Taarifa kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linalojihusisha na Mazingira (UNEP) pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa linalojihusisha na Uhifadhi wa Maliasili (IUCN), zinaonyesha 15% ya dunia ni maeneo ya uhifadhi wa maliasili kama wanyama na mimea. Lakini pia inaonyesha kuwa 7% ya eneo la dunia ni hifadhi ya bahari yenye viumbe hai muhimu.

Taarifa hizi zinatufanya tuone kuwa dunia hii haikaliwi na watu pekee, bali na viumbe hai wengine muhimu. Pamoja na uwepo wa binadamu hapa duniani, pia wanyama, wadudu, miti na viumbe hai wengine wanatakiwa kuwa na nafasi yao ya kuishi kwenye makazi yao bila kusumbuliwa na athari zozote kutoka kwa binadamu.

Juhudi mbali mbali zimechukuliwa na mashirika makubwa duniani kuhakikisha uwepo wetu hapa duniani hautaathiri uwepo wa viumbe hai wengine. Uwepo wa viumbe hai wengine hapa duniani ni muhimu sana kwasbabu wanamchango mkubwa wa kusaidia maisha ya binadamu yaendelee hapa duniani.

Hata hivyo moja ya juhudi hizo ni kuanzishwa kwa Siku ya Wanyamapori Duniani, ambayo ilianzishwa maalumu kabisa ili kutukumbusha nafasi yetu hapa dunini, pamoja na nafasi ya viumbe hai wengine hapa duniani.

Siku ya wanyamapori duniani ilianzishwa tarehe 3 Machi, 2013, huko Bangkok Thailand. Moja ya maazimio makubwa kwenye siku hii ilikuwa ni kuhakikisha wanyamapori walio hatarini kutoweka hawawi tena moja ya bidhaa kwenye biashara za wanyamapori, hasa biashara za kimataifa.

Hivyo, pamoja na mambo mengine, mkutano huo ulipanga kila ifikapo tarehe 3 Machi, kila mwaka tusherekee siku hii ya wanyamapori, kwa kuweka jumbe mbali mbali ambazo zitatufanya tukumbuke kuwa tunawahitaji wanyama, misitu, wadudu, ndege na viumbe wengine kwenye dunia hii.

Dhima hii ni muhimu sana, maana tafiti kutoka shirika la WWF zinaonyesha uwepo wetu hapa duniani tangu mwaka 1970 umeachangia kupungua kwa 68% ya wanyamapori. Kupungua kwa wanyamapori kiasi hiki inatokana na shughuli za kibinadamu kama vile uharibifu wa mazingira na makazi muhimu ya wanyama, wadudu, na ndege, uvunaji na matumizi yaliyopitiliza ya rasimali hizo, uchafuzi wa mazingira pamoja na mabadiliko ya tabia nchi.

Watu hawatilii manani kabisa uwepo wa wanyamapori au viumbe hai kwenye maeneo yao. Mfano, mtu akimuona nyoka anawaza kumua, akiona kinyonga anawaza kumuua, akiona popo wapo kwenye maeneo yao, anatafuta sumu za kuuwaua, ndege wadudu na wanyama wengi wametekekea kwa kuwa hatuoni umuhimu wao kwenye maeneo yetu.

Siku za karibuni hapa Tanzania kuliibuka makundi ya watu sehemu mbali mbali wakitaka popo wanaoishi kwenye maeneo yao waondolewe au wauwawe. Niliona hadi wengine wakitengeneza sumu za kuangamiza wanyama hawa wazuri. Tunatakiwa kuwa na hisia nzuri na wanyama kama hawa wanaopenda kuishi karibu na makazi ya watu, tusiwaua tutafute namna ya kuwahamisha.

Siku hizi watu hawana huruma kwa wanyama, mfano ukipita mtaani kwenu utaona mizoga ya wanyama wengi wadogo kama vile kalunguyeye, nyoka, vyura, kobe, mijusi wamegongwa na magari na wengine wamepigwa na fimbo au mawe hadi kufa. Hii inaonyesha kuwa sisi hatupendi viumbe hawa kwenye maeneo yetu, jambo ambao sio zuri kabisa.

Barabara zetu zinanuka damu ya wanyamapori, mfano barabara kuu inayokatisha hifadhi ya taifa ya mikumi, barabara zinazokatisha maeneo yenye wanyamapori zinanuka damu za wanyama. Wanyamapori, ndege, wadudu wenge wameuwawa kwasababu hatuoni umuhimu wao hapa duniani. Soma zaidi makala hii kufahamu mengi Kilio Kisichoisha Ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi

Ujangili wa wanyamapori na biashara za viungo vya wanyamapori imechangia sana kupungua kwa wanyamapori sehemu nyingi. Tunakosa hisia chanya kwa wanyama na ndege wanaotuzunguka. Katika siku hii ya wanyamapori duniani, ni vizuri tukatumia muda kutafakari na kuona viumbe wengine wana haki ya kuishi na kufurahi maisha kwenye dunia hii.

Uharibifu wa mazingira na makazi muhimu ya wanyamapori ni tishio jingine kwenye uhifadhi wa wanyamapori. Ongezeko la watu na mahitaji makubwa ya watu vimechangia sana watu kutaka maeneo makubwa ya kuzalisha na kuishi, ujenzi wa miundombinu mikubwa kwenye maeneo muhimu ya wanyamapori pia imeleta changamoto kubwa.

Hivyo basi, nitoe wito kila mtu mahali alipo akiona viumbe hai hao asiwaue, usiwagonge na gari, kama mnayama hana nia yoyote ya kukudhuru kwanini umuue? Kama kuna mnyama yupo kwenye maeneo yenu, toa taarifa kwa watu wa maliasili watakuja kumchukua na kumhamisha, ila usimuue.

Wengi ukisema uhifadhi wanafikiria simba, tembo na faru, ni sawa hawa ni muhimu lakini kuna wadudu, kuna ndege, kuna popo, kuna vyura na nyuki, bila hawa na wengine hakuna uhifadhi. Kuna viumbe hai wengine jamii ya reptilia na amfibia wana ngozi laini sana ambayo huathiriwa na jua kali, ndio maana wengi wa wanyama hawa utawakuta sehemu oevu, zenye maji au kwenye misitu ambapo hakuna uharibifu wowote wa mazingira.

Endapo mazingira yataguswa kidogo tu, wengi wa viumbe hawa jamii ya amfibia na reptilia hupata shida sana. Ni viumbe wanaopata shida sana hasa kipindi hiki chenye mabadiliko makubwa ya tabia nchi na uharibifu wa mazingira kama ilivyo sasa.

Katika dhima ya siku ya wanyamapori duniani ambayo ni kuunganisha watu na dunia (Connecting People and Planet). Ni vizuri kujua dunia hii inakaliwa na wanyamapori na viumbe wengine muhimu. Napenda watu wote watilie manani, wawe na hisia nzuri kwa wanyama, ndege, wadudu na mimea.

Tunatakiwa kuwafurahia wanyama na viumbe wengine waliopo kwenye maeneo yetu. Tuwaache waishi tusiwe sababu ya kukatisha uhai wao au kuharibu mazingira yao muhimu. Tutuze mazingira yetu na mazingira yao.

Tuepuke kutupa taka hatarishi kwenye maeneo ya wanyamapori, taka hatarishi ni kama vile taka za plastiki, mifuko, makaratasi, kemikali hatari au madawa hatarishi kwenye maeneo ya wanyamapori.

Pamoja tushirikiane kuifanya dunia kuwa sehemu salama ya kuishi binadamua na viumbe hai wengine.

Tubarikiwe, tutunze viumbe wa Mungu!

Kheri ya Siku ya Wanyamapori Duniani!

Happy World Wildlife Day 2024!

Hillary Mrosso, +255 683 862 481, hmconserve@gmail.com