
Dunia inakabiliwa na majanga mengi sana ya kimazingira, majanga hayo ni uchafuzi wa mazingira, uharibifu wa maeneo ya hifadhi ya misitu na wanyamapori, ongezeko la mimea vamizi, mabadiliko ya tabia nchi na biashara haramu ya mazao ya wanyamapori. Haya ni baadhi tu ya majanga mabaya yanayoisumbua dunia kwa sasa.
Nchi nyingi zenye maeneo ya hifadhi za misitu na wanyamapori zinakabiliwa na hatari kubwa ya kutoweka kwa spishi muhimu za wanyama na mimea kutokana na matumizi makubwa ya wanyamapori na mazao yake. Mazao ya wanyamapori kama vile nyama, kucha, pembe, kwato, ngozi, mafuta, magamba, manyoya, yanatajwa kwa na matumizi mengi sana kwenye nchi mbali mbali.
Mfano, nchi nyingi za Afrika ikiwemo Tanzania hutumia zaidi mazao ya wanyamapori kama kitoweo, dawa, na njia ya kuingiza kipato cha ziada. Nchi za magharibi na Asia, hutumia mazao ya wanyamapori kama chakula cha watu wa hadhi ya juu kwenye maisha, hutumia kama dawa, mapambo, mavazi na vinywaji.
Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani zenye maeneo mengi na makubwa ya hifadhi za misitu na wanyamapori. Takribani 40% ya ardhi ya Tanzania imetengwa kwa ajili ya uhifadhi wa maliasili za misitu na wanyamapori. Maeneo hayo yanakabiliwa na changamoto nyingi sana ikiwemo uvunaji haramu, biashara haramu za wanyamapori na mazao yake.
Matumizi mengi na makubwa ya mazao ya wanyamapori yamepelekea kushamiri kwa ujangili na uvunaji haramu wa wanyamapori. Hali inayoleta tishio kwenye uhifadhi enedelevu wa maliasili hizi muhimu. Tafiti nyingi zinaeleza maeneo ya hifadhi za maliasili hizi yapo hatarini kuvamiwa kila mara kutokana na kuongezeka kwa shughuli za binadamu kwenye maeneo haya.
Mfano, mwaka 2018 shirika la umoja wa mataifa la uhifadhi wa maliasili (IUCN) lilitangaza kuwa zaidi ya spishi 26,500 zipo hatarini kutoweka, ikikadiriwa zaidi ya 41% ya amfibia, 25% mamalia, 31% viumbe wa baharini kama shaki na rays, 33% matumbawe na 14% ni ndege wapo hatarini kutoweka kabisa kutokana na ujangili na biashara haramu.

Biashara haramu ya wanyamapori inakadiriwa kufikia zaidi ya dola za kimarekani bilioni 7 hadi bilioni 23 kwa mwaka. Taarifa za umoja wa mataifa zinaonyesha kuongezeka kwa biashara hizi zaidi ya mara 3 hadi mara 5 kila mwaka. Hizi ni takwimu za kutisha sana kwenye uhifadhi endelevu wa maliasili hizi, Jumuiya ya Kimataifa na nchi zenye maliasili hizi zinatakiwa kuwa msitari wa mbele kupambana na ujangili na biashara hizi haramu za wanyamapori.
Watafiti wa masuala ya wanyamapori wanadai takwimu hizi ni makadirio madogo sana, kuna uwezekano ujangili ukawa zaidi na biashara haramu Zikawa zaidi ya makario yaliyoripotiwa. Kutokana vitendo hivyo kuwa haramu hata upatikanaji wa taarifa za kutosha ni mgumu, hivyo taarifa nyingi hazijapatikana kwenye maeneo mengi.
Maeneo haya ya hifadhi za wanyamapori na misitu yanazungukwa na jamii nyingi za watu wenye vipato duni na maisha magumu. Ugumu wa maisha na umasikini umechangia sana uharibifu kwenye maeneo haya. Tafiti kwenye maeneo haya kuhusu uwindaji haramu, uharibifu wa misitu na biashara haramu za mazao ya wanyamapori zinaonyesha tishio kubwa la kutoweka kwa mimea, wanyama na mifumo muhimu ya ikolojia ya hifadhi hizi.
Licha ya uwepo wa sheria zinazokataza uvunaji haramu na uvamizi kwenye maeneo ya hifadhi za wanyamapori na misitu, bado sehemu nyingi zenye rasilimali hizi zinakabiliwa na uvunaji haramu na matumizi yaliyopitiliza ya mazao ya wanyamapori.
Mfano, sheria ya wanyamapori ya namba 5 ya mwaka 2009 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kifungu cha 18 na 19, vinakataza na kuzuia vitendo vyote vya uharibifu wa maeneo ya hifadhi kama vile kuchoma moto, kuua wanyama, kuwajeruhi wanyama, kukata miti, au kuwinda, kuua au kumsababishia mnyama mateso.
Ifahamike kuwa masuala yote ya uwindaji, au kufanya shughuli zozote ndani ya maeneo ya hifadhi za wanyamapori na misitu yanafanyika kwa kibali cha maandishi na ruhusa maalumu kutoka kwa mamlaka husika na kwa Mkurugenzi wa wanyamapori.
Endapo mtu atakiuka sheria hii kwa kufanya vitendo vya ukataji miti, kuchoma maeneo ya hifadhi, kuwinda au kukamata wanyamapori bila kibali cha maandishi kutoka kwenye mamlaka za usimamizi au kwa Mkurugenzi wa wanyamapori basi anafanya kosa kubwa sana, na adhabu yake ni kifungo cha miaka 5 hadi 10. Au kulipa faini isiyopungua shilingi 500,000 hadi 2,000,000 au vyote kwa pamoja.
