Karibu kwenye shairi linalohamasisha uhifadhi wa ndege aina ya Bundi. Shairi hili limendikwa na Dr. Raymondi Mgeni, maarufu kama Malenga wa Ubena, unaweza kusoma na kuwashirikisha wengine. Karibu!

Bundi aina ya Spotted-Eagle, anapatikana katika milima ya Usambara. Picha na Ezra Mremi

Zipo imani potofu, zimwandamazo bundi
Jamii hujawa hofu, navyo vitu haviendi
Bundi si mharibifu, kwanini hatumpendi ?
Bundi ndege wa pekee, na si vile tujuavyo.

Jamii imeamini, bundi kabeba mikosi
Wakimuona nyumbani, wanajawa wasiwasi
Wasema leo kunani, wataja hii nuksi
Bundi ndege wa pekee, na si vile tujuavyo.

Tena bundi akilia, hawazizimi taa
Hofu inawaingia, kuwa sasa ni balaa
Wanajua lawajia, tetesi zitazagaa
Bundi ndege wa pekee, na si vile tujuavyo.

Kahusishwa na uganga, na haramu biashara
Nia ovu wanapanga, bundi apate madhara
Avamiwa na mapanga, eti anatisha sura
Bundi ndege wa pekee, na si vile tujuavyo.

Bundi anazo faida, na nyingi za ikolojia
Si wa alama ya shida, wa kuleta mbaya njia
Ni ndege wa kawaida, na vingi husaidia
Bundi ndege wa pekee, na si vile tujuavyo.

Twaona zipo dalili, ndege kutupokonyoka
Spishi zake mbalimbali, kuja kesho kutoweka
Hili tulione mbali, na jamii ikazinduka
Bundi ndege wa pekee, na si vile tujuavyo

Tutoe hii elimu, jamii na kila kona
Ni biashara haramu, bundi kutafutwa sana
Uwepo wake muhimu, nayo kubwa tu maana
Bundi ndege wa pekee, na si vile tujuavyo.

Picha ya Bundi, imepigwa na Ezra Mremi

Malenga wa Ubena
+255 676 559 211
raymondpoet@gmail.com
Uhifadhi wa Bundi
Wildlife Tanzania

you might also like