzania, kwa bei ya sasa ya dola) kwa kilo mwaka 1993, lakini kufikia mwaka 2012 pembe ya faru ilikadiriwa kufikia dola za kimarekani 65,000 (sawa na zaidi shilingi milioni mia moja na sitini na mbili za kitanzania, kwa bei ya sasa ya dola) kwa kilo. Kupanda kwa bei ya meno ya tembo kwa nchi za Japani na China inaonyesha bei ya jino la tembo lenye uzani wa kilogram moja liligharimu dola 100 za kimarekani, sawa na zaidi ya shilingi laki mbili na nusu za kitanzania kwa mwaka 1990, lakini kufikia mwaka 2007 jino lenye uzani wa kilogramu moja liligharimu dola 750 za kimarekani, ambazo ni sawa na zaidi ya shilingi milioni moja na laki nane za kitanzania. Kushamiri kwe biashara haramu ni matokeo ya faida kubwa inayopatikana katika biashara hizi, hata hivyo, kuna shaka kuwa bei ya nyara hizi inaweza kuwa kubwa zaidi ya hiyo iliyoandikwa kwasababu ya uendeshaji wa biashara hii haramu na upatikanaji wa taarifa za kina kuhusu biashara hii ni ngumu.

4. Kukosekana kwa njia mbadala za kuingiza kipato; maisha ya watu wengi wanaoishi vijijini au karibu na maeneo yenye rasilimali za wanyamapori hayana shughuli nyingi za uzalishaji na upatikanaji wa kipato. Ujangili na biashara haramu ya mazao ya wanyamapori inakuwa ndio fursa inayoleta fedha haraka, hivyo wengi ni rahisi kuingia kwenye ujangili kwa lengo la kupata kipato cha haraka. Mfano, nchini Zambia wanaojihusisha na ujangili wanaweza kupata hadi zaidi ya dola 100 za kimarekani ambazo ni sawa na shilingi laki mbili na nusu za kitanzania kwa kuwinda mara moja. Kwa kaya nginyi masikini hii ni pesa nyingi sana ambayo husaidia mambo mengi ya kifamilia. Taarifa za ujangili kutoka sehemu nyingine za Afrika kama Namibia zinaonyesha kuwa wanaojihusisha na ujangili wanaweza kupata zaidi ya mara tatu au tano ya mapato yao kwa mwaka kupitia shughuli za ujangili. Hivyo, endapo kutakosekana ajira wengi wataingia kwenye ujagili na biashara haramu za wanyamapori. Tafiti nyingine zinaonyesha shughuli za ujangili zinapungua sana kipindi cha kilimo, ambapo wengi wana kazi nyingi za kufanya.

5.Historia ya ukoloni; watu wanaoishi karibu na maeneo ya wanyamapori wamepitia mengi ambayo yanawafanya waishi kwa kinyongo, huzuni, chuki na hasira dhidi ya wanyamapori, na mamlaka za usimamizi wa wanyamapori. Watu hawa wana machungu kutokana na historia ya kutengwa, kunyang’anywa aridhi yao, mashamba yao na haki zao za kutumia rasilimali zinazowazunguka kama vile wanyamapori. Pamoja na hayo, kumekuwa na ukatili na matumizi ya nguvu kupitiliza kutoka kwa askari wa wanyamapori, wanyamapori kuharibu mazao na mali za watu bila hata kupata fidia au kifuta machozi, faida ndogo na wakati mwingine hakuna faida zinazoenda kwenye jamii kutokana na mapato ya uhifadhi wa wanyamapori walio karibu na jamii. Kutokana na kukosekana uhusiano mzuri kati ya hifadhi za wanyamapori na jamii, imesababisha wengi kuingia kwenye ujangili kama kulipiza kisasi au kukomoana. Mfano, kwenye utafiti wa Harison wa mwaka 2015 unaonyesha kuwa maeneo mengi ya hifadhi za wanyamapori ya nchi ya Uganda yalikuwa ni maeneo na makazi ya asili ya baadhi ya kabila kama vile Batwa, Batooro ambayo yalikuwa ni makazi ya watu yaliyogeuzwa kuwa hifadhi za taifa. Hata hapa Tanzania, mifano ni mingi kuanzia upanuzi wa hifadhi ya Taifa ya Ruaha na maeneo mengine yameshuhudia watu kuhamishwa na kupisha eneo la hifadhi ya wanyamapori.

6. Siasa duni na vita; tafiti zinaonyesha kuwa maeneo yenye changamoto nyingi za kisiasa kama vile vita vya wenyewe kwa wenyewe, au matishio mengine ya kigaidi kumekuwa na ongezeko la vitendo vya ujangili kwenye maeneo hayo, mfano, nchini Zimbabwe vitengo vya ujangili vimeripotiwa kushamiri kipindi cha vita zaidi na kusababisha kupungua kwa idadi kubwa ya wanyamapori kama tembo. Kuna mfano mwingine upande wa Kaskazini Magharibi mwa Tanzania, uwepo wa kambi ya wakimbizi karibu na maeneo ya hifadhi ya wanyamapori imeripotiwa kusababisha kushamiri kwa vitendo vya ujangili kupita kiasi. Wakimbizi waliokimbia nchi zao kutokana na vita wakiweka kambi karibu na maeneo yenye rasilimali muhimu kama za wanyamapori wanaweza kuvamia maeneo hayo na kusababisha kushamiri kwa ujangili wa nyamapori na biashara za mazao ya wanyamapori. Katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, imeripotiwa katika kipindi cha vita na migogoro ya kisiasa ujangili uliongezeka sana na kusababisha kupungua kwa idadi ya tembo 22,000 sawa na asilimia 90 ya kupungua kwa wanyamapori mwaka 2013. Hivyo, mapigano na vita vya wenyewe kwa wenyewe katika baadhi ya nchi za Afrika kumesababisha kushamiri kwa ujangili kwa wanyamapori.

7. Rushwa; rushwa imekuwa kama mafuta, kama vile hewa ya oksijeni katika kuchochea vitendo vya ujangili na biashara haramu ya wanyamapori. Uchunguzi wa kisanyansi umebaini kuwa baadhi ya mazao ya wanyamapori kama meno ya tembo yanayouzwa na kukamatwa sehemu mbali mbali duniani yanaonyesha meno hayo yemetoka katika ghala za serikali. Mwandishi amebainisha kuwa hakuna namna inawezekezana kuuza nyara za serikali bila kuwpo kwa rushwa. Rushwa inawafanya baadhi ya askari wa wanyamapori kujiusisha na kusaidia vitendo vya ujangili, rushwa imesadia sana katika usafirishaji wa mazao ya wanyamapori,  baadhi ya watu kwenye vitengo vya ukaguzi na usimamizi wanapokea sana rushwa ili kuruhusu nyara au mazao mengine ya wanyamapori kusafirishwa bila tabu yoyote. Ruhswa imetumika kugushi vibali ili biashara haramu ionekani ni biashara halali sehemu nyingi duniani, rushwa ni tishio kubwa sana kwenye uhifadhi endelevu wa maliasili zetu. Tatizo hili la rushwa lisipotatuliwa tutakuwa na wakati mgumu sana kudhibiti ujangili na biashara haramu ya wanyamapori.

8. Udhaifu katika usimamizi wa sheria; maeneo mengi mamlaka za usimamizi wa wanyamapori zinapata wakati mgumu sana katika kutekeleza majukumu yao kutokana na vipaumbele vya serikali zao. Nchi nyingi za Afrika zinakabiliwa na changamoto nyingi za kiuchumi, hivyo vipaumbele vya uwekezaji vinatofautiana na mara nyingi sio uhifadhi wa wanyamapori utapewa vipaumbele hivyo. Maeneo mengi hakuna vitendea kazi vya kutosha kwa wasimamizi wa wanyamapori, pia hata wakikamata watuhumiwa wa ujangili mara nyingi hakuna ushahidi wa kutosha wa kumtia mtu hatiani kutokana na kutokuwa na namna nzuri ya kusimamia kesi za aina hii. Hata hivyo, sheria nyingi za usimamizi wa wanyamapori zinatoa faini na adhabu kidogo kulingana na ukubwa wa kosa. Uimara na utekelezaji wa sheria za usimamizi bado ni changamoto kubwa sana katika ukanda huu wa kusini mwa Jangwa la Sahara. Endapo juhudi kubwa zitawekwa kuwezesha na kusaidia katika kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa sheria hii itasaidia sana kuboresha sekta hii muhimu ya wanyamapori.

9.Jamii kukosa haki ya umiliki na usimamizi wa wanyamapori; kwa miaka mingi, jamii zilizo kando ya hifadhi za wanyamapori hazijapata faida kutokana na rasilimali zinazowazunguka. Hata hivyo, serikali za nchi zenye rasilimali hizi zilijitahidi kuanzisha uhifadhi shirikishi kwa kuanzaisha maeneo ya usimamizi wa wanyamapori ambayo yanatokana na jamii kutoa baadhi ya maeneo yao ya vijiji na kuunda jumuiya ya pamoja ya uhifadhi, maarufu kama Wildlife Management Areas, WMA. Lengo ni kuishirikisha jamii katika uhifadhi na jamii ione na kupata faida kutokana na uwepo wa rasilimali zinazowazunguka. Tafiti zinaonyesha maeneo haya ya hifadhi ya jamii, ukiachana na yale ya Namibia, bado hayajafanikiwa na kufikia malengo ya kuanzishwa kwake. Mfano mzuri ni hapa Tanzania, Tanzania ilijitahidi sana kuunda WMA nyingi, zaidi ya 38, lakini ufanisi wake haujafikiwa, na jamii zinalalamika kutoona faida za uwepo wa hizi WMA,  wengine wanadai kurushiwa maeneo yao ili walime na kuchungia mifugo yao. Kutokana na hali hii ujangili kwenye maeneo haya ni mkubwa, na pia kukosekana kwa usimamizi wenye tija kwenye maeneo haya, mengi yamebakia kama mapori tu yasiyo na faida.

Ngudu msomaji wa makala hii, hizi zinaweza kuwa sababu zinazochochea ujangili na biashara haramu ya wanyamapori katika ukanda huu wa Afrika. Mwandishi anasema sababu hizi zinatofautiana kulingana na nchi husika, lakini kwa kiasi kikubwa tafiti zinaonyesha nchi zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara zina changamoto nyingi zinazofanana, kama zilizoainishwa katikama makala hii.

Pamoja na hayo, mwandishi amekiri kuwa ujangili unaweza kuwa na matokeo chanya ya muda mfupi kwa jamii zinazozunguka maeneo ya wanyamapori. Mfano,  nchini Uganda ambako baadhi ya jamii hujihusisha na ujangili kwa ajili ya kukidhi mahitaji muhimu ya maisha kama vile kusomesha watoto na kugharamia gharama za matibabu. Amebaini kuwa faida za ujangili zinaweza kuwa sehemu ya kuvunja mzunguko au mnyororo wa umasikini kwenye familia endapo jangili hatakamatwa. Fikiria kama jangili atafanya ujangili na biashara haramu ya wanyamapori, halafu faida anayopata atasomeshea watoto wake, maana yake watoto wakisoma na kupata kazi hawawezi kuja kujiunga na shuhuli za ujangili kama wazazi wao.

Hivyo, kuna haja ya kuzisaidia jamii hizi hasa kwenye mahitaji muhimu ya kifamilia na kimaisha kama vile ada za watoto shuleni, gharama za matibabu, na wakati mwingine kuwatafutia wazazi namna nyingine ya kuingiza kipato tofauti na kufanya ujangili na biashara haramu za wanyamapori. Kwa kutoa mbadala wa shughuli za kipato utasaidia sana watu na wanyamapori kusitawi, hatimaye tuwe na uhifadhi endelevu.

Kingine, tunatakiwa kuwekeza vya kutosha kwenye hifadhi tulizoanzisha kwa ajili ya uhifadhi wa wanyamapori. Maeneo mengi ya wanyamapori yanatumika kidogo, hasa kwa namna yanavyochangia kipato. Ikumbukwe kuwa kama hakuna juhudi za kuwekeza na kufanya maeneo haya ya hifadhi za wanyamapori kuzalisha itatuwia vigumu sana hata kuyahifadhi. Tunahitaji fedha na vifaa kwa ajili ya uhifadhi wa wanyamapori na mazingira yao, na chanzo kikuu cha mapato ni hifadhi hizi, hivyo tupambane kuhakikisha maeneo haya yanatoa faida, ili watu na wanyamapori wote vifanikiwe.

Asante kwa kusoma makala hii, usiache kuwashirikisha wengine pia,  ukiwa na maoni ushauri na mapendekezo, usisite kuwasiliana na mwandishi wa makala hii kwa anuani hapo chini.

Hillary Mrosso, hmconserve@gamil.com, +255 683 862 481

Shares:
Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *