Hifadhi ya Taifa ya Arusha ni moja ya hifadhi yenye vivutio vingi na vya kusataabisha sana, vya wanyama na uoto wa aina yake. Ni moja ya hifadhi inayopokea wageni wengi kutoka sehemu mbali mbali duniani. Hivyo bila kuwepo kwa utaratibu mzuri wa usimamizi kutakuwa usumbufu kwa wanyama na mazingira kwa ujumla.

Hivyo hifadhi ya taifa ya Arusha imeandaa utarabu na sharia ambazo husaidia kuwaongoza watalii. Sheria hizi ni pamoja na sheria za kupanda mlima Mlima Meru. Hivyo kama utapanga kutembelea hifadhi ya taifa ya Arusha zifuatazo ni sheria na taratibu unazopaswa kuzifahamu. Karibu tujifunze;

SOMA: Hifadhi Ya Taifa Ya Arusha; Utaratibu Wa Kupanda Mlima Meru

  1. Wapanda mlima lazima waongozwe na askari mwenye silaha.
  2. Watalii wanatakiwa kila mara kufuata ushauri wa askari au kiongozi wa wageni. Kila wakati tembeeni kwa kundi, epuka kuteremka au kupanda mlima peke yako.
  3. Kuapanda hadi kwenye Ash- cone inawezekana baada ya kupata kibali cha Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA.
  4. Wapanda kilele cha mlima Meru wanashauriwa kupanda na kuteremka kwa siku sizizopungua 4.
  5. Muda chini ya siku 4 inaweza kusababisha kuchoka sana na homa ya miinuko ya juu ya milimani.
  6. Wapanda mlimani wanatakiwa kuwa na vifaa vyote vya kupandia mlima, chakula na maji kwa siku zote watakazokuwa mlimani.
  7. Watoto chini ya miaka 10 hawaruhusiwi kupanda zaidi ya mita 3700 juu ya usawa wa bahari.
  8. Wapanda mlima lazima waandae safari ya kupanda mlima kupitia mawakala wa utalii waliosajiliwa.
  9. Mawakala wa utalii wanatakiwa kukodisha wapangazi kutoka chama cha wapangazi kilichosajiliwa na uhakiki wa wapangazi lazima ufanyike kwenye malango ya hifadhi.
  10. Mpangazi anaruhusiwa kubeba mzigo wenye uzito usiozidi kilo 20 wakati wa upandaji wa mlimani.
  11. Usienda zaidi ya mita 3000 usawa wa bahari kama una mafua, matatizo ya mapafu, au moyo. Endapo unatumia dawa muone daktari kabla ya kupanda mlima.
  12. Epuka ulevi wakati wa kupanda mlima.
  13. Watalii wataingia hifadhini au kupanda mlima kwa ridhaa yao wenyewe.
  14. Acha hifadhi katika uasilia wake kwa kutoongeza au kuchukua chochote.
  15. Tumia njia au barabara zilizowekwa na hifadhi na zingatia ushauri wa kiongozi wa utalii.
  16. Uchafu huaribu sura ya uasili. Hakikisha wewe na kila mmoja kwenye kundi anatoka na takataka zote nje ya hifadhi.
  17. Usiwashe moto au kusababisha moto hifadhini.
  18. Uendeshapo gari usizidishe mwendo wa kilomita 50 kwa saa. Mwendo uliopendekezwa ni kilomita 25 kwa saa ili kukwepa ajali na kukuwezesha kuona wanyama vizuri.
  19. Usiwasumbue wanyama kwa njia yoyote ile. Kumbuka wanyama wana haki zote wawapo porini.
  20. Tafadhali usipige kelele, honi au kuwasha redio wakati wa uangaliaji wa wanyama, wakati wa kutembea na upandaji mlimani.
  21. Ili kuonyesha unajali na mwenye busara kwa watalii wenzako, usiwasumbue wao wala wanyama wanao waangalia.
  22. Usiingie hifadhini na mnyama wa kufugwa nyumbani au silaha.
  23. Usishuke kwenye gari isipokuwa maeneo yaliyotengwa kuangalia wanyama na mandhari au kambi za wageni maeneo maalumu yanayoruhusiwa.
  24. Using’oe, usikate au kuharibu mmea wowote au kumiliki/ kubeba sehemu au kipande chochote cha mmea hifadhini.
  25. Ni marufuku kuwa ndani ya hifadhi kuanzia saa 12:30 jioni hadi sasa 12:30 asubuhi isipokuwa kwenye kambi za wageni, hotelini, nyumba za kupumzikia au maeneo maalumu yaliyotengwa na hifadhi.
  26. Kibali cha kuingia hifadhini huwa ni halali kwa muda was aa 24 tu.
  27. Kibali cha mpanda mlima ni halali kwa wakati wa mchana tu. (day light)
  28. Ada za hifadhi mara zinapolipwa hazirudishwi.
  29. TANAPA hufanya kazi na mawakala wa utalii wenye leseni halali za TALA.
  30. Kuweka au kushikilia kambi maalum ya watalii malipo ya jumla ya mteja mmoja kwa idadi ya siku atakazolala hufanyika makao makuu TANAPA – ARUSHA. Malipo ya mabanda hufanyika hifadhini.
  31. Mawakala wa utalii wanahitajika kulipa malipo yote kwa jumla ya wateja kwa angalau siku (30) thelathini kabala ya kuingia hifadhini.

Angalizo: watumishi wa hifadhi wapo tayari muda wakati wote kwa moyo mkunjufu kutoa huduma, ushauri au msaada.

Hizi ni baadhi ya sheria ambazo zipo kwa ajili ya kuweka utaratibu wa kutembelea na kufurahia vivutio kwa wageni wawapo hifadhi. Hivyo zingatia utaratibu huu, popote pale unapotembelea hifadhi maana sheria nyingi za hifadhi zinafanana;

Nakushukuru Rafiki yangu kwa kusoma makala hii, naamini haitakusaidia wewe tu, bali hata wale ambao utakuwa nao uwapo hifadhini.

Asante sana!

Hillary Mrosso

+255 683 862 481

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtalaamu.net/wildlifetanzania