Mapinduzi ya viwanda yaliyotokea miaka mingi iliyopita yanaweza yasiwe na msukumo mkubwa kwa ukuaji wa uchumi kwa nchi nyingi za Afrika, ukuaji wa teknologia na urahisi wa kupata taarifa unaweza usituinue maisha ya watanzania masikini waliopo vijijini. Ukuaji wa sekta ya kilimo barani Afrika na kuongezeka kwa ushindani kwenye masoko ya mazao ya shambani unaweza usitutetee kwa kasi ukuaji wa uchumi wa Tanzania kwa miaka mingi ijayo. Kila nchi duniani inatumia kile inachozalisha na kukiboresha zaidi kwa kutumia teknologia zao ambazo ni za kisasa ili bidhaa zao ziweze kuhimili ushindani wa kimataifa dhidi ya bidhaa za nchi nyingine. Hivyo nchi ambazo ndio zina amka sasa kwenye masuala ya kuwa na viwanda vya kuzalisha bidhaa zenye ubora wa kuhimili hadhi ya kimataifa zinaweza kusubiri sana kwenye jambo hilo.

Naandika haya kwa uzoefu na kuona jinsi hali ya mambo inavyokwenda, mara nyingi utasikia malalamiko ya wafanyabiashara wa Tanzania na wakati mwingine Afrika bidhaa zao zikikataliwa kwenye masoko ya kimataifa, wamekua wanaambiwa bidhaa zenu hazina ubora, mara hazifai kuuzwa kwenye masoko ya kimataifa, chanzo sio bidhaa kuwa ni mbaya hapana, bali ni teknologia ambayo inatumika kwenye uzalishaji na ufungaji wa bidhaa hizo. Kwa miaka mingi kumekua na kilo hiki, na wadau wa maendeleo wamekuwa wakizishauri serikali zetu kuweka viwanda vya kisasa na vyenye ubora wa kimataifa ambavyo ndio vitatumika kuzalisha bidhaa na kupata hadhi ya kimataifa.

Hivyo ndivyo hali ya mambo ilivyo kwenye sekta nyingi za uzalishaji na ukuzaji uchumi hapa nchini. Kwa kweli bidhaa nyingi tunazoagiza kutoka nje zinaweza kutengenezwa hapa hapa Tanzania, lakini kikwazo kikibwa ni teknolojia kuwa hafifu na isiyokuwa na ushindani wa kimataifa, matokeo yake wanakuja kuchukua malighafi za kuzalisha bidhaa huku Afrika na kuzalisha bidhaa ambazo wanatuuzia kwa bei kubwa sana. Huu ndio ukweli kwenye mfumo wa ukuaji wa uchumi wetu, tunategemea kukua kiuchumi kwa njia hiyo, ambayo ni ngumu sana na itachukua miaka mingi kufikia uchumi wenye nguvu.

Pamoja na kwamba kwenye maeneo hayo yote tunaonekana kutofua dafu kushindana kiuchumi na mataifa makubwa yaliyoendelea miaka mingi. Bado sisi ndio kiini na kitovu cha utajiri hapa duniani. Nasema hivi kwa kugeuzia jicho langu kwenye sekta ya maliasili na utalii. Haaah watatushinda koote lakini sio hapa, kwa jinsi tulivyobarikiwa na kuwa na hifadhi kubwa sana ya maliasili muhimu na endelevu, hapa hawatatuweza hata kidogo, hili ni jambo ambalo haliangaliwi na watu wengi kama njia ya uhakika na ya kudumu ya kupata fedha ambazo ndio itakuwa kichocheo kikuu cha kukua kwa uchumi.

Ipo hivi rafiki yangu, Tanzania inaheshimika na kuangaliwa zaidi duniani kama sehemu yenye idadi kubwa sana ya hifadhi za asili kabisa za wanyamapori na misitu. Hali ii ndio inatoa matumanini na msukumo mkubwa kwa wadau wa mazingira na uhifadhi wa wanyamapori kuvutika kuja kuwekeza ili iendelee kubaki kama eneo bora zaidi duniani. Hii yote ni kwa sababu ya sera na sheria za nchi yetu kujali na kutenga maeneo ya kutosha zaidi ya asilimia 30 ya ardhi yote ya Tanzania imetengwa kwa ajili ya maliasili. Tanzania ndio sehemu unayoweza kuona idadi kubwa zaidi ya wanyamapori kuliko sehemu yoyote ile Afrika na duniani. Hata wanyamapori ambao wapo hatarini kutoweka au wanyamapori ambao hawaonekani kirahisi ukija Tanzania utawaona wa kutosha.

Kwa kutambua hilo, hapa ndipo pakuonyeshea ubabe wetu na hakuna anayeweza kushindana na sisi kwenye hili wala kusimama mbele yetu. Hivyo basi hii ndio njia yetu ya uhakika ya kutengeneza na kukuza uchumi wa nchi yetu. Kupitia maliasili hizi tunaweza kuwa na uhakika wa kupata pato endelevu linalokua kila kukicha. Na endapo tutakuwa na sera bora kabisa kwenye sekta hii tutanufaika sana na uwepo wa maliasili zetu.

Na ili tuendelee kuwa na ushindani kwenye sekta hii ni lazima juhudi za makusudi zichukuliwa na zifanyike, tunatakiwa kuboresha na kuweka mazingira bora kabisa ya kuinufaisha jamii kwenye usimamizi na matumizi ya maliasili kwa watanzania wote. Tunatakiwa kufika mahali ambapo kila mtanzania hasa wananchi waishio kndo na hifadhi za wanyamapori na misitu wataona fahari kutetea na kulinda maliasili hizi kwa uzalendo wa hali ya juu. Njia hii ndio itakoyotoa mwelekeo wa kudumu wa uhifadhi shirikishi kwenye hifadhi zetu.

Tunatakiwa kujifunza kwa wenzetu na pia kujifunza kutokana na makosa yetu wenyewe kwenye sekta hii, wenzetu hawana tena misitu mikubwa ya asili kama sisi, hawana maeneo ya kutosha ya hifadhi za wanyamapori na pia hata hali ya hewa wamechangia kwa kiasi kikubwa kuiharibu kutokana na sera mbovu na tamaa ya kupata utajiri wa haraka, sasa wanahaha kurejesha tena mazingira ya asili waliayoyaharibu, na wanatumia gharama kubwa sana kufanya urejesho huo. Hili halitakiwi kutokea kwetu. Tunatakiwa kuona mbali zaidi, tunatakiwa kuwa na mfumo bora kabisa na wenye tija kwa jamii na taifa kuhusiana na uhifadhi maliasili zetu.

Hatutakiwi kwenda kwa tamaa ya kupata utajiri wa haraka kwa nia ya kuharibu maeneo ya asili, kwa sababu hata hivyo tulishachelewa kufanya hivyo, hivyo ni bora tukawa na njia nyingine mbadala itakayosaidia kuinua uchumi kuliko kuharibu kitu ambacho hatuwezi kukirudishia kwenye hali yake ya mwanzo, na hata kama tutafanya hivyo tutatumia gharama kubwa sana. Tuwe makini na tuchekeche kila wazo linapokuja kutishia uwepo wa maliasili zetu. Tuwe na ujasiri na nidhamu kubwa ya kuzuia hisia zetu ili tuweze kusimamia vizuri maliasili zetu.

Kwa maoni, maswali, ushauri au mapendekezo karibu uwasiliane nami kwa mawasiliano yaliyopo mwisho wa makala hii.

Ahsante sana!

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 862 481/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania