Binadamu ni kiumbe mwenye sifa za kipekee ukilinganisha na viumbe wengine. Kibaiologia binadamu yaani spishi ya Homo sapiensi imekaribiana sana na wanyama jamii ya maswoke kwa takribani 99% ya vinasaba vyao vinafanana. .Utafiti wa muda mrefu juu ya mnyama aina tembo umebaini baadhi ya tabia mabazo wanyama hawa wanzo zinafanana na zile ambazo binadamu anazifanya katika masiha yake ya kila siku. Kuna aina mbili za Tembo, ambazo ni  (Loxodonta Africana na  Elephas maximus) Makala hii ya leo itazungumzia juu ya tabia hizo za tembo ambazo zinafanana na zile za binadam kama ifuatavyo;

Picha hii inatoa taswira ya mambo mengi na tabia za kipekee zinazofanana kati ya Binadamu na tembo. Picha hii imepigwa na Blacke Rose.
  1. Hatua za ukuajia

Mtafiti Amelia Meyer amebainisha hatua kuu tatu  za ukuaji katika Maisha ya tembo ambazo ni  hatua ya utoto, kubalehe na ukomavu. Hatua ya utoto huanza toka tembo anapozaliwa hadi pale anapoacha kunyonyweshwa. Baada ya hapo tembo huingia hatua ya kubalehe ambayo hutofautiana kutoka jamii moja na nyingine na hata kati ya tembo mmoja na mwingine ndani ya familia, umri huo unakadiriwa kuanzia miaka 7 hadi17. Katika kipindi hiki tembo dume huondoka katika familia zao na kwende kuishi katika makundi na tembo dume wenzake yaani kwa kiingereza huitwa bachelor group.wakati huo tembo jike huendelea kubaki katika familia zao. Baada ya kubalehe tembo huingia hatua ya ukomavu ambapo tembo dume huanza kusaka mwenza katika familia ambazo hawana mahusiano. Katika kipindi hichi tembo jike huweza kupata mimba na kuzaa. Hatua hizi zimefanana na zile za binadamu ikiwa ni pamoja na  umri ambao tembo hutoka hatua moja kwenda nyingine

  1. Wastani wa mri wa kuishi

Watafiti wa tembo wamebainisha kuwa katika mazingira asilia tembo anakadiriwa kuishi   miaka 60- 70. Wapo tembo ambao  wameishi hata zaidi ya miaka 80. Huko Kerala India Tembo aitwaye Dakshyani mwezi July, 2017 aliripotiwa kuwa miongoni mwa tembo wenye umri mkubwa zaidi duniani ambapo alikuwa na miaka 86 huko. kwa mujibu wa taarifa za  umoja wa mataifa za mwaka 2019 wastani wa umri wa binadamu kuishi ni miaka72.6 ambao uunashabiiana na ule wa Tembo.

  1. Huishi katika familia

Binadamu huishi kwenye familia ambayo mara nyingi huusisha watu wenye uhusiano wa karibu. Hivyo hivyo na tembo huishi katika mfumo wa familia ambao huundwa na tembo jike pamoja na tembo dume ambao hawajafikia umri wa kubalehe (ndama) wenye uhusiano wa karibu huku wakiongozwa na tembo jike mwenye umri mkubwa aitwaye Matriach kitaalamu.  tembo dume wafikiashapo umri wa kubalehe, huondoka katika familia zao na wanaweza  kuishi katika vikundi wakiwa na madume wengine au peke yao.

  1. Ni mwiko kupata mwenza kutoka  kwenye familia

Tembo dume hutafuta mwenza kutoka kwenye familia nyingine ambayo hawana mahusiano au undugu. Wanyama hawa huepuka mahusiano ndani ya familia ambayo baadae yanweza kuwa na madhara. Hivyo basi tembo dume hulazimika kwenda kwenye familia nyingine na kutafuta mwenza ambaye huweza kuzaa pamoja. Hii huthibitisha  kuwa tembo wana uwezo mkubwa wa utambuzi kwani huwatambua ndugu zao na kuepuka mahusiano hata kama hajaonanana naye kwa muda mreufu. Hili ni jambo la msingi katika ustawi wa wanyama hawa kwani huweza kupata watoto wenye mchanganyiko wa asili za familia tofauti ambao huwa na uwezo mkubwa wa kumudu mazingira yao. Hekima hii ya tembo kuepuka mahusiano na ndugu haina tofauti na jamii nyingi za wanadamu ambapo ndugu kuoana au kuwa na mahusiano huwa ni mwiko.

  1. Mazishi na kuomboleza

Tembo wawapo katika shughuli zao za kila siku huweza kutambua mifupa au mizoga ya tembo waliokufa ambapo husimama kwa muda na kufanya uchunguzi kwa kugusa mwili au mifupa kwa mkonge kisha huufunika (huzika) kwa nyasi au majani. Na kama mzoga wa tembo huyo ana uhusiano na familia basi tembo hao hukaa na mwili siku kadhaa wakiomboleza. Pia tembo huonekana wakitoa machozi pale wanapogundua kuwa mwenzao kafa hususani tembo jike na watoto. Martin Meredeth ni miongoni mwa watafiti walioshuhudia na kurekodi nanma tembo wanavyowazika wenzao na kuomboleza.

Familia ya tembo ikiomboleza kifo cha tembo mwenzao (Chanzo: National Geographic)
  1. Mapenzi ya mama na mwana

Kama ilivyo kwa binadamu  mama na mwana huonyesha upendo usio kifani. Mama hujitoa kumyonyesha kwa muda mrefu, kumlinda na kuhakikisha usalama wa mtoto hata kwa kujitoa maisha yake. Vivo hivo tembo huwa na mapenzi makubwa kwa mwana, humyonyesha kwa takribani miaka mitano na muda wote huo mama hujitoa kwa ajili ya kumtunza na kumlinda mtoto  dhidi ya maadui. Ingawa  usalama wa mtoto tembo huwa ni jukumu la tembo  jike  wote  katika familia, ila mama huonyesha kuguswa sana na mtoto wake mfano  tembo wanapovuka barabara, mama husimama barabarani na kuhakikisha mtoto wake amevuka ndipo naye avuke. Kutokana na upendo wa mama na mtoto tembo mwenye mtoto huchukua tadhari sana na huwa tayari kupambana na kitu chochote kinachoweza kumkaribia au kumdhuru, hivyo haina budi kuchukua tahadhari kubwa unapomwona mwana tembo, usimkaribie ama kumchezea.

Mama akihakisha usalama wa mwana avukapo barabara. (Chanzo; The Citizen.

  1. Kushirikiana wakati wa shida dhidi ya maadui wao

Kama ilivyo kwa binadamu kusaidiana na hata kuwapa faraja wale wenye matatizo, tembo pia huweza kuwatambua wenzao wasipokuwa na furaha na kuwapa ulinzi pamoja na faraja. Tembo huonesha tabia nyingi za upendo na kujali kama vile kutoa uchafu au kitu chochote kilichojishikiza kwenye wimili  wa tembo menzao. Tembo wana hisia, kama furaha, huzuni na masononeko, na huweza kutambu hisia za tembo wenzao hivyo kushiriki hisia kwa kusaidiana.

  1. Uwezo wa kutambua sura zao

Tembo ni miongoni mwa Wanyama wenye uwezo mkubwa wa kutambua uso wake. Hii imethibitishwa na jaribio liliofanywa kwa kuchora alama kwenye uso wa tembo na baadaye kumuwekea kioo. Tembo alipojitazama kwenye kioo aliweza kugundua alama hiyo usoni mwake na kuanza kuifuta kwa kutumia mkonge wake, hii inathibitisha kuwa tembo anaujua uso wake. Pia tembo hutunza kumbukumbu za maadui wake aliyowahi kukutana nao. Watafiti wameeleza kwamba tembo huweza kuwatambua majangili ambao waliwawinda au waliowauwa wenzao hata kwa miaka  mingi iliyopita.

  1. Husalimia ndugu

Tembo huwa na desturi ya kutembeleana na kuwajulia hali wanafamilia ambao wametengana. Tabia hii imeonekana kwa tembo dume wanapoondoka kwenye familia huwa na tamaduni ya kuzitembelea familia zao za awali ili kuwasalimia. Pia pale familia ya tembo inapotengana au kugawanyika kutokana na sababu mbalimbali mfano familia kubwa, migogoro na uhaba wa chakula tembo huendelea kudumisha undugu kwa kukutana mara kwa mara

  1. Huwa na muda wa kustarehe

Binadamu huwa na desturi ya kutenga muda wa kustarehe kwa kufanya mambo mbalimbali vivo hivo kwa wanyama hawa hutenga muda pia wa kucheza na kufarahi. Mara nyingi Kuchezea matope, hukukaa na marafiki na kuogelea; kam sehemu ya wao kucheza.

Tembo wakiogelea (picha na Peter Chadwick)

Hitimisho

Pamoja na kwamba tembo ameonyesha tabia hizi kumi ambazo zinafanana na baadhi ya tabia za  binadamu bado binadamu ndiye adui namba moja wa tembo. Ikumbukwe  kwamba ni nadra sana porini kuona tembo anawindwa na wanyama wanaokula nyama kama vile samba, fisi,chui, mbwa mwitu na duma. Binadamu pekee ndio amekuwa chanzo kikuu ya kukatisha uhai wa wanyama hawa. Ujangili utokanao na tamaa ya pesa na mali zimekuwa tishio kubwa kwa mnyama huyu. Vile vile migogoro kati ya binadamu na tembo nayo imefanya maisha ya wanyama hawa kuwa hatarini hususani pale wanapowaua kwa ajili ya kulipa kisasi pale tembo anapoharibu mazao.

Hatuna budi kupambambana kwa pamoja kupunguza mauaji ya Tembo na kupunguza migogoro kati ya binadamu na tembo ili kuwalinda tembo wetu.

Asante sana kwa kusoma Makala hii!

Imeandaliwa na Lucia Romward mhitimu wa chuo kikuu cha DSM na kuhaririwa na Alphone Msigwa , Mwikolojia Hifadhi za Taifa Tanzania.

Mawasiliano

Email: luciaromward@gmail.com

Mobile: +255(0)743927610

LinkedIn: https://www.linkein.com/in/lucia-romward-9aa27b1b4