Habari msomaji wa makala za Wildlife Tanzania, karibu tena kwenye makala yetu ya leo ambapo tunajifunza mambo mbali mbali yaliyopo kwenye sheria hii ya wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009. Hivyo kama utakuwa mfuatiliaji mzuri wa makala hizi za kila siku, basi bila shaka tulikuwa tumeanza kuchambua sehemu ya nne ya sheria hii, ambapo tuliangalia uanzishwaji wa mapori ya akiba kwa mujibu wa sheria hii, na pia tuliona ni nani mwenye mamlaka ya kutangaza eneo kuwa ni pori la Akiba, pia tulitaja maeneo 28 yaliyotengwa na kutangazwa kuwa ni mapori ya akiba, kwa kweli nisimalize uhondo wote itafute makala hiyo kwenye blog ya Wildlife Tanzania ujionee mwenyewe.

Leo tunaendelea na uchambuzi kwenye sehemu ya nne ambapo tunachambua uanzishwaji wa Mapori Tengefu na maeneo Oevu ya akiba. Hivyo kwa mujibu wa sheria hii tutakuwa tunaanza kujadili kifungu cha 16. Nakukaribisha tuende sambamba kwenye uchambuzi huu.

  1. (1) Kwa mujibu wa sehemu ya 4(2) ya Sheria ya Ardhi, Waziri anaweza, baada ya kushauriana na mamlaka husika na kwa kutoa taarifa kwenye Gazeti la serikali, kutangaza eneo lolote la ardhi ya Tanzania kuwa pori tengefu. Kipengele hiki kinajieleza vizuri sana, kwenye sheria za ardhi kuna kifungu ambacho kinaruhusu au kutoa nafasi kwa eneo la ardhi kutangazwa na Waziri kuwa pori tengefu, hivyo waziri mwenye dhamana anapaswa kuwasiliana na mamlaka husika za eneo ambalo linatakiwa kutangazwa kuwa pori tengefu.

(2) Waziri anaweza, kwa utaratibu na kanuni katika Gazeti la serikali kuanzisha usimamizi wa mapori tengefu (Menejimenti ya usimamizi wa Mapori Tengefu).

(3) Kufuatana na kifungu kidogo cha (2) na (3) cha sehemu ya 58 ya Sheria ya  Usimamizi wa Mazingira, Waziri anaweza, kwa kushauriana na Waziri anayehusika na mazingira, kuanzisha kuundwa kwa kanuni na maelekezo yanayoelezea uanzishwaji wa usimamizi endelevu wa maeneo Oevu ya akiba na maeneo oevu mengine.

Katika kuanzisha kwa maeneo oevu (wetlands), Waziri wa maliasili na utalii atashauriana na Waziri wa mazingira ili kwa pamoja waunde utaratibu mzuri wa kisheria unaoelekeza usimamizi endelevu wa maeneo yote oevu.

(4) Baada ya kipindi cha miezi kumi na mbili baada ya kutumika kwa sheria hii, Waziri mwenye dhamana baada ya kushauriana na mamlaka husika atapitia orodha ya mapori yote tengefu kwa kusudi la kujiridhisha uwezo wa ukuaji na kuendelea kwa usimamizi kwenye maeneo haya. Kwa hiyo waziri anatakiwa kufuatilia utendaji na hali ya mambo baada ya kutangazwa kwa maeneo kuwa mapori tengefu, hivyo atafanya hivyo kwa kushirikiana na mamlaka husika.

(5) Kwa kusudi la kifungu kidogo cha (4), Waziri atahakikisha kwamba hakuna ardhi yoyote ya Kijiji  itakayojumuishwa kwenye mapori tengefu. Hivyo ardhi yoyote ambayo bado ni mali ya Kijiji husika haitajumuishwa kwenye eneo hili la hifadhi bila kuwapo wazi kwa sheria husika.

(6) Kufuatana na kifungu kidogo (4), waziri kwa kushauriana na mamlaka husika atatengeneza taratubu na kanuni ambazo zinaelezea namna ambayo usimamizi endelevu wa mapori tengefu unafanikiwa.

MAKATAZO YA KUMILIKI SILAHA KWENYE MAPORI YA AKIBA

Katika sehemu hii ya uchambuzi wa sheria ya wanyamapori, kifungu cha 17 kinaeleza katazo la kumiliki au kuwa na silaha kwenye mapori ya akiba.

(1) Mtu yeyote hataruhusiwa kuwa na bunduki, upinde, mshale au silaha nyingine yoyote katika maeneo ya mapori ya akiba bila kuwa na ruhusa ya maandishi kutoka kwa Mkurugenzi ambayo aliipata kabla ya kuingia kwenye maeneo hayo. Hapa ni kwamba hutakiwi kuingia na silaha yoyote ndani ya maeneo yaliyohifadhiwa kama vile mapori ya akiba bila ruhusa ya maandishi kutoka kwa Mkurugenzi.

(2) Mtu yeyote atakayevunja masharti ya kifungu kidogo (1) anafanya kosa na atawajibika kisheria kulipa faini ambayo haitazidi laki mbili(200,000) au kifungo cha muda usiozidi maika mitatu au vyote kwa pamoja.

