Leo tarehe 10 Agasti, ni siku ya simba duniani. Simba ni wanyama wenye historia nzuri ya kuvutia, sio tu wakiwa porini, bali hata watu wengi wanawapenda sana wanyama hawa.
Simba ni mnyama anayependwa sana duniani, utafiti wa Dr. Andrew Loveride unaonyesha zaidi ya nchi 15 duniani zinatumia nembo ya simba kama alama muhimu ya nchi zao. Hii inaonyesha mapenzi na heshima kubwa aliyonayo mnyama huyu.
Simba ni mnyama anayejulikana zaidi na kupendwa na watu wengi, watu wengi wanamchukulia simba kama alama ya ushujaa, ujasiri, nguvu na mamlaka. Dunia imejaa picha nyingi, vinyago na mabango mengi sana yenye nembo na picha za simba. Filamu nyingi, nyumba na hata kwenye sehemu muhimu sana zina nembo ya simba.
Simba amekuwa akihusishwa sehemu nyingi kama alama ya uwezo na uongozi, vitabu vingi vina picha za simba kuliko wanyama wowote wale. Mwandishi na mtafiti nguli wa simba Adrew Loveride, katika kitabu chake maarufu cha the LION HEARTED anasema, katika jiji la London kuna picha, nembo na mapambo mengi yenye nembo ya simba kuliko simba walio hai katika Afrika Magharibi.
Simba anawakilisha ujasiri, uhodari, nguvu, mamlaka na uhodari. Hii ndio maana watu wengi huwapenda simba, hupenda kujiita simba, kuita vitu vyao majina ya simba. Watu hupenda kujihusisha na vitu hodari, jasiri na vinavyopendeza.
Historia ya dunia hii imejaa mifano mingi ya watu maarufu kama vile wafalme, waimbaji, wachezaji wa mpira, wahubiri na hata kwenye mambo ya kiroho, watu huwatumia simba kama alama yao. Sehemu nyingi duniani, utaona watu wakiwa na nguo, vitu au majengo yenye picha za simba.
Mfano, Mfalme Richard I wa Uingereza (“Richard the Lionheart”), Richard I alipewa jina la “Lionheart” ikiwa na maana ya ‘moyo wa simba’ kutokana na ujasiri wake mkubwa na uongozi wake wakati wa Vita vya Msalaba. Alama ya simba ilitumika katika nembo yake ya kifalme, ikiwakilisha ujasiri na nguvu zake za kijeshi.
Mfalme wa Sweden, Gustav II Adolf, Gustav II Adolf, ambaye aliongoza Sweden katika Vita vya miaka thelathini, alitumia alama ya simba katika nembo yake ya kifalme ili kuashiria ujasiri na uwezo wa kijeshi wa taifa lake.
Maharaja wa India, Ranjit Singh, Ranjit Singh, ambaye aliunda na kuongoza Milki ya Sikh, alijulikana kama “Sher-e-Punjab” (Simba wa Punjab). Simba alitumiwa kama ishara ya ujasiri na nguvu za kijeshi, akiwakilisha uongozi wake na uwezo wake wa kutawala.
Mfalme wa Ethiopia, Haile Selassie I, Haile Selassie I alitumia alama ya “Simba wa Yuda” (Lion of Judah) kama ishara ya kifalme. Simba wa Yuda ni alama yenye umuhimu mkubwa katika historia ya Ethiopia, ikiwakilisha nasaba ya kifalme ya Solomoni na urithi wao wa kihistoria.
Wafalme wa Ashanti, Ghana, Katika Ufalme wa Ashanti, simba iliwakilisha nguvu na mamlaka ya mfalme. Nembo za kifalme mara nyingi zilikuwa na simba, zikionyesha mamlaka ya kiongozi wa Ashanti.
Kutokana na mnyama huyu kuwa na mvuto wa kipekee kwa watu, imepelekea kuwa na mahitaji makubwa sana. Historia imejaa matukio mengi yakihusisha matumizi makubwa ya wanyama hawa, hasa familia za kifalme na watu matajiri.
Dan P. van Uhm, katika kitabu chake cha” The Illegal Wildlife Trade, Inside the World of Poachers, Smugglers and Traders”, ameeleza matukio mengi ya wafalme na watu mashughuri kuuwa wanyamapori kwasababu ya starehe na anasa. Mfano, kuna tukio moja lilitokea miaka ya 55 BCE, ambapo mfalme wa Roma wa kipindi hicho, Gnaeus Pompeius Magnus, maarufu kama Pompey aliamuru kuuwawa kwa simba 600 katika tukio moja. Pamoja na hayo wanyama wengine wengi, akiwemo tembo zaidi ya 20, chui zaidi ya 400 waliuwawa kama sehemu ya sherehe na starehe kwa wafalme hao.
Pamoja na wanyamapori wengi kuuwawa kikatili hivyo bila sababu za msingi, historia imejaa matumizi mengi ya wanyama hawa, mfano watu wengi ikiwemo viongozi kama machifu, wafalme na watu maarufu hupenda kuvaa na kutumia ngozi za simba kama ishara ya ufahari, ushujaa na mambo mengine ya kiimani na kimila.
Hata katika bara la Afrika, ambako ndio sehemu pekee duniani yenye idadi kubwa ya simba, kumekuwa na matukio mengi ya ujangili na uuaji wa simba kwa sababu za kitamaduni, kibiashara na kulipiza kisasi. Mfano, kuja jamii za kifugaji hulazimika kuua simba ili wapate wake, mali, au wawe viongozi na kuwa na suti kwenye jamii. Hali hii inachangia sana kuendelea kupungua kwa simba duniani.
Matumizi haya makubwa ya simba yamepelekea wanyama hawa kutoweka sehemu mbali mbali duniani. Mfano, nchi nyingi za Ulaya, Mashariki ya Kati, Kusini Magharibi mwa Asia, pamoja na Afrika Kaskazini, imepoteza kabisa wanyama hawa.
Kwa miaka 30 iliyopita idadi ya simba imeporomoka kwa asilimia 43, hii ni kwasababu mbali mbali kama vile mabadiliko ya matumizi ya ardhi, kuharibiwa kwa makazi asili ya simba, kupungua kwa wanyama walao majani ambao ndio chakula kukuu cha simba, usimamizi duni wa wanyama hawa, ujangili na kushamiri kwa biashara haramu za viungo vya simba. Simba wanaokisiwa kuwepo barani Afrika wanaweza wasifike hata 30,000, hii ni idadi ndogo sana kuliko hata idadi ya tembo.
Pamoja na idadi hiyo ndogo, Tanzania ndio nchi pekee barani Afrika inayoongoza kuwa na idadi kubwa ya simba (17,000). Hii ni kulingana na tafiti zilizofanya na Taasisi ya Utafiti wa wanyamapori Tanzania (TAWIRI), mwaka 2023.
Hii ni ishara nzuri ya uhifadhi wa wanyama hawa hapa Tanzania. Juhudi kubwa za serikali, mashirika ya uhifadhi, na miradi mingi ya utafiti vimesaidia kupunguza vifo vya simba na kuinua uhifadhi maeneo mbali mbali ya nchi yetu. Uhifadhi wa simba unahita maeneo makubwa ya uhifadhi ambao yana wanyama wengi ambao ni chakula, maji na mazingira mazuri kwa simba.
Licha ya faida nyingi za kiuchumi, kitamaduni na kijamii, simba wana umuhimu sana katika kuweka sawia mifumo ya ikolojia ya hifadhi. Simba wanakula wanyama wanaokula nyasi kwa kufanya hivyo husaidia kuweka sawia idadi ya wanyama hao na pia husaidia wanyama wengine jamii yake kama vile chui, duma, fisi, mbwa mwitu na bweha.
Kuna mengi ya kujifunza kuhusu wanyama hawa wa kipekee,
Kwa leo tuishie hapa, nakuahidi makala nyingine nyingi kuhusu simba.
Karibu endelea kufuatilia makala zetu katika blogu hii,
Pia washirikishe wengine!
Kheri ya Siku ya SIMBA duniani!
Imeandikwa na Hillary Mrosso, +255 683 862 481, hmconserve@gmail.com