Habari msomaji wa makala za blog yako ya wildlife Tanzania, naamini umekuwa na wakati mzuri kwa sherehe za Sabasaba zilizopita. Karibu kwenye  makala yetu ya leo kwenye uhifadhi wa wanyamapori. Kila sekta inahitaji watu wanaokidhi vigezo na masharti ambavyo ni pamoja na kusudi na nia ya dhati ya mtu husika kutaka kufanya kitu anachokipenda. Furaha ya maisha siku zote ni kufanya kile kitu ambacho kinakupa furaha, na mara nyingi vitu vinavyokupa furaha ya kweli kwenye maisha ni kujua kusudi la kuumbwa kwako ambalo ndilo litakupelekea kufanya kile ulichoumbwa kukifanya. Kuna mambo mengi sana ya kufanya kwa kila mtu, na sio lazima ufanye kila kitu, tunatakiwa kuchagua sehemu ambayo unajiona unafaa kufanya kazi kwa upendo na kwa moyo wote.

Jinsi siku zinzvyokwenda watu wengi wanaanza kuangalia sehemu zenye hela ndio wanasomea, mtu anakwambia somea wanyamapori hiyo ni kozi ambayo inalipa sana, au mtu anakwambia somea ualimu hiyo ni kozi ambayo inalipa na ina mkopo asilimia mia pamoja na mambo mengine mengi yanayofanana na hayo, ambayo yanawatoa watu kwenye vitu wanavyvipenda. Mtu anapenda uhasibu au mambo ya mahesabu lakini hapo hapo anakutana na ndugu yake au marafiki wanamshauri asome kitu kingine ambacho hakipendi kabisa. Hili ni jambo ambalo lipo sana kwenye jamii zetu. Na hii ndio sababu kubwa inayosababisha kuwa na watu wasiowajibika na watu ambao wanataka hela tu, yani yeye kilichomsukuma kusoma kozi fulani au masomo fulani ni kwasababu ina ajiri sana na pia inatoa pesa nyingi, hii sio sawa kabisa.

Katika kitengo chochote au sehemu yoyote unayotaka kufanya kazi na uache alama ni lazima uipende hiyo kazi, iwe ndio kusudi lako, usiingie tu kichwa kichwa angalia unachopenda kufanya na Maisha yako ukiwa bado hai na ufanye kwa nguvu zako zote. Kila sekta imevamiwa na watu ambao wanafanya kazi ambazo hawazipendi. Kwenye uhifadhi wa wanyamapori nako ni hivyo hivyo, kuna watu wapo huko wanalalamika sana, na wengine wamekuwa mzigo na matatizo badala ya kutatua matatizo ya kazi zao na wanyamapori wao, ndio wamekuwa watu wa mshahara tu, watu wa pesa pesa tu bila kufanya kazi kwa moyo na kwa juhudi.

Wanafunzi na watu wengine wanaopenda kufanya kazi kwenye sekta hii ya maliasili na utalii, ambayo inajumuisha wanyamapori na kila kiumbe hai, kwanza nataka kuwaambia ni lazima ukubali kufanya kazi sehemu ambazo ni za shari, hakuna mtandao, ni porini, hakuna watu, huko utakutana na miti ndege, milima na wanyama, jifikirie sana unapotaka kufanya kazi kwenye sekta hii. Hii ni sekta ambayo haina wanawake wengi kutokana na mazingira yenyewe kuwa ya tofauti kabisa.

Unapotaka kusoma wanyamapori na kozi nyingine kwa lengo la kuja kufanya kazi kwenye sekta hii inatakiwa ujue kabisa unakuja kufanya kazi nchi nyingine kabisa na ni nchi yenye viumbe hai ambao wanautaratibu wao wa maisha na pia wanajua jinsi ya kuishi na wanajua maadui zao na wanajua marafiki zao, unapoamua kuja kufanya kazi kwenye sekta hii huji kuwafundisha viumbe hai walioko huku porini au hifadhini namna ya kuishi au namna ya kupanga matumizi ya siku. Kila kitu kipo wazi kila kiumbe hai anajua mahali pa kupata chakula,na mahali pa kunywa maji, anajua nini kinaliwa na nini hakiliwi. Wapo wanyamapori wengi sana wa aina tofauti tofauti, lakini cha ajabu kila kiumbe kijajua nafasi yake na eneo lake huko porini. Maisha ya porini ni mazuri sana, wanyama huwa hawaongei kama binadamu, lakini kila kitu kinaenda kwa utaratibu na kwa uasili wake.

Hivyo tunapojifunza elimu mbali mbali za wanyamapori na uhifadhi wao, hatujifunzi ili tuje tuwaeleweshe wanyamapori na viumbe wengine wa porini namna ya kuishi, badala yake tunajifunza maisha na mazingira ya wanyamapori hawa ili tujue nini ambacho hatutakiwi kukifanya na nini ambacho tunatakiwa kukifanya tunapokuwa katika nchi hii ya kigeni. Kwa hiyo ukiwa porini au hifadhini wewe sio mwenyeji hapo, mwenyeji yupo na anajua mazingira yote muhimu kuliko sisi. Hata tusome namna gani mambo ya wanyamapori na mazingira yao, kamwe hatuwezi kuyaishi mazingira yao kama wanavyo yaishi wanyamapori hawa. Ni muhimu tujue elimu ni muhimu ili tuweze kuishi na wanyamapori hawa vizuri bila kuwaletea shida. Hivyo basi eleimu na maarifa tunayoyapata shuleni na hata kwenye maeneo yetu ya kazi yatufanye kuheshimu taratibu na sharia za asili za maeneo yaliyohifadhiwa. Isije kuwa tuanapata elimu ili kuja kuwaharibia utaratibu wanyamapori au kuja kuvuruga maisha ya viumbe hawa. Ndio maana sekta hii inahitaji watu walio na moyo na kuipenda kazi hii hata wakikaa porini mwaka mmoja bila kutoka bado anakuwa nafuraha. Sio umekaa tu wiki mbili umechooka! unataka kwenda mjini mara unataka kwenda kwenu, hapana, tuanataka wahifadhi wa kweli, ambaye hata ukimwambia utakaa hapo porini kwa miaka miwili bila kwenda nyumbani au mjini haoni shida.

Tunawahitaji wahifadhi wenye uzalendo, wenye moyo wa dhati na wakujitoa kabisa kwenye kafanya kazi ya uhifadhi kwa nguvu na juhudi na maarifa.

Asante sana msomaji wangu; washirikishe wengine maarifa haya.

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

0742092569/0683248681

hillarymrosso@rocketmail.com