ULINZI WA UOTO KWENYE MAPORI YA AKIBA NA MAENEO OEVU YA AKIBA

Katika kifungu hiki tutaangalia jinsi ambavyo sheria inataka kuhusu uhifadhi wa mimea na uoto mwengine ndani ya maeneo ya mapori ya akiba, na kifungu cha 18 cha sheria hii kinaeleza kama ifuatavyo;

(1) Mtu hata ruhusiwa kwa namna yoyote ile kwa kutaka au kwa bahati mbaya kusababisha uchomaji wa moto kweye uoto wa vichaka au nyasi au kuangusha, kukata, kuchoma, kudhuru au kuondoa mti wowote uliosimama, vichaka, nyasi, miti michanga, miche  au hata sehemu za mimea hiyo kwenye mapori ya akiba isipokuwa kwa ruhusa ya maandishi kutoka kwa Mkurugenzi ambaye amemruhusu kufanya hivyo.

(2) Mtu yeyote hataruhusiwa kuchungia mifugo ya aina yoyote kwenye mapori ya akiba na maeneo oevu.

(3) Mtu yeyote atakayekiuka masharti ya kifungu kidogo cha (1) anafanya kosa na kwa mujibu wa sheria atatozwa faini ambayo sio chini ya shilingi laki mbili (200,000) na kiasi kisichozidi shilingi laki tano (500,000) au kifungo kisicho pungua maika mitatu jela na kisichozidi miaka mitano au vyote kwa pamoja.

(4) Na mtu yeyote atakayekiuka kifungu kidogo cha (2) anafanya kosa na kwa mujibu wa sheria atatozwa faini isiyopungua laki tatu (300,000) na isiyozidi milioni tano (5,000,000) au kifungo kisichopungua miaka miwili jela na ambacho hakizidi miaka mitano au vyote kwa pamoja.

(5) Licha ya mapendekezo yaliyotolewa na kifungu kidogo cha (4), pale ambapo kosa katika sehemu hii itajumuisha mifugo ya kigeni, mmiliki au mwangaliaji wa mifugo, atawajibika kisheria kutoa faini isiyopungua thamani ya mfugo iliyohusika au kifungo cha muda usiopungua miaka mitatu jela lakini kisizidi miaka mitano au vyote kwa pamoja. Hapa sheria inasema hivi endapo mtu mwingine anachunga mifugo eneo ambalo limekatazwa kishearia sehemu za hifadhi ya wanyamapori, atakapokamatwa ataadhibiwa kwa mujibu wa sehemu hii ya sheria ya wanyamapori.

Naamini hadi kufikia hapa umepata mwanga wa kukusaidia kwenye maisha yako kwenye eneo hili la uhifadhi wa wanyamapori na sheria ambazo zinasimamia maeneo haya. Kwa wale wanaoishi na kufanya kazi karibu na maeneo ya hifadhi ya wanyamapori hii ni sehemu muhimu kwao kuielewa vizuri kwani kuna mambo mengi ye kimgogoro kati ya wafugaji na hifadhi ya wanyamapori. Kuna maeonezi na kutozwa faini kwa wale wanaongiza mifugo yao ndani ya mapori ya akiba au maeneo mengine yaliyohifadhiwa kwa mujibu wa sheria kwa sababu hawaijui sheria hasa kipengele hiki, hivyo mfugaji huona kama anaonewa, na wakati mwingine mtozaji faini anaweza kumwonea mfugaji kwa kuwa hajui sheria hii, hivyo kusababisha migogoro isiyoisha.

Kitu cha msingi ni wote kusoma na kuielewa sheria hii ili kila mtu atendewe haki kisheria, pia endapo wafugaji watajua sheria hii vizuri watajua kuingiza mifugo kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya hifadhi ya wanyamapori ni kosa na kwasababu wataelewa ni kosa watawajibika kisheria kulipa faini au kifungo jela. Pia wale wanaoendesha shughuli za kibinadamu kama vile kilimo au kukata miti ya ujenzi ni muhimu sana wakaiangalia sheria hii  hasa kifungu cha 18 kinakataza kabisa kusababisha uharibifu wowote kwenye mapori ya akiba, maeneo oevu na maeneo mengine yaliyotengwa kwa ajili ya hifadhi ya wanyamapori na mimea kwa ujumla. Inabidi wafanye shughuli zao kwa uangalifu na kwa makini sana ili wasisababishe uharibifu kwenye eneo la hifadhi ya wanyamapori na mimea, maana kufanya hivyo ni kosa hata kama ulikuwa hujui kuwa ni kosa.

Mwisho, lakini sio mwisho wa mwendelezo wa uchambuzi wa sheria hii, nakushukuru kwa kuendelea kusoma na kufuatilia matandao huu ambao lengo lake kuu ni kutoa maarifa kwa watu wote ili kwa pamoja tukielewa yanayotokea kwenye maliasili zetu, kwa pamoja tutashirikiana kwenye kutangaza na kuhifadhi au kulinda maliasili zetu.

Ahsante sana!

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 248 681/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania