Picha imepigwa na Hillary Mrosso, katika hifadhi ya Taifa ya Nyerere, Tanzania
1.Ndugu zangu karibuni, nina jambo kutamka
Simba wapo hatarini, majangili wawasaka
Waharibu masikani, kuvuka yao mipaka
Simba wanayo thamani, tutunze makazi yao
2.Simba waisha porini, hali sipobadilika
Hatua tuchukueni, tusije tukaumbuka
Wabaya tuwajueni, ikibidi kuwashika
Simba wanayo thamani, tutunze makazi yao
3.Mikakati tuwekeni, ujangili tumechoka
Mizaha tweke pembeni, na tuingiwe mashaka
Sijekuwa masikini, uchumi wetu kushuka
Simba wanayo thamani, tutunze makazi yao
4.Zaja hela za kigeni, Utalii kifanyika
Tutafuta na madeni, nchi itaheshimika
Tutatamba duniani, washindi tutaibuka
Simba wanayo thamani, tutunze makazi yao
5.Simba haba hifadhini, malaki hawajafika
Waweza usiamini, lakini waongezeka
Siweke silaha chini, bado hatujaridhika
Simba wanayo thamani, tutunze makazi yao
6.Kalamu naweka chini, nimechoka kuishika
Nimefikia mwishoni, wa shairi kuandika
Wekeni haya moyoni, daima kuyakumbuka
Simba wanayo thamani, tutunze makazi yao
Hillary Mrosso| mrossotm@gmail.com
+255 683 862 481 |Morogoro| 10.08.2025