Baada ya kuangalia hifadhi ya Taifa ya Saadani iliyoko katika Pwani ya Tanga na Bagamoyo leo tupandishe milima hadi mji kasoro bahari ili tuikute Milima ya Uduzungwa, hapo ndipo kituvu cha hifadhi hii kilipo. Hii ni Hifadhi ya Taifa ya Uduzungwa iliyopo katika mkoa wa Morogoro. Uduzungwa ni hifadhi inayopendeza na kuvutia sana. Ni hifadhi iliyosheheni uoto wa asili na kujawa na misitu mirefu na mikubwa, ubichi na kijani kwa mwaka mzima ndiyo mwonekano wa hifadhi hii ya kipekee kabisa. Hifadhi hii iliyopo kwenye safu za milima ya Uduzungwa, ni moja kati ya maeneo ya dunia yenye bayoanuai nyingi na zenye uasili wa kutosaha. Vile vile hifadhi hii ni sehemu ya milima ya tao la Mashariki (Easten Arc mountains) inayoanzia katika miinuko ya Taita iliyopo Kusini mwa Kenya mpaka Makambako iliyopo Kusini na katikati ya Tanzania.

Hifadhi hii iliyopo kwenye Mikoa ya Iringa na Morogoro ina ukubwa wa eneo la kilomita za mraba 1990. Ningependa kukujulisha na kukufahamisha baadhi ya mambo mazuri amabayo yatakufanya upange safari ya kutembelea hifadhi hii kabla ya mwaka huu kuisha. Kuna vivutio vingi sana ambavyo vinawafanya wageni kutoka nchi za mbali kulipia gharama kubwa sana ili kuja kujionea maajabu haya yaliyopo kwenye hifadhi ya Taifa ya Milima ya Uduzungwa. Kwa uchache ni bora nikwambie vivutio hivyo adimu na huwezi kuvipata kwenye hifadhi yoyote ile duniani lakini ni rahisi kuvikuta hapa Uduzungwa. Karibu fuatana nami;

  1. Maporomoko ya maji

Hifadhi ya Taifa ya Milima Uduzungwa inajulikana duniani kote kwa maporomoko ya maji kutoka umbali wa zaidi ya mita 170, ni hifadhi pekee nchini Tanzania yenye sifa hii, maporomoko haya ya maji yanajulikana kama Maporomoko ya maji ya Sanje (Sanje Waterfalls) ambayo yapo Mwanihana ambayo hapo mwanzo ilikuwa ni Pori tengefu. Maporomoka haya ya maji ndio kivutio kikuu sana kwa hifadhi hii ya Uduzungwa, wageni na watafiti huja hapa kwa ajili ya kufurahia na kujifunza mambo mbali mbali ya maporomoka haya na hifadhi hii kwa ujumla. Kuna rafiki yangu mmoja kutoka Zambia alikuwa ananielezea kuhusu hifadhi hii ya Uduzungwa, nikamuuliza ni kitu gani kime kufurahisha au umekifurahia kwenye hifadhi hii, akasema yani, nilipoona maporomoko ya maji nilisema waooh!, yani alikosa maelezo ya kutosha ya kuelezea uzuri wa hifadhi hii ya Uduzungwa, alisema nimetembelea hifadhi nyingi sana za ndani na nje ya nchi yangu, lakini nilipofika Uduzungwa nilifurahia zaidi kuliko hifadhi zote za kwao. Hivyo Mtanzania mwenzangu ambaye hujafika au hujawahi kuitembelea hifadhi hii unasubiri nini? Panga kuitembelea hifadhi hii kabla yam waka kuisha.

  1. Kutembea, kupandisha mlima (Mountain Hiking)

Uzuri wa hifadhi hii ni kwamba kuna ubaridi na kivuli cha kutosha ambacho kinasababishwa na misitu minene iliyopo kwenye milima hii, sehemu nzuri kwa ajili ya kutembea kwa miguu kupandisha mlima ambao umewekewa njia nzuri za wanaotembea, hivyo kufanya sehemu hiyo kuvutia zaidi, wakati wa kupanda mlima huu wenye misitu hii minene utasikia sauti za ndege wanaopatikana kwa wingi maeneo hayo ya mlima. Katika kupandisha mlima huu wenye vilele viwili vya Lohomero urefu wa mita 2576 na Mwaniha urefu wa mita 2500, ambapo utakapo fika kileleni utaiona Morogoro nzima yani utashangaa mwenyewe, kwa hiyo kuna kutembea ili uweze kuona kila kinachoonekana kwenye hifadhi hii ya kipekee. Hakuna hifadhi nzuri kama hii jamani. Wageni wengi hupenda kupanda mlimani na wanaona ni sehemu yao nzuri ya kutembelea kwa sababu ya njia zake kupitika vizuri kabisa na bila kuathiri uoto, kila kitu kipo kwenye uasili wake kabisa. Zifuatazo ni njia ambazo mara nyingi hutumiwa na wageni wanapopanda kwenda kileleni mwa milima ya Uduzungwa,

  1. Njia ya Sanjo ( Sanjo trail), ambayo ni kilomita 6 kwa muda wa masaa 3, kwenye njia hii kuna vivutio vingi sana kama, utakutana na wanyama jamii ya nyani, ndege wengi sana na mtakutana na maporomoko ya maji mara mbili, vile vile kwenye njia hii utakutana na uoto wa miti jamii ya miombo na miti mingine yenye kuvutia sana.
  2. Sanje Circuit, ambayo ni umbali wa kilomita kama 5 na nusu ambapo mtatumia muda wa kama masaa manne, kwenye kutumia njia hii ya pili utakutana na vivitio vingi sana kama vile maporomoka madogo madogo 3, wanyama wengi jamii ya nyani na kima, vipepeo wengi sana na pia utaona uoto wa kipekee sana na wa kuvutia mnoo.
  3. Prince Bernhard trail, hii ni njia ya yenye umbali wa kilomita moja, ambayo kwa kutembea utatumia kama dakika 40, vivutio unavyoweza kuviona kwenye njia hii ya tatu ni maporomoko madogo madogo, nyani wekundu, swala wa aina mbali mbali na ndege kwenye mlima Bokela.
  4. Miti/ mimea

Kwa wale wanaopenda zaidi vivutio vya mimea  ya aina mbali mbali yenye kuvutia kutokana na hali nzuri ya hewa basi hapa Uduzungwa ni sehemu yenyewe. Kwa wanaofanya utafiti kwenye miti au wanaojifunza kuhusu miti mbalimbali basi kwenye hifadhi hii ni sehemu ya kufikiria kwenda kufanya hivyo. Eneo hili la hifadhi ya milima ya Uduzungwa lina aina na jamii nyigi sana za miti na mimea mbali mbali zaidi ya 2500, ambayo kati ya hiyo 160 ni miti ya dawa mbali mbali. Hifadhi hii inayosifika kwa kuwa na miti migi ya dawa zenye kutibu maradhi na magojwa mbali mbali. Hivyo panga kutembelea hifadhi hii maridhawa kabisa.

  1. Sehemu nzuri ya kuwaona ndege (bird watching)

Hifadhi hii inasifika Afrika na duniani kote kama sehemu yenye aina nyingi za ndege, hifadhi ya Milima ya Uduzungwa ni ya pili kwa Afrika kwa kuwa na idadi kubwa sana ya ndege. Na pia hifadhi hii ni muhimu zaidi kwa wale wanaopenda ndege au kujifunza kuhusu ndege, kuna aina zaidi ya 250 ya ndege ambao wanapatikana hapa kwenye hifadhi hii tu, na hawapaikani sehemu nyinge.

  1. Reptilia na Amfibia

Hii ni sehemu muhimu zaidi kwa kuwa ina idadi kubwa ya wanyama kama nyoka, mijusi, vyura na wengine wengi wanaopatikana katika hifadhi hii tu. Kwa mazingira na hali ya hewa ya hifadhi hii ya Uduzungwa ndio inapelekea kuwepo kwa makazi na sehemu salama kabisa kwa wadudu wa aina mbali mbali ambo ni vigumu sana kuwaona sehemu nyingine. Katika hifadhi hii hata mjusi na vyura wanahifadhiwa na kuchukuliwa kwa uzito kama vile wanyama wengine, hii ni hifadhi ya kipekee sana. Kwa utafiti uliofanyika hivi karibuni na watalaamu wa wanyama na wadudu, wamegundua aina za reptilia na amfibia ambao hawapatikani sehemu yoyote ile duniani isipokuwa hapa katika hifadhi ya Milima ya Uduzungwa.

  1. Vipepeo

Kutokana na hali nzuri ya mazingira na miti ya maua mengi kwenye hifadhi hii, basi ndio pamekuwa ndio nyumbani kwa vipepeo wengi sana, ambao wanaifanya hifadhi hii kuvutia na kuwa na mwonekano mzuri. Vipepeo wanavutia sana na wana manufaa sana kwenye ikologia na utunzaji wa uasili wa uoto wa asili na mazingira. Ukitaka kuona vipepeo wengi mpaka ushangae tembelea hifadhi hii miezi ya Disembe mpaka Aprili au Mai.

Kwa utajiri na hali nzuri ya mazingira ya hifadhi hii ilitakiwa kuwa na idadi kubwa sana ya watalii au wageni, ndugu zangu watanzania haina haja ya kuwasubiria wageni kutoka Ulaya au Marekani ndio waanze kutembelea hifadhi hizi, tuanze sisi wenyewe kwa kuwa watalii wa ndani kwenye nchi yetu wenyewe. Hii ndi njia nzuri ya kuinua uchumi kwa nchi yetu. Ni jambo ambalo tunaliweza kabisa, ndio maana nimeamua kuandika makala hizi kwa lugha ya Kiswahili ili kuwahamasisha Watanzania kutembelea hifadhi za wanyama na vivutio vingine vilivyopo ndani ya nchi yetu.

Asante sana kwa kusoma makala hii, najua utachukua hatua nzuri za kujipanga kuitembelea hifadhi hii ya Milima ya Uduzungwa. Ni rahisi sana kufika katika hifadhi hii kwa watu waliopo Morogoro, Dodoma, Dar es salaam, Iringa Mbey, Njombe  na maeneo mengine. Karibuni sana hifadhini.

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

0742092569

hillarymrosso@rocketmail.com