Unajua watu wakitaka kukuua au kukuchukia watakupa jina baya, watakusingizia mambo mengi mabaya ili mradi tu watengeneze ubaya juu yako. Mitazamo ya watu juu yako itaanza kubadilika nao watakuona wewe ni mbaya na hufai na unastahili kufa.
Hivyo ndivyo ilivyo kwa baadhi ya viumbe hai wengine muhimu kwenye maisha yetu na kwenye mazingira yetu. Kwasababu watu wengi wamekuwa hawapendezewi na baadhi ya viumbe hai kama CHURA. Hivyo wamekuwa na dhana na hisia hasi kuhusu viumbe hawa wazuri walioumbwa na Mwenyezi Mungu.
Ulimwenguni kote chura ni miongoni mwa viumbe wasipendwa na watu wengi. Wengi hawapendi kabisa kuwepo karibu yao, hata tafiti kuhusu viumbe hawa wa kipekee ni chache sana kutokana na kukosa mvuto kwa watu wengi. Sababu za kuchukiwa kwa chura zinaweza kuchangiwa na maumbile yao yalivyo, ngozi zao, macho yao au sauti zao.
Kwasababu ya mitazamo hiyo ya watu, wanyama viumbe hawa hawapewe kipaumbele kwenye mambo mengi ya kimazingira, utalii na uhifadhi wake.
Wengi tumeshuhudia na kusikia mifano mibaya inapotolewa basi chura anatumika kama moja ya kiumbe mbaya na asiyethaminiwa kwenye jamii. Wakati mwingine ukimuita mtu chura ni sawa na umemtukana tusi kubwa. Hivyo viumbe hawa hawathaminiwi kabisa kwenye jamii zetu.
Kila kiumbe kwa jinsi kilivyo, maumbele au tabia kipo hivyo kwa kusudi maalumu kabisa. Uelewa wetu mdogo kuhusu chura ndio unawaweka viumbe hawa katika hatari ya kutoweka. Kama hujui thamani ya kitu utaishia kukiharibu.
Hatutakiwi kuwadharau baadhi ya viumbe hai kwa muonekano wao ulivyo, tembo yupo vile alivyo kwa kusudi maalumu, simba, nyati, ndege, twiga, sisimizi, siafu, vipepeo, na chura wote wameumbwa tofauti ili watimize kusudio maalumu kwa jinsi walivyo.
Chura ni miongoni mwa makundi makubwa ya wanyama wenye damu baridi, ambao wapo kwenye kundi la AMFIBIA. Katika hili kundi la amfibia kuna chura wa aina mbili. Kuna wanaoitwa kwa kingereza toad na pia frogs. Wote hawa tunawaita chura kwa lugha ya Kiswahili.
Mpiga picha Jan Martin McGuire Chura ni Guttural Toad kutoka mlima Meru
Hadi sasa kuna aina zaidi ya 4,000 za chura waliogundulika duniani, na kwa upande wa Afrika Mashariki kuna aina 200 za chura. Pamoja na kuonekana ni aina nyingi za chura, watafiti na wanasayansi wanasema hii ni idadi ndogo sana, huenda kuna aina zaidi ya viumbe hawa haijagundulika.
Chura ni viumbe wa kushangaza sana, wanaweza kuishi nchi kavu na majini, lakini muda mwingi hupenda kuishi sehemu zenye maji, kama vile kwenye mabwawa, mito, madimbwi na chemichemi. Viumbe hawa wana ngozi laini na yenye unyevu muda wote, hivyo huathiriwa sana na jua na ukame.
Kwasababu hiyo, unaweza kuwakuta chura kwenye maeneo mbali mbali, kama vile savanna, kwenye misitu, kwenye mashamba au kwenye makazi ya watu. Hata hivyo, wanaweza kuwa chini ya mashimo kwa ajili ya kujificha na hali za hatari kama vile ukame, jua na hatari nyingine.
Ni viumbe wasioweza kuvumilia ukame na uharibifu wa mazingira. Hivyo wanasayansi wanasema chura ni viumbe muhimu sana na hutumika kama mojawapo ya kiashiria cha afya ya mazingira.
Uharibifu wa mazingira kama vile kutupa taka zenye kemikali na sumu husababisha uharibifu wa mazingira na makazi ya chura. Pia aina ya ngozi ya chura ina uwezo wa kuhisi hatari za kimazingira kama vile sumu, kemikali hatari na ukame.
Kwasababu ya maumbile yao, chura hufanya kazi zake nyingi wakati wa usiku. Usiku hakuna jua na kuna hali nzuri ya hewa ambayo hufanya vyura wengi kufanya shughuli zao nyingi wakati wa usiku. Hali hii huleta changamoto sana kuwatafiti viumbe hawa. Pia mfumo wao wa maisha, kujificha kwenye mashimo, magome ya miti, au ardhini inapelekea ugumu kuwabaini na kuwagundua kwa haraka na hurahisi.
Licha ya kuwa ni miongoni mwa viumbe wasiopendwa, kuna jitihada zinazofanywa na nchi, pamoja na watafiti wengine kubaini aina, uhifadhi na umuhimu wao kwenye mazingira. Soma makala hii kufahamu mengi kuhusu jitihada za serikali ya Tanzania katika uhifadhi wa Chura wa Kihansi. Makala hii ipo katika link hii Fahamu Jinsi Shughuli Za Binadamu Zilivyoharibu Makazi Ya Chura Anayezaa Nchini Tanzania
Chura ni viumbe wenye umuhimu na pia wana haki sawa na viumbe wengine. Hula wadudu, hivyo wana umuhimu mkubwa sana katika kuiweka sawa mifumo ya ikolojia na huleta usawa wa idadi ya wadudu. Tafiti zinaonyesha wadudu waharibifu wa mazao wanaliwa sana na chura. Hivyo, husaidia kuokoa gharama za kununua dawa za kuuwa wadudu waharibifu ambao wanaliwa na chura.
Chura ni moja kati ya chanzo kikubwa cha chakula kwa ndege na wanyama wanao kula nyama. Pia chura husaidia na hutumika sana katika utafiti wa dawa za binadamu kama vile dawa za kupunguza maumivu pamoja na antibiotiki.
Chura wana macho makubwa yaliyotokeza mbele zaidi, wana miguu kama ya bata webde-feet kwa ajili ya kuogelea na kuruka. Pia wana ulimi mrefe ambao husaidia kukamata wadudu kwa umbali.
Eastern Flat-backed Toad, picha na Ester Matingisa
Kuna baadhi ya chura huwa na rangi yenye kun’gaa sana mfano ni Red Banded Rubber Frog hii hutumika kama ishara ya kuonya na kutoa taarifa kwa viumbe hai wengine kuwa ni sumu na hatari na inaweza sababisha kifo endapo chura huyo ata tumika kama chakula. Pia rangi husaidia chura kujificha katika mazingira anapopatikana.
Chura wanataga mayai na kupitia mchakato unaoitwa metemofosisi. Ni mchakato ambao hufanyika kwa kipindi maalumu hasa kipindi cha mvua na maji.
Maeneo ambayo hayana mvua za mara kwa mara chura huwa na utambuzi wa kujua hilo, hivyo mchakato wa kuzaliana hufanyika haraka kabla ya maji kuisha au mvua kukata.
Chura wana umuhimu kiuchumi, endapo tutawekeza kwenye utafiti na kuwajali wanyama hawa tutakuwa na mazingira mazuri ya kufanya viumbe hawa kuishi na kuwa sababu ya watalii kutembelea nchi zetu na kuleta mapato mengi.
Tunatakiwa kufahamu hakuna kiumbe yupo hapa duniani kwa bahati mbaya, uwepo wake una maana sana kimazingira na kiuchumi. Tunatakiwa kuongeza uelewa wetu kuwajua viumbe hawa na kuwapa thamani kama viumbe wengine.
Kutokana na mabadiliko ya tabianchi yanayoshika kasi kila siku, mazingira yanaharibiwa, maeneo ya hifadhi za misitu na wanyama yanaharibiwa na kulimwa, maeneo oevu yanavaimiwa na watu na mifugo hii inaleta athari nyingi kwa viumbe hai wengi kama chura.
Mpiga picha Butati Nyundo.Chura ni Angolan Reed Frog. Kutoka Hifadhi ya taifa ya Milima ya Mahale
Mfano, kuna aina ya chura walioitwa chura wa dhahabu, walitoweka kutokaka na mabadiliko ya tabianchi na pia shughuli za kibinadamu. Hivyo, tusipoweka nguvu kubwa kulinda mazingira na makazi muhimu ya wanyama, ndege na wadudu tutapoteza viumbe hai wengi hata kabla ya kuwagundua. zaidi soma makala hii Mifano ya Wanyamapori Watano (5) Waliotoweka Duniani na Waliopo Hatarini Kutoweka
Ni wakati sasa wa kutunza mazingira yetu na kuyafanya kuwa sehemu salama kwa viumbe hai wengi kuishi na kufurahia.
Katika kuadhimisha siku ya chura duniani, nitoe rai kwa jamii zetu, kushirikiana na kuweka jitihada katika kuhifadhi mazingira ili kusaidia viumbe hai kama chura kuishi na kuzaliana ili watusaidie kwenye kuleta usawa wa ikolojia na faida nyingine. Hivyo tutoe mitazamo hasi kuhusu wanyama hawa, ni wanyama wazuri,wenye mchango na ni sehemu muhimu sana ya mazingira yetu.
Makala hii imeandaliwa na Hillary Mrosso kwa kushirikiana na Ester Matingisa
Imeandikwa na Hillary Mrosso, +255 683 862 481, hmconserve@gmail.com Pamoja na Ester Matingisa: estermatingisa@gmail.com +255 762 351 997.