Tutatue Tatizo Hili Mapema

Habari ndugu msomji wa makala hizi kutoka katika blog yako ya wildlife Tanzania.

Kati ya vitu vinavyosababisha migogoro mikubwa kwenye nchi mbali mbali au jamii mbali mbali ni kukosekana kwa uelewa na ufahamu wa jambo au mambo mbali mbali. Kuna mambo mengi yanayosababisha migogoro na migongano kwenye jamii zetu kati ya mambo hayo ni kukosekana kwa uelewa wa kutosha kuhusu mambo ya ardhi, mipaka na sharia za ardhi zilizo wazi kwa kila mtu. Kuna mambo mengi yanayosababisha vita, lakini tukifuatilia historia ya dunia na hasa migogoro na vita visivyoisha chimbuko lake kubwa ni ardhi.

Ardhi ni rasilimali muhimu sana kwa maisha na maendeleo ya kila mtu hapa duniani, lazima tukubaliane kwamba hakuna anayeishi hapa duniani bila kutumia ardhi, ardhi imekuwa ndio kila kitu kwa mustakabali wa maendeleo na mafanikio kwa watu wengi.

Tukisoma historia ya maendeleo na mapenduzi ya viwanda yaliyotokea duniani ni kwasababu ya ardhi, kuinuka na kupinduliwa kwa falme, yote haya yamechangiwa na watu kutafuta ardhi, utumwa na ukoloni ulioshamiri katika bara la Afrika kuanzia karne ya 16 na mwishoni mwa karne ya 19 haya yote ni kwa sababu ya kutafuta ardhi, nchi nyingi hasa za mashariki ya kati zina migogoro isiyoisha ikiwa na chimbuko lake ni kumiliki ardhi, ardhi imekuwa ni sehemu muhimu kwa maisha ya binadamu.

Hii ndio imepelekea kuwepo kwa sharia kali na makini sana kwenye maswala yote ya ardhi, kwa mfano sharia za ardhi kwa nchi za Ulaya na Marekani ni ngumu na makini sana kiasi kwamba kama sio mzawa wan chi hiyo sio rahisi kumiliki ardhi, watakupa kila kitu ila sio ardhi yao, nchi nyingine hata kununua ardhi kwa watu ambao sio wazawa sio kazi rahisi. Kumekuwa na umakini mkubwa sana kwenye maswala ya ardhi na sharia kwenye baadhi ya nchi za Magharibi.

Tangu nchi nyingi za kiafrika zitoke kwenye ukoloni, au zipate uhuru zimekuwa nasheria ambazo zilitumika kwa kiasi kikubwa na wakoloni, hivyo bila kuzifanyia marekebisho na maboresho ili ziwafae wananchi wao, badala yake wameziacha na zimekuwa kama za kiloni kwenye baadhi ya maeneo. Hii ni kwasababu ya migogoro isiyoisha ya ardhi hasa kwa baadhi ya maeneo katika nchi ya Tanzania. Migogoro hii maarufu kama migogoro ya wafugaji na wakulima, watu wa mazingira na wafanyabiashara au wawekezaji, wafugaji na watu wa hifadhi za Wanyamapori, watu wa maliasili na wakulima, wafanyabiashara.

Sheria za ardhi zipo, sharia za mazingira zipo, sharia za uhifadhi wa wanyamapori zipo, sharia za misitu zipo. Lakini sharia hizi hazieleweki vizuri kwa watu wengi. Tafiti nyingi zinaonyesha sehemu zenye migogoro mikubwa ya ardhi katika nchi yetu ni kutokana na kutokuweka wazi na kutokueleweka kwa sharia hizi kwa watu wengi hasa jamii za kifugaji, hii vile vile ni kutokana na watu wengi kwenye maeneo ya migogoro hii kutokuwa na elimu ya kusoma na kuandika hivyo huwa wia vigumu kupata msaada wa sharia kwa haraka.

Jinsi ya kumaliza tatizo hili kwa siku za usoni, ni kuhakikisha kunakuwa na mikakati ya dhati kabisa kwa wahusika wenye dhamani ya kushughulikia maswala yote ya ardhi wanatoa mwongozo mwepesi na unaoeleweka kwa jamii kuhusiana na maswala yote ya ardhi, pia serikali ipangilie na kupanga maeneo yote ya wazi na mapori yasiyojulikana yapo kwa matumizi gani, mfano kuyagawa na kuyapima mapori yote na kuyatenga kwa kazi husika, inaweza kuwa pori kwa ajili ya malisho ya Wanyama, au eneo kwa ajili ya makazi au eneo kwa ajili ya msitu wa akiba nk, hii itasaidia jamii husika na watu wengine wanaovamia mashamba au maeneo kuelewa eneo husika mapema hivyo kupunguza migogoro kwa siku zijazo.

Sambamba na hilo ni kupitia sharia zote za ardhi na sharia za ardhi ya vijiji ili kuiweka kwa namna ambayo italeta uwiano sawa kwa watu wote. Kila eneo la ardhi ya nchi yetu linatakiwa kueleweka kwa watu wote kuwa ni eneo la nini, au limetengwa mahususi kwa shughuli gani. Hii itasaidia kuondoa migogoro ya ardhi kwa siku zijazo. Mfano wafugaji wengi wanapata shida sana wanapoingiza mifugo yao eneo la hifadhi ya Wanyamapori, wanapokamatwa na askari wananyamapori wengi wao husema walikuwa hawajui kama wameshaingia na kuvuka mpaka wa eneo la hifadhi. Wafugaji na jamii yote ya wafugaji wanatakiwa kupewa elimu ya ardhi sambamba na kuelewa vizuri maeneo yao ya kulishia mifugo yao.

Nipende kumalizia makala hii kwa kutoa rai kwa wahusika wote na watu wanao tafuta suluhisho kwenye maswala ya ardhi, wanaweza kutumia maarifa haya kuwaongezea uwanja mpana wa kufanya maamuzi sahihi ili kujenga nchi ya amani ambayo kila mtu atafanya shughuli zake kwa utulivu, bila kumkwaza mwenzake. Haya mambo ya kumaliza migogoro ya ardhi na migogoro migine inayohusiana na ardhi ipo ndani ya uwezo wetu kuyatatua na kuyamaliza. Hatuhitaji umoja wa mataifa kwenye hili. Jinsi tunavyochelewa na kuwa wazito kutatua migogoro hii ya ardhi katika nchi yetu, ndivyo magomvi, visasi, wivu, ukabila, udini, na matabaka mengine mabaya yanapata mizizi na kukua hatimaye kuja kutusumbua siku zijazo. Na tutawatengenezea watoto wetu mazingira magumu sana ya kuishi kwenye nchi yao wenyewe. Hivyo basi tuanze sasa, tuanze mapema.

Asante kwa kusoma makala hii, iliyoandikwa na kuandaliwa na;

Hillary Mrosso

0742092569

hillarymrosso@rocketmail.com

 

Shares:
Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *