Habari Rafiki msomaji wa makala hizi za wanyamapori, katika makala hizi tunzaangazia mambo mengi yanayohusu sekta ya maliasili na utalii ambapo tunapeana ufahamu na maarifa ambayo husaidia katika maamuzi na katika kuwa na uwelewa wa mambo fulani kwa ajili ya kuwa na ustawi kwenye maliasili zetu.

Maisha ya binadamu siku zote yanatawaliwa na changamoto, hata ukiwa mjini utakutana na changamoto, ukiwa vijijini utakutana na changamoto popote pale tunapoishi kuna changamoto ambazo hutufanya kufikiria namna nyingi ya kubadili mfumo wa maisha yetu ya kila siku, wakati mwingine tunalazimika kuachana na baadhi ya maisha ya mazoea ili tuweze kumudu maisha yetu.

Leo nimeandika makala hii kwa lengo la kutaka kuifahamisha jamii hizi zinazoishi kando ya hifadhi za wanyamapori kuwa sio wao pekee ndio hupata changamoto ya kuishi maisha yao. Natambua changamoto kubwa iliyopo kwenye maeneo haya, unalima mazao yanaliwa na wanyamapori, unafuga mifugo inaliwa na wanyamapori, na mazingira halisi ya maeneo haya ni magumu sana kwa watu kuwa na njia nyingi za kuzalisha kipato.

Lakini tunatakiwa kutambua kuwa licha ya changamoto hizo, lazima maisha yaendelee na wanyamapori waendelee kuwepo, hatuwezi kuwaua wanayamapori kwa ajili ya changamoto ndogondogo tunazokutana nazo. Tunatakiwa kila mara kubuni njia ya kusuluhisha na kumaliza au kupunguza hali hiyo.

Tunatakiwa kufahamu pia, sisi ni tofauti kabisa na wanyamapori na wala hatupaswi kuwa kwenye ushindani wa kuishi, sisi binadamu tuna akili na utashi wa kutosha kuishi maisha yetu sehemu mbali mbali. Lakini sivyo kwa wanyama na mimea wao hawana utashi wala namna ya kuelewa changamoto tulizo nazo, wao wameumbwa walindwe na kutawaliwa na binadamu. Hivyo basi tunatakiwa kutumia busara na hekima kuishi na wanyamapori kwa manufaa.

Ni wakati wa jamii hizi kufahamu kuwa uwepo wa wanyamapori na maliasili hizi ni muhimu sana kwenye mfumo mzima wa maisha ya viumbe hai hapa duniani. Na kwa kutambua hilo tunatakiwa kuwa na maarifa na hekima ya kutunza mazingira yetu haya kwa gharama zote, ili kuhakikisha hayaharibiwi na yanaleta manufaa kwa vizazi vya sasa na baadaye.

Mfumo wa maisha ya watu kwenye maeneo haya unatakiwa kubadilika ili kuendana na hali halisi ya mambo, kwa ufahamu kuwa wanyamapori watabakia kuwa wanyamapori na kamwe hawatabadilika kutokana na uhalisia huo, hivyo ni wajibu wetu sisi binadamu amabao tumepewa utashi wa kufanya maamuzi na kubadilika, kuishi maisha ambayo hayana madhara kwa viumbe hawa muhimu.

Ni muhimu tukajifunza namna nyingine ya kuishi maisha ambayo sio ya kutegemea maliasili za misitu na wanyamapori moja kwa moja, kwa mfano kama ni wakulima, wakabuni njia bora za kilimo chenye tija hata kama kitafanyika katika eneo dogo, wafugaji na wengine pia wakajifunza namna nyingine za kupata kipato kwenye maisha yao bila kuwa na utegemezi kwenye maeneo ya wanyamapori.

Tukifanya jambo hili kubwa tutakuwa tunaihakikishia dunia kuwa itaendelea kuwa ya kijani, na itabaki kuwa sehemu salama ya kuishi viumbe hai wote, hiki ndicho kitu bora tunaweza kufanya kwenye maisha yetu.

Nakushukuru sana Rafiki kwa kusoma makala hii hadi mwisho, naamini umepata mwanga kwenye masuala haya ya uhifadhi wa maliasili zetu. Karibu tuendelee kujifunza zaidi kwenye makala ijayo hapa hapa kwenye mtandao wako wa Wildlife Tanzania. Pia usiache kuwashirikisha wengingi haya uliyojifunza hapa.

Hillary Mrosso

+255 683 862 481

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtalaam.net/wildlifetanzania