Tangu wakati wa ukoloni jamii ilizuiliwa kisheria kutumia wanyamapori na haki ya kutumia wanyamapori ilibakia mikononi mwa serikali. Kutokana na hali hii jamii ilijitoa kabisa kwenye masuala ya wanyamapori na haikushirikishwa kwa namna yoyote ile kutumia rasilimali za wanyamapori kwa kipindi hiki. Jambo ambalo limetengeneza mtazamo hasi kwa jamii kuhusu wanyamapori na mamlaka zinazosimamia wanyamapori hao. Ingawa jambo hili limeshapita na tangu serikali za kikoloni ziondoke Tanzania, bado kumekuwa na aina ya mfumo wa usimamizi wa wanyamapori ambao sio rafiki kwa jamii, mfumu huu ambao unawasukumia mbali wananajamii kutoshiriki kwenye uhifadhi wa wanyamapori na maliasili nyingine.
“Kikwazo kikuu katika kufikia fursa hii ni kwamba tangu wakati wa ukoloni jamii zilizuiliwa kisheria kutumia wanyamapori na haki za kutumia wanyamapori zilibakia na kuthibitiwa na serikali”.Tanzania Natural resource Forum
Tangu itungwe sera ya wanyamapori ya mwaka 1998, mabadiliko mengi ya kimfumo na kiuendeshaji kwenye maliasili zetu umebadilika ili kuendana na kasi ya ongezeko la watu na pia matumizi ya teknologia, kimsingi mahitaji ya watu yameongezeka sana. Sera hii imetoa nafasi kubwa sana kwa jamii kushirikishwa katika uhifadhi wa maliasili. Pamoja na mambo mengine sera ya wanyamapori imeotoa maelekezo ya moja kwa moja kwa jamii kusiriki katika usimamizi wa maliasili zao. Jambo ambalo limeleta maliasili hizi karibu na jamii na kutoa mwongozo wa jinsi jamii navyotakiwa kuhusishwa kwenye uhifadhi wa maliasili za maeneo hayo. Maeneo haya ambayo yametolewa na vijiji kuwa hifadhi ya wanyamapori au jumuiya za hifadhi ya wanyamapori yanajumuisha vijiji kadhaa vyenye mapori yenye wanyama na vimeridhia kutoa maeneo hayo kuwa ya jumuiya au asasi za kijamii za wanyamapori, maeneo haya yanajulikana kama maeneo ya hifadhi ya jamii (Wildlife Management Areas), WMAs kama wengi wanavyofahamu.
Kifungu cha 31 cha sheria ya uhifadhi wa wanyamapori ya mwaka 2009, inampa Waziri mamlaka ya kutangaza eneo lolote la ardhi ya Kijiji kuwa hifadhi ya jamii au WMA, na waziri atafanya hivyo baada ya kupokea mapendekezo kutoka kwa mkurugenzi wa wanyamapori ikionyesha kwa ufasaha makubaliano na maoni ya wanajumuiya walioamua kutoa ardhi ya vijiji vyao kuwa hifadhi ya jamii kwa mujibu wa kanuni na sheria za wanyamapori. Hivyo kwa kutambua jambo hilo jamii inatakiwa kusimamia na kuendesha hifadhi hizi kwa mujibu wa sheria na kanuni kama itakavyopendekezwa na waziri mwenye dhamana.
Serkali ya Tanzania ilitenga maeneo mengi na makubwa sana kwa ajili ya uhifadhi wa wanyamapori, katika kutenga maeneo haya walizingatia yenye matawanyiko mkubwa wa kibaiologia na pia uwepo wa spishi za wanyamapori ambazo ni muhimu katika mfumo mzima wa ikologia na mazingira. Hivyo meneo mengi ya hifadhi ya wanyamapori yalitengwa na kuwa na hadhi mbali mbali kwa mfano serikali ilishatenga maeneo 38 ya hifadhi ya jamii au WMAs ambazo kati ya hizo ni WMAs 17 tu ndio zimeendelezwa na kutambuliwa na jamii kama maeneo yao ya hifadhi yaliyopo chini ya usimamizi wao. Pia kuna idadi ya Mapori ya Akiba (Game Reserves) yasiyopungua 28, haya ni maeneo muhimu sana kwa uhifadhi na utalii na ni maeneo ambayo shughuli mbali mbali za kitalii kama utalii wa picha na utalii wa uwindaji hufanyika kwa kibali maalumu. Aidha kuna maeneo mengine yanayoitwa Mapori Tengefu (Game Controlled Areas) haya ni maeneo yaliyotengwa na serikali kwa ajili ya uhifadhi na pia uwindaji unaruhusiwa kwa kibali maalumu,idadi ya maeneo haya ni 44. Mbali na maeneo hayo niliyoyataja pia kuna maeneo mengine yanayojulikana sana kama hifadhi za Taifa maeneo haya hadi sasa yapo 16, ni maeneo yanayaosimamiwa na mamlaka ya TANAPA. Kwenye maene haya uwindaji wa aina yoyote hauruhusiwi lakini utalii wa picha unaruhusiwa.
Katika maeneo yote hayo yaliyotengwa kwa ajili ya uhifdhi wa wanyamapori, mengi yalikuwa hayatoi nafasi kwa jamii kuhusika moja kwa moja. Jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa jamii kukosa uelewa wa masuala ya wanyamapori na masuala ya maliasili kwa ujumla. Ilipotungwa sera ya wanyamapori ilikuwa na lengo la kuhakikisha jamii inashiriki na kunufaika na uwepo wa maliasili za wanyamapori kwenye maeneo yao. Hii ikiwa ni njia ya kuleta maliasili za wanyamapori karibu na jamii kwa lengo la kuinufaisha jamii. Aidha kama nilivyoeleza hapa mwanzo kuwa kuanzishwa kwa Asasi hizi umeinua tena matumaini na kufanya jamii kuona wana haki na wanaweza kuhusika na kushiriki katika mambo mbali mbali ya rasilimali hizi. Kwa upande mwingine uanzishwaji wa maeneo haya umetengeneza fursa nyingi sana za watu kujifunza na kupata kipato. Na kwa kuwa halmashauri za wilaya na vijiji ndio wasimamizi wa maeneo haya kumekua na hali nzuri sana ya jamii kujihusisha moja kwa moja kwenye masula ya maliasili na kufahamu kwa kina kuhusu rasilimali zao.
Pamoja na changamoto zilizopo bado uanzishwaji wa WMAs umesaidia sana elimu ya uhifadhi kueleweka kwa urahisi na jamii, na inaifundisha jamii kuhusu masula mengi ya maliasili, utunzaji na uhifadhi na njia za kupambana na ujangili. Kwa namna nyingine kwa kuwa maeneo haya ni mali ya vijiji wanachama au ya jumuiya ulinzi na usimamizi wake unamtaka kila mwanajumuiya kuhusika. Na kwa namna hii jamii inajifunza mbinu mbali mbali za uhifadhi wa maeneo yao na pia namna ya kupambana na majangili na changamoto nyingine zinazotokea kwenye uhifadhi. Kuwepo kwa maeneo haya kumetengeza fursa kwa vijiji husika kuchagua watu ambao watakuwa ni askari wa kusimamia rasilimali za jumuiya yao (Village Game Scout). Watu hawa wamekua na kazi kubwa sana kwenye jamii kuhakikisha usalama wa rasilimali zao na pia kushirikiana na askari wengine wa maliasili kwenye kupiga vita ujangili.
Kwa jambo hili naipongeza sana serikali na wadau wa maliasili kwa kuhakikisha maeneo haya ya WMAs yanakuwepo na kuendelezwa kwa manufaa ya jamii nzima. Ingawa kuna changamoto nyingi kwenye uendelezwaji wa maeneo haya lakini ni muhimu kwa namna yoyote ili maeneo haya yakaendelezwa ili kupunguza utegemezi kwenye maeneo kiini ya uhifdhi kama vile hifadhi za taifa. Naamini kabisa endapo serikali za halmashauri za wilaya na vijiji wataamua kukaa na kuweka mipango bora na kutengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji kwenye maeneo haya basi tutakuwa tumetatua tatizo kubwa sana kwa upande wa jamii na maliasili zetu.
Maeneo haya pamoja na mambo mengine yanahitaji wataalamu na washauri wa mipango na namna ya kuweka fursa nzuri na kuzitangaza ili kuvutia wawekezaji kwenye maeneo hayo. Pia ili kuhakikisha kila kinachopatikana kama mapato kutokana na uwepo wa WMA inawanufaisha wote na kusimamiwa vizuri lazima kuwe na utaraibu mzuri na wa wazi kwenye uongozi wa maeneo haya. Aidha, kwa kuwa maeneo haya bado ni mabichi na watu hawana uzoefu na utalaamu wa kutosha hivyo wanahitaji mafunzo ya mara kwa mara ya usimamizi uongozi na mafunzo mengine muhimu ya kiikologia, jambo hili litasaidia na jamii kufahamu vizuri maliasilizao na kuzitunza.
Asante sana kwa kusoma makala hii, karibu tuendelee kujifunza kwa pamoja makala ijayo. Tuzitunze na kuzilinda maliasili zetu kwa manufaa ya sasa na baadaye.
Ahsanete sana.
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 862 481/+255 742 092 569
www.mtaalamu.net/wildlifetanzania