Kila kukicha kunakuwa na habari mpya, matukio na mambo yanayofanyika wakati mwingine mtu anapoyasikia na kuyaona anaona hakuna tena tumaini la kuishi hapa duniani, akiona juhudi na nguvu wanazochukua Serikali na Mashirika ya kimataifa ili kukabiliana na mambo mabaya yanayotokea watu wanaona kama Serikali na Mashirika ya Kimataifa yanahangaika namna hii kweli mimi ndio nitaweza? Au mimi ndio nitafanya nini sasa.
Kwa miaka michache iliyopita kumekuwa na kiwango kikubwa sana cha ujangili hasa wa tembo kwenye nchi za Afrika hasa Afrika Mashariki na Afrika Magharibi. Kutokana na takwimu zilizoandikwa kwenye gazeti maarufu la National Geographic inaonyesha idadi ya tembo laki moja (100,000) wamepoteza maisha kwa kipindi cha miaka mitatu tu iliyopita katika bara la Afrika. Hii ndio hali mbaya sana ya kutishia usalama na na kukatisha tamaa juhudi nyingi za watu, mashirika binafsi, serikali na mashirika ya kimataifa kwenye vita dhidi ya jambo hili haramu la ujangili.
Kuna watu wakiona hayo wanakata tamaa na kuona kuwa maliasili zimeshaisha, hakuna tena wanyama, hakuna tena miti, hakuna tena misitu, hivyo huanza kupoteza hamasa ya kuwa wafuatiliaji na kutoa ushirikano kwenye uhifadhi wa wanyamapori. Tanzania bado ni mbichi sana na ina maeneo mengi mazuri na salama kwa kuishi wanyama na ndege wengi. Ni jukumu letu kuhakikisha maeneo haya tunaynza kila siku ili yaendelee kuwepo kwa miaka mingi zaidi.
Tanzania yetu ina maliasili na vivutio vingi sana ambavyo bado vinaonekana kama havijaguswa, katika arthi ya Tanzania bado lipo tumaini kwa sababu kwa kiasi kikubwa maeneo yetu bado yapo salama, hakuna uharibifu mkubwa kwenye maliasili zetu. Tunahitaji kuwatunza wanyama na maliasili zetu. Tusichoke kabisa wala kukata tamaa kwenye maliasili hizi muhimu.
Hivyo mambo yanayoendelea hapa Tanzania kwenye maliasili zetu yasitufanye tuone hatuna kitu cha kujivunia tena, tuendelee na juhudi zetu za kufanya mazingira na makazi ya viumbe hai yaendelee kuwa salama kabisa. Tujiwekee jukumu la kuhifadhi na kutunza maliasili zetu katika kizazi chetu. Kwa kuwa bado tupo hai, moja ya jukumu letu kubwa ni kuhakikisha maisha yanaendelea kuwa bora kwa wanyamapori na kwetu wenyewe.
Hatutakiwi kuishia njiani kwenye vita hivi, hatutakiwi kurudi nyuma, hatutakiwi kuacha, wala hatutakiwi kususia mtu mwingine kufanya kazi hii ya thamani.
Asante sana!
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255683 862 481/+255742 092 569
www.mtalaam.net/wildlifetanzania