Bara la Afrika kwa miaka mingi limekuwa likikabiliwa na changamoto kubwa sana kuhusiana na masuala ya kisiasa ambayo yanalegalega sana. Kutokana na kukosekana kwa siasa na mifumo ya kiserikali iliyo imara, bara hili limekuwa likiingia kwenye vita vya mara kwa mara, na vita vingi vimekuwa ni vita vya wenyewe kwa wenyewe na hivyo kukosekana kwa amani na maendeleo.

Ndugu msomaji wa makala za wanyamapori katika mtandao huu, leo nimekuandalia makala nyingine ya uchambuzi kutoka kwenye ripoti hii maarufu inayoitwa, ELEPHANT IN THE DUST, THE AFRICAN ELEPHANT CRISIS. Ripoti hii ilitoka mwaka 2013. Hivyo mambo mengi yaliyopo katika makala hii ni matokeo ya uchambuzi wa ripoti hii. Karibu tuendelee kujifunza yale ambayo nimekuandalia;

Sehemu zenye vita na migogoro ya mara kwa mara imetajwa kuwa ni nchi nyingi za Magharibi mwa Afrika, Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC, Somalia, Ethiopia, Sudani na nchi nyingine chache za Kusini mwa Afrika. Katika hali kama hizi za machafuko, vita na migogoro ya mara kwa mara katika bara hili la Afrka kumechangia sana mambo mengi na shughuli nyingi haramu kushika hatamu, kama vile ujangili wa tembo, uhalifu na uharibifu mkubwa wa mazingira.

Utafiti wa masula haya unaeleza kuwa kunapokuwa na machafuko na ukosefu wa amani katika nchi, biashara haramu zinashamiri sana. Hata hivyo katika sehemu zenye migogoro hii, biashara haramu ya meno ya tembo kwa masoko ya ndani na nje ya nchi yanasitawi sana maana kunakuwa na mwanya mkubwa wa kuendelea kufanya uhalifu katika mazingira kama hayo.

Kwa karne iliyopita, INTERPOL, Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayojihusisha Dawa na Uhalifu, Shirika la Kimataifa linalojihusisha na Uhalifu wa Mazingira, kwa pamoja mashrika haya ya kimataifa yalionya sana kuhusu vita, migogoro, na kukosekana kwa siasa nzuri za amani kunaweza kuleta au kuchochea ujangili wa tembo na hivyo kupungua kwa wanyamapori hawa.

Pia matumizi ya maliasili yaliyopitiliza, uchimbaji wa madini na rasilimali nyingine uaweza kusababisha hali mbaya kwenye uhifadhi wa rasilimali hizo kwa matumizi endelevu.

Kati ya biashara haramu zinazohusishwa kuvuka mipaka ya kimataifa ambazo zimeainishwa na mashirika ya kimataifa kwamba zinatakiwa kudhibitiwa zimelenga maeneo haya matano;

  1. Uvunaji na usafirishaji haramu wa magogo na mazao ya misitu, ukataji mito hovyo
  2. Uvuvi haramu
  3. Uchimbaji haramu wa madini pamoja na biashara za madini,na mgogoro ya almasi
  4. Utupaji taka hovyo na biashara ya vitu au taka zenye sumu
  5. Biashara haramu na ujangili wa wanyamapori na mimeaa.

Kutokana na taarifa zilizopo katika ripoti hii ni kwamba biashara haramu na ujangili wa wanyamapori na mimea unakadiriwa kuzalisha zaidi ya dola za kimarekani bilioni 5-20 kwa mwaka, na fedha hizi mara kwa mara hutumika katika kufadhili vikundi vinavyoleta migogoro ya kivita ndani ya nchi.

Hata hivyo taarifa za kitafiti kutoka sehemu mbali mbali duniani zinaonyesha hali hii katika nchi za Napali ambapo kulikuwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vilifadhiliwa sana na uendeshaji wa biashara haramu ya pembe za faru. Kati ya miaka ya 1996-2006 zaidi ya nusu ya faru wote walioishi katika hifadhi ya taifa ya Bardia waliuliwa na watu wa Mao (Maoists) kutoka China kwa ajili ya kufadhili migogoro hiyo ya kivita.

Pia kuna taarifa za kina kutoka katika nchi za Kusini mwa Afrika, yaani nchi za Zimbabwe wakati huo ikijulikana kama Rhodesia, Namibia, Msumbiji, Afrika ya Kusini na Angola wakati wa vita vya kupigania uhuru katika miaka ya 1960 hadi 1990 kulitokea vifo vingi sana vya tembo na faru. Wakati hayo yakitokea miaka ya 1970 na miaka ya 1980 vikosi na vikundi vya kijeshi vya UNITA nchini Angola na FRELIMO nchini Msumbiji vilikabiliwa na mashtaka ya kuua tembo wengi kwa ajili ya biashara ya meno yao.

Kwa sasa  taarifa nyingi za mauaji ya tembo zinaokea katika ukanda wenye migogoro hii hapa barani Afrika, hivyo basi, nchi za Afrika ya Kati na Magharibi mwa Afrika ndizo ambazo zinakabiliwa sana na majanga haya ya ujangili wa tembo kutokana na uwepo wa migogoro mingi kwenye maeneo yao baadhi ya nchi hizo ni Camerooni, Afrika ya Kati na Sudani Kusini. Hata hivyo ripoti hii tunayoichambua imenonyesha kuwa nchi zilizopo kwenye ukanda huu wa migogoro na vita, ndio kuna taarifa nyingi sana za mauaji ya tembo na ujangili wa wa wanyamapori na mimea. Na ripoti nyingi zikionyesha kupungua kwa tembo kwa zaidi ya asilimia 50 hadi 90 kwa nchi za Afrika ya Kati na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pekee.

Uhalifu na uharibifu wa mazingira unachanua sana katika ukanda wenye migogoro na vita. Kwasababu katika kipindi cha mapigano au migogoro hii ndani ya nchi, utekelezaji na usimamiaji wa sheria za kawaida unalegalega sana na wakati mwingine hausimamiwi kabisa.

Hali ya namna hii ndio inapelekea vitendo vingi vya kihalifu kufanyika katika maeneo hayo, kama vile uvunaji na usafirishaji haramu wa magogo na bidhaa za mimea, ujangili na uchimbaji wa madini unafanyika kiholela bila kufuata sheria zilizowekwa.

Aidha, mapigano yaliyokuwa yakifanyika Mashariki mwa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC, ambayo yamepelekea vifo vinavyo karidiwa kufikia watu zaidi ya milioni 6 katika kipindi cha miongo miwili tu iliyopita; ilisababishwa na uroho, tamaa na ufisadi wa maliasili na rasilimali nyingine za nchi hiyo.

Wanunuzi wa meno ya tembo na pembe za faru huwa wanatumia mwanya huo kununua nyara hizo kwa bei nafuu wakati ambapo zinapatikana kirahisi. Hivyo wanatumia udhaifu wa nchi na serikali za nchi zetu kunyonya rasilimali zetu.

Kwa namna nyingine ipo hivi wakati wenyeji wanaingia kwenye vita, wengine wakikimbia kuokoa maisha yao, wengine kujificha kwa ajili ya usalama wao majangili na watu waliojipanga kufanya uhalifu wanatumia mwanya huo kuiba, kupora, kuchimba madini, kuua wanyamapori wenye thamani kama vile tembo na faru, na kusafirisha bila shida yoyote, maana katika kipindi hiki kila mtu anakuwa na wasiwasi na maisha yake na hata ulinzi na usimamizi wa malisili na rasilimali za nchi unalegea na watu wanajichotea kama wanavyotaka.

Siku zote biashara haramu zinasitawi sehemu zenye vita na migogoro mingi, hii ndio sababu vikundi vya uasi kama vile Janjaweed kinachofanya operesheni zake Darful Sudani na mashariki mwa Chad, vilisafiri kutoka Darful na Chadi hadi Camerooni na kuua zaidi ya tembo 300 na 600 mwaka 2012.

Kikundi cha uasi cha Lord Resistance Amry kilichopo Uganda kimehusishwa sana na mauaji ya tembo nchini Uganda, Afrika ya Kati na Jamhuri ya Kedemokrasia ya Kongo. Hata hivyo kuna vikundi vingine kutoka Kongo, Burundi na Rwanda vikiwa na silaha kali aina ya AK-47, vimehusishwa sana na ujangili wa tembo nchini Tanzania.

Kwa upande wa Kaskazini mwa Afrika, vikundi vya uasi na wakati mwingine jeshi la kawaida linawaua tembo. Tembo wakishauliwa meno yake yanasafirishwa kupitia Darful kwenda Karthum Sudani au kutoka Kampala, Uganda kwenda Mombasa, Kenya au kutoka Afrika ya kati na Cameroon kwenda pwani ya Nigeria, Guinea Ikweta na Gaboni hadi kwenye meli za kibiashara au meli za uvuvi.

Kutokana na taarifa hizo, hakuna shaka yoyote kuwa vikundi vya kigaidi na vile vya waasi kutojihusisha na ujangili wa tembo. Pia kuna taarifa za uhusishwaji wa wanajeshi wakiwa wanatumia helikopta katika kufanya ujangili. Hata hivyo kuna uwezekano wa mamlaka za kiusalama kama vile polisi, na maafisa wa forodha kwa mujibu wa ripoti hii wanahusishwa na ujangili na biashara haramu kwenye baadhi ya maeneo.

Katika operesheni tokomeza iliyoendeshwa hapa Tanzania, kwa ajili ya kuchunguza, kukagua, kukamata na kujua maeneo na majangili. Mambo mengi yalijulikana katika operesheni hii, kiasi kikubwa cha wanaohusika katika ujangili wa tembo na wanyamapori wengine sio watanzania pekee bali hata Wanyarwnda walikamatwa na kushikiliwa katika operesheni hiyo.

Uhusikaji wa mtandao wa uhalifu, na uingiaji wa silaha za kisasa ili majangili wazitumie kufanyia ujangili wa tembo kunawaweka askari wanyamapori katika hatari kubwa sana wanapokabiliana au kupambana na ujangili.

Hivyo tunatakiwa kuwekeza vya kutosha katika kuwapa mafunzo na ujuzi wa kisasa zaidi askari wetu, pia kuhakikisha kunakuwa na uwepo wa vifaa na vitendea kazi vyote muhimu ili kulinda, kusimamia na kuhifadhi wanyamapori wetu.

Asante sana kwa kusoma makala hii, naamini haya machache niliyoyachambua yatakuwa na msaada kwenye uhifadhi na usimamizi wa wanyamapori na maliasili zetu kwa ujumla.

Uchambuzi huu umeandaliwa na;

Hillary Mrosso

+255 683 862 481/255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtalaamu.net/wildlifetanzania