Leo ni siku ya wafanyakazi duniani. Tunajua umuhimu wa kazi kwenye maisha yetu. Bila kazi masiaha hayana maana, bila kazi hatuwezi kufikia malengo yetu. Bila kazi hakuna maendeleo kwenye sekta yoyote ile.

Wote tunajua kazi ni kipimo cha utu. Kwa kutambua hilo, nimeamua kuandika makala hii kuwapongeza wafanyakazi wote wanaofanya kazi zao kwa weledi na kujituma.

Kipekee niwapongeze wanaofanya kazi katika sekta ya maliasili na utalii. Kazi yao kwenye uhifadhi ni ngumu, hatari na ina maana sana katika kuhakikisha wanyama na mimea inaendelea kuwepo kwa vizazi vingi vijavyo.

Katika siku hii ya wafanyakazi duniani kuna ujumbe unasema, usalama na afya za wafanyakazi zina mchango katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi (Safety and health at work in a changing climate).

Wengi tunafahamu mabadiliko ya tabia nchi yanavyochangia kuleta majanga mbali mbali katika. Wafanyakazi wakiwa na afya njema, usalama watakuwa nyenzo muhimu sana katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Kazi za uhifadhi wa wanyamapori na mazingira yao zinahitaji umakini mkubwa sana kutokana na hatari nyingi kama vile uwepo wa majangili ambao wanaweza kuwadhuru, kuwajeruhi, au kuua wafanyakazi wa maliasili.

Pia kufanya kazi porini kuna hatari ya kushambuliwa na wanyamapori wakali kama vile nyoka, simba, nyati, viboko na mamba nk. Hivyo usalama wa wafanyakazi  ni muhimu sana kama vile kuwa na vifaa vya kutosha kama magari, viatu, nguo na silaha za kisasa.

Pamoja na hayo, usalama wa afya za wafanyakazi ni muhimu sana katika maeneo ya kazi, mfano kuna wanyama wanabeba vimelea vya magonjwa hatari ambayo yanaweza kuwaambukiza wafanyakazi endapo wanyama hao watakuwa karibu na makazi ya watu.

Magonjwa kama vile homa ya nyani iliyoibuka hivi karibuni huko DRC Kongo imetokana na wanyama jamii ya nyani, kuna magonjwa ya Ebola, mafua ya ndege na kichaa cha mbwa ambayo pia husambaa na huweza kubebwa na wanyama au ndege.

Kutokana na mvua nyingi zinazonyesha huenda kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, uwezekano wa kusambaa kwa magonjwa ni mkubwa. Magonjwa kama kipindupindu, malaria, typhoid haya yote ni tishio kwa afya za wafanyakazi.

Ili tuwe na wafanyakazi wenye tija na afya bora inabidi tuhakikisha usalama unakuwepo na afya za wafanyakazi zinalindwa kwanza na wafanyakazi wenyewe lakini pia na taasisi zao au serikali.

Napenda kuwatakia wote kila la kheri kwenye majukumu yao muhimu ya kuifanya dunia kuwa sehemu salama ya kuishi.

Hillary Mrosso