Habari msomaji wa makala hizi za wildlife Tanzania, ni matumaini yangu kabisa kwamba unaendelea vizuri na unaendelea kupiga hatua kuboresha maisha yako kila siku. Karibu kwenye makala ya leo ambayo nimeiandika baada ya kujifunza mambo mengi sana kuhusu changamoto kubwa zinaoikabili sekta ya maliasili na utalii hapa Tanzania. Lakini sio tu ni changamoto kwa uhifadhi wa maliasili zetu pekee bali ni changamoto kwa uhifadhi wa maliasili za wanyamapori na rasilimali nyingine popote pale duniani. Leo tunaangalia kitu ambacho kimekua hatari sana kutishia uhai na hata kupotea na kutoweka kwa wanyama na viumbe hai wengine kwa haraka sana kuliko hali yoyote iliyowahi kutokea ya mabadiliko ya tabia nchi.

Utajiuliza nataka kuzungumzi kitu gani hicho ambacho kina uwezo wa kuleta madhara na kuwa hatari zaidi kwa uwepo wa maliasili zetu hapa duniani? Kitu hiki sio tu kimesababisha kutoweka kwa maelfu ya wanyama na mimea yetu kwenye hifadhi zetu, bali kimechangia kwa kiasi kikubwa kukosekana kwa haki kwa jamii nyingi, hasa jamii zinazoishi kando kando ya hifadhi za wanyamapori na misitu. Kitu hiki hakija shamiri kwenye sekta hii ya maliasili na utalii pekee, bali hata kwenye sekta nyingine muhimu, kwenye maofisi na kwenye sehemu muhimu za kutolea maamuzi, kitu hiki ni hatari sana kwa maendeleo ya sekta yoyote ile.

Najua umewahi kusikia kuhusu RUSHWA, rushwa inatutesa sana, inatunyanyasa na kutugandamiza sana, kuanzia tajiri hata masikini rushwa inamtesa, kutoka mjini mpaka vijijini rushwa ina nguvu kubwa sana. Rushwa imewabadili watu kutoka kuwa waadilifu na kuwafanya wahalifu na waharibifu, rushwa imepofusha macho ya wengi waliokuwa nayo.  Hapa nikimaanisha waliokuwa na maono makubwa na ndoto nzuri za kuifanya sekta ya maliasili na utalii kuwa ni sekta yenye mafanikio makubwa na yenye kutoa mchango mkubwa ili kuboresha maisha ya watu, ndoto na maono hayo yamezimwa na mipango mibovu na isiyo na tija kwa kizazi cha sasa na baadaya, hii yote ni kwa ajili ya maslahi binafsi na ya muda mfupi.

Rushwa imewafanya wachapakazi kuwa wavivu na wazembe, rushwa imewafanya watu wenye uwezo kuwa watu wasio makini na wasiojali tena. Rushwa imefungua mageti ya chuma yaliyofungwa kwenye hifadhi zetu kuzuia biashara haramu za meno ya faru, pembe za ndovu na biashara nyingine za wanyamapori. Rushwa imewaondoa na wakati mwengine kuwaua baadhi ya watu waliokuwa na misimamo dhabiti ili kuzuia na kukabiliana na mianya ya rushwa kwenye maeneo yao na kutoa haki. Rushwa imesababisha kutokuwepo kwa watu makini na wenye uwezo na weledi kwenye sekta mabali mbali.

Ukisoma ripoti yoyote kuhusu maendeleo ya sekta ya maliasili na utalii huwezi kukosa neno hili rushwa, ukisoma majarida na makala mambali mbali za maendeleo na za kisayansi kuhusu maendeleo ya wanyamapori na maliasili kwa ujumla huwezi kukosa neno hill. Katika changamoto kubwa sana inayotishia maisha ya viumbe hai kwenye hifadhi za wanyama na misitu ni uwepo wa rushwa kwenye  maeneo hayo. Rushwa imeshamiri kiasi kwamba watu wanaona kwamba maisha hayawezi kwenda bila kutoa na kupokea rushwa; pia wengine wanaamini kama vile rushwa haiwezi kuisha, wala kukosekana kwenye sekta hii nyeti.

Nimesoma ripoti mbali mbali za biashara ya meno ya tembo kuanzia kwenye eneo ambalo tembo anaouliwa hadi kumfikia mteja wa mwisho, ni mlolongo mrefu sana ambao unahusisha watu wengi kuanzia masikini mpaka matajiri wakubwa, unaohusisha wasomi mpaka wasio wasomi, mlolongo huu unahusisha wafanyabiashara wakubwa na wale wadogo kabisa, mlolongo huu kwa mujibu wa ripoti hizo unaingia mpaka kwenye maeneo muhimu na nyeti ya kiserikali. Hakuna wakati nilishangaa kama niliposoma moja ya ripoti ya upelelezi uliofanywa na shirika la kimataifa la Elephant Action League kuwa biashara hizi haramu za meno ya tembo zinahusisha hata vikundi vya kigaidi. Katika milolongo hiyo mirefu hakuna anayekubali kukaa kwenye mlolongo huo bila kupewa rushwa, ni pesa nyingi sana zinatolewa kwa kila mhusika wa biashara hii, lakini mwesho wa siku anayenufaika zaidi ni yule aliyeagiza, yaani wauzaji na wasambazaji wakubwa wa meno na pembe za faru, ambao wapo kwenye mataifa makubwa duniani kama vile China, Japani, Marekani, na baadhi ya nchi za Ulaya.

Chakushangaza zaidi ni pale ambapo maisha na hali za uchumi za watu ambao wanajitoa muhanga kwa ajili ya kuingia poring ili kuua au kukamata wanyamapori kwa kupewa maagizo na vijisenti kidogo, hawakumbukwi na maisha yao ni duni sana. Katika kujifunza na kukaa karibu na watu waliowahi kutumwa kufanya ujangili ili kuwaneemesha na kuwafanya wengine kuwa matajiri, watu hawa wamechoka sana, kazi yao ni ngumu na hatari sana lakini wanaishia kupata tu hela ya kula siku mbili tatu tu, lakini wanaonufaika ni wengine kabisa ambao wapo kwenye mataifa makubwa ambao hawawezi kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria, lakini wale wa chini kabisa hakika wakikamatwa watalipia vitendo vyao viovu kwa gharama kubwa sana inayowagharimu maisha na uhai wao.

Kama dharima yetu ni kuhifadhi maliasili hizi tulizopewa na Mwenyezi Mungu, ili ziwe na manufaa kwa maisha yetu ya sasa na kwa vizazi vingi vujavyo, hatupaswi kuwa wazito kuchukua maamuzi magumu kunusuru hali hii kwenye maliasili zetu. Hakuna njia nzuri ya kupambana na ujangili kwenye maeneo yetu kama kutokomeza na kuziba mianya yote ya rushwa kwenye sekta hii. Kwa kufanya hivyo tutapata watu sahihi ambao wanaipenda kazi na wanaipenda kutoka moyoni hata kama malipo ni kidogo na hakuna mianya ya rushwa. Milango ya rushwa imesababisha kupata watu wasio na sifa kwenye uhifadhi, wasiojali, wasio na hata chembe ya uhifadhi kwenye mioyo na maisha yao, walikuja na kuingia tu kwa sababu kuna fedha na kuna njia nyingi za kupata fedha isivyo halali.

Kama taifa tunatakiwa tuwe na dhamira ya dhati kupambana na rushwa kwenye maeneo yetu, tunatakiwa tujenge tena misingi iliyobomolewa na kuharibiwa na watu wenye tamaa ya kuapata mali na utajiri kwa njia zisizo halali kwa maslahi yao binafsi. Hakuna namna ambavyo tutamaliza janga la rushwa kwa kuwaachia serikali na vyombo vya dola pekee kupambana na jambo hili, rushwa inatuathiri sote, inatukwamisha sote, hivyo basi, kwa kutambua hilo jukumu letu kama taifa ni kumbana kwa vitendo ili kuondoa rushwa kwenye jamii zetu, tutengeneze kizazi cha uadilifu na jambo hili linaanza na mimi mwenyewe, anza wewe kuonyesha mfano kwamba hutaki kupokea wala kutoa rushwa. Utakuwa umeasidia sana kuinua misingi ya wema iliyopotea na kuanguka; tuwe wazalendo tusipokee rushwa.

Asante sana kwa kusoma makala hii, naamini umepata kitu cha kufanyia kazi, usiache kumshirikisha na mwezio maarifa haya muhimu. Tukutane kwenye makala ijayo hapa hapa.

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 862 481/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania