Kama nilivo kudokeza katika makala iliyopita, tunaendelea tena na mfululizo wa makala za nyoka na hasa kwa kuangazia kundi la nyoka wajulikanao kama swila. Leo tutamfahamu swila mwingine kabisa na yule wa makala iliyopita hasa kwa muonekano na tabia kwa ujumla. Katika makala hii nakuletea swila aitwae SWILA WA MISRI (EGYPTIAN COBRA) kwa jina la kisayansi wanaitwa Naja haje. Soma makala iliyopita kuhusu swila msitu ili kupata mwendelezo zaidi.Mfahamu Swila Msitu (Forest Cobra): Nyoka Mwenye Sumu Hatari Sana
Jina swila wa Misri lisikuchanganye na kujiuliza iweje swila wa Misri anaelezewa katika makala hizi hasa ambazo zimelenga zaidi kwa nyoka wapatikanao Afrika mashariki. Swila hawa wanapatikana pia Afrika mashariki ikiwemo hapa nchini Tanzania pia. Asili ya jina hili la swila wa Misri limetokana na mithiolojia ya watu wa karne za zamani nchini Misri ambazo zilikuwa zinajinasibisha ki miungu zaidi hasa zama za Farao na ndio maana mpaka leo ukiangalia kwenye maeneo ya asili nchini Misri utaona sehemu zilizokuwa za kifalme zina picha na masanamu ya kichwa cha nyoka hawa.
Nadhani mpaka kufikia hapo ndugu msomaji wa makala hizi utakuwa umefahamu ni wapi au asili ya jina la nyoka hawa. Kuitwa swila wa Misri haimaanishi kuwa aina hii ya swila wanapatikana nchini Misri pekee, laahasha!
Namna ya Kuwatambua Swila wa Misri
- Wana miili mikubwa na minene, kichwa kipana ambacho mara nyingi huwa na rangi nyeusi, macho makubwa kidogo huku mboni za macho yao zikiwa za duara.
- Hii ni spishi pekee katika spishi zote za swila ambao wana magamba chini ya macho ambayo yanatenganisha macho na sehemu ya mdomo ya juu kwa swila hawa.
- Wana miili ya duara, mikia mirefu kidogo ambayo huchukuwa asilimia 15-18 ya urefu wa mwili mzima.
- Swila hawa wakubwa hufikia urefu wa mita 2.5 na hii inasemekena ndio rekodi kubwa zaidi. Mara nyingi huwa na wastani wa urefu kati ya mita 1.5-2.4.
- Wana rangi tofauti tofauti kidogo hasa kutokana na mazingira wanayo patikana.
- Kwa ambao wanapatikana Afrika mashariki huwa na rangi ya kahawia, kahawia iliyo changanyikana na nyekundu au kahawia iliyo changanyikana na kijivu mgongoni.
- Sehemu za ubavuni na tumboni huwa wana rangi ya njano au krimu.
- Wana shingo fito pana za rangi ya kahawia au kijivu ambapo zinapo tanuka mpangilio wa magamba kuanzia 8-20 huonekana.
- Wana madomadoa mengi yenye rangi ya kahawia ambayo yamesambaa kuanzia sehemu ya shingoni mpaka tumboni.
- Baadhi yao huwa na magamba ya njano sehemu ya nyuma na krimu sehemu ya tumboni hasa kwa wale wanao patikana kusini mwa Kenya na kaskazini mwa Tanzania.
Swila wa Misri (Picha na Wikipedia)
Tabia za Swila wa Misri
- Swila hawa asilimia kubwa ya maisha yao huishi maeneo ya nchi kavu tofauti na swial wa msituni kama tulivoona hupendelea pia maeneo yenye maji maji.
- Ni miongoni mwa swila wepesi na wana uwezo wa kujongea kwa haraka na kasi zaidi.
- Nyoka hawa hufanya shughuli zao mchana na usiku pia.
- Mara nyingi hupendelea kuota jua kipindi cha mchana ila huwa wanawinda muda wowote.
- Wanapendelea kuishi kwenye mashimo yaliyoachwa na mchwa, sehemu zenye miamba iliyo pasuka na hata kwenye baadhi ya mashimo ya viumbe wengine.
- Ni wepesi zaidi wa kuinuka juu na wana uwezo wa kuinuka sentimita 30 au zaidi huku wakiwa wametanua shingo hasa pale wanapo hisi hatari.
- Wanapo kuwa na hasira zaidi hutoa sauti ya onyo na hutumia sekunde chache sana kugonga tena kwa hasira zaidi.
- Hawa ni miongoni mwa swila warushao sumu kwa umbali wa takribani mita 2-3.
