Habari za siku ndugu wasomaji wa makala hizi za wanyamapori. Poleni na hongereni kwa majukumu ya kila siku lakini pia kwa kupata muda wa kusoma makala hizi kwani napata mrejesho na maswali mengi kuhusu wanyamapori hasa kutokana na maelezo ambayo watu hupata kupitia makala hizi. Leo ni siku nyingine tena tunaingia darasani kujifunza kuhusu wanyamapori hivyo kama ilivyo kawaida yetu tutajifunza mambo mengi sana kuhusu wanyamapori. Makala ya leo nitazungumzia kuhusu NDEGE kwani viumbe hawa kwa asilimia kubwa ni kama wamesahaulika sana hapa nchini ukilinganisha na wanyama wengine. Makala ya leo tutajikita zaidi kujua kitu kinaitwa UKOMO au kwa lugha ya kingereza hufahamika kama ENDEMISM. Hapa hasa tutaangalia kwa upande wa ndege wapatikanao nchini Tanzania tu na si kwingineko duniani.

UTANGULIZI

Katika uainishaji wa viumbe hai, ndege ni jamii ya viumbe hai wapatikanao kwenye himaya ya wanyama katika kundi au faila ya viumbe wenye ugwe/uti wa mgongo na ngeli ya ndege. Ni viumbe wapatikanao maeneo mbali mbali hapa duniani hasa kutokana na uwezo wao mkubwa wa kustahimili hali ya hewa na mabadiliko mbali mbali ya tabia ya nchi.

Kutokana na tafiti zilizo fanyika mwaka 2021 na shirika la IUCN inaonesha kuwa kwa sasa duniani kuna spishi za ndege zipatazo 9,000-11,000. Spishi hizi zimeenea maeneo mbali mbali hapa duniani na kuna baadhi hupatikana maeneo machache tu. Ueneaji huu wa ndege katika maeneo mbali mbali ndio ulio nisukuma kukuandalia makala hii ndugu msomaji wa makala hizi za wanyamapori.

Ndege wamegawanyika katika makundi mbali mbali kutokana na mifumo tofauti ya maisha yao hususani chakula na uhamaji. Wapo ambao wanakula nyama mfano wa ndege jamii ya tai, lakini wapo ambao wanakula punje, wengine wanakula kwenye maua n.k. Pia kuna ndege ambao wao huishi kwa kuhama hama kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyinge. Kuhama huku hutokana na sababu mbali mbali kama kuzaliana lakini pia mabadiliko ya hali ya hewa kutoka sehemu zenye baridi kwenda zenye joto au zenye joto kwenda zenye baridi.

UKOMO (ENDEMISM)

Neno ukomo kama linavotumika kwenye lugha ya kingereza (endemism) ni neno ambalo hutumika sana kwenye sayansi na lina maana kubwa sana. Ukomo katika viumbe hai lina maanisha ni upatikanaji wa baadhi ya viumbe hai katika eneo fulani na huwezi kuwapata katika maeneo mengine tofauti ha eneo hilo. Ukomo huu huanzia katika mabara hadi ndani ya nchi husika, na hapa katika nchi husika basi hufika hadi ngazi ya mikoa au hata wilaya. Hivyo unaweza kukuta kuna ndege ambao wanapatikana eneo moja tu (bara, ukanda, nchi, mkoa au wilaya) dunia nzima na hiyo ndo tafsiri kuu ya neno ukomo.

Katika makala hii ya leo nakuletea spishi za ndege ambao wanapatikana nchini Tanzania tu na si kwingineko duniani.

Kuna takribani spishi arobaini na zaidi za ndege ambao wanapatikana nchini Tanzania tu na si sehemu nyingine yoyote hapa duniani. Ndege hawa pia wamegawanyika na wanapatikana kutokana na maeneo mbalimbali hapa nchini kwani kuna ambao wanapatikana maeneo ya kaskazini, kusini, mashariki na magharibi mwa nchi. Hii ni kutokana na uwepo wa mazingira rafiki kwa spishi husika lakini pia upatikanaji wa chakula ambacho ni pendwa na maalumu kwa spishi husika.

Basi kwa uchache na umakini zaidi nitakuchambulia ndege mmoja baada ya mwingine bila kusahau maeneo wapatikayo ndege hao hapa nchini.

  1. Zuwanende wa Usambara (Usambara Akalat)

Hawa ni ndege wadogo wenye rangi ya kahawia wenye mikia yenye rangi ya kutu lakini shingo zao zina manyoya yaliyo pauka au kushabihiana na rangi nyeupe. Sifa pekee ya ndege hawa ni uwepo wa alama ya kiraka iliyo pauka kati ya jicho na mdomo.

Ufuatiliaji wa ndege hawa kwa mara ya mwisho ulifanyika na kuchapishwa 31/3/2021. Ndege hawa wanapatikana maeneo machache sana (kati ya maeneo 2-5) magharibi mwa milima ya Usambara ambayo ina muinuko kati ya mita 1,600 hadi 2,200 kutoka usawa wa bahari.

Idadi ya ndege wakubwa ambao tayari wanauwezo wa kuzaa inakadiriwa kuwa 2,500-9,999 huku idadi yao ikiendelea kupungua kwa kasi kubwa sana. Hii hii imepelekea ndege hawa kuwekwa katika kundi la viumbe ambao wapo hatarini kutoweka duniani. Sababu kubwa ya kupungua kwa ndege hawa ni uharibifu wa mazingira hasa ukataji wa misitu kwani maisha yao hutegemea misitu sana.

Zuwanende wa Usambara (Picha na eBird.org)

2.Zuwanende wa Iringa (Iringa Akalat)

Kama zilivyo jamii nyingine za zuwanende, zuwanende hawa wana miili midogo wenye rangi ya kahawia na nyusi fupi. Ndege wadogo wana Manyoya mengi katika miili yao ukilinganisha na wakubwa.

Hawa ni miongoni mwa ndege ambao wanaishi sehemu moja (hawa hami hami) hivyo ni rahisi sana kuwaona katika mazingira yao asilia. Ndege hawa wanapatikana katika misitu michache sana ipatikanayo katika safu za milima ya Ukaguru, Udzungwa na maeneo ya nyanda za juu kusini wilayani Njombe ambapo maeneo haya yana muinuko wa mita kati ya 1,350 hadi 2,500 kutoka usawa wa bahari.

Idadi ya ndege hawa inakadiriwa kuwa 6,000-15,000 japo tafiti zinaonesha kuwa idadi ya ndege hawa pia inapungua. Miongoni mwa changamoto zinazo pelekea kupungua kwa ndege hawa ni uharibifu wa mazingira utokanao na ufugaji holela, uvunaji wa magogo na kuni lakini pia mabadiliko ya tabia ya nchi. Hii imepelekewa ndege hawa kuwa katika kundi la viumbe walio kwenye mazingira magumu.

Zuwanende wa Iringa (Picha na Birds of the World)

3.Mkesha wa Usambara (Usambara Trush)

Hawa ni mkesha asili ambao wana rangi ya kahawia sehemu ya chini. Rangi hii ukiitazama vizuri ni mjumuisho wa rangi mbili ambazo ni rangi kama ya kahawia chafu na kijivu iliyo pauka. Wana sura zilizo fifia, midomo yenye rangi ya manjano huku maeneo ya shingoni wana alama ya mistari. Hawa ni miongoni mwa ndege wenye aibu sana.

Tafiti kuhusu ndege hawa zilifanyika mara ya mwisho mwaka 2016 na kuonesha ndege hawa wanapatikana kaskazini mwa milima ya Upare na Usambara. Idadi halisi ya ndege hawa bado haijafahamika japo tafiti zinaonesha kuwa ndege hawa pia wanapungua na kupelekea kuwa miongoni mwa viumbe ambao wanakaribia kuingia kwenye tishio la kutoweka. Ndege hawa maeneo yao asilia ni kwenye misitu lakini mara chache pia huonekana katika maeneo yenye misitu iliyo haribiwa. Miongoni mwa sababu zinazo pelekea kupungua kwa idadi ya ndege hawa ni uvamizi wa watu katika maeneo ya misitu hasa kwaajili ya kilimo na uvunaji wa kuni.

Mkesha wa Usambara (Picha na Tanzania Bird Atlas)

4. Zuwanende wa Rubeho (Rubeho Akalat)

Zuwanende hawa wana rangi ya kahawia sehemu ya juu, taji lenye rangi ya mzaituni au kahawia, huku sehemu ya chini wakiwa na rangi ya machungwa iliyo changanyikana na kahawia. Ndege hawa huishi kwa upweke lakini wakati mwingine huonekana wakiwa wali (jike na dume).

