Heri ya siku ya wanawake duniani kwa wanawake wenzangu wote,

Leo ni tarehe 8 machi mwaka 2024, ni siku ya kuadhimisha siku ya wanawake duniani, ambazo ni sherehe za kimataifa  za kuadhimisha  na kutambua mchango na mafanikio ya wanawake katika jamii,uchumi,siasa na utamaduni.

Tukio hili lilianza rasmi huko Umoja wa Mataifa mnamo mwaka 1975 ambapo lilipendekezwa kama siku maalum ya kutafakari na kuchukua hatua kuhusu haki za wanawake, kila mwaka tarehe hii hutoa fursa ya kutathimini maendeleo yaliyopatikana katika kufikia usawa wa kijinsia, kusherehekea mafanikio ya wanawake katika maeneo mbalimbali ya maisha na kutambua changamoto zinazowakabili.

Nami kama mwanamke na kwakudumisha malengo ya siku hii ya wanawake nakukaribisha katika makala hii inayoangazia mchango wa wanawake katika shughuli za kiuhifadhi nchini Tanzania.

Katika ulimwengu wa leo ambapo changamoto za mazingira zimekuwa kubwa , wanawake wamekuwa wakifanya jukumu kubwa katika kuhakikisha wanapunguza changamoto hizi katika maeneo mbalimbali ya nyumbani lakini pia katika maeneo mbalimbali ya hifadhi nchini kwetu. Makala hii itaangazia mchango wa wanawake katika shughuli za uhifadhi na jinsi ambavyo mchango wao umeleta mabadiliko chanya katika ulinzi wa maliasili zetu.Karibu Mpendwa msomaji ujionee maajabu ya wanawake.

MCHANGO WA WANAWAKE KATIKA UHIFADHI

  • Uongozi katika jamii.

Katika jamii mbalimbali wanawake wamechukua nafasi za uongozi katika jamii ambapo wamesimama kidete kuhakikisha rasilimali za eneo husika zinalindwa na kutunzwa kwa maendeleo ya sasa na ya baadae.

Mfano mzuri ni Raisi wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ametoa mchango mkubwa katika kuhakikisha maliasili zetu zinalindwa na kuendelezwa kwa kuhamasisha utalii endelevu, kusimamia jitihada za kuendeleza maliasili,kuchagua viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa sasa wa Maliasili na utalii Mhe. Angellah Kairuki, ambao wanasimamia  vizuri wizara ya maliasili hivyo maliasili wetu na mazingira yetu yanaendelea kuwa salama

  • Ujasiliamali wa utalii wa Ikolojia.

Wanawake wajasiliamali wameanzisha ,makambi ya Ikolojia na miradi endelevu ya utarii, wakisaidia shughuli za uhifadhi huku wakijipatia kipato cha kumudu mahitaji yao.

Mfano kikundi cha Mama misitu, ni kikundi cha wanawake wa Kijiji cha mang’ula wilaya ya Kilombero ambacho kinajishughulisha katika uhifadhi wa misitu , kutoa elimu kuhusu ummuhimu wa misitu na kupambana na uharibifu wa mazingira.

                                                                                                   Chanzo: pamojablog.

  • Uhifadhi wa maarifa ya jadi.

Wanawake mara nyingi wanamiliki maarifa ya jadi kuhusu mazingira ya ndani na tabia za wanyamapori. Ushirikiano wao katika miradi ya wanyamapori  hufanya maarifa hayo yahusishwa au yatumiwe katika harakati za uhifadhi.

Mfano wanawake wa jamii za Pwani wanashiriki katika miradi ya uhifadhi wa mikoko ,wakitegemea maarifa yao ya jadi katika usimamizi endelevu wa rasilimali.

                                                                                   Chanzo:rfi.fr

  • Elimu na uhamasishaji.

Wanawake wamekuwa waelimishaji muhimu katika jamii ,wakitoa elimu kuhusiana na mazoea ya uhifadhi, wanaratibu program za kueneza   uelewa na shughuli za elimu katika maeneo mbalimbali nchini. Pia hata katika familia wanawake wamekuwa mchango mkubwa wa kuwajengea watoto wao uelewa na maarifa mbalimbali juu ya uhifadhi

Chanzo: Nyangeta Magesa. Picha hii inaonyesha muhifadhi akiwa katika uhamasishaji na utoaji wa elimu kwa wanafuzi kuhusu uhifadhi.

  • Utafiti na ufuatiliaji.

Wanawake wanasayansi na watafiti wanachangia katika jitihada za uhifadhi kwa kupitia tafiti mbalimbali wanazofanya kuhusu mazingira, spishi, ikolojia na utarii. Tafiti hizi zinasaidia sana katika uvumbuzi na uboreshaji wa shughuli za uhifadhi nchini

Mfano ni Dkt.Elizabeth Maruma Mrema, ambaye ni mwanasayansi wa mazingira  aliyechangia katika kuanzishwa kwa mipango endelevu ya uhifadhi na usimamizi wa mbuga za wanyama na hifadhi za taifa kupitia tafiti zake.

                                                                                                    Chanzo: news.ctgn,com

  • Jitihada za kupambana na ujangili

Wanawake wanashiriki kikamilifu katika harakati za kupambana na ujangili. Wanawake wengi sasahivi wameajiriwa kama askari pori ambao wanashiriki kwa hali ya juu kupambana na ujangili na kuhakikisha sehemu zetu za hifadhi zinalidwa na kutunzwa.

                                                                                                     Chanzo: WWF Tanzania

  • Udhibiti wa athari za mabadiliko ya hali ya hewa

Wanawake wanashiriki kikamilifu katika harakati mbalimbali za kudhibiti mabadiliko ya hali ya hewa kama vile upandaji miti, matumizi ya njia mbadala za kupikia, kilimo kisichoathiri mazingira na pia katika shughuli mbalimbali hifadhini kama vile kusafisha maeneo na kufyeka mimea vamizi mbalimbali ambayo ni tishio la maeneo yetu ya hifadhi.

Picha hii inaonyesha mwandishi wa Makala hii nikiwa katika harakati za kudhibiti mabadiliko ya hali ya hewa ambapo nilishiriki katika kufyeka mimea vamizi katika Eneo la Hifadhi la Ngorongoro.

Mpenwa msomaji, Leo ni siku ya wanawake duniani ndiyo maana nimezungumzia Zaidi kuhusu wanawake lakini haimaanishi kuwa mchango mkubwa sana wa wanaume mimi kama mwandishi siutambui ,Hapana nautambua sana mchango mkubwa wa wanaume katika kufikisha uhifadhi wa rasilimali zetu hapa tulipo.

Lakini nawapongeza sana wanawake duniani kote kwa yote na vyote mnavyovifanya na kuvitoa kwa ajili ya uhifadhi wa rasilimali zetu.tuendelee kuwa mstari wa mbele kuyatunza mazingiran na rasilimali zetu na pia tuwajengee Watoto wetu tabia na hamasa ya kulinda, kutunza na kupenda maliasili zetu kwani tukimfundisha mtoto maadili mazuri kuhusu wanyamapori wetu atayashika hadi pale atakapokuwa mzee.

Asanteni

HERI YA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI

Mwandishi: Monica Charles Mahilane

0652267935

Mahilanemonica49@gmail.com