Habari msomaji wa makala za wildlife Tanzania, karibu tena siku ya leo tujifunze kitu kuhusu CITES,  kama nilivyoainisha kwenye makala iliyopita CITES ni kirefu cha Convention on International Trade of Endangered Species of wild Fauna  and Flora. Kwa Kiswahili kisicho rasmi ni Makubaliano kuhusu biashara za kimataifa za spishi ambazo zipo hatarini. Na hapo ana maanisha ni mimea ya mwituni na wanyamapori. Makubaliano haya ya ni baina ya nchi mbali mbali ambazo zinataka kuendeleza uhifadhi wa wanyamapori kwenye nchi zao, hivyo kwa nchi kujiunga na CITES ina maana itapata msaada na ushirikiano kwenye uhifadhi wa viumbe hai ambavyo vipo mwituni. Kwa hiyo lengo kuu likiwa ni kudhibiti, na kuangalia vigezo vyote vya usafirishaji na biashara ya spishi za viumbe hai.

Hivyo CITES wameandaa utaratibu wao mzuri wa kuwatenga wanyama na mimea ambayo imo hatarini kulingana na kiasi cha hatari kinachokabili viumbe hai hawa, kwa kuzingatia hilo wamepanga kwenye makundi matatu yanayojulikana kama Apendix, hivyo kuna appendix I, Appendix II, na Appendix III. Hivyo unaweza ukaelewa kulingana na mpangilio huo wa appendix ni spishi gani ipo hatarini zaidi kutoweka, ni  spishi ipi haipo hatarini sana, lakini pia ni spishi ipi ambayo inaweza au kukaribia kuwa kwenya hatari. Kwa kuzipanga hivi inatoa taswira pana sana kwa wahifadhi na kwa nchi wanachama wa CITES kuchukua juhudi za ziada kwenye uhifadhi na usalama wa viumbe hawa, ikiwa ni pamoja na kuzuia biashara za viumbe na spishi hizo, hili ni jambo linaloungwa mkaono na wanachama wote kwa kushirikiana kuhakikisha hawa wanyamapori na mimea inaendelea kuwepo.

Appendix I

Kwa msingi huo ngoja tuangalie kundi la spishi waliopo kwenye appendix I, ambalo ndio kundi la kwanza na la kipaumbele kwenye uhifadhi kwasababu ni kundi la spishi zote ambazo zipo hatarini kutoweka. Hivyo kwenye appendix I ni spishi za wanyama na mimea ambao wapo hatarini zaidi kutoweka kabisa hivyo wanahitaji, nguvu ya ziada kwenye uhifadhi wake.  Ukisoma na kufuatilia orodha ya spishi waliopo kwenye Appendix I utashangaa sana, ni nwengi sana. Unaweza wewe mwenyewe kuangalia www.cites.org ili ujue jinsi ambavyo dunia inaelekea kupoteza viumbe hai ambao hata wengine sijawahi kuwaona sehemu yoyote, ila kwenye vitabu tu na kwenye mitandao.

Kutokana na hali hiyo tulioiona kwenye appendix I, nchi wanachama wa CITES, wamekubaliana kuwa wanyamapori na miti, au mimea ambayo ipo kwenye hii appendix I haitakiwi kuuzwa wala kusafirishwa kibiashara, isipokuwa kwa makusudi maalumu ambayo siyo ya kibiashara kama utafiti wa kisayansi. Hivyo kwa nchi wanachama ambao wamekubaliana kudhibiti biashara ya wanyamapori na miti au mimea ambayo ipo kwenye kundi hili. Pia hawaruhusu hata sampuli, au sehemu ya mwili wa spishi hizi kuuzwa, kwa mfano ngozi, meno, pembe, au kucha haziruhusiwi kabisa na CITES kuuzwa sehemu yoyote. Mfano wa wanyamapori  ambao wamo kwenye kundi hili la appendix I ni Faru, Duma, Sokwe, Chui, Mbwa mwitu, Tembo na Mbuni, hiyo ni baadhi tu ya wanyama na ndege ambao wamo kwenye appendix I, lakini pia kuna nchi ambazo wanyama na ndege niliowataja hawapo kwenye kundi hili. Nitaelezea hili kwenye makala zijazo.

Appendix II

Kwenye kundi hili la pili kuna spishi ambao hawapo kwenye hatari kubwa kwa sasa kwasababu tu ya kuzuia biashara ya usafirishaji na uuzwaji. Endapo biashara ya spishi waliomo kwenye kundi hili haitadhibitiwa na kuendeshwa kwa umakini mkubwa basi itapelekea kupotea kwa wanyama na mimea iliyopo kwenye kundi hili, au wanaweza kuwekwa kwenye kundi la hatari zaidi kutoweka, kundi la kwanza. Kwenye kundi hili CITES hawaruhusu kabisa biashara ya spishi hizi, lakini endapo kuna uhitaji wa lazima sana ambao umeafikiana na masharti na sheria za CITES, nchi wanachama wanaruhusa ya kusafirsha kibiashara, kwa kibali kutoka mamlaka zote zilizopo ndani ya nchi husika na pia mamlaka za nchi zinazouziwa na pia kibali cha CITES lazima kitolewe. Kwa hiyo yote yanatakiwa yafanyike kwa kuangalia usalama wa kiumbe hicho na pia usalama wa viumbe vingine. Baaadhi ya wanyama au spishi waliopo hapa kwenye kundi la pili ni pundamilia, jamii za nyani, spishi za tembo hasa walioko Namibia, na baadhi ya spishi za kobe, na mimea aina ya Aloevera, ni baadhi tu ya spishi nyingi zilizopo kwenye kundi hili la pili.

Appendix III

Kwenye kundi hili la tatu na la mwisho ni spishi za wanyamapori na mimea ambayo nchi inaomba kuwaweka kutokana na kurekebisha biashara kwenye spishi hizi. Hivyo nchi husika itaomba msaada wa kutoka kwa washirika wengine pamoja na CITES kwa ujumla kulinda na kuhifadhi wanyama na mimea hiyo. Pia biashara kwenye spishi waliopo kwenye kundi hili inatolewa kwa mujibu wa makubaliano ya mkutano mkuu wa CITES, na pia kunatakiwa kuwe na uwasilishwaji wa taarifa ya kufanya hivyo kwenye cheti  ambacho mhusika atapewa na mamlaka husika.

Hivi ndivyo wanavyofanya CITES ili kuhakikisha wanyama na mimea inaendelea kuwepo kwenye maeneo yaliyohifadhiwa. Nimejifunza kitu kikubwa hapa masuala yote ya uhifadhi wa maliasili na mazingira sio jambo la nchi moja bali ni jambo ambalo dunia inatakiwa kulivalia njuga ili kuendelea kuwa na sehemu salama ya kuisha wanadamu na viumbe hai wengine. Hakuna wanyama au miti inaweza kufanya jambo hili, ni sisi tu, ambao tumeajaliwa akili na utashi wa kuamua mambo mazuri na mabaya kwenye mazingira yetu.

Naamini kwa makala hii umepata mwanga jinsi ambavyo mambo yanavyotakiwa kuchukuliwa ili kunusuru hali ya viumbe hai na maliasili nyingine kwenye nchi zetu. Ukiangalia orodha ya wanyama na mimiea ambayo ipo hatarini kupotea kwenye uso wa dunia ni idadi kubwa sana kwa mujibu wa CITES, www.cites.org  imefikia 36,000. Ni idadi kubwa sana hiyo. Maarifa haya yatatusaidia kufikiri kwa kina na kwa upana unaotakiwa ili kuamua njia na mbinu za kunusuru viumbe hai  na mazingira yao.

Ahsante sana kwa kusoma makala hii,

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255742092569/+255683248681

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtalaamu.net/wildlifetanzania