Mpaka kufikia mwaka 2017, idadi ya ndege hawa haikuweza fahamika japo ni ndege waliyo hatarini kutoweka duniani. Ndege hawa wanapatikana maeneo ya milima ya Wota, kaskazini magharibi mwa Rubeho, milima ya Ukaguru na mlima Kiboriani ambapo maeneo haya yanapatikana katika muinuko wa mita 1,600 hadi mita 2,400 kutoka usawa wa bahari. Japo kuna tafiti nyingine imeripoti kuonekana kwa ndege hawa katika muinuko wa mita 400 kutoka usawa wa bahari kaskazini mashariki mwa milima ya Uluguru.

Japo ndege hawa wanapatikana katika moja ya tao kubwa ya milima ambayo ni tao la milima ya mashariki, bado wanakabiliwa na changamoto mbali mbali ambazo zinapelekea idadi yao kupungua. Miongoni mwa changamoto hizo ni ukataji wa miti kwaajili ya kilimo, uvunaji wa kuni na ukataji wa magogo hasa kwaajili ya mbao.

Zuwanende wa Rubeho (Picha na eBird)

5. Kinengenenge wa Pemba (Pemba White-eye)

Kinengenenge wa Pemba ni ndege wadogo wenye midomo mikali na rangi ya njano inayo ng’aa sehemu ya chini. Mgongoni wana rangi ya mzaituni iliyo changanyikana na njano na mstari mwembamba mweupe ambao umelizunguja jicho.

Ndege hawa wanapatikana katika visiwa vya Pemba tu na wanapatikana karibu maeneo yote kama vile kwenye bustani, vichaka, maeneo ya mashamba, sehemu zenye miti na maeneo ya misitu. Tafiti zilifanyika kwa mara ya mwisho mwaka 2016 kufuatilia ndege hawa, japo idadi yao haijajulikana kwa ufasaha lakini inaonekana ni ndege ambao bado wapo wa kutosha katika visiwa hivyo vya Pemba.

Kinengenenge wa Pemba (Picha na Tanzania Bird Atlas)

6. Kinengenenge wa Kilimanjaro (Kilimanjaro White-eye)

Kinengenenge hawa wanataka kufanana na wale wa Pemba japo utofauti wao ni duara jeupe kwenye jicho. Kinengenenge hawa wana mstari mweupe mnene uliozunguka jicho tofauti na wale wa Pemba ambao wana mstari mwembamba na unaweza kuwatofautisha hata kwenye picha.

Kwa mara ya mwisho ndege hawa walifanyiwa utafiti mwaka 2016 na wanapatikana maeneo mbali mbali hapa nchini kama kaskazini mashariki mwa Tanzani, maeneo ya nyanda za juu kusini hasa Iringa na baadhi ya maeneo moani Morogoro. Idadi halisi ya ndege hawa bado haijafahamika japo inaonekana ni ya kuridhisha kwani bado wanaonekana kwa urahisi na katika namba nzuri tu. Japo idadi inakadiriwa kupungua kutokana na uharibifu wa mazingira ya ndege hawa.

Maeneo wanayo patikana ndege hawa hawa huwa yana muinuko wa mita 1,380 hadi mita 3,400 kutoka usawa wa bahari.

Kinengenenge wa Kilimanjaro (Picha na eBird)

7. Kinengenenge wa Upare (South Pare White-eye)

Hawa ni miongoni mwa kinengenenge wenye midomo mikali ambao wana manyoya yenye rangi ya njano shongoni lakini pia yaliyo wazi kidogo tofauti na wale wa Kilimanjaro. Baadhi ya sifa nyingine za kimuonekano wanafanana sana na kinengenenge wa Kilimanjaro hasa sehemu ya machoni ambapo kuna mduara mnene wenye rangi nyeupe ambao unalizunguka jicho.

Taarifa za kina kuhusu ndege hawa bado hazijapatikana japo wanapatikana maeneo yenye mimea ambayo haija haribiwa sana na hasa kusini mwa milima ya Upare. Jamii hii ya kinengenenge wanakadiriwa kuwa na idadi ndogo na hivyo kufanya waingie katika kundi la viumbe ambao wanakaribia kuwa hatarini kutoweka duaniani.

Kinengenenge wa Upare (Picha na eBird)

8. Kereng’ende Kidari-kijivu (Grey-breasted Illadopsis)

Hawa ni ndege wenye maumbile madogo ambao wana manyoya ya rangi nyeupe shingoni. Manyoya yao kuanzia sehemu ya kifuani huwa na rangi ya kijivu lakini yanabadilika rangi kuelekea upande wa chini ambapo maranyingi huwa na rangi ya kahawia. Hawa ni miongoni mwa ndege wenye aibu sana lakini pia huonekana kwa tabu sana labda kwa kuwatafuta katika maeneo yao.

Ndege hawa wanapatikana maeneo mbali mbali hapa nchini. Maeneo hayo huwa na muinuko wa mita 1,220 hadi mita 1,700 kutoka usawa wa bahari. Huishi katika maeneo yenye misitu ambayo inapata mvua za kutosha. Maeneo ambayo ndege hawa wanapatikana kwa wingi ni kama Morogoro, Dar es Salaam na Iringa. Idadi yao kwa sasa bado haijafahamika japo kwa tafiti zinaonesha idadi ya ndege hawa bado ni ya kuridhisha hasa kutokana na maeneo wapatikanayo ndege hawa.

Kereng’ende Kidari kijivu (Picha na Birds of the World)

9. Kuzi kijivu (Ashy Starling)

Kuzi kijivu ni ndege wenye rangi ya kijivu na kahawia kwa mbali huku wakiwa na mikia myembamba na mirefu. Wana macho yaliyo pauka, mgongoni na sehemu ya mkiani wana manyoya yenye rangi ya kijani ambayo yanaanza kuota. Tofauti kubwa kati ya kuzi hawa na jamii nyingine za kuzi ni rangi yao ya kijivu ambayo wengine kwa asilimia kubwa hawana. Wengi wao wana rangi bluu iliyo changanyikana na nyeusi.

Ndege hawa wanapatikana sana maeneo ya savana na sehemu zenye miti mingi na hupendelea kula chakula chao wakiwa ardhini. Wanapatikana sehemu nyingi hapa nchini na utawanyikaji wao ni wa maeneo makubwa sana. Moja ya sehemu ambayo utaweza kuwaona ndege hawa kwa ukaribu na kwa muda mfupi sana ni Hifadhi ya taifa ya Tarangire.

Ni jambo la kushukuru idadi ya ndege hawa bado inaridhisha japo idadi kamili ya ndege hawa bado haija fahamika. Ufuatiliaji wa ndege hawa kwa mara ya mwisho ulifanyika mwaka 2016 na kuwaweka ndege hawa kwenye kundi la viumbe ambao bado idadi yao inaridhisha.

Kuzi kijivu (Picha na Tanzania Bird Atlas)

10. Chozi baka (Banded sunbird)

Ndege hawa madume na majike hutofautiana rangi. Dume huwa na rangi ya kijani asili mgongoni mpaka sehemu ya shingoni, nyeusi tumboni na sehemu ya kifuani wana rangi ya bluu na damu ya mzee ambazo zimepangika kwa mstari. Jike hana rangi nyingi kama dume, sehemu ya mgongoni wana rangi ya kijani na sehemu ya chini hasa tumboni wana rangi ya kijivu iliyo pauka.

Ndege hawa wanapatikana maeneo matano tu hapa nchini ambayo yote yapo katika misitu inayo patikana mashariki mwa Tanzania. Maeneo hayo ni milima ya Usambara, Nguu, Uluguru, Nguru na Udzungwa. Utagundua kuwa kwa asilimia kubwa ndege hawa wanapatikana katika maeneo ya misitu ambayo inapata mvua za kutosha. Maeneo haya ambayo wanapatikana chozi baka huwa na muonuko wa mita 750 hadi mita 1,500 kutoka usawa wa bahari.

Tafiti zilizo fanyika mara ya mwisho mwaka 2017 zinaonesha kuwa idadi ya chozi baka ilikuwa kati ya 1,500 hadi 7,000 huku pia ikionesha idadi ya ndege hawa kupungua kila siku. Hali hii imepelekea shirika la umoja wa mataifa la IUCN kuwaingiza tege hawa kwenye kundi la viumbe waliyo kwenye mazingira magumu.

Sababu zinazo pelekea kupungua kwa ndege hawa zinaelezwa kuwa ni kilimo ambaco kinasababisha watu kukata miti sana na uvunaji wa mbao huko misituni lakini pia ukataji wa miti kwenye misitu kwaajili ya matumizi ya kuni.

Chozi baka (Picha na eBird)

11.Chozi wa Moreau (Moreau’s Sunbird)

Hawa ni miongoni pia mwa chozi ambao madume wanakuwa na rangi nyingi tofauti na majike. Dume ana rangi ya shaba inayo ng’aa ambayo imechanganyikana na kijani asili sehemu ya kichwani na mgongoni. Sehemu ya kifuani wana rangi nyeusi, zambarau na nyekundu zilizo jipanga kwa mistari huku pembeni wakiwa na rangi ya njano. Majike wana rangi ya njano iliyo changanyikana na kahawia.

Chozi hawa huwa wana eneo dogo sana la utawanyikaji katika mazingira ambayo wanapatikana. Maeneo ambayo wanapatikana ndege hawa ni milima ya Nguru, Nguu, Uvidunda, Ukaguru na Udzungwa. Maeneo haya yapo muinuko wa mita 1,300 hadi mita 2,500 kutoka usawa wa bahari.

Idadi kamili ya ndege hawa bado haija fahamika japo tafiti zinaonesha kuwa idadi inapungua kwa kasi. Kati ya maeneo ambayo ndege hawa wanapatikana hapa nchini, milima ya Nguu na Ukaguru ndio inasemakana kuwa na idadi angalau inayo ridhisha ukilinganisha na maeneo mengine yaliyo salia. Kutokana na kupungua kwa idadi ya chozi hawa, imepelekea waingizwe kwenye viumbe ambao wanakaribia kuingia kwenye kundi la viumbe waliyo kwenye hatari hapa duniani.

Kupungua kwa ndege hawa kuna sababishwa na ukataji miti, uvunaji mbao, mabadiliko ya tabia ya nchi lakini pia mabadiliko ya hali ya hewa ambayo husababisha ndege hawa kuhama kwenye maeneo yao na kutafuta makazi mengine hali ambazo inasababisha wengi wao kufa katika kuhangaikia makazi mapya.

Chozi wa Moreau (Picha na eBird)

12.Chozi wa Loveridge (Loveridge’s Sunbird)

Chozi hawa wanafanana sana na chozi wa Moreau hasa sehemu ya kicwani na mgongoni. Tofauti yao ni kwamba chozi hawa wana rangi ya njano sehemu ya chini na ubavuni, tumbo la njano na alama yenye rangi ya machungwa sehemu ya kifuani huku majike wakiwa na rangi ya kahawia.

Ndege hawa wanapatikana eneo moja tu hapa nchini nalo ni Hifadhi ya Asilia ya Uluguru. Hapo mwanzo walikuwa wanapatikana mpaka maeneo ya Hifadhi ya Misitu ya Bunduki. Eneo wapatikanalo ndege hawa lipo muinuko kati ya mita 1,200 hadi mita 2,560 kutoka usawa wa bahari.

Tafiti zilizo fanyika mwaka 2020 zinaonesha kuwa idadi ya ndege hawa ni kati ya 21,000 hadi 166,000. Idadi inakadiriwa kupungua japo sio kwa kasi sana lakini ni jambo la kutilia mkazo kwani huenda kasi ya upunguaji wa ndege hawa ikazidi. Kutokana na idadi yao na eneo wapatikanao ndege hawa, chozi hawa wapo hatarini kutoweka duniani. Sababu kubwa ya kupungua kwao ni ukataji miti kwaajili ya matumizi ya kuni lakini pia uvunaji wa mbao hali kadhalika kilimo ambacho kinapelekea kuharibiwa kwa makazi ya ndege hawa.

Chozi wa Loveridge (Picha na eBird)

13.Chozi wa Pemba (Pemba Sunbird)

Madume wana rangi ya kijani asili sehemu ya juu na rangi nyeusi sehemu ya chini, sehemu ya kifuani wana mstari wenye rangi ya zambarau. Majike wana njano sehemu ya tumboni yenye mstari mweusi au wenye rangi ya kufifia huku wakiwa na nyusi zilizo pauka.

Ndege hawa wanapatikana visiwani Pemba tu na wameenea katika kila mazingira katika visiwa hivyo. Idadi kamili ya ndege hawa bado haijajulikana lakini tafiti zilizo fanyika mwaka 2016 zinaenesha ndege hawa bado wanapatikana kwa wingi visiwani Pemba. Changamoto pekee ambayo inaonekana kuwa tishio kwa chozi hawa ni mabadiliko ya tabia ya nchi ambapo kama hali itaendelea kwa kasi zaidi huenda idadi yao ikaanza kupungua pia.

    Chozi wa Pemba (Picha na eBird)

    14.Chozi mabawa-mekundu (Rufous-winged Sunbird)

    Madume wana rangi ya bluu iliyo fifia zaidi ambayo imechanganyikana na zambarau sehemu ya juu, kijivu sehemu ya chini na rangi iliyo fifia sehemu ya kifuani. Majike wana rangi ya kufifia hasa sehemu ya chini. Moja kati ya sifa kubwa ya kuwatambua ndege hawa wote madume na majike ni uwepo wa rangi ya paneli ya uchafu inayong’aa kwenye mbawa zao.

      Spishi hii ya chozi wanapatikana maeneo ya milima ya Udzungwa kwa upande wa Iringa, Njombe na Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro. Katika milima ya Udzungwa wanapatikana misitu ya Mwanihana na Iwonde katika Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa. Wilayani Kilombero wanapatikana misitu ya Iyondo, Ukami, Ndundulu na Nyimbanitu ndani ya Hifadhi ya Asili ya Kilombero na Katemele, Kiranzi-Kitungulu na Hifadhi ya Misitu ya Udzungwa. Maeneo haya yanapatikana katika mwinuko kati ya mita 600 hadi mita 1,850 kutoka usawa wa bahari.

      Idadi ya chozi hawa inakadiriwa kuwa kati ya 2,500 hadi 9,999 huku ikionekana kupungua kutokana na sababu mbali mbali. Hali hii imepelekea ndege hawa kuwekwa kwenye kundi la viumbe hai waliyopo kwenye mazingira magumu. Miongoni mwa sababu zinazo pelekea kupungua kwa ndege hawa ni kilimo na ufugaji wa samaki, ukataji miti, mabadiliko ya tabia ya nchi lakini pia mabadiliko ya hali ya hewa.

      Chozi mabawa-mekundu (Picha na eBird)

      15.Korobindo mkia-mwekundu (Rufous-tailed Weaver)

      Hawa ni miongoni mwa korobindo wakubwa na wakipekee. Wana Manyoya yanayo fanana na magamba, rangi ya uchafu kwenye manyoya ya mkiani na kwenye mbawa, mabega yaliyo chongoka na yenye rangi nyeupe na macho yaliyo pauka.

        Korobindo hawa wanauwezo wa kutawanyika katika maeneo makubwa sana wanapatikana sana maeneo ya kaskazini na kaskazini-mashariki hapa nchini Tanzania. Maeneo haya ambayo unaweza kuwapata ndege hawa yapp katika muinuko wa mita 1,100 hadi mita 2,000 kutoka usawa wa bahari.

        Makadirio ya idadi ya ndege hawa bado hayajafahamika na hata tafiti ambazo zilifanyika mwaka 2016 hazikuweza kuonesha idadi ya jamii hii ya korobindo. Taarifa kuhusu idadi yao zinaonesha kuwa inaridhisha na ipo imara hasa kutokana na upatikanaji wao na mazingira yao halisi wanayoishi.

        Korobindo mkia-mwekundu (Picha na eBird)

        16.Kwera wa Kilombero (Kilombero Weaver)

        Hawa ni mingoni kwera wadogo na wembamba ambao midomo yao pia ni myembamba. Madume ambao tayari wameanza kuzaliana huwa na rangi ya kipekee ya njano inayo ng’aa na alama nyeusi yenye umbo la kitambaa cha kulishia mtoto. Majike wana rangi zilizo fifia lakini wana mstari mweusi na mara nyingi huwa sehemu ya kitako cha mdomo huwa imepauka.

          Jamii hii ya kwera waligunduliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1986 na wana eneo dogo sana ambalo wanatawanyika ambalo ni maeneo ya mafuriko ya mto Kilombero. Maeneo haya yapo muinuko wa mita 300 kutoka usawa wa bahari.

          Tafiri ziliozo fanyika mwaka 2019 zinaonesha kuwa idadi ya ndege hawa ni kati ya 2,500 hadi 9,999 huku idadi hii ikiendelea kupungua siku hadi siku. Miongoni mwa sababu zinazo pelekea idadi ya kwera hawa kupungua ni shughuli za ubadilishaji wa vinamasi katika mto Kilombero na kuwa sehemu za kilomo na ufugaji.

          Upunguaji wa idadi ya kwera hawa katika maeneo hayo umepelekea ndege hawa nao kuingizwa kwenye kundi la viumbe ambao wapo kwenye mazingira magumu na kama hali itaendelea hivi basi watakuwa miongoni mwa viumbe waliyo hatarini kutoweka. Hii ni kwasababu ndege hawa wanapatikana katika eneo moja tu lakini pia eneo hili ni dogo sana hivyo inakuwa rahisi kuwapoteza.

          Kwera wa Kilombero (Picha na eBird)

          17.Kwera wa Usambara (Usambara Weaver)

          Hawa ni jamii nyingine ya kwera ambao wana rangi nyeusi mgongoni, rangi ya machungwa sehemu ya kifuani na njano sehemu ya tumboni. Madume wana rangi ya njano sehemu ya mbele kichwani ambayo inawatofautisha na majike ambao hawana rangi hii.

            Ndege hawa wanapatikana mashariki na magharibi mwa milima ya Usambara, milima ya Uluguru na milima ya Udzungwa hapa nchini Tanzania. Magharibi mwa Usambara wanapatikana maeneo ya Magamba na Mazumbai wakati mashariki mwa Usambara wanapatikana katika Hifadhi za Misitu wa Nilo. Katika milima ya Uluguru ndege hawa wanapatikana sana kaskazini mwa Hifadhi za Misitu ya Uluguru huku kwa upande wa milima ya Udzungwa wanapatikana Hifadhi ya Taifa ya Udzungwa, Msitu wa Ndundulu milima ya Nyumbanitu. Maeneo wapatikanayo ndege hawa ni muinuko wa mita kati ya 900-1,850 kutoka usawa wa bahari.

            Kwera hawa kwa mara ya mwisho walifanyiwa utafiti mwaka 2021 na idadi yao ilikuwa 600-1,700 na idadi hii bado inaendelea kupungua kila siku. Hali hii imepelekea ndege hawa kuwa miongoni mwa viumbe ambao wanakaribia kuingia kwenye kundi la viumbe waliyopo kwenye tishio. Sababu kubwa ya kupungua kwa idadi ya ndege hawa ni uharibifu wa misitu unao sababishwa na ongezeko la idadi ya watu wanao endeleza shughuli za kilimo, uanzishwaji wa mashamba makubwa na uvunaji wa miti misituni kwa ajili ya mbao na kuni.

            Kwera wa Usambara (Picha na Tanzania Bird Atlas)

            18. Kidenenda mkia-mweupe (White-tailed Cisticola)

            Hawa ni ndege wenye rangi kiasi. Sehemu ya katikati ya mkia wana rangi nyeusi lakini sehemu ya mkiani kwenye ncha wana rangi nyeupe. Mgongoni wana rangi ya kijivu na kahawia na mstari mnene mweusi, Manyoya yenye rangi ya uchafu kwenye mbawa na chepeo huku sehemu ya tumboni ikiwa na rangi nyeupe.

              Ndege hawa wanapatikana eneo la maporomoko au mafuriko ya Bonde la Kilombero tu. Hii ni eneo la kibia ambalo ni tambarare ambalo linatengenezwa na mito mingi toka milima ya Udzungwa na kutoka kaskazini na magharibi lakini pia nyanda za juu za Mahenge kwa upande wa mashariki. Kidenenda hawa wanapatikana maeneo yenye muinuko kati ya 240 hadi mita 305 kutoka usawa wa bahari.

              Kwa mara ya mwisho ndege hawa walifuatiliwa mwaka 2022, na idadi yao ilikuwa kati ya 20,000-100,000 japo idadi inaonekana kupungua kutokana na changamoto mbali mbali. Japo idadi inaonekana kuwa ni kubwa lakini ndege hawa pia wapo kwenye kundi la viumbe ambao wanakaribia kuingia kwenye kundi la viumbe walio hatarini au tishio.

              Sababu kuu zinazo pelekea idadi yao kupungua ni kilimo na ufugaji wa Samaki. Maeneo yao mengi ya makazi yamekuwa yakiaribiwa kutokana na shughuli hizi za kibinadamu hivyo lazima watu wawe makini katika nyanja hii ili kuendelea kuwa na ndege hawa hapa nchini.

              Kidenenda mkia-mweupe (Picha na eBird)

              19.Kidenenda wa Kilombero (Kilombero Cisticola)

              Hawa kidenenda wakubwa kidogo kuliko wale wa mkia mweupe japo nao pia wana rangi kiasi. Wana chepeo yenye rangi ya uchafu, wana nyusi fupi na nyeupe zenye mstari lakini pia sehemu ya mkiani wana mistari iliyo pauka na myeusi kwenye ncha za mikia yao.

                Kidenenda hawa pia wanapatikana maeneo ya mafuriko ya bonde la Kilombero, hasa kwenye maeneo yenye majani sana ukilinganisha na wale wengine ambao nimewaelezea hapo juu. Tofauti nyingine ni kwamba hawa wenyewe hawawezi kutawanyika sana kama jamii nyingine za kidenenda.

                Tafiti pia kwa kidenenda hawa zilifanyika mwaka 2022 na kuonesha idadi yao kuwa kati ya 5,700-47,000 japo nao pia idadi yao inaonekana kupungua. Jamii hii ya kidenenda wapo katika kundi la viumbe ambao wapo au wanaishi katika mazingira magumu. Hawa pia ni ndege ambao hawaishi kwa kuhamahama kama walivyo baadhi ya ndege wengine.

                Changamoto zinazo pelekea kupungua kwao ni zile zile tu kama za kidenenda mkia-mweupe ambazo ni kilimo na ufugaji wa Samaki hali inayo pelekea kuharibiwa kwa mazingira yao.

                Kidenenda wa Kilombero (Picha na eBird)

                20.Kwale wa Rubeho (Rubeho Forest Partridge)

                Hawa ni miongoni mwa jamii ya kwale wenye umbo dogo wenye urefu unao kadiriwa kuwa wa sentimita 29. Wana rangi ya kahawia na uso wenye rangi ya uchafu huku sehemu ya chini wakiwa na rangi ya kijivu. Wana taji la kahawia lenye umbo la zaituni kichwani, mdomo mwekundu, mboni za kahawia na miguu ya njano.

                Ndege hawa wanapatikana katika misitu ya Milima ya Rubohe hapa nchini. Mwanzo ndege hawa walikuwa wanachanganywa sana na kwale wa Udzungwa kwani wana fanana sana. Lakini kutokana na tafiti mbali mbali imegundulika kuwa ndege hawa ni tofauti na wale wa Udzungwa kabisa.

                Kutokana na uharibifu wa mazingira, idadi yao kuwa ndogo, kupatikana eneo moja tu na kuwindwa kwa kasi kubwa sana, ndege hawa wapo kwenye kundi la viumbe ambao wapo hatarini kutoweka duniani. Taarifa za kina kuhusu ndege hawa bado hazijafahamika vizuri kwasababu hata kwenye shirika la IUCN bado hawajawekwa. Hivyo niwajibu wa watu kufanya utafiti wa kina kuhusu ndege hawa ili watu waweze kujifunza mambo mengi hasa ikolojia na tabia za ndege hawa.

                Kwale wa Rubeho (Picha na Animal Database)

                Ndugu msomaji wa makala hii, kumbuka hii ni sehemu ya kwanza ya makala hii, usiache kufuatilia sehemu ya pili ili kupata mtiririko wote wa makala hii.

                Makala hii imehaririwa na Ezra Peter Mremi, ambaye ni mwanafunzi wa shahada ya Uzamili (Masters) ya Uhifadhi na Usimamizi wa Wanyamapori katika chuo kikuu cha Kilimo cha Sokoine. Kama una maswali, maoni, na mapendekezo, usisite kuwasiliana na mwandishi wa makala hii kwa mawasiliano hapo chini.

                Sadick Omary Hamisi

                Simu: 0714116963/0765057969

                Facebook: Sadicq Omary Kashushu

                Instagram: sadicqlegendary

                Au tembelea blog yetu: www.wildlifetanzania. home. blog

                ……………. I’M THE METALLIC LEGEND …