Moja ya kesi iliyotikisa mkoa wa Iringa na Tanzania kwa ujumla ni kesi ya mama Maria Ngoda, aliyehukumiwa kifungo cha miaka 22 baada ya kukutwa na vipande 12 vya nyama ya swala kinyme na sheria.
Sheria zipo ili kulinda watu, mali, kutoa haki na usawa kwa watu. Fikiria nchi ingeongozwa bila sheria, fikiria kusingekuwa na sheria nini kingetokea. Bila shaka kungekuwa na uharibifu mkubwa sana, watu tungekosa ustarabu, amani ingeondoka, mali zingekuwa za wachache wenye nguvu, haki isingekuwepo. Hivyo uwepo wa sheria ni jambo zuri sio tu kwenye kulinda watu bali kulinda na mali na rasilimali nyingine za nchi ili ziwe na manufaa kwa wote.
Sheria inavyofanya kazi ni jambo jingine tunalotakiwa kufahamu, sheria ikitumika inaweza kuleta haki, lakini upande mwingine inaweza kuumiza usipoitii. Hivyo tafsiri ya sheria ni muhimu pia, ndio maana watu wanasoma miaka 4 na zaidi kwa ajili ya kuijua sheria na kuitafsiri kwenye maeneo mbali mbali inakotumika.
Matumizi ya sehria ndio yalimfanya Maria Ngoda aonekana amefanya kosa, tafsiri ya sheria ikamhukumu Maria miaka 22 jela kwa kosa alilofanya. Kwa mujibu wa sheria ya wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009 kifungun cha 86, Maria alifanya kosa na adhabu yake imeanishwa kwenye sheria hizo.
Tukio na kesi ya Maria, ilionekana kama ya kipekee kutokana na hali yake ya maisha na adhabu kubwa aliyopata. Hali yake ya maisha duni pamoja na wategemezi aliyokuwa nao ilifanya watu kuwa na hisia sana kwenye maamuzi ya kesi yake. Wengi waliona kama ameonewa na mahakama haikutenda haki.
Sheria inapofanya kazi haingalii una hali gani kimaisha, ni tajiri au masikini, mweupe au mweusi. Lengo la uwepo sheria ni kutenda haki bila kujali utaumia kiasi gani. Ndio maana Mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Iringa ilifikia kutoa maamuzi hayo juu ya mama mjane masikini na mwenye utegemezi mubwa kutoka kwa watoto wake.
Jamii inatakiwa kufahamu umasikini sio tiketi ya kufanya ujangili au kujihusisha kwenye vitendo ambavyo ni kinyume na sheria za nchi. Kukosa mahitaji muhimu ya kuishi kama vile chakula haikupi uhalali wa kuingia porini kuwinda wanyama bila kibali.
Hata hivyo, umasikini unatajwa sana kama sababu moja wapo kubwa ya watu kujihusisha na kushiriki katika ujangili wa wanyamapori na biashara haramu. Tafiti zinaonyesha kaya au jamii zinazoishi kando ya maeneo yenye wanyamapori wanashiriki katika ujangili wa wanyamapori kwa ajili ya kupata kitoweo na biashara.
Tangu zamani kabla ya ukoloni kuingia katika nchi zetu, wazee wetu walikuwa wawindaji na walitumia wanyamapori kwa matumizi mbali mbali kama vile chakula, dawa, urembo, mavazi, na mambo mengine ya kitamaduni yaliyohusisha kutumia viungo mbali mbali vya wanyamapori.
Matumizi hayo hayakuwa na athari kubwa katika mifumo ya ikolojia, maana yalikuwa ni matumizi ya kawaida na idadi ya wanyama haikupungua wala haikuwa kwenye hatari kama ilivyo sasa. Pamoja na matumizi yote hayo, wazee wetu walikuwa na mahusiano mazuri na wanyamapori, pia kuna wanyama wengine hawakuwindwa kwasababu ya mambo ya mila zao.
Katika kipindi hicho angekuwepo Maria Ngoda na vipande vyake 12 vya nyama ya swala asingehukumiwa kifungo wala kupewa adhabu kwasababu hakukua na sheria kali kama zilivyo leo.
Tangu waje wakoloni kwenye nchi zetu historia ya uhifadhi wa wanyamapori ilibadilika sana. Mfano, waliamua ni nani atatumia wanyamapori, nani hatatumia wanyamapori. Walitunga sheria za wanyamapori kwa matatizo waliosababisha wao wenyewe. Sheria hizo hizo hazikuwa rafiki kwa watu wa chini na masikini, hasa ambao waliishi karibu na wanyama hao.
Ujio wao haukuwa na manufaa kwa wanyamapori wetu kwasababu wanyamapori waliwindwa sio tu kwa ajili ya chakula bali kwa ajili ya biashara. Walivamia mapori na hifadhi zetu za wanyama na kuua wanyama wenye thamani kubwa kama vile tembo, faru, nyati, simba, mamba nk. Wanyama walivunwa kwa kasi kubwa mno kiasi cha kupelekea wanyamapori wengi kupungua kwenye maeneo yao. Mfano, wanyama jamii ya faru hadi sasa bado haijatengemaa kwababu ya ujangili waliofanya.
Wengi katika kipindi hicho waliwinda kwa ajili ya kupata ngozi, mifupa, pembe, meno ya tembo, magamba, kucha, na nyama. Pamoja na kuchukua sehemu za miili ya wanyama, wanyamapori walikamatwa na kuuzwa wakiwa hai. Mfano aina nyingi za ndege, nyani, simba, duma walichukuliwa wakiwa hai na walimilikiwa na familia za kifalme na watu matajiri.
Kutokana na uvamizi kwa wanyamapori kuwa mkubwa na wanyama wengi kuuwawa na kuendelea kupungua. Ilibidi wachukue hatua za kunusura hali hiyo, na hapo ndipo zilipoingia sheria za kusimamia wanyamapori, ambazo kwa kiasi kikubwa ndio zinatumika hadi sasa.
Sheria hizo zilizotungwa na wakoloni zilikuwa na maana zaidi kwao kuliko kwa wazawa. Maana sheria hizo zilikuwa na masharti magumu sana kwa watu masikini kuyatimiza. Hivyo, wazee wetu walinyimwa uhalali wa kuwinda na kutumia wanyamapori kwa uwepo wa sheria hizo.
Sheria hizo zilitoa kibali kwa watu wa ngazi za juu kwenye utawali kuwa na uwezo wa kuwinda na kutimia wanyamapori. Ili uweze kutumia wanyamapori lazima utimize masharti mengi na magumu ya sheria ambayo watu masikini wasingeweza kabisa kuyatimiza. Hivyo, tangu kipindi hicho cha utawala wa sheria za wanyamapori kuingia ndio ikawa ni mwisho wa kuwinda na kutumia wanyamapori kwa watu masikini.
Licha ya sheria hizo kusaidia kwenye uhifadhi wa wanyamapori kwa kiasi fulani, tafiti nyingi zinaonyesha kuwa watu wengi masikini wanabaguliwa kwa sheria hizo, lakini pia wengi hawana furaha na wanyamapori na taasisi zinazosimamia wanyamapori. Hii imetengeneza migogoro mingi isiyoisha kati ya watu na hifadhi za wanyamapori.
Licha ya uwepo wa sheria hizi kali, ujangili na biashara haramu za wanyamapori inatajwa na Shirika la Umoja wa Mataifa kama moja ya biashara kubwa inayofanyika kwa njia haramu, ikishika nafasi ya nne duniani ikiwa sambamba na biashara nyingine haramu kama vile uuzaji wa silaha, biashara ya binadamu na madawa ya kulevya.
Pamoja na kwamba tulipata uhuru miaka mingi iliyopita, bado tunatumia sheria zile zile ambazo tuliachiwa na wakoloni ili kusimamia wanyamapori. Ndio maana hadi sasa ni ngumu sana kwa watu masikini kumiliki na kutumia wanyamapori kihalali.
Mfano mzuri ni uanzishwaji wa bucha za wanyamapori ulioanza mwaka 2020. Lengo la uwepo wa bucha hizi ni ili kila mwananchi apate kitoweo cha nyamapori, lakini pia uwepo wa bucha hizi usaidie kupunguza ujangili, jambo hili lilisemwa tu, lakini utekelezaji wake ulikuwa mgumu sana kutokana na mambo ya kisheria lakini pia mradi huu ulikuwa mgumu kwa watu masikini kuutekeleza.
SWALI; Je, kuna haja ya kupitia na kufanya maboresho sheria zetu zinazosimamia wanyamapori, au zibaki kama zilivyo?
Pia tafiti zinaonyesha gharama na mchakato wa kupata kumiliki wanyamapori kihalali ni kubwa kuliko gharama na hatari za kufanya ujangili. Ujangili kwa ajili ya nyamapori unafanyika sana sehemu nyingi Tanzania. Mfano, fikiria kama mtu anaingia porini mara moja anawinda swala anakuja kumuuza laki tisa (900,000 hii ni makadirio ya vipande 12 vya nyama ya swala aliyokuwa nayo Maria Ngoda, baada ya askari kukadiria thamani ya hiyo nyama). Sasa hii hela sio ndogo kwa watu wanaoishi vijijini. Maana hapo anaweza kukidhi mahitaji yake yote ya msingi.
Pamoja na hatari nyingi za watu kujihusisha na ujangili bado ujangili wa nyamapori unaendelea kushamiri sehemu zenye wanyamapori. Jamii inatakiwa kufiria na kupima tena athari za ujangili, miaka 22 jela, kuwa mbali na jamaa, watoto na marafiki au laki 900,000 ya kufanya ujangili. Najua utachugua kukaa mbali na vitendo vya ujangili.
Jamii inatakiwa kujua kuwa kujihusisha na vitendo vya ujangili au biashara za nyamapori au nyara za serikali unajiweka kwenye hatari kubwa sana. Hata kama hutakamatwa kwa mara ya kwanza, siku zako zinahesabika, hata kama unafanya ujangili na biashara ya nyamapori kwa siri kiasi gani, kuna siku isiyo na jina utakamatwa, kama unabisha muulize Maria Ngoda.
Siku hizi ulinzi wa wanyamapori sio tu kule porini, siku hizi askari wanavaa kiraia, wanaishi nasi mitaani kwetu, wana intelijensia kubwa sana ambayo kama unajihusisha na vitendo vya ujangili ni rahisi sana kukamatika.
Nitoe wito kwa jamii, usiache shida na umasikini ukufanye uongeze tatizo kwenye maisha yako kwa kuingia kwenye vitendo vya ujangili wa wanyamapori. Umasikini ulio nao ukusukume kuchukua hatua sahihi kuuondoa na kamwe usiingie kwenye ujangili, ni hatari mno.
Kesi na tukio la Maria Ngoda litufunze kuachana na ujangili wa wanyamapori, na kuwa sheria za kusimamia wanyamapori zipo vile vile; licha ya Maria kusaidiwa kisheria na kuachiwa huru, isifanye tuingie kwenye vitendo vya ujangili, msaada kama huo sio rahisi kuupata, ndio maana wengi wanaojihusisha na ujangili wapo jela hadi sasa.
Tuwe mabalozi wazuri wa kulinda na kushirikiana na mamlaka za usimamizi wa wanyamapori ili kwa pamoja tulinde na kutunza wanyama wetu kwa vizazi vingi vijavyo.
Imeandikwa na Hillary Mrosso, +255 683 862 481, hmconserve@gmail.com