Habari ndugu msomaji wa makala za wildlife Tanzania, karibu kwenye makala ya leo ambayo nataka kwa pamoja tujifunze na kufikiri kwa kina kuhusu jambo hili muhimu. Kwamba uhifadhi wa maliasili na uwajibikaji kwenye maeneo yetu na kwenye nafasi tulizopewa kama dhamana. Maisha bora sehemu yoyote yanahitaji zaidi ya kuishi na kufanya kazi za kawaida, kila unapoona mafanikio kwenye nyanja yoyote ile kwenye maisha jua kuwa kua hatua za ziada zilichukuliwa na maamuzi magumu kufanyika. Kwenye maeneo yetu na kwenye nafasi zetu kama wahifadhi na wadau wa maliasili, mazingira na uhifadhi kwa ujumla ni kuona tunachokisimamia na kukifanya kinakuwa na mafanikio na manufaa ya kudumu.

Kwa vyovyote vile, kama unafanya kazi kwenye maliasili au kwenye sekta ya wanyamapori, mazingira, misitu au utalii, kuna jambo moja muhimu kulijua siku zote, jambo hilo ni uwajibikaji. Uwajibikaji ni neno ambalo limezoeleka kwa wengi na watu wengi wanalitumia bila kuelewa uzito wake na kuishia kufanya kazi kwa kawaida ili mradi tu wanapata mshahara na siku zinaenda. Kwa nafasi yako kwenye kitengo chochote ulichopewa kama afisa, msimamizi, askari, au meneja. Kuna jambo moja nataka tulielewe jambo hilo ni kuwajibika, na ili uweze kuwajibika vizuri unatakiwa kuelewa kazi uliyopewa na majukumu yako ya kila siku, unatakiwa kuelewa mipaka yako ya kufanya kazi, unatakiwa kuelewa unafanya kazi na nani, unashirikiana na nani kwenye kitengo hicho, hapa namaanisha kuwa unatakiwa kuelewa vizuri kabisa mazingira yote ya kazi zako.

Kwa mfano kama wewe ni afisa wanyamapori wa wilaya, unatakiwa kujua na kuelewa kila kitu kinachofanyika kwenye wilaya yako kuhusiana na wanyamapori, unatakiwa kufahamu kila kinachuhusiana na kuwa karibu na wanyamapori, kuelewa hali na maendeleo ya wanyamapori kwenye wilaya yako, wajue wadau wote wa maliasili na wawekezaji wote wa wanyamapori kwenye wilaya yako. Elewa kwa kina kabisa kila kinachoendelea na kila kitu kinachofanywa na wadau wengine wa wanyamapori kwenye wilaya yako. Usiishie tu kukaa ofisini na kusubiri taarifa kutoka kwa watu wengine, unatakiwa kufika maeneo yote yenye changamoto, unahitaji kufika na kupata taarifa zote muhimu za wanyamapori kwenye wilaya yako.

Ukielewa kazi na majukumu yako vizuri ni rahisi kuchukua hatua za uwajibikaji, usipoelewa au kama huelewi huwezi kuwajibika. Kuelewa jambo ni uwajibikaji pia, kama wewe ni kiongozi kwenye ngazi yoyote ile na huelewi vitu vinavyoendelea kwenye eneo lako la kazi wewe sio muwajibikaji, lakini kama unaelewa basi wewe ni muwajibikaji na utachukua hatua za kukabiliana na hali zote za uharibifu kwenye eneo lako mapema.

Nimeandika makala hii baada ya kuyaona mambo haya sehemu nyingi, kupitia kusoma taarifa mali mbali, kuangalia kupitia TV, na redio na pia kuona kwenye maeneo yetu mambo ambayo kama yataendelea hayatakuwa na manufaa kwenye uhifadhi wa maliasili zetu, tunahitaji kuchukua hatua na kufanya mapinduzi kwenye majukumu tuliyopewa, tuyasimamie kwa nidhamu na kwa uwajibikaji wa hali ya juu. Kwa kufanya hivyo tutaziacha maliasili zetu kwenye mikono salama na hivyo kuwafikia vizazi vijavyo.

Naamini tutajifunza na kufanyia kazi mambo haya tuliyojifunza kwenye makala hii, makala hii itupe nafasi ya kujiangalia na kufanya kila kinachotuhusu kwenye nafasi zetu. Ili kuwe na uhifadhi endelevu inatakiwa kazi kubwa na ya kujitoa kwa kila aliyepewa majukumu ya usimamizi wa maliasili zetu na vitengo vingine, tuna uwezo mkubwa wa kutatua changamoto zetu wenyewe, tuna uwezo mkubwa wa kuhifadhi na kutunza maliasili na rasilimali zetu wenyewe. Linahitajika jambo moja muhimu zaidi ambalo ni uwajibikaji. Kwenye uwajibikaji kuna uwazi, kuna bidii, kuna fursa na pia kuna maendeleo.

Nakushukuru kwa kusoma makala hii, tukutane kwa makala nyingine hapa hapa, mshirikishe na wmingine makala hii. Asante sana.

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 862 481/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania