Kuna mabo yanaoendelea kwenye jamii zetu na watu wengi hawayaelewi, na wengine wanaelewa lakini wanapotezea, watu wengi wamekosa fursa kwa sababu ya tabia yao ya kupotezea mambo, watu wengi kwenye jamii yetu wamekuwa walalamikaji kwa sababu ya kutokushiriki kwenye mambo nyeti kwenye jamii zao, hivyo mambo yanapoenda ndivyo sivyo wanaanza kuwalaumu viongozi na watu walioamua mambo hayo. Watu wengi wamekuwa na ulimbukeni wa kishamba, hawataki kushiriki kwenye mambo ya kimsingi ya kijamii, hawataki kunekana kwenye vikao au mikutano muhimu yenye hatma na yenye kugusa maisha ya watu wengi. Nimejifunza na nimeona jambo hili lipo sana kwa vijana, wegi hawataki kushiriki mambo muhimu ya kijamii.
Kuna kitu nataka kuwashirikisha leo ndugu zangu, hiki ni kitu ambacho nimekiona sehemu nyingi sana tangu nakua hadi nafikia hapa. Nimejifunza, watu wengi wana ulimbukeni unaokera kama sio wa kishamba, na ulimbukeni huu ni wa watu ambao hawataki kushiriki kwenye mambo muhimu ya kijamii kwa sababu zisizo na msingi wowote. Kwa mfano kwenye Kijiji unaingia mradi mpya wa utunzaji wa mazingira na wanaangaza kwenye Kijiji hicho kila mwanajamii anapaswa kuhudhuria mkutano na mafunzo muhimu ya utunzaji wa mazingira, lakini siku ya tukio unakuta watu wachache sana, na wengine wapo tu wanaendelea na shughuli zao kama vile hawaoni kinachoendelea.
Wakati mwingine miradi hii inaingia na kuanzishwa kwenye maeneo yetu, wanajitoa kufundisha elimu mbali mbali muhimu kama vile afya, utunzaji wa mazingira, uhifadhi wa maliasili, masuala ya lishe na nk. Watu wengi huwa hawashiriki kabisa hawataki mambo ya msingi kwenye maisha yao, hawataki kujifunza , wengine wanajifanya wajuaji hawataki hata kushiriki. Mbaya zaidi wakati mwingine hata viongozi wanakataa kwa makusudi kabisa kuhudhuria na kutoa ushirikiano kwenye mambo muhimu na ya msingi kwenye Kijiji chao, ukiwauliza kwanini hamhudhurii kikao au mafunzo hayo wanasema hakuna posho, wanataka fedha, looh!
Haya ni mambo niliyoyaona kwa macho yangu kwenye jamii nyingi katika nchi yetu, wakati mwingine unakuta miradi hiyo inahitaji watu wa kujitolea ili kufanya jambo fulani kufanikisha mrdi huo wa maendeleo kijijini hapo, tena unaweza kukuta eneo hilo kuna wasomi wana madigrii yao mfukoni hawataki kushiriki kwenye shughuli za maendeleo, ukiwauliza wanakwambia siwezi kufanya kazi ya bure, hawatoe hela hao watu wa mradi, au wakati mwingine mradi unatoa hela kidogo au wakati mwingine hakuna hela, hivyo ushirikiano unakosekana kwenye vitu muhimu sana kwenye jamii zetu.
Ninalotaka kusema hapa ni hili, watanzania wenzangu tunatakiwa kushiriki na kujua kila mradi unaogusa maslahi mapana kwenye jamii yetu, tunatakiwa kuelewa kwa undani ni kitu gani kinafanyika kwenye maeneo tunayoishi, tunatakiwa kuielewa kwa kina miradi yote ya maendeleo kwenye maeono yetu, tusiwaachie vionozi peke yao mambo hayo, tunatakiwa kushiriki na kutaka kujua zaidi malengo, na sababu za msingi za miradi hiyo kuwekeza kwenye maeneo yetu. Tushiriki kwenye vikao na mikutano yote ya vijiji, halmashauri, semina, na mfunzo yoyote yanayotolewa kwenye maeneo yetu.
Sababu kubwa ya sisi kuwa washiriki kwenye mambo muhimu kwenye jamii zetu ni nyingi na ni muhimu sana, itatusaidia hata kutambua ni miradi gani ni mizuri na ni miradi gani ni mibaya, pia tutajua ni mradi gani yenye tija na ni miradi gani isiyo na tija kwenye jamii zetu. Pia ushiriki wetu utawafanya viongozi tuliowapa dhamana kuwajibika na kutenda haki kwenye mambo yote, ushiriki wetu utatengeneza kizazi kinachohoji na kuuliza maswali, kutaka kujua mustakabali wa maendeleo kwenye jamii, na namna rasilimali za nchi yetu zinavyotumika,ushiriki wetu ni muhimu sana kwa maendeleo ya maliasili zetu.
Tunatakiwa tuache kulalamika tushiriki, tuulize, tujifunze na tuchukue hatua mara moja. Hatutakiwi kuwaachi watu wachache waamue mambo nyeti kwenye jamii zetu. Hatutakiwi kuzubaa tena na kujiondoa na kuona huna hadahi ya kushiriki kwenye mambo ya kijamii. Inashangaza sana jamii tuliyonayo, kwa mfano wakitangaza anakuja msanii fulani maarufu kwenye eneo fulani watu watajitokeza kwa wingi sana hata kama wataambiwa walipie. Lakini waambie watu hao hao kwamba kutakuwa na siku ya upandaji wa miti au siku ya usafi kwenye eneo hilo, utashangaa mwitikio wa watu utakavyokuwa wachache; nini ambacho tunakipa kipaumbele kwenye jamii yetu?
Watanzania, hasa vijana wenzangu, tuamke tuache kuwa washabiki wa mambo yasiyo na mchango kwetu wala kwenye jamii yetu, tunatakiwa kuwa nguzo na msaada wa kutegemewa kwenye jamii yetu. Nakwambia hata kama haulipwi na mtu yeyote kwenye kufanya jambo jema kwenye jamii yako usikate tamaa, fanya tu kwa nguvu zako, na kwa ujuzi wako wote. Mungu atakutana na wewe huko huko na atakubariki. Kumbuka sisi vijana ndio wenye nguvu, na tumejaliwa uwezo mkubwa, hivyo tunatakiwa kusimama na kuitetea jamii, Kijiji na nchi yetu. Simama kwa ajilia ya kizazi kichacho, simama utetee maliasili za Kijiji na jamii yako, simama imara uwe sauti ya kizazi kijacho.
Asante kwa kusoma makala hii, washirikishe wengine makala hii.
Ahsante sana!
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 862 481/+255 742 092 569
www.mtaalamu.net/wildlifetanzania