Habari ndugu msomaji wa makala hizi za wanyamapori ambazo hukuletea uchambuzi wa kina kuhusu wanyamapori na kukufanya ujifunze mengi zaidi kuhusu wanyama hawa. Leo tena tunaendelea na mfululizo wa makala za nyoka jamii ya swila ambao tumeanzanao katika makala zilizopita. Katika makala hii ya leo nakusogezea aina nyingine ya swila wapatikanao hapa Afrika mashariki na hasa hapa nchini Tanzania. Swila katika makala hii ya leo ni swila ajulikanae kama SWILA WA MSUMBIJI ambao kwa lugha ya kingereza hujulikana kama MOZAMBIQUE SPITTING COBRA huku jina la kisayansi ni NAJA MOSSAMBICA.

Jina hili la swila wa Msumbiji lisikuchanganye sana kwani historia ya swila huyu na jina lake ni kutokana na tafiti zilizo fanyika katika ugunduzi wa swila hawa. Mnamo mwaka 1854 mtafiti aliye julikana kwa jina la Wilhelm Peters aliwaelezea aina hii ya swila baada ya kuwagundua nchini Msumbiji kwa mara ya kwanza na hivyo kupelekea jina Msumbiji kuwa sehemu ya jina la swila hawa. Historia hii inaturudisha nyuma pia hata tulipoona asili ya jina la swila wa Misri kuwa baadhi ya viumbe hai wanapewa majina kutokana na matukio mbali mbali lakini haimaanishi kuwa wanapatikana eneo hilo tu.

JINSI YA KUWATAMBUA SWILA WA MSUMBIJI

Ni swila wadogo, miili yao ni ya wastani yaani sio minene wala sio myembamba sana.

Wana vichwa butu, macho ya wastani huku mboni za macho zikiwa na umbo la duara.

Miili yao ina umbo la bomba na wana mikia mirefu ambayo huchukua asilimia 10-15 ya mwili mzima.

Wana rangi ya zeituni iliyo changanyika na kijivu au kahawia mgongoni huku sehemu ya chini wakiwa na rangi ya pinki au manjano na mistari myeusi sehemu ya shingoni.

Wana magamba malaini/nyororo ambayo yamejipanga kwa safu kati ya 23-25 sehemu ya katikati ya mwili, safu 177-205 sehemu ya tumboni na safu 52-69 sehemu ya nyuma. Magamba ya swila hawa nchani huishia la alama za rangui nyeusi.

Urefu wa mwisho kabisa  wa swila hawa huwa ni mita 1.5 ambapo wastani wao wa urefu hukadiriwa kuwa kati ya sentimita 80 hadi mita 1.3.

Swila wa Msumbiji (Picha na African Reptiles and Venom)

TABIA ZA SWILA WA MSUMBIJI

Wanapo hisi hatari au kutishiwa, swila hawa huinua vichwa juu, wanapanua shingo na kutema sumu. Ikumbukwe kwamba sio lazima kuinua kichwa au kupanua shingo ndio waweze kutema sumu, wana uwezo wa kutema sumu hata bila kufanya hivyo. Njia hii hutumika kwaajili ya kujilinda tu na sio kuwinda. Meno yao yametengenezeka kwa maumbile maalumu kwaajili ya kutema au kurusha sumu. Umahiri wao katika kurusha sumu ni miongoni mwa sababu za swila hawa kuitwa Mozambique spitting cobra.

Kwa kiasi kikubwa swila hawa huishi maeneo ya nchi kavu na wana uwezo pia wa kupanda kwenye miti. Swila hawa ambao ni wakubwa huwa wanapanda miti na wakati mwingine huonekana wakiwa wamelala kabisa kwenye miti hiyo.

Huwa wanapendelea sana majira ya usiku maeneo ya kuzunguka nyumba lakini pia hata kwenye nyumba ambazo hujengwa maeneo ya mshambani wakitafuta mawindo yao kwaajili ya chakula. Hii inatupa picha kuwa nyoka hawa hufanya mawindo yao zaidi majira ya usiku japo kwa watoto huwa wanafanya mawindo zaidi mchana ili kuepuka kugombania chakula na swila wakubwa au hata wakati mwingine wasiliwe na nyoka wakubwa.