Licha ya uwepo wa sheria hizi na adhabu zake, bado tunashuhudia kushamiri kwa uwindaji haramu na biashara haramu za mazao za wanyamapori. Endapo juhudi kubwa hazitachukuliwa tatizo hili litaendelea kuwa kubwa na kujenga mtandao mkubwa na mataifa ya nje kama China na nchi za Ulaya ili kuendesha biashara haramu za nyara za wanyamapori.
Tunatakiwa kuchukua kila hatua kupunguza au kutokomeza ujangili kwenye hifadhi zetu. Jamii inapaswa kujua madhara ya uwindaji haramu kiuchumi, kiikolojia na kiafya kuliko hata faida zake. Tunatakiwa kushirikiana na serikali pamoja na wadau wengine kupiga vita ujangili na biashara haramu za mazao ya wanyamapori.
Ungana nami hapa, kupiga vita ujangili na uharibifu wa mazingira.
Washirikishe wengine Makala hii.
Makala hii imeandikwa na,
Hillary Mrosso
+255 683 863 481


Kazi ya kutunza uoto wa asili Ni muhimu ingawa mamlaka za serikali za miji,manispaa na vijiji hawajali kivile.Hapa IRINGA, ukataji miti kwa shughuli mbalimbali za kibinadam ,kilimo na ujenzi imekuwa tatizo kubwa hifadhi ya msitu wa asili wa Igeleke.Jamii inawaona na kuwachukulia Kama watu wabaya wote waliosimamia ulinzi na utunzaji was msitu huuo Hadi kutaka kuwakata mapanga.
Asante sana Mbonayo kwa mrejesho huu. Ni kweli maeneo mengi kuna changamoto kubwa sana ya watu na wakati mweingine mamlaka za usimamizi wa maliasili na uoto asilia kutowajibika vya kutosha kuzuia uvunaji haramu. Maeneo mengine kuna jamii zinawachukia wanaotunza na kusimamia maliasili hizi, kwasababu mbali mbali, kubwa ikiwa ni kunufaika na maliasili hizo kinyume na sheria. Hivyo ndio lengo la makala hizi kusaidia jamii kutambua wajibu wao ni kushiriki kikamilifu katika ulinzi wa maliasili hizi, pamoja na kutoa ushirikiano kwa wanaofanya shughuli hizi muhimu za uhifadhi wa maliasili zetu.
[…] Makala iliyopita niliandika kuhusu changamoto mbalimbali ambazo wanyamapori wanakabiliana nazo ikiwepo ujangili na biashara za mazao ya wanyamapori. Katika makala ile nilieleza jinsi matumizi yaliyopitiliza yanavyo weza kusababisha kukosekana kwa uhifadhi endelevu wa misitu na maeneo ya hifadhi za wanyamapori. Makala hiyo inapatikana katika tovuti yetuTishio Kubwa Kwa Wanyamapori Na Mazingira Tanzania […]
Kazi nzuri sana
[…] Wakati nasoma utafiti huu nilishituka sana kuona kuwa zaidi ya 91% ya majangili waliokamatwa katika eneo la Serengeti walikiri kuwa wanawinda wanyamapori kipindi nyumbu wanapohama (Wildebeest Migration). Hizi ni takwimu za kutisha sana zinazoonyesha kikuthiri kwa ujangili kwenye maeneo yeneye wanyamapori. Hivyo, juhudi za usimamizi na ulizi wa wanyamapori zinatakiwa kuongezwa zaidi sehemu zenye takwimu kubwa za ujangili kama sehemu hizi za njia za wanyama wanapohama kutoka eneo moja kwenda jingine. Soma zaidi hapa Tishio Kubwa Kwa Wanyamapori Na Mazingira Tanzania […]
[…] Wakati nasoma utafiti huu nilishituka sana kuona kuwa zaidi ya 91% ya majangili waliokamatwa katika eneo la Serengeti walikiri kuwa wanawinda wanyamapori kipindi nyumbu wanapohama (Wildebeest Migration). Hizi ni takwimu za kutisha sana zinazoonyesha kikuthiri kwa ujangili kwenye maeneo yeneye wanyamapori. Hivyo, juhudi za usimamizi na ulizi wa wanyamapori zinatakiwa kuongezwa zaidi sehemu zenye takwimu kubwa za ujangili kama sehemu hizi za njia za wanyama wanapohama kutoka eneo moja kwenda jingine. Soma zaidi hapa Tishio Kubwa Kwa Wanyamapori Na Mazingira Tanzania […]
[…] Pamoja na hayo, sheria hii pia inatoa ruhusa na vibali kwa watu kumiliki baadhi ya nyara. Hivyo, kama unapenda kumiliki nyara za wanyamapori unaweza kuwasiliana na mamlaka husika na kupeleka maombi yako ili upewe kibali cha kumiliki nyara unazotaka. Ikumbukwe kuwa, nyara zote za wanyamapori ni mali ya serikali kwa mujibu wa sheria ya uhifadhi wa wanyamapori Tanzania. Endapo utafanya kinyume na utaratibu huo, utakuwa umefanya kosa kwa mujibu wa sheria hii. Soma zaidi makala hii Tishio Kubwa Kwa Wanyamapori Na Mazingira Tanzania […]