Habari Rafiki yangu, mara kwa mara huwa tunaandika makala za wanyamapori, uhifadhi na utalii, ambazo zinalenga kutoa elimu na kuwahamasisha watu kutembelea vivutio na kushiriki katka uhifadhi wa wanyamapori na maliasili kwa ujumla.
Leo tarehe 1 septemba, dunia inasherekea siku ya usafi, ambapo wito unatolewa kwa nchi zote duniani kuangalia tena namna mazingra tunayoishi tunavyoweza kuyaweka katika hali ya usafi na ubora zaidi. Usafi ni muhimu sana kwa mustakabali wa afya zetu, bila kuwa na sera za usafi wa mazingira, tutakuwa katika hatari kubwa ya kupata magonjwa ya milipuko na kusababisha maisha yetu hapa duniani kuwa mafupi.
Usafi wa mazingira unagusa sehemu kubwa sana, usafi wa mazingira ndio uhifadhi wa mazingira. Tunashuhudia sehemu mbali mbali duniani zikikabiliwa na hali mbaya ya uchafuzi wa mazingira, mfano kwenye nchi zetu, miji yetu hata nyumbani tunapoishi mazingira mengi sio salama sana.
Utupaji wa taka hovyo, mpangilio mbaya wa utunzaji wa taka maji, matumizi ya vyoo, matumizi ya chupa za plastiki, matumizi ya mifuko ya plastiki, bado ni changamoto kubwa kwa nchi zetu, hasa jamii zetu. Watu wanakosa ustarabu, anatupa taka sehemu yoyote ile anayojisikia, jambo hili linafanya mazingira kuwa mabaya na pia ni hatari kwa viumbe hai wengine.
Kwa mfano watu wanaosafiri kwenye mabasi au kwenye magari bianfsi, unakuta mtu anakunywa maji na anatupa chupa ya maji nje, au anakula chips na kutupa mifuko na matakataka mengine nje ya gari, huwa nachukia sana, na kama nikikaa na mtu anayefanya hivyo kwenye basi wakati wa safari huwa namwambia, sio vizuri kutupa chupa ya maji au manailoni sehemu ambayo haisatahili.
Uchafuzi wa mazingira una athari kubwa sana sio tu kwa maisha ya binadamu, lakini pia kwa wanyama na mimea, kwa mfano endapo taka zenye sumu zinapotupwa sehemu ambazo sio sahihi husababisha uharibifu wa udongo, pia viumbe hai walopo ndani ya udaongo hufa na kusababisha udongo kukosa rutuba na hewa.
Kuna wale wanaotupa taka kwenye vyanzao vya maji, hii ndio hatari kubwa sana kwa maisha ya watu na viumbe waishio majini, sehemu nyingi tumeshughudia maji machafu ya viwandani yakielekezwa kwenye vyanzo vya maji ambayo hutuiwa na watu na viumbe wengine. Pia hata maumizi mabaya ya vyanzo vya maji ni uharibifu na uchafuzi wa mazingira.
Pia kuna wale wanaopenda kwenda ufukweni, sehemu za fukwe za bahari ni mandhari nzuri sana kwa ajili ya utalii na sehemu za watu kupumzika. Lakini endapo sehemu hizi zinachafuliwa kwa takataka kama vila mifuko, makaratasi, makopo, chupa nk. Zinasababisha sehemu hizi kukosa mvuto kabiasa na ni uharibifu wa mazingira ya fukwe za bahari.
Sehemu yoyote ile unapofika au unapoishi, ikiwa ni barabarani, sokoni, nyumbani, ofisini, viwandani, porini au mbugani, kisimani au bombani tunza mazingira sehemu zote hizo. Onyesha kuwa umestaarabika kwa kutotupa taka sehemu ambazo sio sahihi. Kuwa mfano eneo lako la kazi, nyumbani kwako au kwenye uwanja wa michezo kuwa msafi, tunza mazingira.
Kuna usemi unasema tunza mazingira yakutunze, usemi huu una ukweli mkubwa sana ndani yake. Na kama tunakubaliana na usemi huu, suala la usafi wa mazingira so la siku moja tuu pekee, au la tarehe 1 septemba tu, ni suala la kila siku na inatakiwa kuwa ni mfumo wetu wa maisha kutunza mazingira na kuyaweka safi wakati wote.
Fanya kila unaloweza, kuweka mazingira yako katika hali ya usafi kila wakati. Panga mazingira yako ya nyumbani, ofisini, shambani, au kwenye kituo chako cha boda boda, popote pale ulipo weka utaratibu mzuri wa kutunza mazingira, tenga sehemu maalumu kwa ajili ya kutupia au kuweka taka, wafunze wengine utaratibu huu, hasa watoto na watu wengine ulionao.
Ahsante sana!
Hillary Mrosso
+255 683 862 481
www.mtalaamu.net/wildlifetanzania