Swila wa Misri akiwa ameinuka akitema mate yake nyenye sumu (Picha na Wild Animals! Amino)
Maeneo Wapatikanayo Swila wa Misri
Swila hawa wanapatikana maeneo mengi barani Afrika. Kwa hapa Afrika mashariki swila hawa wanapatikan sana maeneo savana, maeneo yenye nyasi, maeneo yenye miti kidogo na kamwe hawapatikani maneno yenye misitu. Maeneo haya huwa na muinuko wa mita kati ya 1000-1600 kutoka usawa wa bahari.
Hapa nchini Tanzania nyoka hawa wanapatikana sana maeneo ya Arusha kuelekea kanda ya ziwa hadi maeneo ya Shinyanga. Kuna baadhi ya taarifa ziliripoti kuonekana kwa swila hawa wilayani Kilosa magharibi mwa mkoa wa Morogoro. Hakuna taarifa za kuonekana kwa swila hawa maeneo ya kusini mwa Tanzania japo huenda pia wakawepo kutokana na kuenea kwao katika maeneo mengi sana barani Afrika.
Chakula
Chakula pendwa cha swila hawa ni wanyama jamii ya vyura. Kwa wastani mkubwa sana nyoka hawa wanapendelea kula vyura japo huwinda wanyama wengine pia kama panya, ndege na baadhi ya reptilia wengine wakiwemo mijusi na mayai.
Kuzaliana
- Jike hutaga mayai kati ya 10-20 ambayo huwa na wastani wa ukubwa wa sentimita 5-6 x 3-3.5.
- Mayai huatamiwa kwa siku 48-70, kama miezi miwili
- Watoto wanapotoka kwenye mayai huwa na wastani wa urefu wa sentimita 25-30.
- Watoto wanapozaliwa tu huanza kujitegemea, hakuna malezi ya watoto
- Watoto huwa na rangi ya kahawia, kijivu, machungwa au nyekundu.
- Sifa pekee ya kuwatofautisha watoto wa swila hawa na swila au nyoka wengine ni uwepo wa alama ya pete au ringi nyeusi kwenye shingo.
- Sifa hii huwezi kuikuta kwa watoto wa nyoka wengine duniani.
Sumu
- Hawa ni miongoni mwa swila wenye sumu kali na hatari zaidi. Sumu ya nyoka hawa huathiri pia mfumo wa neva (neurotoxin).
- Sumu hii husababisha hali ya kupooza, kupata shida kwenye kupumua na hatimae husababisha kifo endapo mtu hatopata huduma ya haraka.
- Dalili za mwanzo zinazo onekana endapo mtu ameumwa na nyoka huyu huwa ni maumivu makali eneo la jeraha na uvimbe katika eneo hilo.
- Ukiona dalili kubwa zaidi zimetokea ndani ya saa moja ujue sumu iliyopo mwilini ni nyingi sana na dalili kuu huwa ni kupooza maeneo ya usoni hasa kushindwa kufanya kazi kwa taya, kuto sikia vizuri, kuchanganyikiwa akili, michirizi kwenye misuli na misuli kukaza.
- Baada ya dalili hizo inafata changamoto kwenye upumuaji na kupooza ambapo huanzia kwenye miguu.
- Endapo utaona dalili hizo basi huduma ya kwanza kabisa huwa tunasema ni (pressure bandaging), yaani unamfunga mtu na nguo au kitambaaa juu ya jeraha ili kuzuiya mzunguko wad amu zaidi.
- Pili hakikisha mtu huyo hatembei au kuhangaika ili kupunguza kasi ya mzunguko wada mu na baada ya hapo kama kuna dalili za kushindwa kupumua basi hakikisha unatumia njia yoypote ya asili kumfanya apate hewa ya kutosha ili kumsaidia kupumua.
- Baada ya kutekeleza hayo hakikisha unamuwahisha hospitali ili aweze kutibiwa kitaalamu zaidi.
Mwisho
Makala ijayo tutaendelea tena na aina nyingine ya swila mpaka pale tutakapo maliza swila wapatikanao Afrika mashariki. Hivyo nikusihi ndugu msomaji wa makala hizi kuendelea kufuatilia mtoririko huu wa nyoka aina ya swila mpaka mwisho wake.
Kwa maswali, ushauri au maoni kuhusu makala hii usisite kuwasiliana nami,
Sadick Omary Hamisi
Simu; 0714116963
Email; swideeq.so@gmail.com
Instagram; wildlife_articles_tanzania
Facebook; Sadicq Omary Kashushu/Envirocare and wildlife conservation
Tovuti; www.wildlifetanzania.co.tz
……………………….I’M THE METALLIC LEGEND………………….