Wana uwezo wa kujongea kwa haraka sana na huchukuwa tahadhari ya haraka sana hasa pale wanapohisi kuna hatari.

Majira ya mchana au hata usiku kwa muda ambao wanakuwa hawapo mawindoni swila hawa hupendelea kupumzika kwenye vichuguu, mashimo, kwenye nyufa za miamba au sehemu za chini ambazo zina maeneo salama kwaajili ya kujifichia.

Swila wa Msumbiji (Picha na African Snakebite Institute)

MAENEO WAPATIKANAYO SWILA WA MSUMBIJI

Swila hawa wanapatikana nchi chache sana hapa duniani, nchi hizo zipo bara la Afrika tu huku na sisi hapa nchini Tanzania tukijivunia uwepo wa spishi hii ya swila. Nchi ambazo wanapatikana swila hawa ni Msumbiji, Tanzania, Botswana, Afrika kusini, Angola, Malawi, Namibia, Zambia na Zimbabwe. Aina nyingine za nyoka Mambo Usiyoyajua Kuhusu Tofauti Zilizopo Kati Ya Nyoka Aina Ya Cobra(Fira/Swila) Na Black Mamba(Koboko)

Hapa nchini swila hawa wanapatikana zaidi maeneo ambayo ni chini ya mita 1000 kutoka usawa wa bahari hasa maeneo ya kusini mashariki mwa Tanzania na maeneo ya Morogoro kuelekea kusini hasa hasa maeneo ya ukanda wa pwani, Liwale na Tunduru. Maeneo mengine wapatikao swila haw ani visiwa vya Pemba na Unguja japo kwu Unguja ni kwa nadra sana kuwaona swila hawa.

CHAKULA

Swila wa Msumbiji wanakula aina mbali mbali za viumbe hai wakiwemo vyura, nyoka jamii yao na jamii nyingine, mijusi na wanyama wadogo kama jamii ya panya. Tafiti zinaonesha kuwa swila hawa kuna wakati wanakula mpaka wadudu.

KUZALIANA

Jike huweza kutaga mayai kati ya 10-22 na mara nyingi huwa ni kipindi cha kiangazi kati ya mwezi Disemba-mwezi Januari. Hii ni kwa maeneo yapatikanayo zaidi kusini mwa Afrika. Mayai huwa na ukubwa wa sentimita 3.5 x 2. Mara nyingi watoto hutoka kwenye mayai kwa siku kati ya 48-68.

Watoto wa swila hawa huwa na urefu kati ya sentimita 23-25. Watoto hujitegemea kwa kila kitu mara tu watikapo kwenye mayai. Hawa ni miongoni mwa nyoka ambao huwa hawana malezi kwa watoto hivyo unakuta ni asilimia chache sana ya watoto hukuwa na kufikia umri wa kuzaliana.

SUMU

Swila wa Msumbiji ni miongoni mwa swila hatari na wenye sumu sana ambayo kwa asilimia kubwa sumu yao huathiri misuli na kwa kiasi kidogo sana huathiri mfumo wa veva au mfumo wa fahamu. Soma zaidi makala hii kufahamu nyoka wengine wenye sumu Swila wa Misri (Egyptian Cobra): Nyoka Mwenye Sumu Inayoua Haraka Zaidi

Swila hawa huwa wanauma au kugonga kutokana na hali halisi au mazingira kwa muda huo. Hii inamanisha sio kila wakati watagonga kwa nguvu zaidi au kwa hali ya kawaida. Mazingira na hali ya muda huo ndio hupelekea aina ya shambulio toka kwa swila hawa. Swila hawa wana sumu ambayo ina dhuru kwa njia mbili;

1.Njia ya kurusha sumu (spitting)

Miongoni mwa dalili ambazo hutumiwa ili kujua kwamba mtu kashambuliwa kwa kutemewa na sumu ya swila hawa huwa ni kumuangalia sumu kwenye macho. Dalili ya sumu kwenye macho ni maumivu ya haraka na makali zaidi. Mtu hupata shida kufumbua macho, machozi hutoka bila kutarajia, utandu unaozunguka maeneo ya macho huanza kuvimba na mboni za macho hubadilika na kuwa na rangi nyekundu.

Endapo mtu atachelewa kupata tiba basi sehemu ya kwenye kope huanza kuvimba, utandu wa kwenye macho huanza kuvuja damu na vidonda sehemu ya konea hutokea ndani ya saa 24 na hatimae mtu hupata upofu. Soma zaidi makala hii kufahamu zaidi aina nyingine za nyoka wenye sumu Mfahamu Swila Msitu (Forest Cobra): Nyoka Mwenye Sumu Hatari Sana

Kma sumu imeingia kwenye macho njia haraka ya kwanza ni kuosha macho kwa maji safi yanayo jongea. Endapo maji hakuna basi maziwa pia huruhusiwa kutumika katika kuosha macho. Na endapo upatikanaji wa maziwa ni mgumu basi kwa dharura mtu anaweza kutumia pombe(bia) au mkojo kuoshea macho. Hakikisha unafumbua macho wakati unaosha huku ukiendelea kuzungusha mboni ya jicho ili maji yafike kila sehemu kuondoa sum una baadaya hapo majeruhi apelekwe hospitali kwa matibabu zaidi.

2.Njia ya kugonga (kuuma)

Hii ni njia nyingine ambayo mtu anaweza kudhurika kupitia nyika hawa. Swila waMsumbiji wana uwezo wa kutoa sumu yenye ujazo wa miligramu kati ya 80-200 ambao ni wastani wa miligramu 140 pale wanapo gonga.  Kiwango cha sumu ambacho huweza kusababisha kifo kwa binaadamu ni miligramu 50 tu, hivyo unaweza ukaona ni kwa jinsi gani nyioka hawa pia wana sumu hatari na nyingi zaidi pale wanapo ginga.

Sumu ya nyoka hawa kama nilivo dokeza hapo juu huathiri sana misuli na kama mtu hatopata tiba haraka basi husababisha kuharibika kwa misuli hasa kuanzia maeneo ya sehemu ya jeraha. Hali hii huweza kusababisha mtu kukaa hospitali kwa muda mrefu ili kuhakikisha anapata tiba ya kurudisha sawa hali ya misuli iliyo haribika au kuoza kutokana na sumu ya swila hawa. Lakini kama mtu atawahi kupata tiba mapema basi hali ya kuharibika kwa misuli inaweza isitokee kabisa au ikatokea kwa kiwango kidogo sana.

Tukumbuke tiba pekee ni kupitia kuchomwa sindano ambazo zinakuwa na dawa ya kupambana na sumu ya nyoka husika (anti-venom) ambazo zinapatikana hospitalini tu. Mfahamu Nyoka Hatari Zaidi Duniani, Ana Uwezo Mkubwa Sana Wa Kuua Anapouma

Kuna baadhi ya taarifa kuhusu vifo ambavyo vilitokana na watu kudhuriwa na nyoka hawa japo ni kwa uchache sana. Japo hili haliwezi kutupa ujasiri wa kutokuwahi tiba haraka hasa pale tunapopata madhara yatokanayo ya spishi hii ya swila.

MWISHO

Nakusihi mpenzi msomaji wa makala hizi kuendelea kufuatilia mfululizo wa makala hizi ili uzidi kujifunza mambo mengi sana kuhusu nyoka jamii ya swila. Katika makala ijayo nitakuwekea mezani spishi nyingine ya swila mpaka pale tutakapo wamaliza swila mwapatikanao Afrika mashariki hususani hapa nchuni Tanzania.

Kwa maswali, ushauri au maoni kuhusu makala hii usisite kuwasiliana nami,

Sadick Omary Hamisi

Simu; 0714116963

Email; swideeq.so@gmail.com

Instagram; wildlife_articles_tanzania

Facebook; Sadicq Omary Kashushu/Envirocare and wildlife conservation

Tovuti; www.wildlifetanzania.co.tz

.I’M THE METALLIC LEGEND…